Index   Back Top Print

[ AR  - BE  - DE  - EN  - ES  - FR  - IT  - LA  - PL  - PT  - RU  - SL  - SW  - ZH_CN  - ZH_TW ]

WOSIA WA KITUME
BAADA YA SINODI
AMORIS LAETITIA
WA BABA MTAKATIFU
FRANSISKO
KWA MAASKOFU,
MAPADRE NA MASHEMASI
KWA WATU WENYE NADHIRI
KWA WANANDOA WAKRISTO
NA KWA WAAMINI WOTE WALEI
JUU YA UPENDO KATIKA FAMILIA

 

 

Faharasa

SURA YA KWANZA
KATIKA MWANGA WA NENO LA MUNGU

Wewe na mkeo.
Wanao kama miche ya mizeituni
Njia ya mateso na kumwaga damu.
Taabu ya mikono yako.
Upole wa kukumbatia.

SURA YA PILI
HALI HALISI NA CHANGAMOTO ZA FAMILIA

Hali halisi ya familia wakati huu.
Changamoto nyingine.

SURA YA TATU
KUMTAZAMA YESU: WITO WA FAMILIA.

Yesu anahuisha na kuukamilisha mpango wa Mungu.
Familia katika hati za Kanisa.
Sakramenti ya ndoa.
Mbegu za Neno na hali zenye mapungufu.
Uzazi na malezi ya watoto.
Familia na Kanisa.

SURA YA NNE.
UPENDO KATIKA NDOA.

Upendo wetu wa kila siku.

Uvumilivu.
Moyo wa ufadhili 
Kuponya husuda.
Bila kutakabari wala kujivuna.
Adabu.
Kujibandua na ubinafsi kwa ukarimu.
Bila ukatili wa ndani 
Msamaha.
Kufurahi pamoja na wengine.
Huvumilia yote.
Unaamini 
Hutumaini 
Hustahimili yote.

Kukua katika mapendo ya kindoa.

Kwa maisha yote, mambo yote katika umoja.
Furaha na uzuri 
Kufunga ndoa kwa upendo.
Upendo unaojidhihirisha na kukua.
Mazungumzano.

Upendo wa tamaa.

Ulimwengu wa mihemuko.
Mungu anapenda furaha ya watoto wake.
Upendo kama mapenzi 
Ukatili na ulaghai 
Ndoa na ubikira.

Mabadiliko ya upendo.

SURA YA TANO.
UPENDO UZAAO MATUNDA.

Kuukaribisha uhai mpya.

Upendo wakati wa kusubiri ujauzito.
Upendo wa mama na wa baba.

Kupanuka kwa uzaaji 

Kuutambua mwili 

Maisha katika familia pana.

Kuwa wana.
Wazee.
Kuwa ndugu.
Moyo mkuu.

SURA YA SITA.
BAADHI YA MITIZAMO YA KICHUNGAJI.

Kuitangaza Injili ya familia leo.

Kuwaandaa wachumba kwa ajili ya ndoa.

Maandalizi ya adhimisho.

Kusindikiza mwanzoni mwa maisha ya ndoa.

Baadhi ya mbinu za kufanya.

Kutia mwanga kwenye migogoro, fadhaa na magumu.

Changamoto ya migogoro.
Vidonda vya zamani 
Kusindikiza baada ya kuvunjika uhusiano wa ndoa na baada ya talaka.
Baadhi ya mazingira magumu.

Maumivu makali ya kifo.

SURA YA SABA.
KUIMARISHA MALEZI KWA WATOTO.

Watoto wako wapi?
Mafundisho ya kimaadili kwa watoto.
Umuhimu wa adhabu kama kichocheo.
Kukubali hali halisi kwa uvumilivu.
Maisha ya familia kama mazingira ya malezi 
Hitaji la elimu ya jinsia.
Kurithisha imani 

SURA YA NANE.
KUSINDIKIZA, KUPAMBANUA NA KUTEGEMEZA UDHAIFU.

Kazi ya kichungaji hatua kwa hatua.
Upambanuzi wa hali zinazoitwa “zisizo kadiri ya kanuni”
Mambo tetezi katika upambanuzi wa kichungaji 
Kanuni na upambanuzi 
Mantiki ya huruma ya kichungaji. 

SURA YA TISA.
TASAUFI (MAISHA YA KIROHO) KATIKA NDOA NA FAMILIA.

Tasaufi ya ushirika wenye kupita maumbile.
Kuungana katika sala kwa mwanga wa Pasaka.
Tasaufi ya upendo unaojitoa kwa mwenzake tu kwa uhuru.
Tasaufi ya kujali, kufariji na kuhamasisha.

Sala kwa Familia Takatifu.

 

1. Furaha ya upendo (Amoris Laetitia) ambayo watu wanaiishi katika familia ni furaha ya Kanisa pia. Kama walivyosisitiza Mababa wa Sinodi, licha ya dalili nyingi za migogoro ya taasisi ya ndoa, “hamu ya kuwa na familia inadumu kuwa hai, hasa kati ya vijana, na hamu hiyo inalihimiza Kanisa”[1]. Kama jibu la matamanio haya “tangazo la Kikristo kuhusu familia ni kwa hakika habari njema”[2].

2. Mwendo wa sinodi uliruhusu kuchanganua hali ya familia katika ulimwengu wa leo, kuupanua mtazamo wetu na kuihuisha dhamiri yetu juu ya umuhimu wa ndoa na familia. Wakati huohuo, mchangamano wa mada zilizopendekezwa umetuonyesha hitaji la kuendelea kuchambua kwa uhuru masuala kadhaa ya kimafundisho, kimaadili, kiroho na kiuchungaji. Tafakari ya wachungaji na wanateolojia, ikiwa ni aminifu kwa Kanisa, nyofu, ikizingatia hali halisi kwa ubunifu, itatusaidia kuufikia utambuzi wa kina zaidi kuhusu masuala haya. Mijadala inayofanyika katika vyombo vya mawasiliano au katika machapisho au hata kati ya wahudumu wa Kanisa, inahusu mambo mengi mbalimbali, kuanzia hamu isiyo na lijamu ya kupindua kila utaratibu bila kutafakari au kuwa na msingi tosha, hadi ule msimamo unaodai kutatua kila suala kwa kukazia kanuni za jumla au kwa kuchukua uamuzi mkali kutokana na matafakari fulani ya kiteolojia.

3. Kwa kukumbuka kuwa wakati ni muhimu kuliko mahali, ninapenda kusisitiza kwamba si lazima mijadala yote ya kimafundisho, ya kimaadili au ya kiuchungaji itatuliwe kwa njia ya matamko ya majisterio. Bila shaka katika Kanisa inatakiwa kuwa na umoja wa mafundisho na wa utendaji, lakini hilo halizuii kuwepo kwa namna mbalimbali za kufasiri masuala kadha wa kadha ya mafundisho au mambo mengine yatokanayo nayo. Na hali hiyo itaendelea hadi hapo Roho atakapotuongoza atutie kwenye kweli yote (rej. Yn 16:13), yaani atakapotuingiza kikamilifu katika fumbo la Kristo na tutaweza kuona yote kwa mtazamo wake. Aidha, katika kila nchi au ukanda inawezekana kutafuta masululisho yaliyotamadunisha zaidi, yanayozingatia desturi na changamoto za mahali husika. Kwani, “tamaduni zinatofautiana sana, na kila kanuni msingi […] inahitaji kutamadunishwa, ikipaswa kushikwa na kutekelezwa”[3].

4. Kwa vyovyote, lazima niseme kwamba mwendo wa sinodi ulikuwa una uzuri mkubwa na kutoa mwanga kwa wingi. Ninatoa shukrani kwa michango mingi iliyonisaidia kutazama matatizo ya familia za sehemu zote za dunia katika upana wake wote. Ujumla wa hoja walizotoa Mababa, ambazo nilizisikiliza daima kwa makini, umeonekana kwangu kama poliedri yenye thamani, iliyojaa kero zilizo halali na maswali manyofu na ya kweli. Ndiyo maana niliona vema kuandika Wosia wa Kitume wa baada ya sinodi unaokusanya michango ya sinodi hizi mbili za hivi karibuni kuhusu familia, kwa kuunganisha pia mawazo mengine yanayoweza kutoa dira kwa matafakari, mazungumzano na matendo ya kiuchungaji, na wakati huohuo yatie moyo, yawe kichocheo na yalete msaada kwa familia zote katika juhudi wanazofanya na magumu wanayokutana nayo.

5. Wosia huu unapata maana maalumu katika muktadha wa Mwaka huu wa Jubilei ya Huruma. Kwanza kabisa, kwa sababu nimenuia uwe kama mwaliko kwa familia za kikristo, wa kuwahimiza kuthamini tunu za ndoa na familia, na kudumisha upendo thabiti uliojaa tunu za ukarimu, juhudi, uaminifu na ustahimilivu. Pili, kwa sababu unaazimia kuwatia wote moyo ili kuwa ishara za huruma na ukaribu popote pale maisha ya kifamilia hayatimizwi kikamilifu au yanakosa amani na furaha.

6. Kuhusu mpangilio wa sura za Wosia huu, nitaanzia kwa utangulizi uliovuviwa na Maandiko Matakatifu, utakaoutia Wosia wenyewe kwenye kiwango kifaacho. Kutokana na hayo, nitaangalia hali ya kisasa ya familia, kwa lengo la kutokwepa hali halisi ya dunia ya leo. Halafu nitakumbushia vipengele vichache vya msingi vya mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia, ili kuandaa nafasi kwa sura mbili za kati, zinazohusu upendo. Baadaye nitasisitiza njia kadhaa za kiuchungaji zinazoweza kutuelekeza katika uundaji wa familia imara na zenye kuzaa matunda kadiri ya mpango wa Mungu, na nitatumia sura moja kwa kuzingatia malezi ya watoto. Baada ya hayo, nitabakia katika mwaliko wa kuwa na huruma na kufanya upambanuzi wa kichungaji mbele ya hali za maisha ambazo haziendani kikamilifu na mashauri ya Bwana, na mwisho nitachora mistari michache juu ya tasaufi ya kifamilia, yaani maisha ya kiroho katika familia.

7. Kutokana na utajiri wa miaka miwili ya kutafakari ulioletwa na mwendo wa sinodi, Wosia huu unachambua, kwa mitindo mbalimbali, mada nyingi na za aina tofauti. Jambo hilo linaelezea kwa nini hati hii haikuweza kuwa mfupi. Na ndiyo sababu mimi nishauri isisomwe yote katika ujumla wake kwa haraka. Itapokelewa vizuri zaidi na katika thamani yake yote, kwa upande wa familia na vilevile wa wahudumu wa uchungaji wa familia, ikiwa wataitafakari polepole sehemu kwa sehemu, au wakiwa watatafuta humu yale ambayo wanahitaji katika kila mazingira mahsusi. Inawezekana, kwa mfano, kwamba wenzi wa ndoa watatambua kwa urahisi zaidi kuwa sura ya nne na ya tano zinawaongelea wao, au kwamba wahudumu wa uchungaji wataona ni muhimu zaidi sura ya sita, na kwamba wote wanajadiliwa na sura ya nane. Ninatumai kwamba kila mmoja, kwa njia ya kuusoma, ajisikie kuwa ameitwa kuwajibika kwa upendo juu ya maisha ya familia mbalimbali, kwa sababu zenyewe “wala si tatizo, bali hasa ni fursa”.[4]

SURA YA KWANZA

KATIKA MWANGA WA NENO LA MUNGU

8. Katika Biblia zinapatikana habari nyingi za familia mbalimbali, vizazi, mapenzi, shida zilizokumba mazingira ya kifamilia; kuanzia ukurasa wa kwanza, ambao unaonyesha familia ya Adamu na Eva, pamoja na mambo ya ujeuri yaliyoilemea, lakini pia na nguvu ya uhai unaoendelea katika vizazi (taz. Mwa 4), hadi ukurasa wa mwisho unaoonyesha ndoa ya Bibi arusi na Mwanakondoo (taz. Ufu 21:2,9) Mfano uliotolewa na Yesu wa nyumba mbili zilizojengwa moja juu ya mwamba na moja juu ya mchanga, unadokeza hali nyingi za kifamilia zinazotokana na uhuru wa wana familia, kwa maana, kama alivyoandika mshairi, “kila nyumba ni kama kinara”.[5] Na tuingie sasa katika moja ya nyumba hizo, kwa kuongozwa na Mzaburi kwa njia ya utenzi ulioimbwa hadi leo katika liturujia ya ndoa ya kiyahudi, na ya kikristo pia.

“Heri kila mtu amchaye Bwana,
aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila,
utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
vyumbani mwa nyumba yako;
Wanao kama miche ya mizeituni
wakizunguka meza yako.
Tazama, atabarikiwa hivyo,
yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
uone uheri wa Yerusalemu
siku zote za maisha yako.
Naam, ukawaone wana wa wanao.
Amani ikae Israeli!” (Zab 128)

Wewe na mkeo

9. Tuvuke mlango na kuingia katika nyumba hii ya amani, ambayo familia yake wamekaa wakizunguka meza yake siku ya sherehe. Kiini chake ni jozi: mama na baba, pamoja na maisha yao ya kupendana. Katika hao unatimizwa mpango ule wa asili ambao Kristo mwenyewe anakumbuka wazi, “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba Mtu mume na mtu mke?” (Mt 19:4) Naye anataja ile amri ya kitabu cha Mwanzo, “Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja” (Mt 19:5; taz. Mwa 2:24)

10. Sura mbili nzuri sana za kwanza za kitabu che Mwanzo zinatuonyesha jozi la mume na mke katika kweli yake ya msingi Katika matini hizi za mwanzo za Biblia, kauli kadhaa muhimu sana zinang’aa. Kauli ya kwanza, ambayo Yesu ametaja kwa kifupi, ni, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Mwa 1:27) Inashangaza kuwa “mfano wa Mungu” ni sambamba na jozi “mnanamume na mwanamke” kama maelezo yake. Je, maana yake ni kwamba Mungu mwenyewe ana jinsia yake, au ana mwenzi wake wa kike, kama zilivyodhani dini fulani za zamani? La, sivyo! Maana, twajua jinsi Biblia inavyokataa kwa wazi dini hizi zilizoenea kati ya Wakananayo wa Nchi Takatifu kwa kuona kuwa ni kuabudu miungu. Dhana ya upekee usiofikika wa Mungu inahifadhika; lakini, kwa kuwa yeye ni Muumba pia, uzaaji wa jozi la kibinadamu ni “mfano”, hai na wa maana, na alama inayoonekana ya kazi ya kuumba.

11. Jozi lililo na upendo, na kuzalisha uhai, ni kwa kweli “ikona” hai, yenye uwezo wa kumdhihirisha Mungu muumbaji na mwokozi, kinyume na sanamu za jiwe au dhahabu ambazo Amri kumi zinakataza. Kwa hiyo upendo wenye kuzaa unakuwa ni ishara ya mtima wa Mungu (taz. Mwa 1:28; 9:7; 17:2-5,16; 28:3; 35:11; 48:3-4) Ndiyo sababu simulizi la kitabu cha Mwanzo, kwa kufuata mapokeo yaliyoitwa “ya kikuhani”, lina ndani yake orodha nyingi za vizazi (taz. Mwa 4:17-22,25-26; 5:10; 11:10-32; 25:1-4,12-17,19-26;36): maana, uwezo wa jozi la kibinadamu wa kuzaa ni njia ambayo kwa hiyo historia ya wokovu yaendelea. Kutokana na hayo, uhusiano wenye kuzaa wa jozi ni mfano kwa ajili ya kugundua na kuonyesha fumbo lile la Mungu, la msingi katika mtazamo wa kikristo wa Utatu Mtakatifu, ambalo humdhihirisha Mungu kama Baba, Mwana, na Roho wa upendo. Mungu Utatu Mtakatifu ni ushirika wa upendo; na familia ni kioo hai kinachomwakisi. Maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II yanatuangaza: “Mungu wetu, katika fumbo lake la undani zaidi, si upweke, bali ni familia, kwa sababu ana ndani yake ubaba, umwana, na uhai wa familia, yaani upendo. Upendo huo, katika familia ya kimungu, ndiye Roho Mtakatifu”.[6] Familia, basi, si jambo geni kwa uhai wenyewe wa Mungu.[7] Hali hii ya jozi inayohusiana na Utatu Mtakatifu, inaonyeshwa kwa namna mpya katika teolojia ya Paulo, pale ambapo Mtume analihusisha na “fumbo” la muungano wa Kristo na Kanisa (taz. Efe 5:21-33).

12. Lakini Yesu, anapotafakari juu ya ndoa, anatukumbusha pia sehemu nyingine ya kitabu cha Mwanzo, yaani sura ya pili, pale ambapo inapatikana picha nzuri sana ya jozi la mume na mke, na yenye sifa zinazolieleza wazi. Tuzichague mbili tu. Ya kwanza ni hamu isiyotulizika ya mtu ya kutafuta “msaidizi wa kufanana naye” (Mwa 2:18,20), anayeweza kushinda upweke wake unaomlemea, ambao hata wanyama na viumbe vyote vinavyomzunguka haviwezi kuutuliza. Msemo wa Kiebrania wa asili unatudokezea fikra ya uhusiano wa moja kwa moja, kama wa mtu mmoja mbele ya mwingine, uso kwa uso, macho kwa macho; katika mazungumzano ambayo ni ya unyamavu pia, kwa kuwa katika kupendana, mara nyingi kubaki kimya kunaeleza kwa namna bora kuliko kunena. Ni kukutana na uso wa mtu mwingine, na“mtu-wewe” anayeakisi upendo wa Mungu, na ambaye ni “mali iliyo bora, msaidizi wa kumfaa, na nguzo ya kumtegemeza”, (YbS 36:24), kama anavyosema mwenye hekima wa Biblia. Au, kama anavyosema bibi arusi wa Wimbo Ulio Bora, kwa kukiri kwa namna nzuri sana hisia ya kupendana na ya kutoleana mmoja kwa mwingine, “Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake è [...] Mimi ni wake mpendwa wangu, naye ni wangu” (Wim 2:16; 6:3).

13. Kufuatana na kukutana huko, kunakoponya upweke, uzazi na familia vinaanza. Nalo ni jambo la pili tunaloweza kusisitiza: Adamu, aliye pia mfano wa mtu wa kila wakati na kila mahali pa dunia yetu hii, anaanzisha familia mpya pamoja na mke wake, kama anavyorudia kusema Yesu kwa kunukuu kitabu cha Mwanzo: “Ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja” (Mt 19:5; taz. Mwa 2:24) Kitenzi “kuambatana” kwa lugha ya asili ya Kiebrania, kinaonyesha ulinganifu mkubwa, muambatano wa kimwili na wa undani; kiasi kwamba kinatumika ili kueleza muungano na Mungu: “Nafsi yangu inaambatana na Wewe” (taz. Zab 63:8), kama alivyoimba mzaburi. Kwa hiyo muungano wa ndoa unaonyeshwa si tu katika ujinsia na umwili, bali pia katika matoleo yake ya upendo kwa hiari. Tunda la muungano huo ni “kuwa mwili mmoja”, nalo ni kweli kimwili, na katika muungano wa mioyo na ya maisha pia, na, kama itatokea, katika mtoto atakayezaliwa na hao wawili, ambaye atapokea ndani yake na kuunganisha “miili” yote miwili, si kijenetiki tu bali kiroho pia.

Wanao kama miche ya mizeituni

14. Tuangalie tena utenzi wa Mzaburi: ndani ya nyumba ambapo mume na mke wake wamekaa mezani, wapo pia pamoja nao wanao, walio “kama miche ya mizeituni”, yaani wamejaa nguvu na ari motomoto. Wazazi ni kama misingi ya nyumba; na wanao ni kama “mawe hai” ya familia (taz. 1Pet 2:5). Ni jambo la maana kwamba neno linalopatikana mara nyingi zaidi katika Agano la Kale, usipofikiria jina la Mungu (YHWH, Bwana), ni “mwana” (Kiebrania: ben), neno linalohusiana na kitenzi cha Kiebrania “banah”, ambacho maana yake ni “kujenga”. Ndiyo sababu katika Zaburi 127, zawadi ya wana inafananishwa na picha zinazohusu ujenzi wa nyumba, na pia shughuli za kijamii na za biashara zilizofanywa kwenye lango la mji: “Bwana asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure [...] Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, uzao wa tumbo ni thawabu. Kama mishale mkononi mwa shujaa, ndivyo walivyo wana wa ujanani. Heri mtu yule aliyelijaza podo lake hivyo. Naam, hawataona aibu wanaposema na adui langoni” (Zab 127:1,3-5). Ni kweli kwamba picha hizo zinahusiana na utamaduni wa jamii ya kale, lakini uwepo wa wana ni kwa vyovyote alama ya utimilifu wa familia katika mfululizo wa historia ya wokovu, kizazi baada ya kizazi.

15. Kutokana na hayo, tunaweza kusisitiza sifa nyingine ya familia. Twajua kuwa katika Agano Jipya inasemwa kuhusu “Kanisa linalokusanyika nyumbani” (Taz. 1Kor 16:19; Rum 16:5; Kol 4:15; Flm 2). Mahali pa kuishi kwa familia palikuwa pakigeuka kuwa kanisa la nyumbani, mahali pa kuadhimisha Ekaristi Takatifu, pa kuwepo kwa Kristo amekaa kwenye meza ileile. Haiwezekani kusahau yaliyoandikwa katika Kitabu cha Ufunuo, “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; Mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” Ufu 3:20). Basi, hapa tunapata picha ya nyumba yenye ndani yake uwepo wa Mungu, sala ya pamoja, na, kwa hiyo, baraka ya Mungu. Hayo ndiyo yanayosemwa katika Zaburi 128, iliyo msingi wa kauli yetu, “Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana. Bwana akubariki toka Sayuni” (Zab 128:4-5).

16. Biblia inafikiria familia pia kama mahali pa katekesi kwa wana. Hiyo inaonekana wazi katika maelezo ya adhimisho la Pasaka (taz. Kut 12:26-27; Kum 6:20-25); na halafu ilikuwa dhahiri katika haggadah ya kiyahudi, yaani katika mazungumzo simulizi yaliyopo katika ibada ya karamu ya kipasaka. Zaidi, Zaburi moja inakutilia mkazo kutangaza imani katika familia; “Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, ambayo baba zetu walituambia, hayo hatutawaficha wana wao; huku tukiwaambia kizazi kingine, sifa za Bwana na nguvu zake, na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, na sheria aliiweka katika Israeli, aliyowaamuru baba zetu wawajulishe wana wao; ili kizazi kingine wawe na habari, ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao” (Zab 78:3-6). Kwa hiyo, familia ni mahali ambapo wazazi wanakuwa ni walimu wa kwanza wa imani kwa wana wao. Si huduma ya hadhara, bali ya mtu kwa mtu: “Itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza keshoni [...] utamwambia ...”(taz. Kut 13:14). Hivyo, vizazi tofauti vitamwimbia Bwana wimbo wao, “vijana waume, na wanawali, wazee, na watoto” (Zab 148:12).

17. Ni wajibu wa wazazi kutimiza kwa makini utume wa kulea, kama wanavyofundisha mara nyingi wenye hekima wa Biblia (Mit 3:11-12; 6:20-22; 13:1; 22:15; 23:13-14; 29:17). Wana wanaitwa kushika na kutimiza amri: “Waheshimu baba yako na mama yako” (Kut 20:12); pale ambapo kitenzi “kuheshimu”, maana yake ni kutekeleza kwa utimilifu wajibu wao wa kifamilia na wa kijamii, bila kuuacha kwa visingizio vya kidini (taz. Mk 7:11-13). Maana, “Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi” (YbS 3:3-4)

18. Injili inatukumbusha pia kwamba wana si mali ya familia, bali wao wana mwendo ulio wa pekee kwa ajili ya maisha yao ya mbeleni. Ni kweli kuwa Yesu amejionyesha kama mfano wa utii kwa wazazi wao wa kidunia, maana “alikuwa akiwatii” (taz. Lk 2:51); lakini kwa hakika ameonyesha pia kwamba mwana kuchagua njia yake ya kuishi, na wito wake wa kikristo pia, kunaweza kudai ajitenge ili kutimiliza kujitoa kwake kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (taz. Mt 10:34-37; Lk 9:59-62). Yesu mwenyewe, alipokuwa na umri ya miaka kumi na miwili, aliwajibu Maria na Yosefu kuwa yeye ana utume wa juu zaidi wa kutimiza, licha ya kuheshimu familia yake ya kidunia (taz. Lk 2:48-50). Ndiyo sababu anasisitiza kwamba inabidi kuwa na vifungo vingine, vya kina zaidi, hata katika mahusiano ya kifamilia: “Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya” (Lk 8:21). Zaidi, ingawa katika jamii ya kale ya Mashariki ya Kati watoto walikuwa wakifikiriwa kama wasio na haki maalumu na kama sehemu ya mali za ukoo, ni kweli kwamba Yesu anawaangalia sana, kiasi cha kuwatambulisha mbele ya watu wazima kama walimu wao, kutokana na watoto kuwategemea wengine kwa moyo safi na kwa hiari: “Amin, nawaambia: Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama Mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni” (Mt 18:3-4)

Njia ya mateso na kumwaga damu

19. Hali ya kupendana sana inayodhihirishwa katika Zaburi 128, haifuti hali nyingine inayoonyeshwa katika Maandiko Matakatifu yote, yaani uwepo wa huzuni, maovu, ujeuri, vitu vinavyorarua maisha ya familia na ushirika wake wa uhai na upendo. Ndiyo sababu, hata mazungumzo ya Yesu juu ya ndoa (taz. Mt 19:3-9) yamo ndani ya majadiliano juu ya talaka. Neno la Mungu ni shahidi daima juu ya kweli hii ya giza ambayo asili yake inapatikana mwanzoni, pale ambapo kwa sababu ya dhambi, uhusiano wa upendo na usafi wa moyo kati ya mwanaume na mwanamke umegeuka kuwa utawala: “Tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala” (Mwa 3:16).

20. Ni njia ya mateso na kumwaga damu inayopatikana katika kurasa nyingi za Biblia, kuanzia ukatili wa Kaini juu ya ndugu yake Abeli, na mabishano mengi kati ya wana na kati ya wake wa mababu Ibrahimu na Isaka na Yakobo, hadi kufikia misiba ya umwagaji damu iliyokumbana sana na familia ya Daudi, na shida za kifamilia zinazopatikana katika simulizi la kitabu cha Tobiti, au ungamo la Ayubu alipoachwa na wengine: “Ndugu zangu wamejiepusha nami, na wanijuao wametengwa nami kabisa. [...] Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, nami ni machukizo kwa watoto wangu” (taz. Ayu 19:13,17)

21. Yesu mwenyewe amezaliwa katika familia ya hali ya chini; na mapema walipaswa kukimbia kwenda katika nchi ya kigeni. Yeye anaingia nyumbani kwa Petro, ambapo mkwewe amelala, hawezi homa (taz. Mk 1:30-31); na kukubali kushirikishwa katika msiba wa kifo nyumbani kwa Jairo na nyumbani kwa Lazaro (taz. Mk 5:22-24,35-43; Yn 11:1-44). Anasikiliza kilio cha mjane wa Naini mbele ya maiti ya mwanae (taz. Lk 7:11-15), na kupokea ombi la baba wa kijana mwenye kifafa kwenye kijiji kidogo cha mashambani. (taz. Mk 9:17-27; Lk 17:14-20). Anakutana na watoza ushuru kama Matayo na Zakayo nyumbani kwao (taz. Mt 9:9-13; Lk 19:1-10), na wenye dhambi, kama yule mwanamke aliyeingia katika nyumba ya Farisayo (taz. Lk 7:36-50). Anajua mahangaiko na mivutano vilivyopo katika mazingira ya familia, na anavitumia anapotunga mifano: kama vile wana wanaoacha nyumba yao ili kuishi maisha ya vituko (taz. Lk 15:11-32), au wana wagumu wenye mienendo isiyoelezeka (taz. Mt 21:28-31), au wanaodhulumiwa kwa ukatili (Mk 12:1-9). Au, tena, anajali mafanikio ya arusi, inapojitokeza shida ya divai kuwatindikia (taz. Yn 2:1-10), au ya walioalikwa kukataa kuishiriki (taz. Mt 22:1-10); naye anafahamu jinsi familia iliyo maskini inavyopata wasiwasi inapopoteza sarafu moja (taz. Lk 15:8-10).

22. Hata kwa muhtasari mafupi hayo, tunaweza kuona kuwa Neno la Mungu si mlolongo wa dhana za kinadharia, bali ni mwenzi katika safari hata kwa familia zenye migogoro au huzuni, na kuonyesha kwao kikomo cha safari, Mungu “atakapofuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena” (Ufu 21:4).

Taabu ya mikono yako

23. Mwanzoni mwa Zaburi 128, baba anaonekana kuwa mfanyakazi ambaye kwa kazi ya mikono yake anaweza kutegemeza ustawi na usalama wa familia yake, “Taabu ya mikono yako utaila, utakuwa heri, na kwako kwema” (Zab 128:2). Kwamba kazi ni sehemu muhimu sana ya hadhi ya maisha ya wanadamu, ni fikra tunayoipata katika kurasa za kwanza za Biblia, pale ambapo imeandikwa, “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza” (Mwa 2:15). Ni picha ya mfanyakazi ambaye, kwa kulima ardhi na kwa kutumia nguvu za vilivyoumbwa, anazalisha “chakula cha taabu” (Zab 127:2), pamoja na kustawisha karama zake mwenyewe.

24. Wakati huohuo, kazi inawezesha kupata maendeleo ya jamii, riziki kwa ajili ya familia, pamoja na uthabiti wake na uzaaji wake: “Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako; Naam, ukawaone wana wa wanao.” (Zab 128:5-6). Tena, kitabu cha Mithali kinatuonyesha wajibu wa mama wa familia, ambaye kazi yake ya kila siku inaelezwa kinaganaga; nayo ni sababu ya mume na wana wake kumsifu (taz. Mit 31:10-31). Mtume Paulo mwenyewe alijisifu kwa sababu ya kutowalemea wengine, kwa kujipatia riziki kwa njia ya kazi ya mikono yake (taz. Mdo 18:3; 1Kor 4:12; 9:12). Alikuwa na uhakika kwamba kufanya kazi ni kitu cha lazima, kiasi cha kuweka sheria kali hii kwa jumuiya zake: “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula” (2The 3:10; taz. 1The 4:11).

25. Kutokana na hayo, inaeleweka kuwa kukosa ajira au kutokuwa na uhakika wa kazi kunasababisha taabu, kama kinavyoonyesha kijitabu cha Ruthu na kama anavyokumbusha Yesu katika mfano wa vibarua waliosimama sokoni bila kazi (taz. Mt 20:1-16), au kama alivyoonja Yeye mwenyewe mara nyingi alipokutana na watu maskini na wenye njaa. Hiyo ndiyo balaa inayojitokeza kwenye jamii katika nchi nyingi; na huko kukosa kazi kunaathiri amani ya familia kwa namna mbalimbali.

26. Wala hatuwezi kusahau upotovu ambao dhambi huingiza katika jamii, wanadamu wanapokandamiza viumbe vya dunia, kwa kuharibu mazingira, na kuvitumia viumbe kwa faida yake binafsi na kwa ukatili pia. Athari ya hayo ni hali ya ujangwa wa ardhi (taz. Mwa 3:17-19) na wakati huohuo tofauti zisizo za haki za kiuchumi na kijamii, ambazo dhidi ya hizo sauti ya manabii imevuma wazi, kuanzia Eliya (taz. 1Fal 21), hadi maneno aliyosema Yesu mwenyewe dhidi ya udhalimu (taz. Lk 12:13-21; 16:1-31).

Upole wa kukumbatia

27. Kristo ameweka kama sifa bainishi ya wanafunzi wake hasa sheria ya upendo na ya kujitoa nafsi kwa ajili ya wengine (taz. Mt 22:39; Yn 13:34); naye amefanya hilo kwa msimamo ambao baba au mama hushuhudia kwa kawaida katika maisha yao: “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn 15:13). Huruma na msamaha pia ni matunda ya upendo. Ishara dhahiri ya hayo ni sura ya yule mama mzinifu penye mahali pa hekalu la Yerusalemu, ambaye, washtaki wake wakiisha kumzunguka, akabaki peke yake tu pamoja na Yesu ambaye hakumhukumu, akamhamasisha kuishi maisha maadilifu zaidi (taz. Yn 8:1-11).

28. Katika upeo wa upendo, ulio kiini cha mang’amuzi ya kikristo katika ndoa na familia, ina umuhimu fadhila nyingine inayosahauliwa mara nyingi katika nyakati hizi za mahusiano ya haraka haraka na ya juujuu: moyo mpole. Tuangalie Zaburi ya 131, ambayo ni mwanana na imejaa maana. Kama inavyopatikana pia katika matini nyinginezo, (taz. Kut 4:22; Isa 49:15; Zab 27:10), muungano wa mwamini na Bwana wake unadhihirishwa kwa sifa za upendo wa kibaba na wa kimama. Katika hiyo Zaburi ya 131, unaonekana uhusiano wa undani, wa upendo mwanana na mpole, unaounganisha mama na mtoto wake mchanga aliyelala mikononi mwake alipokwisha kunyonyeshwa. Ni mtoto aliyekwisha kuachishwa, kulingana na maana ya neno la kiebrania gamul, ambaye kwa utambuzi anamshika mama yake anayemwinua kifuani pake. Ni uhusiano wa undani wenye utambuzi, wala si tu wa kimaumbile. Kwa hiyo mzaburi anaimba, “Hakika nimeituliza nafsi yangu na kuinyamazisha; kama mtoto aliyeachishwa kifuani mwa mama yake” (taz. Zab 131:2). Sambamba na hayo, tunaweza kufikiria sura nyingine, ambapo nabii Isaya anaweka maneno haya yenye kugusa moyo midomoni mwa Mungu, kama baba, “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nakipenda [...] Nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu [...] Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama baba amwinuaye mtoto mchanga mpaka shavuni mwake, nikaandika chakula mbele yao” (taz. Hos 11:1-4).

29. Kwa mtazamo huu, wenye imani na upendo, neema na bidii, unaounganisha familia ya kibinadamu na Utatu wa kimungu, tunatazama fumbo la familia ambalo Neno la Mungu anawakabidhi baba na mama na watoto ili waunde ushirika wa watu ulio mfano wa umoja wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Tena, kazi ya kuzaa na ya kulea, inaakisi kazi ya Mungu ya kuumba. Wanafamilia wanaitwa kushirikishana sala ya kila siku, somo la Neno la Mungu na komunyo ya Ekaristi ili kukuza upendo na kugeuka kuwa zaidi na zaidi kwa pamoja hekalu anamokaa Roho.

30. Kila familia ina mbele ya macho yake mfano wa familia ya Nazareti, pamoja na maisha yake ya kila siku yenye taabu na hata majinamizi, kwa mfano walipoteswa kwa ukatili usioeleweka wa Herode; nalo ni msiba unaoendelea kutokea hadi leo kwa familia nyingi za wakimbizi wanaokataliwa na wasio na msaada. Sawa na mamajusi, familia zinaitwa kumtazama Mtoto pamoja na Mamaye, kusujudu na kumwabudu (taz. Mt 2:11) Sawa na Maria, zinahimizwa kukabiliana kwa ujasiri na amani na changamoto za kifamilia, na kutunza na kutafakari moyoni mambo ya ajabu ya Mungu (taz. Lk 2:19,51). Katika hazina ya moyo ya Maria, pana matukio yote ya kila moja ya familia zetu, ambayo yeye anatunza kwa upendo angalifu. Ndiyo sababu anaweza kusaidia kutoa fasili ya hayo matukio, ili kutambua ujumbe wa Mungu katika maisha ya familia.

SURA YA PILI

HALI HALISI NA CHANGAMOTO ZA FAMILIA

31. Ustawi wa familia ni jambo la msingi kwa mustakabali wa ulimwengu na Kanisa Chambuzi nyingi sana zimefanyika kuhusu ndoa na familia, matatizo yao na changamoto za nyakati zetu. Ni vizuri kuangalia kwa makini hali halisi, kwa sababu “wito na maagizo ya Roho yapatikana pia katika matukio ya historia”. Kupitia matukio hayo “Kanisa linaweza kuongozwa kulielewa kwa kina zaidi fumbo lisilo na mwisho la ndoa na familia”.[8] Sina nia ya kuainisha na kufafanua hapa yale yote yahusuyo familia katika mazingira ya sasa. Lakini, kwa vile Mababa wa Sinodi walichangia uchambuzi wa hali halisi ya familia toka pande zote za dunia, naona vema kati ya michango yao ya kichungaji niipokee mingine, na kuongeza mawazo mengine yanayotokana na mtazamo wangu mimi.

Hali halisi ya familia wakati huu

32. “Huku tukiwa waaminifu kwa mafundisho ya Kristo tunaangalia hali halisi ya familia wakati huu, katika mchangamano wa miali yake ya mwanga na vivuli vya giza. […] Mabadiliko ya kianthropolojia na kitamaduni yanaathiri leo hali zote za maisha na kudai yatazamwe kwa kutumia mbinu mbalimbali za kiuchambuzi”.[9] Katika mazingira ya karibu miaka arobaini iliyopita Maaskofu wa Hispania tayari walikuwa wakitambua kwamba katika maisha ya nyumbani kulikuwa na uhuru zaidi, na "majukumu, uwajibikaji na kazi ziligawiwa kwa usawa zaidi [...] Kwa kuthamini zaidi mawasiliano ya ndani na ya kiutu kati ya wanandoa, maisha ya kifamilia yanakuwa na utu zaidi [...]. Wala jamii tunamoishi wala tunapoelekea inaruhusu tuendeleze mitindo na mifumo ya zamani bila kuichambua”.[10] Lakini “tunafahamu mwelekeo mkuu wa mabadiliko ya kianthropolojia na kitamaduni, ambayo yanasababisha watu binafsi wasiweze kuutegemea kama zamani msaada wa jamii kwa maisha yao ya kifamilia”.[11]

33. Kwa upande mwingine, ni lazima kuzingatia pia hatari inayozidi kuongezeka kutokana na ubinafsi wa kupita kiasi, unaopotosha mahusiano ya kifamilia hadi kusababisha kumtazama kila mwanafamilia kuwa sawa na kisiwa, ukishabikia, mara nyingine, picha ya mtu anayejijenga kadiri ya mapenzi yake yanayochukuliwa kama pekee yenye maana”.[12] “Migogoro inayosababishwa na utamadumi unaotukuza ubinafsi wa kumiliki mali na wa kula raha inazaa ndani ya familia hali ya kutovumiliana na kushambuliana”.[13] Ningependa kuongeza mchakamchaka wa maisha ya sasa, uchovu unaotokana na kubanwa na kudaiwa kila wakati, mfumo wa jamii na wa utendaji kazi, kwa sababu ni tamaduni zinazohatarisha uwezo wa kuwa na chaguo la kudumu. Wakati huohuo tunaona kwamba kuna mambo yanayoweza kuchukua sura mbili. Kwa mfano, yanathaminiwa zaidi malezi yanayomwezesha mtu kuwa na msimamo wake halisi kuliko kuiga tabia iliyokwisha pangwa. Ni tunu iwezayo kuviendeleza vipaji tofauti na uhuru wa kutenda, lakini ikielekezwa vibaya, inaweza kuzaa tabia ya kutoaminiana, kukwepa majukumu, kujifungia katika starehe, ubabe. Uhuru wa kuchagua unamwezesha mtu kuweka malengo katika maisha yake na kukuza kilicho bora ndani yake, lakini, bila malengo safi na nidhamu, huharibika na kupoteza uwezo wa kujitoa kwa ukarimu. Tukiangalia hali halisi, katika nchi nyingi ambapo idadi ya ndoa inapungua, inaongezeka idadi ya watu wanaoamua kuishi peke yao, au wanaoshirikiana bila kukaa pamoja. Tunatambua pia kwamba watu huitafuta zaidi haki, Lakini kama jambo hilo halieleweki vizuri, raia wanageuzwa kuwa wateja wanaodai tu kupewa huduma.

34. Hatari hizi zikiathiri namna ya kuielewa familia, familia yenyewe inaweza kugeuzwa kuwa mahali pa kupitia tu, mahali pa kukimbilia inapoonekana kuna manufaa binafsi, au ambapo mtu anakwenda kwa kudai haki zake, na wakati huo vifungo vinavyounganisha wanafamilia vinasahauliwa kwa kutegemea tamaa geugeu na mazingira tu. Kimsingi, leo ni rahisi kuchanganya uhuru halisi na itikadi ya kuwa kila mmoja huweza kuamua kadiri anavyopenda, kana kwamba kilicho na maana ni mtu binafsi tu, hakuna tena ukweli, tunu, na misingi inayotuelekeza, kana kwamba mambo yote ni sawa na kila kitu kinaruhusiwa. Katika mazingira hayo, tarajio la ndoa, likiwa na jukumu la chaguo pekee na la kudumu, linafutwa kwa kuzingatia marupurupu ya papo kwa hapo au matamanio ya kipuuzi. Watu huogopa upweke, hutamani mahali penye usalama na uaminifu, lakini wakati huohuo hofu ya kufungwa katika uhusiano unaoweza kuchelewesha mafanikio ya matamanio binafsi hukua.

35. Kama wakristo hatuwezi kuacha kupendekeza maisha ya ndoa kwa lengo ya kutopingana na mawazo ya kisasa, kwa kufuata mitindo, au kwa sababu tunaona hatuna nguvu za kupambana na mmomonyoko wa maadili na wa utu. Tungefanya hivyo tungeinyima dunia tunu ambazo tunaweza na tunapaswa kuitolea. Kwa kweli, haina maana kubaki kuyalaumu tu maovu yanayotendeka kana kwamba kwa kufanya hivyo tungeweza kubadili kitu. Wala haisaidii kutaka kuzilazimisha sheria kwa nguvu ya mamlaka. Tunadaiwa kuwa na juhudi yenye uwajibikaji na yenye ukarimu zaidi, yaani kueleza mantiki na sababu za kuchagua ndoa na familia, hivyo watu wawe tayari zaidi kuitikia kwa neema wanazopewa na Mungu.

36. Wakati huohuo inatupasa kuwa wanyenyekevu na wenye kuzingatia uhalisia ili tuweze kukiri kwamba namna yetu ya kueleza mafundisho ya kikristo na namna yetu ya kuwatendea watu imesaidia kuyasababisha yale ambayo leo tunayalaumu, hivyo inabidi na inafaa tujichunguze sisi wenyewe. Mara nyingi tulipokuwa tunalijadili suala la ndoa tulikuwa kama tunaliweka pembeni lengo lake la kuwa kitu kimoja, wito wa kukua katika upendo na shabaha ya kusaidiana, na kuweka msisitizo, kama si msisitizo pekee, kwa jukumu la kuzaa. Wala hatukuwasindikiza vizuri wanandoa wapya katika miaka yao ya mwanzo wanapoanza maisha ya ndoa, hatukujali taratibu zao, msamiati wao na mahangaiko yao halisi na ya kawaida. Mara nyingine tumeeleza mafundisho ya kidini yanayohusu ndoa kinadharia mno, kama mchezo wa kiakili tu, mbali na mazingira halisi na uwezo halisi wa familia jinsi zilivyo. Namna hii ya kiitikadi mno, hasa kama hatujachochea roho ya kuitegemea neema ya Mungu, haijasaidia watu wavutiwe na watamani maisha ya ndoa, bali kinyume chake.

37. Kwa muda mrefu tuliamini kwamba kwa kusisitiza tu masuala ya kiitikadi na ya kimaadili bila kuelekeza kujikabidhi kwa neema ya Mungu, tumeshazisaidia ya kutosha familia, kuimarisha muungano wa wanaarusi, na kuyajazia na maana kubwa maisha yao ya pamoja. Tuna ugumu zaidi kueleza ndoa kama mchakato, kama safari ya kuelekea ukomavu na utimilifu, kuliko kama mzigo wa kuubeba kwa uvumilivu kwa maisha yote. Hatujawa wepesi pia kuziachia nafasi dhamiri za waamini, ambao mara nyingi wanaitikia vizuri jinsi wanavyoweza wito wa Injili katika mipaka ya udhaifu wao na wanaweza kuendeleza upambanuzi wao katika nafsi yao mbele ya mazingira ambapo mifumo yote imefumuka. Tunaitwa kuzilea dhamiri, wala si kuzichukua nafasi zao.

38. Lazima tushukuru kwa sababu watu walio wengi wanayaheshimu mahusiano ya kifamilia yanayolenga kudumu na yanayohakikisha heshima kwa kila mmoja. Hivyo inapendezwa Kanisa linapokuwa na nafasi ya kusindikiza na kusaidia katika masuala yahusuyo kukua katika upendo, kufikia mwafaka katika migogoro na malezi ya watoto. Wengi hutambua nguvu wanayopewa na neema inayopatikana katika sakramenti ya Upatanisho na ya Ekaristi, nguvu hii huwezesha kupambana na changamoto za ndoa na familia. Katika nchi nyingine, hasa katika sehemu nyingi za Afrika, mfumo wa kumweka Mungu pembeni haujafaulu kudhohofisha tunu za jadi na katika kila ndoa koo mbili zinaungana kwa nguvu, na hivyo huwa na mfumo unaoeleweka wa kutatua migogoro na shida. Katika dunia ya leo inathaminiwa pia ushuhuda wa watu wa ndoa ambao si kwamba walidumu katika ndoa yao kwa muda mrefu tu, lakini pia huendelea na mpango wao wa pamoja na hudumu katika kupendana. Hali hiyo inafungua mlango kwa kazi ya kichungaji yenye lengo la kujenga, yenye tabia ya kupokea kwa ukarimu, na hivyo kuwezesha kupiga hatua katika kuyaelewa kwa kina zaidi majukumu yatokanayo na Injili. Hata hivyo, mara nyingi tumetenda kama kwa kujihami na tunapoteza nguvu za kiuchungaji kwa kuishambulia dunia inayopotea, tukiwa na uwezo mdogo tu wa kuwaelekeza watu katika njia ziendazo kwenye furaha. Wengi hawatambui kwamba mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia yametokana wazi na mahubiri na mwenendo wa Yesu, ambaye kwa wakati mmoja alikuwa akipendekeza lengo linalowajibisha bila kuacha kamwe kuwa karibu na watu wadhaifu kama mwanamke Msamaria au mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi.

39. Hilo halina maana ya kutotambua mmomonyoko wa kiutamaduni unaofifisha upendo na moyo wa kujitolea. Maoni yaliyotolewa kabla ya Sinodi mbili za mwisho yameibua dalili mbalimbali za "utamaduni wa yaliyo ya muda tu”. Kwa mfano, tunaona jinsi watu wanavyobadilisha wapenzi wao haraka. Wanaamini kwamba upendo, kama inavyotokea katika mitandao ya kijamii, anaweza kuufunga au kuufungua anavyotaka mlaji na hata kuusimamisha ghafla. Ninawazia pia hofu inayowaingia watu wanapofikiria juu ya majukumu ya kudumu, hali ya kutingwa na wazo la kuwa na muda wa kutumia binafsi tu, mahusiano yaliyo kama ya kibiashara kwa kupima mapato na matumizi na ambayo yanadumu yakiwa tu kama njia ya kuukwepa upweke, kuwa na usalama au kupata huduma fulani. Mahusiano ya kimapenzi kati ya watu yanakuwa kama mahusiano kati ya watu na vitu, kati ya watu na mazingira: yote yaweza kutupwa, kila mmoja hutumia na kutupa, hutumia bila kiasi na kuharibu, hunyonya na kukamua mpaka kushiba. Na baadaye basi, nenda zako! Tabia ya kinarchizo hufanya watu washindwe kuangalia zaidi ya mipaka yao, matamanio yao na haja zao. Lakini atumiaye wengine hatimaye naye pia atatumiwa, atarubuniwa na kuachwa kwa mtindo huohuo. Ni jambo la kutafakari kwamba mahusiano yanavunjika mara nyingi kati ya watu wazima ambao wanatafuta namna fulani ya "kujitegemea (uhuru)” na wanakataa wazo la kuzeeka pamoja kwa kutunzana na kutegemezana.

40. "Ingawa kuna hatari ya kuongea kijuujuu, tunaweza kusema kwamba tunaishi katika utamaduni unaowasukuma vijana wasijenge familia, kwa sababu wanakosa uwezo kwa siku zao za mbele. Lakini utamaduni huohuo kwa wengine unawapatia machaguo mengi kiasi kwamba wao pia hushawishiwa kutojenga familia”.[14] Katika nchi nyingine vijana wengi wanasukumwa kuahirisha ndoa yao kwa sababu ya shida za kiuchumi, za kikazi, au za kimasomo. Mara nyingine kwa sababu zingine pia, kama vile ushawishi wa itikadi zinazoishusha hadhi ya ndoa na familia, kuogopa kushindwa kwa kuona walivyoshindwa wengine katika ndoa yao, hofu mbele ya jambo ambalo wanaliona zito mno na takatifu, fursa za kijamii na unafuu wa kiuchumi zinazotokana na kuishi pamoja bila kufunga ndoa, kuelewa upendo kama jambo la kihisia tu, hofu ya kupoteza uhuru na uwezo wa kujitegemea, kukataa jambo linaloonekana kama la kitaasisi na lenye urasimu”.[15] Tunahitaji kupata maneno, sababu na ushuhuda zitakazotusaidia kuwagusa mpaka ndani kabisa vijana pale ambapo wana uwezo zaidi wa kuwa na ukarimu, na ari, na upendo, na hata kuwa na ushujaa, ili kuwaalika wakubali kwa moyo wa furaha na kwa ushupavu changamoto ya ndoa.

41. Mababa wa Sinodi wamejadili kuhusu hali ya sasa ambapo “mielekeo ya kitamaduni ni kama inataka kulazimisha mapenzi bila mipaka [...], mapenzi ya kutafuta faida binafsi, yasiyo ya kudumu na yenye kubadilika, ambayo hayawasaidii watu kufikia ukomavu mkubwa zaidi”. Wamesema kwamba wanahangaika na “hali ya kuenea kwa ponografia (picha za ngono) na biashara ya mwili, kunakochangiwa hata na matumizi mabaya ya mtandao wa intaneti, na “hali ya watu kulazimishwa kufanya ukahaba”. Katika mazingira haya, “majozi mara nyingine yanayumba, yanasita na yanapata shida kuona njia ya kukua. Wengi wanaelekea kubaki katika hatua za chini kabisa kimihemuko na kimapenzi. Mgogoro katika jozi unayumbisha familia, na kutokana na matengano na talaka, athari kubwa zinawapata watu wazima, watoto na jamii, na hivyo hudhoofisha mtu na mahusiano ya kijamii”.[16] Migogoro ya wanandoa mara nyingi inakabiliwa “juujuu na bila ushujaa wa subira, wa uchambuzi wa kina, wa kusameheana, wa upatanisho na wa sadaka pia. Basi, kuvunjika kwa ndoa kunaanzisha mahusiano mengine, majozi mwngine, miungano mingine na ndoa nyingine, na hivyo kunasababisha hali ya kifamilia kuwa ngumu na yenye utata kwa chaguo la kikristo”.[17]

42. “Hata kushuka kwa idadi ya vizazi kunakotokana na fikra na mitazamo ya kupunguza uzazi iliyoenezwa na sera za kiulimwengu juu ya afya ya uzazi, si tu kwamba kunatengeneza mazingira ambamo kubadilishana kwa vizazi hakuna uhakika, bali kuna hatari ya kutufikisha kwenye zama za umaskini mkubwa wa kiuchumi na kupoteza matumaini ya wakati ujao. Maendeleo ya kibioteknolojia nayo yameathiri sana uzazi.[18] Tunaweza kuorodhesha mambo mengine kama "maendeleo ya viwanda, mapinduzi ya kijinsia, hofu ya ongezeko la idadi ya watu, matatizo ya kiuchumi, [...]. Jamii ya kiulaji inaweza pia kuwashawishi watu wasizae watoto ili wabaki na uhuru wao na mtindo wao wa maisha”.[19] Ni kweli kwamba dhamiri sahihi ya wanandoa, baada ya kupata watoto wengi, inaweza kuwaelekeza kuchukua uamuzi wa kuweka mipaka katika idadi ya watoto kwa sababu zilizo za msingi, lakini “Kanisa daima kwa kuipenda heshima hii ya dhamiri linakataa kwa nguvu zake zote hatua za serikali zinazowalazimisha watu kuzuia mimba, kufunga njia ya uzazi au hata kuiharibu mimba”.[20] Hatua hizi hazikubaliki kamwe hata pale ambapo watu wanazaa sana, lakini tunaona kwamba wanasiasa wanazishinikiza hatua hizo hata pale ambapo kuna janga la ongezeko kidogo mno la watu. Kama walivyosema maaskofu wa Korea, “namna hii ya kutenda inajipinga yenyewe na inakwepa majukumu”.[21]

43. Katika jamii nyingine kudhoofika kwa imani na kwa ushiriki katika ibada kunaathiri familia na kuziacha pweke wanapokabiliana na matatizo yao. Mababa wanasema kwamba “katika utamaduni wa leo upweke ndio sura kuu mmojawapo wa umaskini, nao unasababishwa na kumweka Mungu mbali na maisha ya watu, pia na udhaifu wa mahusiano. Kuna pia hisi ya jumla ya kutoweza kitu mbele ya hali halisi ya kijamii na kiuchumi, ambayo, mara nyingi, inafikia hatua ya kuzigandamiza familia. […] Mara nyingi familia zinajihisi kuwa zimeachwa kwa sababu ya kutojali na mapungufu ya uangalifu kwa upande wa taasisi. Matokeo hasi, kwa mtazamo wa mpangilio wa kijamii, ni wazi: kuanzia mpunguo wa kupita kiasi wa uzazi na shida katika kulea, ugumu wa kupokea kuzaliwa kwa mtoto, kuwaona wazee kama mzigo, hadi kuenea kwa fadhaa za kimapendo zinayoweza kumfikisha mtu hata katika kutenda ukatili. Ni wajibu wa Serikali ya Nchi kutunga sheria na kuongeza nafasi za ajira ili kuhakikisha mustakabali mzuri kwa vijana, na kuwasaidia kutekeleza mpango wa kuunda familia yao”.[22]

44. Kukosa makazi yenye hadhi au yanayofaa mara nyingi kunasababisha kuahirisha kuweka uhusiano katika mfumo ulio rasmi. Lazima tukumbuke kwamba “familia ina haki ya kuwa na makazi yenye hadhi, yanayofaa kwa maisha ya familia na yanayolingana na idadi ya wanafamilia, katika mazingira yenye huduma za msingi kwa ajili ya familia na jumuiya”.[23] Familia na nyumba ni mambo yanayoendana. Mfano huo unatuonyesha kwamba inatupasa kusisitiza haki za familia, na si haki za mtu binafsi tu. Familia ni tunu ambayo haiwezi kukosekana katika jamii, lakini inahitaji kulindwa.[24] Utetezi wa haki hizo “ni wito la kinabii kwa ajili ya familia kama taasisi, ambayo lazima iheshimiwe na ilindwe na kila aina ya unyanyasaji,[25] hasa katika mazingira ya sasa ambapo kawaida ina nafasi ndogo katika sera ma mipango ya kisiasa. Kati ya haki zingine familia zina haki “ya kutegemea mamlaka ya kiraia iandae na kusimamia sera ya familia inayofaa katika nyanja ya sheria, uchumi, jamii na kodi”.[26] Mara nyingine familia inapata mahangaiko ya kutatanisha wakati mpenzi wao unaugua, lakini hawawezi kupata huduma ya kiafya inayofaa, au wanapobaki muda mrefu bila kupata ajira yenye hadhi. “Masharti ya kiuchumi yanazinyima familia uwezekano wa kupata elimu na kushiriki vizuri maisha ya kiutamaduni na ya kijamii. Mfumo wa uchumi wa sasa unasababisha familia zikataliwe na jamii kwa namna nyingi. Kwa namna ya pekee familia zinaumia kwa sababu ya shida zinazohusiana na kazi. Nafasi wanazopewa vijana ni chache na nafasi za ajira zina masharti mengi na ni za wasiwasi. Saa za kazi kwa siku ni nyingi na mara nyingi mtu hutumia muda mrefu kwa kusafiri kufika kazini. Hali hii haisaidii wanafamilia wakutane wao kwa wao na pamoja na watoto wao ili kuustawisha kila siku mahusiano kati yao”.[27]

45. Katika baadhi ya nchi, watoto wanaozaliwa nje ya ndoa ni wengi, na wale ambao baadaye wanalelewa na mzazi mmoja au katika mazingira ya familia pana au yaliyoundwa upya, nao ni wengi. […] Moja ya kashfa kubwa na jambo linalodhihirisha kupotoka kwa jamii ya sasa ni udhalilishaji wa kingono wa watoto. Hata jamii zilizojeruhiwa kwa vita, ugaidi au kuwepo kwa mfumo wa uhalifu, zinajikuta zikiwa katika hali ya kifamilia iliyodhoofika, na hasa katika miji mikubwa na pembezoni mwake idadi ya watoto wanaoitwa ‘wa mitaaani’ inazidi kuongezeka”.[28] Ubakaji wa watoto unakuwa kashfa kubwa zaidi ikitokea pale ambapo watoto waliwekwa ili walindwe: familia, shule, jumuiya na taasisi za kikristo.[29]

46. Uhamiaji “ni alama nyingine ya nyakati inayotakiwa kuangaliwa na kueleweka pamoja na matokeo yake mazito kwa maisha ya familia”.[30] Sinodi ya mwisho imelipa suala hilo umuhimu mkubwa, ikisema kwamba: “linayagusa, kwa namna tofauti, mataifa mengi, katika sehemu mbalimbali duniani. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana nalo. Ulazima wa kudumisha na kustawisha ushuhuda huu wa kiinjili (taz. Mt 25:35) leo inaonekana kama jukumu nyeti kabisa. […] Kuhama kwa watu, ambalo ni jambo la kawaida katika historia ya mataifa, kunaweza kuwa nafasi ya kujitajirisha kwa familia za wahamiaji na kwa wale wanaozipokea. Jambo lingine, tofauti, ni uhamisho wa familia kwa kulazimishwa, kutokana na mazingira ya vita, madhulumu, umaskini, udhalimu, uhamisho ulio na hatari nyingi safarini ambapo mara nyingi watu wahatarisha maisha yao, wanachanganyikiwa, na familia zinavurugwa. Kuwasindikiza wahamiaji kunadai kazi ya uchungaji ya pekee inayozielekea familia zinazohama, lakini pia wanafamilia waliobaki nyumbani. Kazi hii lazima ifanyike kwa kuziheshimu tamaduni zao, malezi ya kidini na ya kiutu ya mahali wanapotoka, utajiri wa kiroho wa ibada zao na mapokeo yao, pia kwa kuwahudumia kwa matunzo ya kichungaji ya pekee. […] Uhamiaji unakuwa wa kusikitisha na wenye maumivu makali kwa namna ya pekee unapokuwa haramu na wenye kutegemea mitandao ya kimataifa ya wafanyabiashara ya watu. Vilevile kwa akinamama na watoto wasio na msaada, wanaolazimishwa kukaa kwa muda mrefu kwenye makampi ya mapito, kwenye makampi ya wakimbizi ambapo haiwezekani kabisa kujenga mtangamano wa maana. Umaskini wa kupindukia na mazingira mengine magumu kabisa mara nyingine yanawasukuma familia hata kuwauza watoto wao kama malaya au kwa ajili ya biashara ya viungo”.[31] “Madhulumu ya wakristo na pia ya makabila madogo au makundi mengine ya kidini, sehemu mbalimbali duniani, hasa Mashariki ya Kati, huwa majaribu makubwa: si kwa Kanisa tu, bali pia kwa jumuiya nzima ya kimataifa. Inapaswa kutegemeza kila juhudi inayolenga kuzisaidia familia na jumuiya za kikristo zibaki katika maeneo yao ya asili”.[32]

47. Mababa waliangalia kwa umakini wa pekee pia “familia walio na walemavu, ambapo ulemavu unaoibuka katika maisha yao unaleta changamoto kali na isiyotarajiwa, na huvuruga utulivu, matamanio na matarajio. [...] Familia zinazopokea kwa upendo jaribio zito la kuwa na mtoto mlemavu zinastahili pongezi kubwa. Zinatoa kwa Kanisa na kwa jamii ushuhuda wenye thamani wa uaminifu kwa zawadi ya uhai. Familia itaweza kugundua, pamoja na jumuiya ya kikristo, matendo mapya, msamiati mpya, namna ya kujielewa na kujitambua, katika safari ya kulipokea na kulitunza fumbo la udhaifu. Walemavu kwa ajili ya familia wanakuwa kama zawadi na nafasi ya kukua katika upendo, katika kusaidiana na katika umoja. [...] Familia inayopokea kwa jicho la imani uwepo wa walemavu itaweza kuutambua na kuutetea ubora na tunu ya kila uhai, pamoja na mahitaji yake, haki zake na fursa zake. Familia hiyo itahamasisha huduma na matunzo, na itaendeleza ukaribu na mapendo, wakati wote wa maisha”.[33] Napenda kusisitiza kwamba uangalifu unaotumika kwa ajili ya wahamiaji na walemavu ni dalili ya Roho. Hali hiyo ni kama ya mfano: inaonyesha hasa jinsi leo tunavyojali mapokezi yenye huruma na mtangamano na watu wadhaifu.

48. “Familia zilizo nyingi zinawaheshimu wazee, zinawapenda na kuwapokea kama baraka. Pongezi wa pekee kwa mashirika na makundi ya kifamilia zinazofanya kazi kwa ajili ya wazee, kwa upande wa kiroho na wa kijamii [...]. Katika jamii zenye viwanda vingi, ambapo idadi ya wazee inazidi kuongezeka wakati idadi ya watoto inapungua, kuna hatari ya kuwachukua wazee kama mzigo. Kwa upande mwengine matunzo wanayohitaji mara nyingi ni majaribu makubwa kwa jamaa zao”.[34] “Kukithaminisha kipindi cha mwisho wa maisha, leo ni ya lazima zaidi kutokana na kujaribu zaidi kuweka kando hatua ya kuaga dunia, kwa kutumia kila njia. Udhaifu na utegemezi wa wazee mara nyingine hutumika kikatili kama nafasi ya kupata faida ya kiuchumi. Familia nyingi zinatufundisha kwamba inawezekana kuzikabili hatua za mwisho wa maisha kwa kuthamini maana ya utimilifu wa maisha katika fumbo la kipasaka. Idadi kubwa ya wazee wamepokelewa katika taasisi za Kanisa ambapo huweza kuishi katika mazingira ya utulivu na ya kifamilia wakipata huduma ya kiroho na ya kimwili. Kifo laini na kujiua kwa msaada ni vitisho vikali kwa familia duniani kote. Katika nchi nyingi matendo hayo yamepata uhalali wa kisheria. Kanisa, wakati linaposhupaa kuyapinga matendo hayo, linapokea jukumu la kuzisaidia familia zinazotunza wazee na wagonjwa”.[35]

49. Nataka niweke wazi zaidi hali ya familia zinazogubikwa na unyonge, zinazobanwa kwa namna nyingi, ambapo magumu ya maisha yanawasababishia majeraha makali. Wote tunayapata matatizo, lakini katika nyumba iliyo maskini sana yanakuwa makali zaidi.[36] Kwa mfano, kama mama hulazimika kumlea mtoto peke yake, kwa sababu ya kutengana na mumewe au kwa sababu nyingine, na anapofanya kazi hawezi kumwachia mtu mwengine, mtoto huyo atakua katika upweke wa mazingira hatarishi, na kukomaa kwake kutaathirika. Katika hali ngumu ya maisha inayowakabili watu wenye shida, Kanisa linapaswa kuwatunza kwa namna ya pekee kwa kuwaelewa, kuwafariji, kuwashirikisha, bila kuwabana na sheria nyingi zinazoonekana kama mzigo unawalemea, jambo ambalo lingewafanya watu kujisikia wamehukumiwa na kuachwa na Mama yule ambaye kiukweli hutumwa kuwapelekea huruma ya Mungu. Kwa namna hiyo, badala ya kuwapatia watu nguvu ya kuponya ya neema na mwanga unaotokana na Injili, wengine wanataka kushinikiza “ufundishaji” wa Injili, na kuibadilisha kuwa “mawe yasiyo na uhai ya kuwatupia wengine”.[37]

Changamoto nyingine

50. Majibu yaliyopatikana katika mashauriano mawili yaliyofanyika wakati wa maandalizi ya Sinodi, yameonyesha mazingira na hali mbalimbali na tofauti sana zinazoleta changamoto mpya. Zaidi ya zile zilizotajwa hapo juu, wengi waligusia kazi ya malezi, kazi ambayo ina shida kutokana na kwamba, pamoja na sababu nyingine, wazazi wanarudi nyumbani hali wamechoka na hawana hamu ya kuongea, katika familia nyingi hata desturi ya kula pamoja imepotea, na, zaidi ya kuwa tegemezi wa televisheni, namna za kupoteza mawazo kwa kujiburudisha zinazidi kuongezeka. Hali hii inasababisha kazi ya wazazi ya kuwarithisha imani watoto kuwa ngumu. Wengine wameona kwamba mara nyingi familia ni kama zinaugua mfadhaiko mkubwa sana. Inaonekana kama wanahangaika sana kuwaganga matatizo yajayo kuliko kushirikiana katika maisha ya leo. Hali hii, ambayo ni suala la kiutamaduni, huwa mbaya zaidi kutokana na wasiwasi kuhusu ajira kwa siku za mbele, kuyumba kwa uchumi, au hofu kwa maisha ya watoto siku za mbele.

51. Yameongelewa pia utegemezi unaotokana na dawa ya kulevya kama moja kati ya majeraha ya wakati wetu, ambalo linazitesa familia nyingi, na si mara chache linazimaliza kabisa. Jambo linalofanana linatokana na ulevi, michezo ya kamari, na utegemezi wa namna nyingine. Familia ingeweza kuwa mahali pa kinga na pa kujifunza kanuni nzuri, lakini jamii na siasa zinashindwa kuelewa kwamba familia iliyo katika mazingira hatarishi “hupoteza uwezo wa kutenda kwa kuwasaidia wanafamilia [...]. Tunaona matokeo mazito ya hali hiyo katika familia zilizovunjika kabisa, watoto wasio na msingi, wazee waliotelekezwa, watoto yatima ingawa wazazi wao wako hai, vijana wasio na mwelekeo wala nidhamu”.[38] Kama walivyoeleza maaskofu wa Meksiko, kuna mazingira ya kusikitisha ya ukatili katika familia ambayo yanakuwa chanzo cha ukatili mpya katika jamii kwa sababu “mahusiano ya kifamilia pia yanamwelekeza mtu kutenda kwa ukatili. Familia zenye mwelekeo huo ni zile ambapo zinakosekana mawasiliano; zile ambapo kila mmoja anajihami na wanafamilia hawategemeani; Ambapo zinakosekana shughuli zinazosaidia kuonyesha ushirikiano; Ambapo mahusiano kati ya wazazi mara nyingi ni migongano na ya kikatili, na kati ya wazazi na watoto ni migogoro. Ukatili ndani ya familia ni shule ya kinyongo na chuki kwenye uhusiano wa msingi wa kibinadamu”.[39]

52. Hakuna mtu anayeweza kufikiri kwamba kwa kuidhoofisha familia kama jamii asilia iliyo na msingi katika ndoa ni jambo linaloisaidia jamii. Ni kinyume chake: ni kikwazo kwa ukomavu wa mtu, kwa utunzaji wa tunu za jumuiya na kwa maendeleo ya maadili ya miji na vijiji. Haieleweki tena kwa dhahiri kwamba muungano tu wa pekee na usiofunguliwa kati ya mwanamume na mwanamke una nafasi timilifu katika jamii, kwa sababu ni jukumu thabiti na kwa vile unavyowezesha uzaaji. Inatupasa kuzitambua aina nyingi za hali ya kifamilia zinazowezesha kuongozwa na kanuni fulani za maisha, lakini watu kuishi pamoja tu bila kufunga ndoa, au ndoa ya jinsia moja, kwa mfano, haziwezi kuhesabiwa sawa kama ndoa. Hakuna muungano usio wa kudumu na usiowezesha uzazi ambao huweza kutuhakikishia maendeleo ya jamii kwa siku za mbele. Lakini ni nani leo aliye na bidii ya kutegemeza wanandoa, anayewasaidia kuzishinda hatari zinazowatisha, kuwasindikiza katika jukumu lao la kulea, anayewasaidia kuimarisha muungano wao wa kindoa?

53. “Katika jamii nyingine bado kuna desturi ya mitara; katika mazingira mengine bado unaendela utaratibu wa ndoa zinazopangwa na wakubwa tu. Katika sehemu nyingi, na wala si katika nchi za Magharibi tu, unaenea sana mfumo wa kuishi unyumba kabla ya ndoa, au kuishi unyumba bila kuwa na lengo la kufunga ndoa rasmi”.[40] Katika nchi mbalimbali sheria zinarahisisha uwepo wa aina nyingi za kuishi pamoja, kwa namna hiyo ndoa ya mume mmoja na mke mmoja, isiyovunjika na inayotarajia kupata watoto, hatimaye inaonekana kama jambo lililopitwa na wakati kati ya aina nyingi za kuishi pamoja. Katika nchi nyingi wengine wanaendelea kudhoofisha sheria zinazolinda familia wakielekea kuutetea mfumo unaojali tu uhuru wa kijiamulia. Ingawa ni haki kuukataa mfumo wa zamani wa familia ya "kimapokeo” yenye tabia ya udikteta na pia yenye ukatili, lakini haitakiwi jambo hilo lielekee kuidharau na kuichukia ndoa, bali liwe nafasi ya kuielewa upya maana yake ya kweli na kuifanya upya. Nguvu ya familia tunaiona hasa katika uwezo wake wa kupenda na wa kufundisha kupenda. Familia hata iwe na jeraha kubwa namna gani, ikitegemea upendo itakuwa daima na nafasi ya kukua”.[41]

54. Katika kuiangalia kwa kifupi hali halisi, napenda niseme kwamba, ingawa leo haki za mwanamke na ushiriki wake katika jamii zinatambulika zaidi, katika nchi nyingine safari bado ni ndefu. Bado tamaduni zisizokubalika hazijang’olewa. Kabla ya yote ukatili wa aibu wanaofanyiwa mara kwa mara wanawake, kutendewa vibaya nyumbani na namna mbalimbali ya utumwa ambazo hazionyeshi nguvu za wanaume bali fedheha. Ukatili wa maneno, dhidi ya mwili na wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake katika ndoa ni kinyume kabisa na asili ya muungano wa kindoa. Nafikiria kuhusu ukeketaji wa wanawake unaofanyika kwa kuzingatia tamaduni za sehemu fulani, lakini pia ubaguzi unaofanyika katika kutoa ajira yenye heshima na katika kupata nafasi zinazowawezesha kutoa maamuzi mazito. Historia inafuata nyayo za ukali wa tamaduni za mfumo dume, ambapo mwanamke alihesabiwa kama mtu wa daraja la pili, lakini tunakumbuka pia mtindo wa “tumbo la kupanga”au “jinsi mwili wa mwanamke katika utamaduni wa mawasiliano wa siku hizi unavyodhalilishwa na kutumiwa kibiashara”.[42] Wengine wanafikiri kwamba matatizo mengi tuliyo nayo sasa yameanza kujitokeza wanawake walipoanza kupata nafasi zaidi. Lakini hoja hii aina nguvu, “ni uongo, na haina ukweli. Ni mtazamo unaotokana na mfumo dume”.[43] Heshima sawa kwa mwanamke na mwanamume inatufurahisha kwa sababu mifumo ya ubaguzi ya zamani inakoma na katika familia inaendelezwa mfumo wa kutegemeana. Hata kama zinaweza kuwepo namna za kutetea haki za wanawake ambazo zina kasoro, tunastaajabia kazi ya Roho kwa kuona jinsi heshima ya mwanamke na haki zake zinavyotambulika kwa namna iliyo wazi zaidi.

55. Mwanamume “ni muhimu katika maisha ya familia, mintarafu ulinzi na huduma kwa mke na watoto. […] Wanaume wengi wanaelewa umuhimu wa nafasi yao katika familia na huwajibika kwa namna inayoendana na tabia ya wanaume. Kutokuwepo kwa baba kunaathiri sana maisha ya kifamilia, malezi ya watoto na ushiriki wao katika jamii. Kutokuwepo kwa baba kunaweza kuchukua sura nyingi: kutokuwepo kimwili, kimapendo, kiakili na kiroho. Upungufu huo unafanya watoto wokose mfano unaofaa wa tabia ya kibaba”.[44]

56. Changamoto nyingine inaibuka kutokana na aina mbalimbali za itikadi zinazoitwa kwa jumla gender. Itikadi hiyo “inakataa kwamba kiasili katika mwanamume na mwanamke kuna tofauti na kuna kukamilishana. Mtazamo wa itikadi hiyo ni kuwa na jamii ambapo utofauti wa jinsia haupo, na kwa namna hiyo kuuondoa msingi asilia ya familia. Itikadi hiyo inakuwa msingi na nguvu kwa mipango ya malezi na mielekeo ya kisheria inayohamasisha tabia binafsi na moyo wa kimapenzi ambavyo havijali kabisa utofauti wa kimwili kati ya mwanamume na mwanamke. Hivyo utambulisho wa mtu unakuja kutegemea chaguo lake binafsi, linaloweza pia kubadilika baada ya muda”.[45] Inatisha kuona kwamba itikadi nyingine za namna hii, ambazo zinadai kuwa jibu kwa matamanio ambayo mara nyingine ni ya maana, zinajaribu kulazimisha itikadi hiyo kama wazo pekee linalotawala pia malezi ya watoto. Haipaswi kutojua kwamba “jinsia asilia (sex) na nafasi ya jinsia kijamii na kiutamaduni (gender) zinaweza kutofautishwa, lakini bila kutenganishwa”.[46] Kwa upande mwingine mapinduzi ya bioteknolojia katika medani ya uzazi wa binadamu yamewezesha kuingilia tendo la kuzaa, na kulifanya lisitegemee tena mahusiano ya kijinsia kati ya mwanamume na mwanamke. Kwa namna hiyo, uhai wa binadamu na uzazi yamekuwa mambo yanayoweza kuunganishwa au kutenganishwa, yakitegemea zaidi matamanio ya mtu binafsi au ya jozi”.[47] Kitu kimoja ni kuuelewa udhaifu wa kibinadamu au ugumu wa maisha, kitu kingine kuzikubali itikadi zinazodai kuzitenganisha mambo ambayo kiasilia hazitenganishwi. Tusianguke katika dhambi ya kudai kuchukua nafasi ya Muumba. Sisi ni viumbe, hatuwi na enzi isiyo na mipaka. Ulimwengu umetutangulia na lazima tuupokee kama zawadi. Wakati huohuo tunaitwa kuulinda utu wetu, na kwa mantiki hiyo kabla ya yote tuukubali na kuuheshimu kama ulivyoumbwa.

57. Namshukuru Mungu kwa sababu familia nyingi, ingawa ni mbali na kujisikia kamilifu, huishi katika upendo, hutekeleza wito wao na zinasonga mbele ingawa zinaanguka mara nyingi njiani. Tukizingatia tafakari za Sinodi hatubaki na picha moja ya familia kamili, bali mifano mbalimbali zinazotokana na mazingira tofauti, iliyojaa furaha, machungu na ndoto. Mambo yanayotuhangaisha yanakuwa changamoto Tusianguke katika mtego wa kuishia kuwa na malalamiko ya kujitetea badala ya kuuibua ubunifu wa kimisionari. Katika kila aina ya mazingira “Kanisa linaelewa haja ya kutamka neno la ukweli na la tumaini. […] Tunu kubwa za ndoa na familia ya kikristo zinaendana na kile binadamu anachokitafuta katika maisha.”[48] Tukikabiliana na shida nyingi - kama walivyosema Maaskofu wa Kolombia - shida hizo ni mwaliko wa “kuzipa nafasi nguvu za tumaini zilizo ndani yetu zizae ndoto za kinabii, matendo yaletayo mabadiliko na mapendo yenye ubunifu”.[49]

SURA YA TATU

KUMTAZAMA YESU: WITO WA FAMILIA

58. Mbele na ndani ya familia inatakiwa isikike mbiu msingi, iliyo “nzuri zaidi, iliyo kubwa zaidi, inayovutia zaidi na wakati huohuo iliyo muhimu”[50], na “inatakiwa iwe kiini cha shughuli ya uinjilishaji”.[51] Ni mbiu msingi, “ile ambayo hatuna budi daima kurudi kuisikiliza kwa namna tofauti na tunayotakiwa kurudi kuitangaza katika katekesi kwa namna moja au nyingine”.[52] Kwani “hakuna kilicho thabiti zaidi, kilicho cha ndani zaidi, cha uhakika zaidi, kilicho imara zaidi na kilicho cha hekima zaidi ya mbiu hiyo" na “malezi yote ya kikristo kabla ya yote ni uelewa wa kina wa kerigma”.[53]

59. Mafundisho yetu kuhusu ndoa na familia hayawezi kutovuviwa na kung’arishwa na mbiu hii ya upendo na upole, ili yasiwe ni kulinda tu mafundisho baridi na yasiyo na uhai. Kwa kweli, haiwezekani kulielewa kikamilifu fumbo la familia ya kikristo bila mwangaza wa upendo usio na mwisho wa Baba, uliofunuliwa katika Kristo, ambaye amejitoa mpaka mwisho na yupo hai kati yetu. Kwa hiyo ninapenda kumtazama Kristo aliye hai na aliyemo ndani ya historia nyingi za upendo, na kuomba moto wa Roho uzishukie familia zote duniani.

60. Katika picha hii, sura hii fupi inakusanya ufupisho wa mafundisho ya Kanisa juu ya ndoa na familia. Pia nitanukuu michango mbalimbali ya Mababa wa sinodi katika fikra zao kuhusu mwangaza tunaopewa na imani. Mababa walianza na mtazamo wa Yesu na wakaonyesha kwamba Yeye “aliwatazama wanawake na wanaume aliokutana nao kwa upendo na upole, akiwasindikiza katika hatua zao kwa ukweli, uvumilivu na huruma, katika kutangaza masharti ya Ufalme wa Mungu”.[54] Na kwa mtindo huohuo, leo Bwana anatusindikiza katika bidii ya kuishi na kutangaza Injili ya familia.

Yesu anahuisha na kuukamilisha mpango wa Mungu.

61. Mbele ya wale waliokuwa wanazuia ndoa, Agano Jipya linafundisha kuwa “kila uumbaji wa Mungu ni mzuri, Wala hakuna cha kukataliwa” (1Tim 4:4). Ndoa ni “zawadi” ya Bwana (1Kor 7:7). Wakati huohuo, kutokana na tathmini chanya, unawekwa mkazo mkubwa wa kuitunza zawadi hii ya Mungu: “Ndoa iheshimiwe na wote na kitanda cha ndoa kisiwe na doa” (Ebr 13:4). Ujinsia na tendo la ndoa ni sehemu ya zawadi hii ya Mungu: “Msinyimane” (1Kor 7:5).

62. Mababa wa sinodi wamekumbusha kuwa Yesu, “akirejea mpango asili wa Mungu juu ya jozi la wanadamu, anathibitisha tena muungano usiovunjika kati ya mwanaume na mwanamke, pamoja na kusema kwamba “kwa ugumu wa mioyo yenu Musa aliwaruhusu kuwapa talaka wake zenu, lakini toka mwanzo haikuwa hivi” (Mt 19:8). Kutovunjika kwa ndoa (“Aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe”: Mt 19:6), hili kwanza kabisa halitakiwi lichukuliwe kama “nira” waliyotwishwa watu, badala yake lichukuliwe kma “zawadi” wanayopewa watu walioungana katika ndoa. [...] Uhisani wa Mungu unasindikiza daima watu katika safari yao, huponya na hugeuza moyo mgumu kwa neema, ukiwaongoza kuelekea asili yao, kwa njia ya msalaba. Katika Injili tunauona waziwazi mfano wa Yesu, ambaye [...] alitangaza ujumbe unaohusu maana ya ndoa kama ukamilifu wa ufunuo unaorudisha mpango asili wa Mungu (taz. Mt 19:8)”.[55]

63. “Yesu, aliyepatanisha yote katika nafsi yake, amerudisha ndoa na familia kwenye hali yake ya asili (taz. Mk 10:1-12). Familia na ndoa zimekombolewa na Kristo (taz. Efe 5:21-32), zimekarabatiwa kwa mfano wa Utatu Mtakatifu, fumbo ambalo kwalo upendo wote wa kweli unatoka. Agano la kindoa, lililoanzishwa katika uumbaji na likafunuliwa katika historia ya wokovu, linapata ufunuo kamili wa maana yake katika Kristo na katika Kanisa. Familia na ndoa zinapokea toka kwa Kristo kwa njia ya Kanisa neema inayohitajika ili kushuhudia upendo wa Mungu na kuishi kwa kushirikiana. Injili ya familia inaipitia historia yote ya ulimwengu tangu kuumbwa kwa mwanadamu kwa sura na mfano wa Mungu (taz. Mwa 1:26-27) hadi utimilifu wa fumbo la Agano katika Kristo mwisho wa nyakati kwa njia ya arusi ya Mwanakondoo (taz. Ufu 19:9)”.[56]

64. "Mfano wa Yesu ni msingi kwa Kanisa. [...] Yeye aliyazindua maisha yake ya hadhara kwa ishara ya Kana, aliyoifanya kwenye muktadha wa arusi (taz. Yn 2:1-11). [...] Alishiriki maisha ya kila siku ya familia ya Lazaro na dada zake (taz. Lk 10:38) na familia ya Petro (taz. Mt 8:14). Alisikiliza kilio cha wazazi kwa ajili ya watoto wao, akawafufua (taz. Mk 5:41; Lk 7:14-15), akaonyesha hivyo maana halisi ya huruma, inayomaanisha kuweka Agano upya (taz. Yohane Paulo II, Dives in misericordia, 4). Hili linaonekana wazi anapokutana na mwanamke Msamaria (taz. Yn 4:1-30) na yule mzinifu (taz. Yn 8:1-11), ambapo utambuzi wa dhambi unaamshwa mbele ya upendo wa bure wa Yesu”.[57]

65. Umwilisho wa Neno katika familia ya kibinadamu, Nazareth kwa upya wake unagusa historia ya ulimwengu. Tunahitaji kuzama kwenye fumbo la kuzaliwa kwa Yesu, katika ndiyo ya Maria wakati wa kupashwa habari na malaika, Neno alipotungwa mimba tumboni mwake; hata katika ndiyo ya Yosefu, aliyempa jina Yesu na akamtunza Maria; katika sherehe ya wachungaji pangoni; katika maabudu ya Mamajusi; katika kutorokea Misri, ambapo Yesu alishiriki mateso ya Taifa lake lililopelekwa uhamishoni, likateswa na kudhalilishwa; katika subira ya Zakaria na katika furaha inayosindikiza kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji; katika ahadi iliyotimizwa kwa Simeoni na Anna hekaluni; katika mshangao wa walimu wa sheria wanaposikiliza hekima ya Yesu kijana mdogo. Na hivi yatupasa kuingia ndani ya miaka thelathini wakati Yesu alipojipatia mkate kwa kufanya kazi kwa mikono yake, akisali na kufuata mapokeo ya imani ya watu wake na kuzidi kujifunza imani ya wazee wake, hata kuifanya izae katika fumbo la Ufalme. Hili ni fumbo la Noeli na siri ya Nazarethi, iliyojaa manukato ya familia! Ni fumbo lililowavutia sana watakatifu: Fransisko wa Asizi, Teresia wa Mtoto Yesu na Charles de Foucauld, na linalotazamwa na familia za kikristo ili kuhuisha matumaini na furaha zake.

66. “Agano la upendo na uaminifu, ambalo kwalo Familia Takatifu ya Nazareth inaishi, linauangaza mwanzo unaotengeneza msingi wa familia zote na linaziwezesha vema zaidi kukabiliana na changamoto za maisha na historia. Juu ya msingi huu, kila familia, pamoja na udhaifu wake, inaweza kuwa mwanga katika giza la ulimwengu. “Hapa tunaelewa namna ya kuishi katika familia. Nazareth itukumbushe nini maana ya familia, nini ushirika wa upendo, uzuri wake usio na anasa na wa kawaida, utakatifu wake na kutoharibika kwake; itufanye tuonje utamu wa malezi ya familia, ambayo hayawezi kukasimishwa kwa yeyote, ituonyeshe nafasi yake ya asili katika jamii” (Paulo VI, Hotuba huko Nazarethi, 5 Januari 1964)”.[58]

Familia katika hati za Kanisa

67. Mtaguso wa kiekumene wa pili wa Vatikano, katika kostitusio ya kichungaji Gaudium et spes, umeshughulikia ukuzaji wa hadhi ya ndoa na familia. 47-52). “Umeileza ndoa kama jumuiya ya uhai na upendo (taz. na. 48), ukiweka upendo kama kiini cha familia [...]. ‘Upendo wa kweli kati ya mume na mke’ (na. 49) unamaanisha mmoja kujitoa kwa mwingine, ikiwemo mahusiano katika tendo la ndoa na mapenzi, kadiri ya mpango wa Mungu (taz. na. 48-49). Zaidi ya hayo Mtaguso unakazia juu ya Kristo kuwa msingi wa wanandoa: Kristo Bwana ‘anakutana na wanandoa wakristo katika sakramenti ya ndoa’ (na. 48) na anabaki pamoja nao. Katika umwilisho, Yeye anauchukua upendo wa kibinadamu, anausafisha, anautimiliza, na kwa Roho wake anawapa wanandoa uwezo wa kuuishi, ukiyapenya maisha yao yote ya imani, matumaini na mapendo. Kwa mtindo huu wanandoa wanakuwa kama wamewekwa wakfu na, kwa neema ya pekee, wanajenga Mwili wa Kristo na wanakuwa Kanisa la nyumbani (taz. Lumen Gentium, 11), kiasi kwamba Kanisa, ili lijitambue kikamilifu katika fumbo lake, linaitazama familia ya kikristo, linalodhihirishwa nayo katika uhalisia”.[59]

68. Baadaye, “mwenye heri Paulo VI, tokana na Mataguso wa II wa Vatikano ametoa mafundisho ya ndani juu ya ndoa na familia. Kwa namna ya pekee, katika Ensiklika Humanae Vitae, ameweka wazi uhusiano uliopo kati ya upendo wa wanandoa na uzazi. “Upendo kati ya wanandoa unawataka wautambue utume wao wa kuwa wazazi wanaowajibika, jambo ambalo siku hizi kwa usahihi kabisa kinakaziwa na ambalo lingetakiwa lieleweke kwa usahihi. [...] Uzazi unaowajibika kwa hiyo unamaanisha kwamba wanandoa wanatakiwa kuzijua wajibu zao kwa Mungu, kwao wenyewe, kwa familia na kwa jamii, kwa kuzingatia ngazi sahihi ya tunu” (na. 10). Katika Wosia wa Kitume Evangelii nuntiandi, Paulo VI ameeleza uhusiano uliopo kati ya familia na Kanisa".[60]

69. “Mt. Yohane Paulo II katika katekesi zake juu ya upendo wa kibinadamu, Barua kwa familia Gratissimam sane na hasa katika Wosia wa Kitume Familiaris consortio, ametoa nafasi kubwa kwa familia. Katika hati hizo, Baba Mtakatifu ameitaja familia kuwa “njia ya Kanisa”; ametoa mtazamo wa ujumla juu ya wito wa upendo wa mwanaume na mwanamke; amependekeza misingi elekezi ya uchungaji wa familia na kwa uwepo wa familia katika jamii. Kwa namna ya pekee, akiongelea mapendo ya kindoa (taz. Familiaris Consortio, 13), ameieleza namna ambayo wanandoa, katika kupendana, wanapokea zawadi ya Roho wa Kristo na wanauishi wito wao wa kuwa watakatifu”.[61]

70. “Benedikto XVI, katika Ensiklika Deus caritas est, ameileta tena mada ya ukweli wa upendo kati ya mume na mke, unaoangazwa kikamilifu na upendo wa Kristo msulibiwa (taz. na. 2). Yeye anarudia kusisitiza kuwa “ndoa ambayo msingi wake ni upendo kati ya mume mmoja na mke mmoja na wa kudumu inakuwa ikona ya uhusiano wa Mungu na taifa lake na pia kinyume chake: namna ya kupenda ya Mungu inakuwa kipimo cha upendo wa kibinadamu” (na. 11). Zaidi ya hayo, katika Ensiklika Caritas in veritate, anaeleza umuhimu wa upendo kama chimbuko la uhai katika jamii (taz. na. 44), mahali ambapo watu hujifunza kuzoea mafaa ya pamoja”.[62]

Sakramenti ya ndoa

71. “Maandiko Matakatifu na Mapokeo hutufungulia mlango wa kuweza kuufahamu Utatu Mtakatifu unaojifunua kwa sura ya kifamilia. Familia ni mfano wa Mungu, ambaye ni [...] ushirika wa nafsi. Katika Ubatizo, sauti ya Baba inamtaja Yesu kama Mwanae mpendwa, na katika upendo huu tunaweza kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu (taz. Mk 1:10-11). Yesu, aliyepatanisha kila kitu katika Yeye na amemkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi, si tu kwamba ameirudisha ndoa na familia katika hali yake ya asili, bali pia ameikuza ndoa na kuifanya ishara ya kisakramenti ya upendo wake kwa Kanisa (taz. Mt 19:1-12; Mk 10:1-12; Efe 5:21-32). Katika familia ya kibinadamu, iliyokusanywa na Kristo, imerudishwa “sura na mfano” ya Utatu Mtakatifu (taz. Mwa 1:26), fumbo ambalo toka kwalo unatoka kila upendo wa kweli. Toka kwa Kristo, kupitia Kanisa, ndoa na familia hupokea neema ya Roho Mtakatifu, ili kushuhudia Injili ya upendo wa Mungu”.[63]

72. Sakramenti ya ndoa si desturi ya kijamii, ibada tupu au ishara ya nje tu ya wajibu fulani. Sakramenti ni zawadi kwa ajili ya kutakatifuza wanandoa na ya wokovu wao, kwa sababu "ukweli kwamba kila mmoja ni wa mwingine, unaonyesha kwa ishara ya kisakramenti uhusiano wa Kristo na Kanisa. Wanandoa kwa hiyo wanalikumbusha Kanisa juu ya kile kilichotokea juu ya Msalaba; wanaishi mmoja kwa ajili ya mwingine, na kwa ajili ya watoto, mashahidi wa wokovu, ambao kwa sakramenti wanafanywa waushiriki".[64] Ndoa ni wito, kwani ni jibu kwa mwito maalum wa kuuishi upendo kati ya wanandoa kama ishara isiyo kamili ya upendo kati Kristo na Kanisa. Kwa hiyo, uamuzi wa kuoana na kuunda familia ni lazima utokane na upambanuzi wa kimwito.

73. “Kujitoa kila mmoja kwa mwenzake ambako ni sifa ya msingi ya ndoa ya kisakramenti, kuna mizizi yake katika neema ya ubatizo unaoweka agano la msingi la kila mtu na Kristo ndani ya Kanisa. Katika kupokeana na kwa neema ya Kristo wanaofunga ndoa wanaahidiana kila mmoja kujitoa kikamilifu kwa mwingine, pia wanaahidiana uaminifu na utayari wa kupokea uhai, yaani kuzaa, wanatambua kuwa zawadi wanazopewa na Mungu ni msingi wa ndoa yenyewe, wanazichukua kwa umakini wajibu zao, katika jina lake na mbele ya Kanisa. Sasa, katika imani inawezekana kuyapokea mema ya ndoa kama wajibu ambazo zinabebeka kirahisi zaidi kwa msaada wa neema ya sakramenti. [...] Kwa hiyo, Kanisa linawatazama wanandoa kama moyo wa familia nzima ambayo nayo inamtazama Yesu”.[65] Sakramenti si “kitu” fulani au “ nguvu” fulani, kwa sababu kwa kweli Kristo mwenyewe “anakuja kukutana na wanandoa wakristo kwa njia ya sakramenti ya ndoa. Yeye anabaki nao, anawapa nguvu ya kumfuasa wakichukua msalaba wao, nguvu ya kuinuka wakianguka, ya kusameheana, ya kuchukuliana mizigo kila mmoja ya mwenzake".[66] Ndoa ya kikristo ni ishara ambayo si tu kwamba inaonyesha jinsi Kristo alivyolipenda Kanisa lake katika Agano lililowekwa msalabani, bali inaufanya upendo huo uwepo katika ushirika wa wanandoa. Wakiungana katika mwili mmoja, wanakuwa ishara ya ndoa ya Mwana wa Mungu na ubinadamu. Kwa sababu hii, "katika furaha za upendo wao na za maisha yao ya kifamilia, Yeye huwapa, tayari hapa duniani, nafasi ya kuonja karamu ijayo ya arusi ya Mwanakondoo".[67] Hata kama “mfano wa jozi mume-mke na Kristo-Kanisa” ni “mfano usio kamili”,[68] unasaidia kumwomba Bwana amimine upendo wake kati ya wanandoa pamoja na mapungufu yao.

74. Muungano wa kijinsia, unaofuata taratibu za kibinadamu na uliotakatifuzwa na sakramenti ya ndoa, unawasaidia wanandoa kukua katika maisha ya neema. Ndilo "fumbo la ndoa".[69] Thamani ya muungano wa miili inaonyeshwa katika maneno ya makubaliano, pale ambapo wanandoa wanapokeana na kujitoa kila mmoja kwa mwingine ili kushirikiana kwa maisha yao yote. Maneno haya yanatia maana kwa ujinsia, na yanauondolea utata wote. Hata hivyo, kwa kweli, maisha yote ya pamoja ya wanandoa, mtandao wote wa mahusiano watakaoutengeneza kati yao, pamoja na watoto wao na kwa ulimwengu, utajengwa na kuimarishwa na neema ya sakramenti inayobubujika toka fumbo la Umwilisho na la Pasaka, ambamo Mungu ameonyesha upendo wake wote kwa ubinadamu na akajiunganisha nao kabisa. Hawatakuwa kamwe peke yao kukabiliana na changamoto zitakazotokea. Wao wanatakiwa kupokea zawadi ya Mungu kwa kuwajibika, kwa ubunifu wao, kwa uvumilivu na mapambano ya kila siku, lakini wataweza daima kumwomba Roho Mtakatifu aliyeweka wakfu muungano wao, ili neema waliyopokea iweze kudhihirika upya katika kila hali.

75. Kadiri ya mapokeo ya kilatini ya Kanisa, katika sakramenti ya ndoa wahudumu ni mume na mke wanaooana,[70] ambao kwa kutamka wazi makubaliano yao na kuyadhihirisha katika kujitoa kimwili kila mmoja kwa mwenzake, wanapokea zawadi kubwa. Makubaliano yao na muungano wa miili ni nyenzo ambazo kwazo Mungu anawafanya kuwa mwili mmoja. Katika ubatizo uliwekwa wakfu uwezo wao wa kuungana katika ndoa kama wahudumu wa Bwana ili kuitikia wito wa Mungu. Kwa hiyo, wanandoa wasio wakristo wanapobatizwa, si lazima kwao kurudia viapo vya ndoa na inatosha kwamba hawavikatai, kwani, kutokana na Ubatizo wanaopokea, muungano wao unakuwa papo hapo wa kisakramenti. Sheria za Kanisa zinazitambua kuwa ni halali hata ndoa zilizoadhimishwa bila uwepo wa mhudumu mwenye daraja takatifu.[71] Maana, utaratibu wa asili umechukuliwa na ukombozi wa Yesu Kristo, kwa namna ya kwamba “kati ya wabatizwa hapawezi kuwepo mkataba halali wa kindoa, usio kwa wenyewe sakramenti”.[72] Kanisa linaweza kutaka tendo lifanyike hadharini, wawepo mashahidi, na mambo mengine ambayo yamebadilika katika historia, lakini hili haliondoi kwa wanandoa ile hali yao ya kuwa wahudumu wa sakramenti, wala halipunguzi umuhimu wa makubaliano ya mume na mke, ambayo ndiyo yanayoweka kifungo cha kisakramenti. Kwa vyovyote vile, tunahitaji kutafakari zaidi juu ya tendo la kimungu katika madhehebu ya ndoa, jambo ambalo linakaziwa zaidi katika Makanisa ya Mashariki, hasa kwa kuonyesha umuhimu wa pekee kwa baraka ya wafunga ndoa kama ishara ya zawadi ya Roho.

Mbegu za Neno na hali zenye mapungufu

76. "Injili ya familia inazilisha pia zile mbegu ambazo bado zinasubiri kukomaa, nayo inapaswa kuitunza miti ile iliyokauka na inayohitaji kutotelekezwa",[73] kiasi kwamba, kwa kuanzia na zawadi ya Kristo katika sakramenti, “[watu] waongozwe kwa uvumilivu mbele zaidi, hadi kufikia ufahamu mkubwa zaidi na hata kulizamisha kabisa Fumbo hili katika maisha yao”.[74]

77. Mababa wa sinodi wakizingatia mafundisho ya kibiblia, ambayo kadiri yake kila kitu kimeumbwa kwa njia ya Kristo na kwa ajili ya Kristo, (taz. Kol 1:16), wamekumbusha kuwa “mpango wa ukombozi unauangaza na kuukamilisha ule wa uumbaji. Ndoa ya asili, kwa hiyo, inaeleweka kwa ukamilifu katika mwanga wa utimilifu wake wa kisakramenti: kwa njia tu ya kumtazama Kristo inawezekana kuuelewa kwa undani kabisa ukweli juu ya mahusiano ya kibinadamu. “Kwa kweli fumbo la binadamu linapata mwanga wa kweli katika fumbo la Neno aliyetwaa mwili. […] Kristo, ambaye ni Adamu mpya, akifunua fumbo la Baba na la upendo wake, anamfunua pia kikamilifu mtu kwa mtu mwenyewe na anamwonyesha wito wake wa juu kabisa” (Gaudium et spes, 22). Inakuja kwamba ni muhimu kwa namna ya pekee kuzielewa kwa mtazamo wa Kristokati tabia asili za ndoa, zile zinazounda mafaa ya wanandoa (bonum coniugum)”,[75] ambayo ni umoja, utayari wa kuwa wazazi, uaminifu na kutovunjika kwa ndoa, na ndani ya ndoa ya kikristo hata kusaidiana katika safari ya kuelekea kwenye ukamilifu wa urafiki na Bwana. "Upambanuzi wa uwepo wa mbegu za Neno hata katika tamaduni nyingine (rej. Ad gentes, 11) unaweza kufanyika hata katika masuala ya ndoa na familia. Zaidi ya ndoa ya kweli ya asili kuna vitu chanya katika aina nyingine za ndoa zinazopatikana katika tamaduni za kidini tofauti tofauti”,[76] hata kama vinapatikana pia vivuli. Tunaweza kutamka kuwa "kila mtu anayetaka kuiunda katika ulimwengu huu familia inayofundisha watoto kufurahia kila tendo linalonuia kushinda uovu – familia inayoonyesha kuwa Roho ni hai na anafanya kazi –, atapata shukrani na heshima, awe ni mtu wa taifa lolote lile, au dini au kanda".[77]

78. “Mtazamo wa Kristo, ambao mwanga wake unamwangaza kila mtu (taz. Yn 1:9; Gaudium et spes, 22), unalivuvia Kanisa katika uchungaji wake kwa waamini wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa au waliofunga ndoa za kiserikali tu au wametalikiana na kufunga ndoa nyingine. Katika mtazamo wa malezi ya kimungu, Kanisa linawaangalia kwa upendo wale wanaoshiriki maisha yake kwa namna isiyo kamilifu: linaomba pamoja nao neema ya wongofu, linawahamasisha kutenda mema, kutunzana kwa upendo na kutoa huduma kwenye jumuiya wanamoishi na wanamofanya kazi. […] Muungano usio rasmi unapofikia hatua thabiti kwa njia ya kifungo cha hadharani – na unaonyesha mapendo makubwa, unawajibika kwa watoto, una uwezo wa kushinda magumu – unaweza kuwa fursa ya kuwasindikiza kuelekea sakramenti ya ndoa, pale inapowezekana".[78]

79. “Mbele ya hali ngumu na familia zilizojeruhiwa, inatakiwa kukumbuka kanuni hii ya jumla: ‘Wachungaji watambue kuwa, kwa ajili ya ukweli, wanatakiwa kuzipambanua vyema hali mbalimbali” (Familiaris consortio, 84). Kiasi cha wajibu hakilingani katika kila hali, na inawezekana ziwepo sababu zinazopunguza uwezo wa kuamua. Kwa hiyo, wakati mafundisho yanatakiwa yaelezwe kwa uwazi, tunatakiwa tuepukane na hukumu zisizozingatia ugumu wa hali tofauti, na ni muhimu pia kuzingatia hali tofauti wanazoishi watu na maumivu waliyo nayo kutokana na hali zao".[79]

Uzazi na malezi ya watoto

80. Ndoa, kwanza kabisa ni “jumuiya ya undani ya maisha na ya mapendo ya kindoa"[80] ambayo ndiyo hasa mafaa kwa wanandoa wenyewe,[81] na ujinsia “unalenga kudhihirisha upendo wa kindoa wa mwanamke na mwanaume”.[82] Kwa hiyo hata “wanandoa ambao Mungu hakuwajalia watoto, wanaweza kuwa na maisha ya kindoa yenye maana, kiutu na kikristo”.[83] Pamoja na hayo, muungano huu “kwa asili yake unalenga uzazi”.[84] Mtoto anayezaliwa “si kwamba anajiongeza kutoka nje ya mapendo ya wanandoa; anachipua kutoka kwenye moyo wenyewe wa majitoleo ya kila mmoja kwa mwingine, na anakuwa tunda na utimilifu wake".[85] Hafiki kama hitimisho la mchakato, bali ni kwamba tayari yupo tangu mwanzo wa mapendo yao kama kiini ambacho hakiwezi kukataliwa bila kuudhuru upendo wenyewe. Tangu mwanzo upendo unagoma kujifungia ndani yake wenyewe na hivi unajifunua katika uzaaji ambao unaendeleza uwepo wake. Hivyo, hakuna tendo la ndoa la wanandoa ambalo laweza kuikataa maana hii,[86] hata kama kwa sababu mbalimbali si daima maisha mapya yanaweza kuzaliwa.

81. Mtoto anahitaji kuzaliwa kutokana na upendo wa mtindo huo na si katika mtindo mwingine wowote, kwa vile yeye “si kitu kinachodaiwa, bali ni zawadi”,[87] ni “tunda la tendo maalum la upendo wa kindoa wa wazazi wake”.[88] Kwa sababu “kadiri ya mpango wa uumbaji, upendo wa kindoa kati ya mume na mke na uzazi hutegemezana (taz. Mwa 1:27-28). Kwa namna hii Muumba amewashirikisha mwanaume na mwanamke katika kazi ya uumbaji wake na wakati huohuo akawafanya kuwa vyombo vya upendo wake, akiwawajibisha kuhusu mustakabali wa wanadamu kwa njia ya kuendeleza uhai ulimwenguni”.[89]

82. Mababa wa sinodi wametamka kuwa “si haba kuona watu wanavyozidi kuwa na mtazamo unaodunisha uzazi kuwa ni jambo mojawapo tu la mipango ya mtu au jozi".[90] Mafundisho ya Kanisa “yanasaidia kuishi kwa utulivu na uelewa ushirika kati ya wanandoa, katika nyanja zake zote, ikiwa ni pamoja na wajibu wa kuzaa. Inafaa kurudi kwenye ujumbe wa Ensiklika Humanae vitae ya Paulo VI, unaokazia hitaji la kustahi hadhi ya mtu wakati wa kuzitathmini kimaadili njia za kupanga uzazi [...]. Chaguo la kumwasilisha mtoto au kuwapokea watoto wasio wa wanandoa – hata ikiwa ni kwa muda – na kuwatunza ni namna nyingine ya pekee ya kuuishi uzazi katika maisha ya wanandoa.[91] Kwa shukrani ya pekee, Kanisa “linaziunga mkono familia zinazowapokea, zinazowalea na kuwaonyesha upendo watoto wao walemavu”.[92]

83. Katika muktadha huo, siwezi kutotamka kuwa, ikiwa familia ni hekalu la uhai, mahala ambapo uhai huzalishwa na kutunzwa, ni mkanganyiko mkubwa kuona kwamba mahala hapohapo uhai unakataliwa na kuharibiwa. Uhai wa binadamu una thamani kubwa hivi, na haki ya kuishi ya mtoto, ambaye hana kosa, hainyang’anyiki hivi akingali anakua katika tumbo la uzazi la mama, kiasi kwamba kwa namna yoyote haiwezekani kufanya hivyo, eti, kwa hoja ya haki binafsi ya mwili, yaani kufanya maamuzi yanayodhulumu uhai huo, ambao kwa wenyewe unajitegemea na usingetakiwa utawaliwe na binadamu mwingine. Familia hulinda uhai katika kila hatua yake na hata katika mwisho wake. Kwa hiyo "wale wanaotoa huduma kwenye taasisi za afya wanakumbushwa wajibu wa kimaadili wa kufuata ukinzani wa dhamiri. Hali kadhalika, Kanisa si tu linaona ulazima wa kusisitiza haki ya kukutwa na kifo cha kawaida, bila kulazimisha matibabu ya ghali sana wala kukubali kifo laini”, lakini pia "linapinga kwa dhati adhabu ya kifo".[93]

84. Mababa wa sinodi wametaka kusisitiza pia kwamba "changamoto mojawapo ya msingi ambayo familia leo zinakabiliwa nayo bila shaka ni malezi, ambayo imekuwa ngumu na yenye utata zaidi kutokana na mabadiliko ya kitamaduni na mvuto wa vyombo vya habari".[94] “Kanisa linafanya kazi yenye thamani kubwa ya kuzisaidia familia, kuanzia na mafundisho ya kuwaingiza katika ukristo, kwa kupitia jumuiya zenye ukarimu wa ukaribishaji”.[95] Hata hivyo naona muhimu sana kukumbusha kuwa malezi kamili ya watoto “ni wajibu mkubwa mno” na wakati huohuo "ni haki msingi” ya wazazi.[96] Si suala la wajibu au mzigo tu, bali pia haki msingi ya wazazi isiyoweza kukasimishwa, nao wanatakiwa kuitetea na hakuna mtu anayeweza kudai kuiondoa toka kwao. Serikali inaweza kuwasaidia tu wazazi katika kutoa huduma ya elimu kwa watoto, ikiwasindikiza wazazi katika jukumu lao la kimalezi pasipo kuchukua nafasi yao, ambao wanayo haki na uhuru wa kuchagua aina ya elimu – iliyo rahisi na bora – wanaopenda kutoa kwa watoto wao kadiri ya fikra na imani yao. Shule haiwezi kuchukua nafasi ya wazazi, ila huduma inayotoa inakamilishana na wajibu wa wazazi. Hii ni kanuni msingi: "Mshiriki yeyote mwingine katika mchakato wa kutoa elimu kwa watoto ni lazima afanye hivyo kwa niaba ya wazazi, kwa ridhaa yao na, kwa kiasi fulani, ni lazima wazazi wampe mamlaka".[97] Lakini "umetokea mpasuko kati ya familia na jamii, kati ya familia na shule; mkataba wa kimalezi leo hii umevunjika; na hivi, agano la kimalezi la jamii na familia limeingia katika mvurugiko”.[98]

85. Kanisa linaalikwa kushiriki, kwa tendo la kichungaji stahiki, ili wazazi wenyewe waweze kutekeleza utume wao wa kulea. Linatakiwa liwasaidie kuthamini nafasi yao ya pekee, na kutambua kuwa wale waliopokea sakramenti ya ndoa hufanyika kuwa wahudumu hasa wa malezi, kwa sababu katika kuwalea watoto wao wazazi wanalijenga Kanisa,[99] na kwa kufanya hivyo wanaitikia wito ambao kwao Mungu amewaita.[100]

Familia na Kanisa

86. “Kanisa huzitazama kwa furaha ya dhati na faraja kubwa familia zinazodumu aminifu kwa mafundisho ya Injili, likizishukuru na kuzitia moyo kwa ushuhuda unaooneshwa nazo. Kwa njia yao, kwa kweli, uzuri wa ndoa isiyovunjika na aminifu daima unashuhudiwa kama jambo la kuaminika. Katika familia, “inayoweza kuitwa Kanisa la nyumbani” (Lumen Gentium, 11), ndimo tunaanza kujifunza kuuishi ushirika wa kikanisa, ambamo, kwa neema, fumbo la Utatu Mtakatifu unaakisiwa. “Hapa ndipo mmoja anapojifunza ugumu na furaha ya kazi, upendo wa kidugu, msamaha mkarimu, unaofanywa upya tena na tena, na hasa ibada takatifu kwa njia ya sala na toleo la maisha yake” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1657)”.[101]

87. Kanisa ni familia ya familia nyingi, ambalo daima hutajirishwa na maisha ya Makanisa yote ya nyumbani. Kwa hiyo, "kwa njia ya sakramenti ya ndoa kila familia inakuwa kwa ukamilifu faida kwa Kanisa. Kwa mtazamo huu, hakika itakuwa zawadi ya thamani kwa Kanisa la leo, kuzingatia hata uhusiano wa kusaidiana uliopo kati ya familia na Kanisa: Kanisa ni faida kwa familia, familia ni faida kwa Kanisa. Kuilinda zawadi ya sakramenti ya Bwana hakuihusishi familia moja pekee, bali jumuiya nzima ya kikristo”.[102]

88. Upendo uliopo kwenye familia ni nguvu ya kudumu kwa uhai wa Kanisa. "Hatima ya ndoa ya kudumisha umoja ni mwito wa daima wa kukua na kujikita katika upendo huu. Katika muungano wao wa upendo wanandoa wanang’amua uzuri wa kuwa baba na mama; wanashirikishana mipango na uchovu, matamanio na mahangaiko; wanajifunza kutunzana na kusameheana. Katika upendo huu wanaadhimisha nyakati zao za furaha na wanasaidiana katika hatua ngumu za maisha yao [...]. Uzuri wa kuwa mmoja zawadi kwa mwingine, furaha kwa watoto wanaozaliwa, na matunzo yenye upendo kwa wanafamilia wote, kuanzia watoto hadi wazee, ni baadhi ya matunda yanayofanya jibu kwa wito wa familia liwe pekee na lisilobadilishika",[103] kwa ajili ya Kanisa na vilevile kwa jamii nzima.

SURA YA NNE

UPENDO KATIKA NDOA

89. Hayo yote yaliyosemwa hayajitoshelezi ili kuelezea Injili ya ndoa na ya familia kama hatuchukui nafasi ili kunena kwa namna maalumu juu ya upendo. Kwani hatuwezi kuhimiza mwendo wa uaminifu na wa kujitoa kila mmoja kwa mwenzake ikiwa hatuchochei ukuaji, udumishaji na uimarishaji wa upendo kati ya wanandoa na katika familia. Kwa kweli, neema ya sakramenti ya ndoa inaelekea kwanza kabisa "kukamilisha upendo kati ya wanandoa".[104] Katika uwanja huo pia ni sahihi ule msemo, kwamba, hata “nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu" (1Kor 13:2-3). Neno "upendo" lakini, ambalo ni mojawapo ya maneno yanayotumiwa zaidi, mara nyingi linaonekana kurembuka.[105]

Upendo wetu wa kila siku

90. Katika ule utenzi tuliozoea kuuita ‘wa upendo’, ulioandikwa na mtakatifu Paulo, tunakuta sifa kadha wa kadha za upendo wa kweli:

"Upendo huvumilia,
upendo hufadhili,
hauhusudu,
upendo hautakabari,
haujivuni,
haukosi kuwa na adabu,
hautafuti mambo yake,
hauoni uchungu;
hauhesabu mabaya;
haufurahii udhalimu,
bali hufurahi pamoja na kweli.
Huvumilia yote,
huamini yote,
hutumaini yote,
hustahimili yote (1Kor 13:4-7).

Upendo huo unaonjwa na unasitawishwa katika maisha ambayo wanayashiriki kila siku wanandoa, kati yao na pamoja na watoto wao. Kwa hiyo inasaidia kutafakari kwa kina maana ya maneno haya [ya Paulo], ili kujaribu kuona namna yanavyoweza kuwa kweli kwa maisha halisi ya kila familia.

Uvumilivu

91. Neno la kwanza linalotumika ni makrothimei. Tafsiri sahihi si moja kwa moja “wenye kustahimili yote”, kwa sababu wazo hilo linatolewa mwishoni mwa aya ya 7. Maana yake inaweza kupatikana katika tafsiri ya Kigriki ya Agano la Kale, pale ambapo inasema kwamba Mungu “si mwepesi wa hasira” [, au ni “mpole wa hasira”] (Kut 34:6; Hes 14:18). Inajionyesha pale ambapo mtu hakubali kuongozwa na misukumo ya hasira na anakwepa kuwashambulia wengine. Ni sifa bainifu ya Mungu wa Agano anayeita kumwiga pia katika maisha ya kifamilia. Matini ambamo Paulo ametumia neno hilo zinapaswa kusoma katika muktadha wa kitabu cha Hekima (taz. 11:23; 12:2,15-18): wakati sifa inapotolewa kwa upole wa Mungu anayetaka kuacha nafasi kwa toba, hapohapo husisitizwa uweza wake unaodhihirika anapotenda kwa huruma. Uvumilivu wa Mungu ni zoezi la huruma kwa mwenye dhambi, nao hudhihirisha uweza halisi.

92. Kuwa wavumilivu maana yake si kukubali wengine watutese mara kwa mara, au kuvumilia kupigwa au kutendewa ukatili, au kuacha watuhesabu kama vitu. Tatizo linaanza pale ambapo tunadai kwamba mahusiano yawe kama hadithi tamu au kwamba watu wawe wakamilifu, au tunapojiweka katikati na kunasubiri tu kwamba mapenzi yetu yatimizwe. Hapo kila kitu kinavunja uvumilivu wetu, kila jambo linatusukuma tusisimue kwa ukali. Ikiwa hatusitawishi uvumilivu, tutakuwa daima na sababu ya kujibu kwa hasira, na hatimaye tutakuwa watu ambao hawajui kuishi pamoja na wengine, watu wanaochukia jumuiya, wasioweza kutawala mihemko, na familia itapindua kuwa kiwanja cha vita. Ndiyo sababu Neno la Mungu linatuhimiza: "Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu" (Efe 4:31). Uvumilivu huo unaimarika ninapotambua kwamba pia mwingine huyu anayo haki ya kuishi duniani humu pamoja na mimi, hivi alivyo. Haidhuru kama yeye huleta usumbufu kwangu, kama anabadili mipango yangu, kama namna yake ya kuishi au mawazo yake hunisumbua, kama hawi katika yote kadiri nilivyotegemea. Upendo unaendana daima na hisia ya kina ya huruma, inayoongoza kumpokea mwingine kama sehemu ya dunia hii, pia anapotenda tofauti na nilivyotamani.

Moyo wa ufadhili

93. Linafuata neno krestevetai, ambalo ni pekee katika Biblia nzima, likitokana na krestos (mtu mwema, anayeonyesha wema wake katika matendo). Lakini, kwa kuzingatia mahali hapa linapopatikana, yaani sambamba kabisa na kitenzi kinachotangulia, linakuwa shamirisho yake. Kwa namna hiyo, Paulo anataka kuweka dhahiri kwamba "uvumilivu" uliotajwa awali si hali ya kutendwa tu, bali unaendana na utendaji maalumu, na marejesho yenye juhudi na ubunifu kuhusu wengine. Unamaanisha kwamba upendo unawatendea wema wengine na unawaendeleza. Kwa hiyo, tafsiri yake ni "wa fadhili".

94. Katika ujumla wa matini hii, inaonekana kwamba Paulo anataka kusisitiza ukweli wa kwamba upendo si hisia tu, bali unatakiwa kufasiriwa katika maana ambayo kitenzi "kupenda" kinayo katika lugha ya Kiebrania, yaani: "kutenda wema". Kama alivyosema mtakatifu Ignasi wa Loyola, "upendo lazima utiwe katika matendo kuliko maneno".[106] Kwa namna hiyo, unaweza kuonyesha uwezo wake mkuu wa kuzaa matunda, na unatuwezesha kung'amua furaha ya kutoa, ubora na ukuu wa kujitolea kupita kiasi, bila kipimo, bila kudai thawabu, kwa ajili tu ya kutoa na kutumikia.

Kuponya husuda

95. Kwa hiyo inakataliwa kama kinyume cha upendo ule msimamo unaoelezwa na neno zelos (wivu au husuda). Ina maana kwamba katika upendo hakuna nafasi ya kuchukizwa kwa sababu ya mema anayopata mwingine (taz. Mdo 7:9; 17:5). Husuda ni uchungu kwa sababu ya mema wanayopata wengine, unaodhihirisha kwamba sisi hatujali furaha ya wengine, kwani tunatafuta tu manufaa yetu. Upendo unatutoa nje na sisi wenyewe, husuda inatusukuma kujikusanya ndani ya umimi wetu binafsi. Upendo wa kweli unafurahia mafanikio ya wengine, bila kuwaona kama kitisho, nao unajiokoa na uchungu wa husuda. Unakubali kwamba vipawa na njia ya maisha ya kila mmoja hutofautiana. Kwa hiyo, unajitahidi kugundua njia yake pekee ili kuwa na furaha, na kuwaachia wengine nao waione ya kwao.

96. Kimsingi ni suala la kutimiza kilichoagizwa na amri mbili za mwisho za Sheria ya Mungu: "Usitamani nyumba ya jirani yako, usitamani mke wa jirani yako, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala chochote alicho nacho jirani yako" (Kut 20:17). Upendo unatuongoza kumthamini kwa dhati kila mwanadamu, kwa kutambua haki yake ya kuwa na furaha. Ninampenda mtu yule, ninamtazama kwa mtazamo wa Mungu Baba, atupaye vitu vyote "ili tuvitumie kwa furaha" (1Tim 6:17), na ndiyo sababu ninakubali ndani yangu kwamba aweze kuifurahia nafasi njema. Kwa vyovyote, mzizi huuhuu wa upendo ni ule unaoniongoza kukataa utovu wa haki ambao kwao wengine wana vitu vingi mno na wengine hawana kitu, au ule unaonisukuma kutenda ili pia wale wanaotupwa na jamii waweze kuishi kwa furaha walau kidogo. Hili lakini si husuda, bali ni hamu ya haki sawa.

Bila kutakabari wala kujivuna

97. Linafuata neno perperevetai, linalomaanisha majivuno, hamasa ya kujionyesha wakubwa kuliko wengine na kuwashangaza kwa msimamo wa kisomi na mkali hasa. Mwenye kupenda, si tu anajinyima kusema habari zake mwenyewe, lakini pia, kwa vile ametia wengine kama kiini cha maisha yake, anajua kujitia katika nafasi yake, bila kudai kuwa kiini yeye mwenyewe. Neno linalofuata – fisioutai – linafanana sana, kwa sababu linamaanisha kwamba upendo hauna kiburi. Kwa fasiri sisisi linaelezea kwamba "haujikuzi" mbele ya wengine, na linadokeza jambo penyevu zaidi. Si tu shauku isiyotulizika ya mtu kuonyesha sifa zake, lakini hupotezesha pia hisia ya uhalisia wa mambo. Ni mtu kujihesabu mkubwa zaidi kuliko alivyo kwa sababu anaamini kuwa yeye ni "wa rohoni" au "mwenye busara" zaidi. Paulo anatumia kitenzi hiki mara nyingine pia, kwa mfano anaposema kwamba "ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga" (1Kor 8:1). Ndiyo kusema kwamba wengine wanaamini kuwa ni wakubwa kwa sababu wanajua zaidi kuliko wengine, na wanafanya bidii kudai mambo kutoka kwao na kuwadhibiti, wakati kile kinachotufanya kuwa kweli wakubwa ni upendo unaowaelewa, kuwatunza na kuwategemeza walio dhaifu. Katika aya nyingine analitumia ili kuwalaumu wale ambao "wanajivuna" (rej. 1Kor 4:18), lakini kiukweli wanayo maneno tu kuliko "nguvu" ya kweli ya Roho (rej. 1Kor 4:19).

98. Ni muhimu wakristo waishi kwa msimamo huo katika namna yao ya kuwatendea ndugu zao wasio na imani thabiti, au walio dhaifu au hawana uhakika katika fikra zao. Mara nyingine lililo kinyume linatokea: wale ambao, ndani ya familia yao, inadhaniwa kwamba wamekua zaidi, wanageuka kuwa watu wenye kiburi na wasiostahimilika. Moyo wa unyenyekevu unaonekana hapa kama sehemu ya upendo, kwa sababu ili mtu aweze kuwaelewa, kuwasamehe na kuwatumikia wengine kutoka moyoni, anapaswa kuponya kiburi na kusitawisha unyenyekevu. Yesu alikuwa akiwakumbusha wanafunzi wake kwamba katika ulimwengu wa ukuu na mamlaka kila mmoja anajitahidi kuwatawala wengine, na ndiyo maana anawaambia: "Haitakuwa hivyo kwenu" (Mt 20:26). Mantiki ya upendo wa kikristo si ile ya mwenye kujisikia mkubwa kuliko wengine na anahitaji kuwaonjesha uzito wa mamlaka yake, bali ni ile ambayo kwayo "mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu" (Mt 20:27). Katika maisha ya kifamilia haiwezi kumiliki mantiki ya utawala wa mmoja juu ya mwingine, wala mashindano ili kuona ni nani aliye na akili zaidi au mwenye nguvu, kwani mantiki hiyo hufutilia mbali upendo. Pia kuhusu familia lina nguvu himizo hili: "Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema" (1Pet 5:5).

Adabu

99. Kupenda maana yake kutaka kupendeza pia, na hapo ndipo neno askemonei linapopata maana yake. Linataka kuonyesha kwamba upendo hautendi kwa ufidhuli, haukosi kuwa na heshima, sio mkali wa tabia. Matendo yake, maneno yake, ishara zake vina neema, wala si vyenye kuchubua au ugumu. Huchukia kuwaumiza wengine. Uungwana "ni shule ya kuheshimu hisia za wengine na ya kutotafuta faida ya binafsi" inayomdai mtu "achunge mawazo yake na hisia zake, ajifunze kusikiliza, kunena na – wakati mwingine – kunyamaza".[107] Tabia ya kupendeza si mtindo ambao mkristo aweza kuchagua au kukataa: ni sehemu ya masharti yasiyoepukika ya upendo, kwa sababu "kila mwanadamu anapaswa kuwa na adabu mbele ya wale wanaomzunguka".[108] Kila siku, “kuyaingilia maisha ya mwingine, hata kama yeye ni sehemu ya maisha yetu, kunahitaji msimamo mpole na mvumilivu, unaompa upya daima imani na heshima. [...] Na upendo, kwa kadiri unavyozidi kuwa wa ndani na wa kina, kwa kadiri hiyohiyo huzidi kudai kuheshimu uhuru wa mwingine na kuweza kusubiri hadi mwingine atakapofungua mlango wa moyo wake".[109]

100. Ili kujiandaa kukutana na mwingine katika ukweli, inatakiwa kuwa na mtazamo mpendevu juu yake. Jambo hilo halitawezekana iwapo inatawala tabia ya kukosa rajua, inayosisitiza makasoro na makosa ya mwingine, kana kwamba mtu ataka kufidia hisia zake za kuonewa. Mtazamo mpendevu unatuwezesha kutobaki sana kutazama mapungufu wa mwingine, na hivyo tunaweza kumvumilia na kuungana naye katika mradi wa pamoja, hata kama tuko tofauti. Upendo mpendevu unazalisha vifungo, unasitawisha miungano, unaunda mitandao mipya ya mtangamano, unajenga mfumo thabiti wa kijamii. Kwa namna hiyo unajilinda, kwa sababu bila kujisikia kuwa wa mwingine mtu hawezi kustahimili hali ya kujitolea kwa wengine, na hatima ya kila mmoja ni kutafuta tu maslahi yake binafsi, na kuishi pamoja kunakuwa jambo lisilo na uwezekano. Mtu anayechukia jumuiya anaamini kwamba wengine wapo kwa ajili ya kutimiza mahitaji yake, na kwamba wanapofanya hivyo ndipo wautimiza wajibu wao tu. Kwa hiyo hakuna nafasi kwa upendevu wa upendo na wa misamiati yake. Mwenye kupenda anaweza kutamka maneno ya kutia moyo, yenye kutuliza, yanayotia nguvu, yenye kufariji na kuhimiza. Tutazame, kwa mfano, maneno machache ambayo Yesu alikuwa akiwaambia watu: "Jipe moyo mkuu, mwanangu!" (Mt 9:2). “Imani yako ni kubwa!” (Mt 15:28). "Inuka!" (Mk 5:41). "Enenda zako kwa amani" (Lk 7:50). "Msiogope" (Mt 14:27). Hayo si maneno yanayodhalilisha au kuhuzunisha, yanayofadhaisha au yenye kudharau. Katika familia inatakiwa kujifunza lugha hii pendevu ya Yesu.

Kujibandua na ubinafsi kwa ukarimu

101. Tumewahi kusema mara nyingi kwamba tukitaka kuwapenda wengine inabidi kwanza kujipenda wenyewe. Lakini, utenzi huu wa upendo unatamka kwamba upendo "hautafuti mambo yake", au kwamba "hautafuti maslahi yake". Usemi huo unatumika pia katika sehemu nyingine: "Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine" (Flp 2:4). Mbele ya kauli hiyo ya Maandiko iliyo wazi namna hii, ni lazima tusiweke kipaumbele katika kujipenda wenyewe kana kwamba ni jambo bora kuliko tendo la kujitolea kwa wengine. Kwa namna fulani tu kuweka kipaumbele katika kujipenda ni sawa ikiwa kunaeleweka kama hali ya kisaikolojia tu, kwa maana ya kwamba asiyeweza kujipenda anaona ugumu kuwapenda wengine. "Aliye mbaya kwa nafsi yake, atakuwa mwema kwa nani? […] Hakuna mbaya zaidi kuliko yeye anayejihusudu mwenyewe" (YbS 14:5-6).

102. Lakini Tomaso wa Akwino mwenyewe alieleza kwamba “ni sifa maalumu ya mapendo kutaka zaidi kupenda kuliko kupendwa”[110] na kwamba, katika hali halisi, “kina mama, ambao ni wale wanaopenda zaidi, wanatafuta zaidi kupenda kuliko kupendwa”.[111] Kwa hiyo upendo unaweza kuvuka mipaka ya haki na kufurika bure, “bila kutumaini kupata malipo” (Lk 6:35), hadi kufikia kilele cha upendo, ambao ni “kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengine” (taz. Yn 15:13). Je, ukarimu huu unawezekana bado, unaofanya tutoe bila kutumaini kupata malipo, na kutoa mpaka mwisho? Bila shaka unawezekana, kwa sababu ndicho Injili inachodai: "Mmepata bure, toeni bure" (Mt 10:8).

Bila ukatili wa ndani

103. Ikiwa neno la kwanza la utenzi lilitualika kuwa na uvumilivu ule usiorejesha kwa hasira mbele ya udhaifu au makosa ya wengine, sasa linaonekana neno jingine – paroksinetai – linaloelekeza rejesho la ndani la uchungu linalosababishwa na tukio fulani la nje. Ni suala la ukatili wa ndani, la hali ya kuchukizwa isiyodhihirika ambayo inatufanya tuwe na hisia ya kujihami mbele ya wengine, kana kwamba watu ni maadui wachokozi ambao ni lazima kuepukana nao. Kulisha ujeuri huo wa ndani haikusaidii kitu. Kunatudhoofisha, na hatima yake ni kututenga na wengine. Uchungu ni mzuri pale ambapo unatusukuma kutenda lolote dhidi ya uonevu mkubwa, lakini ni hasara ukiathiri kila namna yetu ya kuhusiana na wengine.

104. Injili inatualika kuangalia kwanza boriti iliyo ndani ya jicho letu (taz. Mt 7:5), na kama wakristo hatuwezi kusahau kuwa Neno la Mungu mara nyingi linatualika kutochochea hasira: "Usishindwe na ubaya" (Rum 12:21). "Tena tusichoke katika kutenda mema" (Gal 6:9). Kitu kimoja ni kuhisi nguvu ya ujeuri unaotaka kujitokeza, na kitu kingine ni kuukubali, kuruhusu ukawe msimamo wa daima. "Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka" (Efe 4:26). Ndiyo sababu, haitakiwi kuacha iishe bila kuleta amani katika familia. "Na nilete amani kwa namna gani? Kwa kupiga magoti? Hapana! Tendo dogo tu, kitu kidogo hivi, na amani inarudi katika familia. Inatosha busu moja, si lazoma kusema neno. Lakini siku isiishe kamwe bila kuleta amani katika familia!"[112] Kishindo cha ndani mbele ya usumbufu uliosababishwa na wengine kingetakiwa kuwa hasa kubariki moyoni, kutamani wema wa mwingine, kumwomba Mungu amwokoe na kumponya: "Mwe watu wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa na Mungu ili mrithi baraka" (1Pet 3:9). Tukitakiwa kushindana na uovu, tushindane, lakini kwa kusema daima "hapana" mbele ya ukatili wa ndani.

Msamaha

105. Tunaporuhusu hisia mbaya ipenye nafsini mwetu, tunatoa nafasi kwa chuki ile kuvimba moyoni. Maneno logizetai to kakon, maana yake ni "kuhesabu mabaya", "kuendelea kuyakumbuka", yaani kutunza chuki. Kinyume chake ni msamaha. Msamaha wenye msingi katika msimamo chanya, unaojaribu kuelewa udhaifu wa wengine na kutafuta udhuru kwa mtu mwingine, kama vile Yesu alivyosema: "Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo" (Lk 23:34). Lakini mara nyingi mwelekeo ni ule wa kutafuta zaidi na zaidi hatia [za mwingine], kuwaza zaidi mambo maovu, kudhania kila namna ya nia mbaya, na kwa namna hiyo chuki inaongezeka na kutia mizizi. Hivyo, kosa au kwazo lolote la mwenzi wa ndoa laweza kudhuru kifungo cha upendo na uthabiti wa familia. Shida ni kwamba mara nyingine mtu anahesabu kila jambo kuwa na uzito sawa, kwa hatari ya kuwa mkatili mbele ya kosa lolote la mwenzie. Jitihada iliyo halali ya mtu ya kudai haki zake inageuka kuwa uchu wa daima na wa kudumu wa kulipa kisasi kuliko kuwa utetezi mzuri wa hadhi ya mtu.

106. Baada ya kudharauliwa au kutahayarika, tendo la kusamehe linawezekana na linatamaniwa; lakini hakuna asemaye kwamba li rahisi. Ukweli ni kwamba "umoja katika familia unaweza kuhifadhiwa na kukamilishwa tu kwa moyo mkuu wa kujisadaka. Maana, unadai kwa wote na kwa kila mmoja utayari mwepesi na mkarimu kwa maelewano, stahamala, msamaha na upatanisho. Hakuna familia yoyote ambayo haijui kwamba ubinafsi, mabishano, mivutano, magomvi hushambulia vikali na mara nyingine huupiga hadi kuufisha umoja wake: namna nyingi na mbalimbali za mafarakano katika maisha ya kifamilia zinatokana na haya".[113]

107. Leo tunajua kwamba ili tuweze kusamehe tunahitaji kufanya kwanza mang'amuzi yanayotuweka huru ya kujielewa na kujisamehe sisi wenyewe. Mara nyingi makosa yetu, au mtazamo mkali wa watu tunaowapenda, vimetuondolea nia ya kujiheshimu. Na hilo linatuongoza hatimaye kusita kuwakaribia wengine, kukimbia upendo, kujaa hofu katika mahusiano na watu wengine. Na hivyo, kuwahukumu wengine kunageuka kuwa tulizo la uongo. Tunahitaji kusali pamoja na historia ya maisha yetu, kujipokea jinsi tulivyo, kujua kuishi pamoja na makasoro yetu, pia kujisamehe, ili kuweza kuwa na msimamo huohuo juu ya wengine.

108. Lakini kinachotakiwa kabla ya hayo ni mang'amuzi ya kuwa tumesamehewa na Mungu, kuhesabiwa haki bure wala si kwa mastahili yetu. Tumefikiwa na upendo unaokuja kabla ya kila tendo letu, unaotoa daima fursa mpya, unaohimiza na kuendeleza. Tukikubali kwamba upendo wa Mungu hauna masharti, kwamba mahaba ya Baba hayanunuliwi wala kulipwa, hapo basi tutaweza kupenda upeo, kuwasamehe wengine hata pale watakapokuwa wametutendea bila haki. La sivyo, maisha yetu katika familia hayatakuwa tena nafasi ya kuelewana, kusindikizana na kuhimizana, bali yatakuwa tu kiwanja cha mizozo ya sikuzote na ya kupeana adhabu.

Kufurahi pamoja na wengine

109. Maneno hairei epi ti adikia yanamaanisha chochote kiovu kilichomo mtimani mwa moyo wa mtu. Ni msimamo wenye sumu wa mtu anayefurahi anapoona kwamba wengine wanatendewa pasipo haki. Sentensi hiyo inakamilishwa na maneno yanayofuata, yanayoelezea kwa jinsi chanya: sinhairei ti alithia: hufurahi pamoja na kweli. Yaani, hufurahi mwingine anapopata mema, inapotambuliwa hadhi yake, unapothaminiwa uwezo wake na matendo yake mema. Kufanya hivyo haiwezekani kwa mtu anayetaka daima kujilinganisha na kushindana na wengine, hata na mwenzi wake wa ndoa, kiasi cha kufurahi moyoni kila wanaposhindwa.

110. Kila mara mtu anayempenda mwingine anapoweza kumtendea mema, au anapoona kwamba kwake yule mwingine mambo yote ni salama, na anafurahi kwa hayo na kwa namna hiyo anamtukuza Mungu, kwani "Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo ya ukunjufu" (2Kor 9:7), basi, Bwana wetu anapendezwa kwa namna ya pekee na yule mtu anayefurahi kwa furaha ya mwingine. Tusipokuza uwezo wetu wa kufurahi kila mara mwingine apatapo mema na tunazingatia hasa mahitaji yetu binafsi tu, tunajihukumia adhabu ya kuishi kwa furaha haba, kwa vile Yesu alivyosema kwamba "Ni heri kutoa kuliko kupokea!" (Mdo 20:35). Familia inapaswa kuwa daima mahali ambamo mmoja akitenda mema yoyote katika maisha, anajua kuwa humo watayasherehekea pamoja naye.

Huvumilia yote

111. Orodha [ya sifa] inatimilizwa kwa maneno manne yanayosema ukamilifu: yanafuatwa na neno “yote". Huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Kwa namna hiyo, unasisitizwa kwa nguvu uwezo wa upendo kama utamaduni kinzani, uwezao kukabili chochote kinachoutishia.

112. Kwanza hutamkwa kwamba upendo "huvumilia yote" (panta stegi). Ni tofauti na usemi "hauhesabu mabaya", kwa sababu neno hili linahusiana na matumizi ya ulimi; laweza kumaanisha pia "kuutunza ukimya" juu ya mabaya yanayoweza kuwepo katika mtu mwingine. Pia linadokeza nia ya kupunguza kuhukumu, kuzuia mwelekeo wa kulaumu kwa hasira kali na isiyo na huruma. "Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa" (Lk 6:37). Ingawa linakwenda kinyume na matumizi yetu ya kawaida ya ulimi, Neno la Mungu linatuagiza: "Ndugu, msisingiziane" (Yak 4:11). Kukazia kuchafua sifa ya mwingine ni namna ya kujitukuza mwenyewe, ya kumtupia hasira na husuda zote bila kujali madhara tunayosababisha. Mara nyingi tunasahau kwamba kusengenya huweza kuwa dhambi kubwa, na kosa zito mbele ya Mungu, pale kunapoathiri vibaya sifa ya wengine na kuwaletea madhara ambayo ni vigumu sana kuyaondoa baadaye. Ndiyo sababu Neno la Mungu ni kali kiasi gani kuhusu ulimi, hadi kuusema kwamba ni "ulimwengu wa uovu" ambao "ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile" (Yak 3:6), "ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti" (Yak 3:8). Na iwapo "kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu" (Yak 3:9), upendo huitunza sifa ya wengine, kwa ujazo wa uangalifu unaoweza kulinda hata sifa njema ya walio adui. Katika kutetea sheria ya Mungu tunapaswa tusisahau kamwe sharti hili la upendo.

113. Wanandoa wanaopendana na kuwa kila mmoja mali ya mwenzake, husema mema juu ya mwingine, hujaribu kuonyesha sura njema ya mwenzi wa ndoa, licha ya udhaifu wake na makosa yake. Kwa vyovyote, hutunza ukimya ili wasiidhuru sifa yake. Lakini si suala la tendo la nje, bali latokana na msimamo wa ndani. Wala si ujinga wa mtu anayedai kutokuona magumu na mapungufu wa mwingine, bali ni mtazamo mpana wa mwenye uwezo wa kuweka mapungufu na makosa yale katika muktadha wake, mwenye kukumbuka kwamba makasoro hayo ni sehemu tu, wala si ujumla wa nafsi ya mwingine. Kasoro moja katika uhusiano fulani si ujumla wa uhusiano ule. Kwa hiyo twaweza kukubali kwa urahisi kwamba sote ni ambatano changamani la mianga na vivuli. Mwenzangu si tu yule mwenye kunisumbua. Ni zaidi sana kuliko hilo. Kwa sababu hiyohiyo, siwezi kudai kwamba upendo wake uwe mkamilifu ili nianze kuuthamini. Ananipenda kama alivyo na kama awezavyo, kwa mapungufu yake, lakini upendo wake usipokuwa mkamilifu haimaanishi kwamba si kweli au si halisi. Ni halisi, lakini una mipaka, ni wa duniani. Kwa hiyo, nikidai mno kwake, kwa namna fulani atanifahamisha hilo, kwa sababu hataweza wala hatakubali kujielewa kana kwamba yeye ni kiumbe cha mbinguni, wala hatavumilia kunitumikia katika mahitaji yangu yote. Upendo unadumu pamoja na kutokamilika kwake, huvumilia, na hujua kubaki kimya mbele ya mapungufu wa mwenzi mpendwa.

Unaamini

114. Panta pistevi: "huamini yote". Katika muktadha huu, "imani" hiyo haitakiwi kueleweka kwa maana ya kiteolojia, bali kwa maana ya kawaida ya "kuwa na imani na mtu". Si tu suala la kutokuwa na mashaka kwamba mwingine anaongopa au kudanganya. Imani hii ya msingi inatambua ule mwanga uliowashwa na Mungu unaofichika ndani ya giza, au kinga kinachowaka bado chini ya majivu.

115. Imani hiihii inawezesha kuwepo kwa uhusiano wenye uhuru. Hakuna haja ya kumdhibiti mwenzi, ya kuchungulia kila hatua anakoenda, kwa lengo la kuzuia asitoke mikononi mwetu. Upendo una imani, unaacha huru, hautaki kudhibiti kila kitu, kukamata, kutawala. Uhuru huo, unaowezekanisha kuwepo kwa kila mmoja nafasi ya kujiamulia kwa hiari, kuwa wazi kwa ulimwengu unaotuzunguka na kwa mang'amuzi mapya, unaruhusu uhusiano kati ya wenzi wa ndoa utajirishwe wala ile isibaki kuwa ndoa ijifungayo ndani bila upeo wa fikra. Kwa namna hiyo, wenzi wa ndoa, kila wanapokutana, waweza kuishi furaha ya kushirikishana yale waliyopokea na kujifunza walipokuwa nje ya duru ya familia. Wakati huohuo unawezekanisha ukweli na uwazi, kwa sababu pale ambapo mmoja ajua kwamba wengine wana imani naye na wanathamini wema wake wa ndani, papo hapo yeye anajionyesha kama alivyo, bila kuficha lolote. Kama mmoja anajua kwamba kila dakika wana mashaka juu yake, kwamba wanamhukumu bila huruma, wanashindwa kumpenda bila kudai lolote, atapendelea kutunza siri zake, kuficha maanguko na udhaifu wake, kujisingizia kuwa tofauti na alivyo. Kinyume chake, familia ambamo imani thabiti na yenye upendo inatawala, na ambamo kila mmoja daima anarudia kuwa na imani na wengine licha ya tukio lolote, inawezesha kuchanua tabia ya kweli ya kila mwanafamilia na inajenga moyo wa kukataa moja kwa moja udanganyifu, uongo na ulaghai.

Hutumaini

116. Panta elpizi: haukati moyo juu ya mustakabali. Kwa kuungana na neno linalotangulia, linadokeza tumaini la yeye ambaye anajua kwamba mwenzie anaweza kubadilika. Unatumaini daima ukomavu uweze kuwepo, kuchanua uzuri kama kwa namna ya ajabu, na kwamba vipaji vya ndani zaidi vya maumbile yake vifunuke siku moja. Si kusema kwamba mambo yote yatabadilika katika maisha haya. Inadokeza kukubali kwamba mambo mengine hayaendi sawa kama mmoja anavyotazamia, lakini kwamba labda Mungu ananyosha yaliyopotoka ya mwingine na kuzalisha mema fulani kutoka kwa maovu ambayo huyo hawezi kushinda katika dunia hii.

117. Hapa linajitokeza tumaini katika maana yake timilifu, kwa sababu linahusisha uhakika wa kuwepo maisha baada ya kifo. Mtu yule, pamoja na udhaifu wake wote, anaitwa kwenye utimilifu wa Mbinguni. Huko, akiisha kugeuzwa kikamilifu na ufufuko wa Kristo, hakutakuwepo tena udhaifu yake, giza lake wala makasoro yake. Kule, nafsi halisi ya mtu huyo itang'aa kwa uwezo wake wote wa wema na uzuri. Aidha, hilo litatuwezesha kumtazama mtu yule, kati ya masumbufu ya dunia hii, kwa mtazamo wa kimbingu, kwenye mwanga wa tumaini, na kusubiri ule utimilifu ambao siku moja ataupokea katika Ufalme wa mbinguni, ingawa kwa sasa hauonekani.

Hustahimili yote

118. Panta ipomeni, maana yake ni kwamba inastahimili kwa roho chanya yote yaliyo kinzani. Inamaanisha kudumu imara katika mazingira yenye uadui. Si tu kuyastahimili mambo machache yanayoleta usumbufu, ila ni msimamo wenye mtazamo mpana zaidi: ni upinzani wa kimkikimkiki na wa kudumu, unaoweza kushinda changamoto yoyote. Ni upendo licha ya yote, hata pale mazingira yanaposhauri kuwa na hisia nyingine. Unaonyesha kiasi cha uhodari thabiti, cha nguvu dhidi ya mkondo wowote wa ubaya, chaguo la wema ambalo hakuna kitu kinachoweza kulipindua. Hayo yananikumbusha maneno ya Martin Luther King, alipokuwa akisisitiza chaguo la upendo wa kindugu hata kati ya madhulumu na madhalilisho mabaya sana. "Mtu anayekuchukia kuliko wote, anacho walau kitu kilicho chema ndani yake; hata taifa linalochukia zaidi, lina chochote chema ndani yake; pia kabila lenye kuchukia zaidi, lina chochote chema ndani yake. Na unapofikia kwenye hatua ya kumtazama usoni kila mwanadamu na kuona sana ndani yake kile ambacho dini inakiita "mfano wa Mungu", ndipo unapoanza kumpenda licha ya yote. Haidhuru anachofanya, wewe unaona ndani yake mfano wa Mungu. Kuna punje ya wema ambayo huwezi kuifutulia mbali kamwe [...]. Namna nyingine ya kumpenda adui wako ndiyo hii: unapopata fursa ya kumshinda adui wako, ndipo wakati wa kuamua usitende hivyo [...]. Unapojiinua kwenye upeo wa upendo, wa uzuri na uwezo wake mkubwa, kitu pekee unachotaka kukishinda ni mifumo miovu. Watu walionaswa na mfumo ule wewe unawapenda, lakini unajaribu kushinda mfumo ule [...]. Kulipa chuki kwa chuki kunakuza tu kuwepo kwa chuki na uovu ulimwenguni. Kama mimi ninakupiga wewe, na wewe unanipiga mimi, nami ninakurudishia pigo nawe unanirudishia pigo, na hivyo kadhalika, ni wazi kuwa tutaendelea bila mwisho. Yaani hatutamaliza kamwe. Kwa upande fulani, mmoja lazima awe na busara walau kidogo, naye ndiye mtu mwenye nguvu. Mtu mwenye nguvu ni mtu awezaye kuvunja mnyororo wa chuki, mnyororo wa uovu [...]. Inapaswa apatikane ambaye anayo imani na maadili ya kutosha ili kuuvunja na kupenyeza kwenye mfumo wenyewe wa ulimwengu kipengere chenye nguvu na uweza cha upendo”.[114]

119. Katika maisha ya kifamilia kuna hitaji ya kusitawisha nguvu hiyo ya upendo, inayowezesha kushindana dhidi ya uovu unaoyatishia. Upendo haukubali kutawaliwa na chuki, na dharau dhidi ya watu, na hamu ya kujeruhi au kulipiza chochote. Lengo la Ukristo, na kwa namna ya pekee katika familia, ni upendo licha ya yote. Inatokea kwamba ninaguswa, kwa mfano, na msimamo wa watu waliolazimishwa kuachana na mwenzi wa ndoa ili kujilinda na ukatili wa kimwili, na hata hivyo, kutokana na mapendo ya kindoa yanayojua kuvuka hisia, wameweza kumtendea mema, ijapokuwa kwa kupitia wengine, katika nafasi za ugonjwa, za mateso au za shida. Hata huo ni upendo licha ya yote.

Kukua katika mapendo ya kindoa

120. Utenzi wa mtakatifu Paulo, tuliouchambua, unatuwezesha kuelekea sasa kwenye mapendo ya kindoa. Hayo ndio upendo unaowaunganisha wanandoa,[115] uliotakatifuzwa, kutajirishwa na kuangazwa na neema ya sakramenti ya ndoa. Ni “muungano wa kimahaba”,[116] wa kiroho na wa kujisadaka, ambao lakini unakusanya ndani yake upole wa urafiki na nyege ya kiashiki, ingawa unaweza kuendelea kuwepo hata wakati ambapo hisia na hamu zitakuwa zimedhoofika. Papa Pius XI alifundisha kuwa upendo wa namna hii unapenya katika kila wajibu wa maisha ya wanandoa na "unashika kama nafasi ya kwanza katika ubora".[117] Kwani, huo upendo thabiti, uliomiminwa na Roho Mtakatifu, ni kioo cha Agano lisilovunjika baina ya Kristo na wanadamu, lililotimilika katika kujitoa mpaka mwisho, juu ya msalaba: "Roho, ambaye Bwana anamimina, analeta kipaji cha moyo mpya na anawafanya mwanamume na mwanamke waweze kupendana kama Kristo alivyotupenda. Upendo kati ya wanandoa unafikia ule utimilifu ambao ndio shabaha yake ya ndani, yaani mapendo ya kindoa".[118]

121. Ndoa ni ishara yenye thamani, kwa sababu "kila mara mwanamume na mwanamke wanaadhimisha sakramenti ya Ndoa, ni kana kwamba Mungu ‘angejiakisi’ ndani yao, inachora ndani yao sura yake na tabia isiyofutika ya upendo wake. Ndoa ni ikona ya upendo wa Mungu kwetu. Maana, pia Mungu ni ushirika: nafsi tatu ya Baba, ya Mwana na ya Roho Mtakatifu huishi tangu milele na hata milele katika umoja kamili. Nalo ndilo fumbo la Ndoa: Mungu anawafanya wanandoa wale wawili wawe ni umoja wa maisha".[119] Hilo lina matokeo yanayoonekana katika maisha ya kila siku, kwa sababu wanandoa, “kwa nguvu ya Sakramenti, wanakabidhiwa utume halisi na maalumu, ili weweze kuonyesha, kutokana na mambo ya kawaida na rahisi, ule upendo ambao Kristo amelipenda Kanisa lake, akiendelea kutoa uhai wake kwa ajili yake”.[120]

122. Lakini, si vema kuchanganya mambo ya viwango tofauti: haitakiwi kuwabebesha watu wawili wenye udhaifu mzigo unaotisha wa kulazimika kunakili umoja kamili uliopo baina ya Kristo na Kanisa lake, kwani ndoa kama ishara inajumuisha pia "safari ya maisha ambayo inaendelea, hatua kwa hatua, katika kujaliwa na kupokea zaidi na zaidi karama za Mungu".[121]

Kwa maisha yote, mambo yote katika umoja

123. Baada ya upendo unaotuunganisha na Mungu, upendo kati ya wanandoa ni "aina ya urafiki iliyo kubwa kuliko zote".[122] Ni muungano wenye sifa zote za urafiki mwema: kutafuta mema ya mwingine, kutendeana kwa usawa, ukaribu sana, tulizo, udumifu, na mfanano kati ya rafiki unaojengeka katika kushiriki maisha ya pamoja. Lakini ndoa inaongeza juu ya hayo yote umoja usiochanganyikana na wengine na usiovunjika, unaojionyesha katika mpango thabiti wa kushiriki na kujenga pamoja maisha yote. Tuwe wakweli na tutambue ishara ya hali halisi: anayemchumbia mtu hapangi kwamba uhusiano huo uweze kudumu kwa muda tu, anayeishi kwa ari furaha ya kufunga ndoa haidhanii itakuwa jambo la kupita; wanaosindikiza adhimisho la muungano uliojaa upendo, ijapo dhaifu, watumai uweze kudumu sikuzote; watoto si tu wanatamani wazazi wao wapendane, lakini pia wawe waaminifu na wadumu umoja daima. Ishara hizi, na nyingine pia, zinaonyesha kwamba upo katika maumbile yenyewe ya upendo wa kindoa utayari wa kuutambua kuwa ndio jambo la daima. Muungano unaothibitishwa kwa ahadi ya daima ya ndoa, ni zaidi ya utaratibu wa kijamii au mapokeo, kwa sababu mizizi yake imo katika maelekeo ya dhati ya binadamu; na, kwa waamini, ni agano mbele ya Mungu linalodai uaminifu: "Bwana amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako: […] mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana. Maana mimi nakuchukia kuachana" (Mal 2:14,15,16).

124. Upendo ulio dhaifu au mlegevu, usioweza kupokea ndoa kama changamoto inayohitaji wanandoa wawe tayari kupambana na magumu, kuhuishwa tena na tena, kujibuni na kuanza upya daima hadi kifo, hauwezi kustahimili juhudi za hali ya juu. Unashindwa na utamaduni wa yaliyo ya muda tu, unaozuia mchakato endelevu wa ukuzi. Lakini "kuahidi upendo wa daima kunawezekana pale unapovumbuliwa mpango ulio mkuu zaidi kuliko miradi yetu binafsi, unaotutegemeza na kutuwezesha kutoa maisha yetu yote ya mbeleni kwa yule tunayempenda".[123] Ili upendo wa namna hiyo uweze kushinda majaribu yote na kudumu kuwa mwaminifu licha ya yote, inatakiwa iombwe zawadi ya neema yenye kuuimarisha na kuuinua. Kama alivyosema mtakatifu Roberto Belarmino, "tukio la kwamba mwanamume na mwanamke wanaungana na mwenzi mmoja tu kwa kifungo kisichovunjika, kwa namna ambavyo hawataweza kutengana, licha ya magumu yoyote yatakayojitokeza, na hata likipotea tumaini la kupata watoto, jambo hilo haliwezi kutokea pasipo fumbo kubwa".[124]

125. Aidha, ndoa ni urafiki wenye sifa zile zilizo maalumu za tamaa, lakini inayoelekea daima kwenye muungano ulio zaidi na zaidi thabiti na wenye mhemuko. Kwani ndoa “haikuwekwa kwa ajili ya uzazi tu”, lakini pia ili upendo wa mmoja kwa mwenzie “uwe na madhihirisho yake ya haki, usitawi na kufikia kwenye ukomavu”[125]. Urafiki huo wa pekee kati ya mwanamume na mwanamke unapata tabia ya kujumuisha yote ambayo ni maalumu katika muungano wa wanandoa. Na kwa vile muungano huo unajumuisha yote, ndiyo sababu ni pia wa mwenzi mmoja, una uaminifu na uko wazi kupokea watoto. Kwao, kila kitu ni cha kushirikishana, ikiwa ni pamoja na ujinsia, daima katika kuheshimiana. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ulisisitiza jambo hilo kwa kusema kwamba "upendo wa namna hiyo, unaounganisha pamoja tunu za kibinadamu na za kimungu, huwaongoza wanandoa kujitoa kwa hiari kila mmoja kwa mwenzie; kadhalika, unathibitishwa na hisia na vitendo vya upendo mtamu na kupenya vipengele vyote vya maisha ya wanandoa".[126]

Furaha na uzuri

126. Katika ndoa ni vema kusitawisha furaha ya upendo. Pale ambapo kusaka ashiki kunashikilia kila tamaa, kunawafunga wanandoa katika uwanja mmoja tu wala hakuruhusu kuona namna nyingine za ridhaa. Kinyume chake, furaha inapanua uwezo wa kustarehe na inaruhusu kuyafurahia mambo mbalimbali, hata katika awamu za maisha ambapo ashiki hufifia. Ndiyo sababu mtakatifu Tomaso alisema kwamba neno "furaha" latumika ili kuelezea kuongeza kwa kimo cha moyo.[127] Furaha ya ndoa, inayoweza kung'amuliwa hata katika mateso, inajumuisha pia kukubali kwamba ndoa lazima iwe ni mseto wa furaha na uchungu, wa mivutano na utulivu, wa mateso na uhuru, wa kuridhika na kutafuta, wa masumbufu na matulizo, daima katika mwendo wa urafiki, unaosukuma kila mwanandoa kumtunza mwenzake: "wakisaidiana na kutumikiana".[128]

127. Upendo wa kirafiki unaitwa "mapendo" pale ambapo panahisiwa na kuheshimiwa "thamani kuu" ya mwingine.[129] Uzuri, yaani “thamani kuu” ya mwingine ambayo si moja kwa moja vivutio vya mwili wake au vya saikolojia yake, unatuwezesha kuonja utakatifu wa nafsi yake bila hitaji la nguvu la kummiliki. Katika jamii ya ulaji hisia ya ujumi hudhoofika na hivyo furaha huzimika. Kila kitu kipo ili kinunuliwe, kimilikiwe na kuliwa; hata watu. Kinyume chake, urafiki mwanana ni dhihirisho la upendo huo unaojinasua na tamaa ya kiumimi ya kumiliki kila kitu kibinafsi. Unatusukuma kuhamanika mbele ya mtu kwa heshima kuu na kwa hofu fulani ya kumdhuru au ya kumwibia uhuru wake. Upendo kwa mwenzio unajumuisha pia faraja hii ya kutazama na kupendezewa na kila chema na kitakatifu cha nafsi yake, ambayo ipo licha ya ujumla wa kumhitaji kwangu. Hayo yananiwezesha kutafuta mema kwa ajili yake pia ninapojua kwamba hawezi kuwa wangu, au mwili wake utakapokuwa haupendezi tena, au yeye amekuwa mkali au msumbufu. Kwa hiyo, "kutokana na upendo ambao kwao mmoja anapendezwa na mwingine, unategemea ukweli wa kwamba atampatia chochote kwa bure".[130]

128. Mang'amuzi ya kiujumi ya upendo yanadhihirika katika mtazamo ule unaomwangalia mwingine kwa heshima, kama mwenye kikomo katika yeye mwenyewe, hata endapo yu mgonjwa, mzee au hana tena mivutio ya kihisia. Mtazamo unaoweza kuthamini una umuhimu mkubwa sana, na, kwa kawaida, kuupunguza unaleta madhara. Wanandoa na watoto wao mara nyingine wanafanya mambo mangapi ili kutazamwa na kuhesabiwa kwamba wapo! Majeraha mengi na migogoro mingi asili yake ndiyo pale tunapoacha kutazamana kwa heshima. Hilo ndilo jambo ambalo manung'uniko na malalamiko mengine yanayosikika katika familia yanalitokeza. "Mume wangu haniangalii, mimi kwake ni kama mtu asiyeonekana". "Tafadhali, uniangalie ninapoongea nawe". "Mke wangu haniangalii tena, sasa macho yake ni kwa watoto tu". "Nyumbani hakuna anayenijali, wala hawanioni, ni kama mimi singalikuwepo". Upendo huyafumbua macho na kutuwezesha kuona thamani ya binadamu, licha ya yote.

129. Furaha ya upendo wa namna hii uwezao kutazama inapaswa kusitawishwa. Kwa vile sisi tulivyoumbwa ili kupenda, tunajua kwamba hakuna furaha iliyo kubwa zaidi kuliko kushirikishana mema: "Toa na kupokea, na ujiburudishe roho yako" (YbS 14:16). Furaha kali zaidi katika maisha zinatokea pale ambapo mtu anaweza kusababisha furaha kwa wengine, kama malimbuko ya Mbinguni. Inafaa kukumbusha onyesho lile zuri la filamu "Karamu ya Babette", ambamo yeye mpishi mkarimu anakumbatiwa kwa nia ya kumshukuru na kumsifu: "Utawapendeza namna gani hata malaika!". Ni tamu na yenye kuleta faraja ile furaha inayotokana na kuwapatia wengine tulizo, kuwaona wanafurahi. Furaha hiyo, tunda la upendo wa kindugu, si ile ya majisifu ya mwenye kujitazama yeye tu, bali ni ile ya mwenye kupenda na kufurahia mema ya mpendwa, unaoelekea mwenzi na unakuwa wenye kuzaa matunda ndani yake.

130. Kwa upande mwingine, furaha hufanywa upya katika huzuni. Kama alivyosema mtakatifu Augustino, "kadiri ilivyokuwa kubwa hatari ya mapigano, ndivyo inavyokuwa kubwa furaha ya ushindi".[131] Baada ya kuteseka na kushindana kwa pamoja, wenzi wa ndoa wanaweza kung'amua kwamba ilikuwa muhimu kufanya hivyo, kwa sababu wamejipatia chochote kilicho chema, wamejifunza chochote kwa pamoja, au kwa sababu wanaweza kufurahia zaidi kile ambacho tayari wanacho. Kuna furaha chache za kibinadamu ambazo ni za kina na heri kama pale ambapo watu wawili wanaopendana wamefanikisha kwa pamoja kitu ambacho kilihitaji juhudi kubwa ya kushirikishana.

Kufunga ndoa kwa upendo

131. Ninataka kuwaambia vijana kwamba hakuna lolote la hayo linalohatarishwa iwapo upendo unachukua taratibu za taasisi ya ndoa. Muungano unapata katika taasisi hiyo namna ya kuwa na dira kwa uthabiti wake na kwa ukuzi halisi na kweli. Ni kweli kwamba upendo ni zaidi kuliko ukubaliano wa nje au kuliko aina fulani ya mkataba wa ndoa, lakini vilevile ni kweli kwamba uamuzi wa kuipa ndoa muundo unaoonekana katika jamii, ambao una wajibu maalumu, unadhihirisha umuhimu wake: unaonyesha umakini wa kujitambua kitu kimoja na mwenzi, unaashiria kuachana na ile tabia ya ubinafsi wa ujanani, na kuelezea uamuzi mkataa wa kuwa kila mmoja mali ya mwenzie. Kufunga ndoa ni namna ya kuonyesha wazi kwamba kweli mtu ameacha kiota cha wazazi ili kufunga mahusiano mengine thabiti na kushika wajibu mpya mbele ya mtu mwingine. Hilo lina thamani kubwa zaidi kuliko ushirikiano tu wa hiari kwa ajili ya kupendezana, ambao ungekuwa ubinafsishaji wa ndoa. Ndoa kama taasisi ya kijamii ni ulinzi na chombo kwa ajili ya ahadi waliyopeana, kwa kukomaza upendo, ili uamuzi kwa mwingine ukue katika uthabiti, ukweli na kina, na wakati huohuo ili uweze kutimiza utume wake katika jamii. Ndiyo sababu ndoa unashinda kila mtindo wa mpito na inadumu. Uwamo wake unatokana moja kwa moja na maumbile yenyewe ya binadamu na tabia yake ya kijamii. Ndoa inajumuisha masharti kadhaa, yanayotokana lakini na upendo wenyewe, na upendo ulioamua kabisa na unataka kujitolea na unaweza kukabiliana na changamoto za mbeleni.

132. Kuchagua ndoa kwa namna hiyo kunaonyesha uamuzi halisi na kweli wa kufanya kwamba njia mbili zigeuke kuwa njia moja tu, liwalo na liwe na licha ya changamoto yoyote. Kutokana na ukweli wa ahadi hiyo ya hadharani ya kupendana, uamuzi huo hauwezi kuwa wa haraka, lakini kwa sababu hiyohiyo hauwezi kuahirishwa bila mwisho. Kuweka ahadi ya kuishi na mwenzi mmoja kwa namna ya kudumu kuna daima kiwango cha hatari na cha kamari hodari. Kukataa kufanya uamuzi huo kunaonyesha tabia ya ubinafsi, yenye kutafuta maslahi yake tu, finyu, ya mtu asiyeweza kutambua haki za mwenzie wala hafikii kamwe kwenye hatua ya kumtambulisha kwa jamii kama anayestahili kupendwa bila mwisho. Kwa upande mwingine, wale ambao wanachumbiana kwelikweli, wanataka kwamba upendo wao ujulikane kwa wengine. Upendo unaokuwa thabiti katika ndoa ifungwayo mbele ya watu, pamoja na masharti yote yanayotokana na kujifunga kwa taasisi hiyo, ni dhihirisho na ulinzi wa ile "ndiyo" inayotamkwa kwa hiari na bila mipaka. Ile "ndiyo" inamaanisha nia ya kumwambia mwenzi kwamba ataweza kuwa daima na imani nami, kwamba hatatelekezwa iwapo atapoteza mvuto, kama atakutwa na magumu, au kama zitapatikana kwangu fursa nyingine za kujipendezesha au maslahi ya kibinafsi.

Upendo unaojidhihirisha na kukua

133. Upendo wa urafiki unaunganisha vipengele vyote vya maisha ya ndoa na kuwasaidia wanafamilia wote kuendelea mbele katika awamu zake zote. Kwa hiyo, vitendo vinavyoonyesha upendo wa namna hiyo vinatakiwa vistawishwe siku kwa siku, bila ubahili, vikiwa vimejaa maneno ya ukarimu. Katika familia "ni lazima kutumia maneno matatu. Ningependa kusisitiza tena. Maneno matatu: tafadhali, asante, samahani. Maneno matatu ya msingi!"[132] Pale ambapo katika familia hakuna mwenye kutiisha na wote wanaomba kwa kusema ‘tafadhali’, pale ambapo katika familia hakuna ubinafsi na wote hujifunza kusema ‘asante’, na kila mara mmojawapo anapogundua kwamba ametenda jambo baya na anajua kusema ‘samahani’, katika familia ile kuna amani na furaha”.[133] Tusiwe wanyimifu katika kutumia maneno hayo, tuwe wepesi katika kuyarudia siku baada ya siku, kwa sababu “kuna namna za ukimya zinazolemea, mara nyingine hata katika familia, baina ya mume na mke, kati ya wazazi na watoto, kati ya ndugu”.[134] Kinyume chake, maneno yanayofaa, ya kusemwa wakati muafaka, yanatunza na kukuza upendo siku baada ya siku.

134. Haya yote yanatekelezwa katika mwendo wa ukuzi endelevu. Aina hii ya pekee ya upendo iliyo ndoa, huitwa kukomazwa siku kwa siku, kwani inatakiwa kutumika kwa ajili yake usemi ambao mtakatifu Tomaso wa Akwino alisema kuhusu mapendo: "Mapendo, kutokana na maumbile yake, hayana kikomo katika ukuzi wake, kwa vile yanavyoshiriki maumbile ya mapendo yale yasiyo na mipaka, yaani ya Roho Mtakatifu. […] Wala hayawezi kutiwa mipaka na mwenye kuwa nayo, kwa sababu kwa njia ya kukua mapendo, hukua zaidi na zaidi pia uwezo wa kuyakuza hata zaidi."[135] Mtakatifu Paulo alihimiza kwa nguvu: "Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote" (1The 3:12); na akaongeza: “Katika habari ya upendano [...] twawasihi, ndugu, mzidi sana” (1The 4:9-10). Zaidi sana. Upendo wa ndoa haulindwi kabla ya yote kwa kutaja tabia yake ya kutokuvunjika kama ya sharti, au kwa kukariri mafundisho fulani, bali kwa kuuimarisha kwa njia ya ukuzi wa daima kwa msukumu wa neema. Upendo usiokua unaanza kuhatarika, na twaweza kukua tu kwa kuiitikia neema ya Mungu kwa njia ya matendo mengi zaidi ya upendo, kwa vitendo vya mahaba vya mara kwa mara, vyenye mhemuko zaidi, vyenye ukarimu zaidi, vya kutuliza zaidi, vyenye uchangamfu zaidi. Mume na mke "wanang'amua maana ya umoja kati yao na wanazidi kuufikia kwa ukamilifu zaidi".[136] Zawadi ya upendo wa Mungu unaowajaza wanandoa ni wakati huohuo mwito wa kuisitawisha daima zawadi hii ya neema.

135. Hazifai njozi nyingine juu ya upendo wa hadithi tamu na ulio kamili, unaonyimwa kwa namna hiyo kila changamoto ya kuukuza. Dhana ya kimbinguni ya upendo wa kidunia husahau kwamba hali iliyo bora ndiyo ile ambayo bado haijafikiwa, ni divai inayoivishwa na miaka. Kama walivyokumbusha Maaskofu wa Chile, "Familia zilizo kamili kama yanavyotuonyesha matangazo ya kibiashara na ya kiulaji hazipo. Kwa familia hizo miaka haipiti, wala hayapo magonjwa, wala huzuni, wala kifo [...]. Matangazo ya kiulaji yanaonyesha ndoto mazingaombwe isiyolingana katu na hali halisi ambayo kina baba na kina mama wa familia zetu wanapaswa kukabiliana nayo siku kwa siku.[137] Ni sahihi zaidi kuyakubali kwa dhana halisi mapungufu, changamoto na makasoro, na kusikiliza miito ya kukua pamoja, ya kukomaza upendo na kusitawisha uthabiti wa muungano, licha ya lolote linaloweza kutokea.

Mazungumzano

136. Mazungumzano ni namna bora na isiyoepukika ya kuishi, kuonyesha na kukomaza upendo katika maisha ya ndoa na ya familia. Lakini yanahitaji uanagenzi mrefu na mzito. Wanaume kwa wanawake, wazee kwa vijana, wana namna tofauti za kuwasiliana, wanatumia misamiati tofauti, wanaishi kadiri ya kanuni nyingine nyingine. Namna ya kuuliza maswali, namna ya kutoa majibu, sauti inayotumika, wakati na mambo mengine mengi yaweza kuathiri mawasiliano. Aidha, daima ni muhimu kuchochea misimamo ambayo inaonyesha upendo na kuwezesha mazungumzano ya kweli.

137. Kujipatia muda, na muda ulio bora, wa kusikiliza kwa uvumilivu na umakini, hadi mwingine amesema yote aliyohitaji kusema. Hayo yanadai mtu afanye bidii ya kutoanza kusema kabla ya wakati mwafaka. Badala ya kuanza kutoa maoni au mashauri, inatakiwa kuhakikisha kuwa tumesikiliza yote ambayo mwingine anahitaji kusema. Hilo linahitaji pia kutunza ukimya wa ndani ili kusikiliza bila kelele moyoni na akilini: kuvua kila haraka, kuweka pembeni mahitaji na vipaumbele vyetu binafsi, na kuwapatia wengine nafasi. Mara nyingi mwenzi hahitaji utatuzi wa matatizo yake, ila tu anachotafuta ni kusikilizwa. Anahitaji kuhisi kwamba uchungu wake umegunduliwa, au kushindwa kwake, au hofu, au hasira, au tumaini lake, au matarajio yake. Lakini mara nyingi husikika malalamiko kama haya: "Hanisikilizi. Inapoonekana kwamba labda ananisikiliza, kwa kweli anawaza kitu kingine". "Ninaongea; lakini ninahisi kwamba anasubiri tu hatimaye nimalize kunena". "Ninapoongea mimi, anajaribu kuanza kuongea kitu kingine, au ananijibu haraka haraka ili kufunga mazungumzo".

138. Kuchochea mazoea ya kumjali kweli mwenzio. Yaani, kuthamini nafsi yake, kutambua kwamba yeye anayo haki ya kuwepo, ya kuwa na mawazo yake, ya kuwa na furaha. Lazima yasipuuzwe yale anayosema au kudai, ingawa inafaa kuelezea mtazamo wako pia. Chini ya dhana hiyo kuna imani ya kwamba kila mmoja anao mchango wake wa kutoa, kwa sababu wote wana mang'amuzi mbalimbali ya maisha, kila mmoja anayaangalia mambo kwa mtazamo mwingine, amegundua wasiwasi tofauti na kuwa na ustadi au uvumbuzi wake. Inawezekana kutambua ukweli wa mwenzio, umuhimu wa kero zake za ndani zaidi na maana ya chinichini ya yale anayoyatamka, hata yakiwa yamefichwa na maneno ya ukali. Kwa sababu hiyo inabidi kujaribu kujiweka katika nafasi yake na kufasiri kina cha moyo wake, kufumbua ni nini kinachompendeza zaidi na kuchukua kitu kile anachokitamani kama chanzo cha kuanzisha na kuendeleza mazungumzano.

139. Upana wa mawazo, kusudi la kutojifungia katika dhana chache kwa hofu isiyotulia, na utayari wa kubadili au kukamilisha maoni yangu: haya ni mambo ya muhimu. Inawezekana kwamba kutokana na mawazo yangu na mawazo ya mwenzangu upatikane usanisi unaotutajirisha wote wawili. Umoja ambao tunahitaji kutarajia si wote kuwa sawa, bali ni "umoja katika utofauti" au "utofauti uliopatanishwa". Katika mtindo huo unaotajirisha ushirika wa kindugu, walio tofauti wanakutana, wanaheshimiana na kuthaminiana, pamoja na kutunza kila mmoja vidokezo na misisitizo yake pekee ambayo inatajirisha manufaa ya wote. Tunahitaji kujiokoa na faradhi ya kudhani kwamba tunapaswa wote kufanana. Pia unatakiwa werevu ili kugundua mapema "kelele" zinazoweza kujipenyeza, zisije zikaharibu mchakato wa mazungumzano. Kwa mfano, ni muhimu kutambua hisia mbaya zinazozuka na kuweza kuzipunguza ili zisiathiri mawasiliano. Ni muhimu kuweza kutamka yale ninayohisi, bila kujeruhi, kutumia lugha na namna ya kuongea ambazo zaweza kupokelewa au kuvumiliwa kwa urahisi zaidi na mwenzangu, ingawa maudhui huenda ni mazito; kueleza malalamiko yangu lakini bila kufoka kwa hasira kama kwa kulipa kisasi, na kuachana kabisa na kutumia lugha ya kudhalilisha inayotafuta tu kushambulia, kuzomea, kulaumu, kuumiza. Magomvi mengi katika jozi yanatokea kwa sababu zisizo nzito sana. Mara nyingine ni mambo madogo, yasiyo na maana sana; lakini kinachoozesha mioyo ni ile namna ya kuyatamka au msimamo ambao kila mmoja anachukua katika mazungumzano.

140. Kuwa na vitendo vya kumjali mwenzio na kumwonyesha mahaba. Upendo hushinda vizuizi vyote, hata vilivyo vikubwa mno. Inapotokea kwamba twampenda mtu au twajisikia kwamba yeye anatupenda, twaweza kuelewa kwa urahisi zaidi anachotaka kusema na kutueleza. Twaweza kushinda udhaifu unaotufanya tuwe na hofu mbele ya mwenzi kana kwamba ni "mshindani" wangu. Ni muhimu sana mtu ajenge msimamo wake thabiti juu ya machaguo yaliyofanywa kwa makini, juu ya imani na tunu, wala si juu ya kushinda katika mjadala mmoja au kwa sababu ataka akukubaliwe kuwa na haki.

141. Hatimaye, tunatambua kwamba ili mazungumzano yawe na mafanikio inatakiwa kuwa na chochote cha kusema, na jambo hilo linahitaji tuwe na utajiri wa ndani unaojilisha kwa kusoma, kutafakari binafsi, kusali na kuwa wazi kwa jamii. Vinginevyo, mazungumzo yanakuwa ya kuchosha na yasiyo na maana. Inapotokea kwamba kila mwenzi wa ndoa hailishi roho yake wala hakuna mahusiano ya namna nyingi na watu wengine, maisha ya kifamilia yanakuwa ya ndoa ijifungayo ndani na mazungumzano yanakuwa hafifu.

Upendo wa tamaa

142. Mtaguso wa Vatikano wa II ulifundisha kwamba upendo huo kati ya wanandoa "unauhusu wema wa mtu mzima. Kwa sababu hiyo, upendo huo unaweza kuzitajirisha hisia za rohoni na matendo yake ya kimwili kwa heshima ya pekee; na pia yaweza kuzitukuza hisia na matendo hayo kama ishara na alama mahsusi za urafiki wa kindoa".[138] Lazima viwepo visa fulani vinavyosababisha kwamba upendo usio na faraja wala tamaa hautoshi ili kuashiria muungano kati ya moyo wa binadamu na Mungu: "Wamistiki wote wamesisitiza kwamba upendo wa kimungu na upendo wa kimbingu unatafuta ishara zake na kuzipata tu katika upendo kati ya wanandoa, kuliko kwenye urafiki, au kuliko hisia ya kimwana, au kuliko kufanya juhudi kwa kusudi maalum. Na sababu yake kwa haki ipo katika utimilifu wake”.[139] Kwa nini, basi, tusichukue muda kusema kuhusu hisia na ujinsia katika ndoa?

Ulimwengu wa mihemuko

143. Hamu, hisia, mihemuko, mambo haya ambayo wasomi wa zamani walikuwa wanaita "tamaa", yanachukua nafasi muhimu katika ndoa. Yanazaliwa pale ambapo "mwingine" anatokea na kujionyesha katika maisha ya mtu. Ni kawaida ya kila kiumbe chenye uhai kuvutwa kwenye kitu kingine, na mvuto huo unaonyesha kila mara ishara za msingi za huba: faraja au huzuni, furaha au uchungu, tulizo au hofu. Haya ni sababu za utendaji wa msingi wa kisaikolojia. Binadamu ni kiumbe hai katika dunia hii na kila anachokifanya na kukitafuta kimejaa tamaa.

144. Yesu, kwa jinsi alivyokuwa binadamu kwelikweli, alikuwa anayaishi mambo yote kwa ujazo wa mihemuko. Ndiyo sababu, alijaa huzuni alipokataliwa na Yerusalemu (rej. Mt 23:37), na hali hiyo ilimsababisha alie machozi (rej. Lk 19:41). Hali kadhalika, yeye alikuwa anaona huruma mbele ya mateso ya watu (rej. Mk 6:34). Alipoona wengine wanalia machozi, yeye aliugua rohoni akafadhaika (rej. Yn 11:33); na Yeye mwenyewe akalia machozi kwa sababu ya kifo cha rafiki (rej. Yn 11:35). Madhihirisho haya ya hisia zake yalionyesha kwa kiasi gani moyo wake ulikuwa wazi kwa wengine.

145. Kupata mhemuko si jambo ambalo kimaadili ni jema au baya kwa lenyewe.[140] Kuanza kuona hamu au chuki si jambo lenye dhambi au la kulaumiwa. Lililo jema au baya ni tendo ambalo mtu analitenda akisukumwa au akiambaa na tamaa fulani. Lakini, ikiwa hisia zinachochewa, zinatafutwa na kwa sababu ya hizo tunatenda matendo maovu, uovu umo katika uamuzi wa kuzichochea na katika matendo maovu yanayotokana nazo. Kwa maana hiyohiyo, kupendezwa na mtu si moja kwa moja jambo jema. Ikiwa kwa kupendezwa naye mimi ninatenda ili mtu yule akawe mtumwa wangu, hisia ile itakuwa kwa ajili ya ubinafsi wangu. Kuamini kwamba sisi ni wema kwa sababu tu "tunahisi kitu fulani" ni kujidanganya vibaya. Kuna watu ambao wanajihisi kuweza kuwa na upendo mkubwa kwa sababu tu wana hitaji kubwa la kupendwa, lakini hawawezi kuipigania furaha ya wengine, nao wanaishi wamejifungia katika tamaa zao. Kwa namna hiyo, hisia zinapeleka mbali na tunu zilizo kuu na zinaficha ndani yake umimi usiowezesha kuyasitawisha maisha katika familia yaliyo mazuri na yenye furaha.

146. Kinyume chake, ikiwa tamaa inaendana na tendo huru, inaweza kudhihirisha kina cha chaguo lile. Upendo wa kindoa unaelekeza kujitahidi ili maisha yote ya kimihemuko yawe jambo jema kwa familia, nayo yaweze kusaidia maisha ya pamoja. Familia unafikia ukomavu pale ambapo maisha ya kimihemuko ya wanafamilia wake yanageuka kuwa tabia yenye kukataa kutawala au kufunika machaguo makuu na tunu, na – kinyume chake – huhakikisha uhuru wake,[141] inayatajirisha, inayapamba na kuyafanya mwanana zaidi kwa mema ya wote.

Mungu anapenda furaha ya watoto wake

147. Hayo yanahitaji mwendo wa kipedagojia, mchakato unaosababisha kiasi fulani cha kujinyima. Hilo ni sehemu ya imani ya Kanisa ambayo mara nyingi haikukubaliwa, kana kwamba i adui ya furaha ya binadamu. Benedikto XVI alipokea swali hilo kwa wazi kabisa: "Kanisa kwa njia ya amri zake na marufuku linayoweka si kwamba pengine linageuza kuwa uchungu kile kitu kizuri kuliko vyote vya maisha? Je, si kwamba huenda limeweka alama za makatazo pale penyewe ambapo furaha, iliyoandaliwa na Muumba kwa ajili yetu, inatupatia faraja inayotuonjesha tayari kitu kilicho cha Kimungu?"[142] Lakini yeye alikuwa akijibu kwamba, ijapo havikukosekana katika Ukristo amri ya kupita kiasi au kujinyima kupotovu, mafundisho rasmi ya Kanisa, yaliyo aminifu kwa Maandiko Matakatifu, hayakukataa “mapenzi kwa yenyewe, lakini yamepiga vita dhidi ya tabia ya kuyaumbua na kuyatia uharibifu, kwani juhudi ya kuyageuza mapenzi kuwa kama miungu ya uongo [...] inayanyima hadhi yake, na kuyafanya kuwa ni kitu kisichomstahili binadamu”.[143]

148. Kulea mihemuko na silika ya mtu ni lazima, na kwa lengo hilo mara nyingine ni lazima kujiwekea mipaka fulani. Kuzidisha kiasi, kukosa kujidhibiti, kufuatilia kwa pupa aina moja tu ya anasa, mwisho wake ni kudhoofisha na kuozesha anasa na tamaa yenyewe,[144] na kuyadhuru maisha ya familia. Kwa kweli inawezekana kutimiza mwendo mzuri na tamaa, maana yake kuzielekeza zaidi na zaidi kwenye mpango wa kujitolea na kujitimiliza unaotajirisha mahusiano ya watu ndani ya familia. Hilo halimaanishi kujikatalia vipindi vya furaha kubwa,[145] lakini kuvipokea katika mfumo wa vipindi vingine vya kujitolea kwa ukarimu, vya tumaini lenye kuvumia, vya uchovu usioepukika, vya juhudi kwa lengo maalumu. Maisha katika familia ndivyo hivyo vyote, nayo yanastahili tuyaishi kwa utimilifu.

149. Kuna madhehebu ya kitasaufi yanayosisitiza umuhimu wa kufuta kila hamu ili kuepukana na huzuni. Lakini sisi tunaamini kwamba Mungu anapenda furaha ya binadamu, na kwamba Yeye ameviumba vitu vyote "ili tuvitumie kwa furaha" (1Tim 6:17). Tuache furaha ifurike mbele ya upendo wake mwanana anapotuambia: "Mwanangu, ujifanyizie mema [...]. Usijinyime siku ya furaha” (YbS 14:11,14). Pia jozi la wanandoa linaitikia mapenzi ya Mungu kwa kufuata mwaliko huu wa Biblia: "Siku ya kufanikiwa ufurahi" (Mhu 7:14). Suala ni kuwa na uhuru wa kukubali kwamba mapenzi yapate namna nyingine ya kujidhihirisha katika nafasi mbalimbali za maisha, kadiri ya mahitaji ya upendo wa kila mmoja kwa mwenzie. Kwa maana hiyo, inawezekana kupokea shauri la walimu wengine wa Mashariki ambao wanasisitiza juu ya kupanua dhamiri, ili kutonaswa katika mazoea yaliyo finyu mno ambayo yangebana matazamio yetu. Kupanua huko kwa dhamiri si kukatalia au kuteketeza hamu, bali ni kutanuliwa na kukamilishwa kwake.

Upendo kama mapenzi

150. Hayo yote yanatuelekeza kutaja maisha ya kimapenzi ya wenzi wa ndoa. Mungu mwenyewe ndiye aliyeumba ujinsia, ambao ni zawadi nzuri ajabu kwa viumbe vyake. Kwa kuyaheshimu na kuachana na kukosa kuyadhibiti, tunazuia isitokee "udhalilishaji wa tunu hiyo halisi".[146] Mtakatifu Yohane Paulo II alifukuzia mbali dhana ya kwamba mafundisho ya Kanisa yanaleta kwenye "kukataa thamani ya ujinsia wa binadamu” au kwamba yanauvumilia tu “kwa hitaji lenyewe ya kuzaa watoto”.[147] Hitaji la kijinsia la wenzi wa ndoa si suala linalodharaulika wala “kwa vyovyote si hoja kulitilia mashaka hitaji hilo”.[148]

151. Kwa wale wanaohofia kwamba kwa njia ya malezi ya tamaa na ujinsia huweza kuhatarishwa uhiari wa upendo wa kujamiiana, mtakatifu Yohane Paulo II alijibu kwamba binadamu "huitwa kufikia uhiari kamilifu na mkomavu wa mahusiano", ambao ni "tunda linalopatikana hatua kwa hatua la upambanuzi wa misukumo ya mioyo ya mtu".[149] Ni kitu kinachopatikana kwa kukipigania, kwa vila kila binadamu “anapaswa kujifunza kwa subira na msimamo maana ya kweli ya mwili”.[150] Ujinsia si mali yenye lengo la kupendezesha au kuburudisha, kwa sababu ni lugha baina ya watu wawili, pale ambapo mwenzi anajali mwenzake, ikiwa ni pamoja na thamani yake takatifu na isiyonyakuliwa. Kwa namna hiyo, "moyo wa binadamu anashiriki, tuseme hivi, uhiari wa mwingine".[151] Katika muktadha huu, mapenzi yanaonekana kuwa dhihirisho la ujinsia lililo maalum kwa binadamu. Ndani yake inawezekana kukuta ile "maana ya kindoa ya mwili, na hadhi halisi ya kuwa zawadi".[152] Katika katekesi zake juu ya teolojia ya mwili wa binadamu, mtakatifu Yohane Paulo II amefundisha kwamba hali ya mwili kuwa na ujinsia “si tu chimbuko la uwezo wa kuzaa matunda na wa uzaaji wa watoto”, bali inao ndani yake “uwezo wa kudhihirisha upendo: yaani, upendo ule ambao kwao mtu-nafsi anakuwa zawadi".[153] Mapenzi yaliyo safi zaidi, ijapo yameungana na hamu ya kutafuta ashiki, inatangulizwa na ushangao, na kwa hiyo yaweza kuzifanya tamaa ziwe za kiutu.

152. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile hatuwezi kufasiri hali ya kimapenzi ya upendo kama uovu ulioruhusiwa au kama mzigo wa kubebwa kwa ajili ya mema ya familia, bali kama zawadi ya Mungu inayotia nakshi kwenye kukutana kwa wenzi wa ndoa. Kwa vile ni tamaa iliyoboreshwa na upendo unaoheshimu hadhi ya mwenzi, inakuwa "dhihirisho kamilifu na angavu la upendo" lenye kutuonyesha jinsi moyo wa binadamu unavyoweza maajabu, na hivyo kwa kitambo "huonjwa kwamba maisha ya binadamu yamekuwa mafanikio".[154]

Ukatili na ulaghai

153. Katika muktadha ya mtazamo huo chanya ya ujinsia, inafaa kulitazama suala hili katika ujumla wake na kwa utambuzi halisi ulio sahihi. Maana, hatuwezi kusahau kwamba mara nyingi ujinsia unatenganishwa na utu, pia unajaa magonjwa, kwa jinsi ya kwamba "unakuwa zaidi na zaidi nafasi na chombo cha kutawaza umimi wa mtu na cha kujiridhisha kibinafsi katika tamaa na mivuto".[155] Katika nyakati hizi imekuwa kubwa ile hatari ya kwamba hata ujinsia unatawaliwa na roho yenye sumu ya "tumia ukatupe”. Mwili wa mwenzi mara nyingi hufanywa kana kwamba ni kitu cha kutwaa hadi hapo unapokuridhisha na cha kutupa hapo unapopoteza mvuto. Itawezekanaje kuzisahau au kuficha zile namna endelevu za kutawala, kuonea, kunyanyasa, za ufasiki na ukatili wa kijinsia, ambazo ndiyo matunda ya ughoshaji wa maana ya ujinsia na ambazo zinafukia hadhi ya wengine na wito wa upendo chini ya hamu ya kigiza ya kusaka ridhaa za binafsi?

154. Si ya ziada kukumbusha kwamba pia katika ndoa ujinsia unaweza kugeuka kuwa asili ya mateso na vurugu. Ndiyo sababu ni lazima tusisitize kwa wazi kwamba "kumshurutisha mwenzi wa ndoa kufanya tendo la ndoa bila kujali hali yake na hamu zake za haki si tendo halisi la upendo na kwa hiyo kunaenda kinyume na madai ya utaratibu wenye haki wa kimaadili mintarafu mahusiano baina ya wenzi wa ndoa."[156] Matendo maalumu ya muungano wa kijinsia wa wenzi wa ndoa yanaendana na maumbile ya ujinsia alivyopanga Mungu ikiwa “yametekelezwa kwa namna iliyo ya kibinadamu kwelikweli”.[157] Ndiyo sababu mtakatifu Paulo alihimiza: "Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili" (1The 4:6). Ingawa yeye aliandika katika zama ambapo ulikuwa ukitawala utamaduni wa kibabe, ambamo mwanamke alihesabiwa mwenye hali ya chini kabisa kulingana na mwanamume, hata hivyo alifundisha kwamba ujinsia ni suala ambalo lahitaji mawasiliano baina ya wenzi wa ndoa: alidokeza uwezekano wa kunyimana kwa muda mahusiano ya kijinsia, lakini "isipokuwa mmepatana" (1Kor 7:5).

155. Mtakatifu Yohane Paulo II alitoa tahadhari ya busara sana aliposema kwamba mwanamume na mwanamke "wanatiishwa na hali ya kutoshiba".[158] Maana yake, wanaitwa kwenye muungano unaokuwa mkubwa zaidi na zaidi, lakini hatari ni kudai kufuta tofauti zilizopo na ule umbali usioepukika uliopo kati ya hao wenzi wawili. Kwa sababu kila mmoja anayo hadhi yake isiyo kifani. Pale ambapo ile hali yenye thamani ya kuwa kila mmoja mali ya mwenzie inageuka kuwa unyanyaso, "muundo wa ushirika katika uhusiano baina ya watu unabadilika kimsingi".[159] Katika mantiki ya kutaka kutawala, pia yule anayetawala mwisho wake ni kukataza hadhi yake mwenyewe[160] na kuachana na “kujitambua kibinafsi kitu kimoja na mwili wake”,[161] kwa kadiri anavyounyima maana yoyote. Anaishi ngono kama kukimbia mbali naye mwenyewe na kama katazo kwa uzuri wa muungano.

156. Ni muhimu kuwa wazi katika kukataa kila namna ya unyanyasaji wa kijinsia. Kwa hiyo inafaa kuepukana na kila aina ya ufasiri usio sahihi wa maneno ya Waraka kwa Waefeso yanayoagiza kwamba “wake watii waume zao” (Efe 5:22). Mtakatifu Paulo hapa anaandika kwa kufuata dhana za kitamaduni zilizo maalum kwa wakati wake, lakini sisi hatupaswi kujivika utamaduni huo, bali kupokea ujumbe uliofunuliwa ndani ya ujumla wa matini hiyo. Tuchukue tena maelezo yenye busara aliyotoa mtakatifu Yohane Paulo II: "Upendo unazuia kila aina ya unyanyasaji, ambao kwao mke angekuwa mtumishi au mtumwa wa mume [...]. Jumuiya au umoja ambao wao wanatakiwa kuunda kwa sababu ya ndoa, unafanyika kwa njia ya kujitoa kila mmoja kama zawadi kwa mwenzie, tendo ambalo ni pia kila mmoja kujiweka chini ya mwenzie".[162] Ndiyo sababu inasemwa pia kwamba “inawapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe” (Efe 5:28). Kihalisi maneno haya ya Biblia yanaalika kushinda ustarehe wa ubinafsi ili kuishi kwa kuwaelekea wengine: "Mnyenyekeane katika kicho cha Kristo" (Efe 5:21). Kati ya wenzi wa ndoa "kunyenyekeana" huku kunapata maana maalumu na kunaeleweka kama uamuzi wa hiari wa kuwa kila mmoja mali ya mwenzie, ikiwa ni pamoja na sifa ya uaminifu, heshima na matunzo. Ujinsia ni kwa namna isiyofutika msaada kwa urafiki wa namna hiyo kati ya wenzi wa ndoa, kwa sababu unaelekea kufanya mwingine aweze kuishi kwa utimilifu.

157. Lakini, kuukataa ughushaji wa ujinsia na mapenzi kusingetakiwa kutuongoza kamwe kuvidharau au kuvipuuzia. Lengo bora la ndoa haliwezi kuelezwa tu kama kujitoa kwa ukarimu na kujisadaka, ambako kila mmoja anajikatalia hitaji lolote la kibinafsi na anajali tu kutenda kwa ajili ya mema ya mwenzie bila ridhaa yoyote kwake binafsi. Inafaa tukumbuke kwamba upendo wa kweli unajua pia kupokea mema kutoka kwa mwingine, unaweza kujitambua kama wenye vidonda na mahitaji, haukatai kupokea kwa shukrani zenye furaha na ukweli vitendo vya kimwili vya upendo katika bembelezo, katika kumbatio, katika busu na katika muungano wa kijinsia. Benedikto XVI alikuwa wazi kuhusu jambo hilo: "Ikiwa binadamu anatarajia kuwa roho tu, na kukataa mwili kama urithi ulio wa kinyama tu, hapo roho na mwili hupoteza hadhi yake".[163] Kwa sababu hiyo “binadamu wala hawezi kuishi katika upendo tu wa kujisadaka na kujishusha. Hawezi daima kutoa zawadi tu, anapaswa pia kupokea zawadi. Anayetaka kutoa upendo, lazima yeye mwenyewe aupokee kama zawadi".[164] Jambo hilo linadai, kwa vyovyote, kwamba tukumbuke kuwa msimamo wa mtu ni dhaifu, kwamba daima kuna chochote kinachokataa kufanywa kuwa cha kiutu na kwamba wakati wowote hicho chaweza kulipuka upya, na kuchukua tena mielekeo yake ya kiasili na kibinafsi zaidi.

Ndoa na ubikira

158. "Watu wengi wanaoishi bila kufunga ndoa sio tu wanajitolea kwa ajili ya familia yao ya asili, lakini pia hutoa huduma nyingi katika duru ya marafiki zao, katika jumuiya ya kikanisa na katika maisha ya kitaaluma. [...] Zaidi ya hayo, wengi wanatumia talanta zao kwa kuitumikia jumuiya ya kikristo katika ishara ya matendo ya huruma na ya kujitolea. Halafu wapo wasiofunga ndoa kwa sababu wanaweka wakfu maisha yao kwa kumpenda Kristo na ndugu zao. Kwa njia ya juhudi zao familia, katika Kanisa na katika jamii, hutajirishwa sana".[165]

159. Kuishi katika ubikira ni aina ya upendo. Kama ishara, unatukumbusha moyo wa kujishughulisha kwa ajili ya Ufalme, utayari wa kujitolea bila mipaka kwa utumishi wa uinjilishaji (rej. 1Kor 7:32), pia ni kioo cha utimilifu wa Mbinguni, ambapo "hawaoi wala hawaolewi" (Mt 22:30). Mtakatifu Paulo aliupendekeza sana kwa sababu alikuwa akitazamia kuwa Yesu atarudi mara na alitaka wote wapate kuwa makini juu ya uinjilishaji pekee: "Muda ubakio si mwingi" (1Kor 7:29). Lakini ilikuwa wazi kwamba hilo lilikuwa oni lake binafsi na matamanio yake (rej. 1Kor 7:6-8) wala si agizo la Kristo: "Sina amri ya Bwana" (1Kor 7:25). Wakati huohuo, alikiri thamani ya miito mbalimbali: "Kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi" (1Kor 7:7). Kwa maana hiyo mtakatifu Yohane Paulo II alisema kwamba Maandiko Matakatifu “hayatoi sababu ya kutegemeza wazo la kuwa ndoa 'ina mapungufu', wala kuwa ubikira au useja 'ni bora zaidi'”[166] kwa sababu ya kujinyima tendo la ndoa. Zaidi kuliko kunena juu ya ukuu wa ubikira kwa hali zote, inaonekana kufaa zaidi kuonyesha kwamba hali mbalimbali za maisha zinakamilishana, kwa namna ya kwamba hali moja inaweza kuwa kamili zaidi kwa sehemu fulani, na ile hali nyingine inaweza kuwa kamili zaidi kwa mtazamo mwingine. Aleksanda wa Hales, kwa mfano, alisema kwamba kwa namna fulani ndoa inaweza kuhesabiwa kubwa kuliko sakramenti nyinginezo: kwa sababu inaisharisha kitu kilicho kikubwa sana, yaani "muungano wa Kristo na Kanisa au umoja wa tabia ya kimungu na maumbile ya kibinadamu".[167]

160. Kwa hiyo, “si suala la kupunguza hadhi ya ndoa ili kuongeza thamani ya kujinyima tendo la ndoa”[168] na “kinyume chake hakuna msingi wowote wa kutegemeza ushindani kati yake [...]. Endapo, kufuatana na mapokeo fulani ya kiteolojia, inawezekana kutaja hali ya ukamilifu (status perfectionis), hutajwa hivyo si kwa sababu tu ya kujinyima tendo la ndoa, bali kuhusiana na ujumla wa maisha yenye misingi juu ya mashauri wa kiinjili".[169] Hata hivyo, mtu wa ndoa anaweza kuishi mapendo kwa kiwango cha juu kabisa. Na hivyo "anaufikilia ule ukamilifu unaotokana na mapendo, kwa njia ya kuwa mwaminifu kwa roho ya mashauri yale. Ukamilifu huo unawezekana, nao u karibu na kila mtu".[170]

161. Ubikira unayo thamani ya kiishara ya upendo usiohitaji kummiliki mwenzi, na unaakisi kwa namna hiyo uhuru wa Ufalme wa Mbinguni. Ni mwaliko kwa wanandoa ili waishi upendo wao wa ndoa katika mtazamo wa upendo kamili kwa Kristo, kama mwendo wa pamoja kuelekea utimilifu wa Ufalme. Kwa upande wake, upendo wa wanandoa unaonyesha tunu nyingine za kiishara: kwa upande mmoja, ni kioo mahsusi cha Utatu Mtakatifu. Maana Utatu Mtakatifu ni umoja kamili, ambamo ndani yake unaendelea kuwepo pia utofauti. Zaidi ya hayo, familia ni ishara ya Kristo, kwa sababu inadhihirisha ukaribu wa Mungu anayeshiriki maisha ya binadamu kwa kuungana naye katika Umwilisho, katika Msalaba na katika Ufufuko. Na kila mwanandoa anakuwa "mwili mmoja" na mwenzie wa ndoa, na anajitoa mwenyewe ili kushirikishana na mwenzie mpaka mwisho. Wakati ubikira ni ishara ya "kieskatolojia" ya Kristo mfufuka, ndoa ni ishara "katika historia" kwa ajili ya wale wanaosafiri duniani, ishara ya Kristo wa duniani aliyekubali kuungana nasi na kujitoa hadi kumwaga damu yake. Ubikira na ndoa ni, kama ilivyo lazima viwe, namna tofauti za kupenda, kwa sababu "binadamu hawezi kuishi bila upendo. Maana, mtu anaendelea kuwa kwa mwenyewe kiumbe kisichoeleweka, na maisha yake hayana maana, kama upendo haufunuliwi kwake”.[171]

162. Useja una hatari ya kuwa upweke wenye mustarehe, unaojalia uhuru wa kujitegemea, wa kuhama mahali wajibu na machaguo, wa kuweza kutumia pesa binafsi, wa kuhusiana na watu mbalimbali kadiri ya mvuto wa kila muda. Ikiwa hivyo, unang'aa zaidi ushuhuda wa watu wa ndoa. Walioitwa kuishi ubikira waweza kuona katika majozi mengine ya wanandoa ishara wazi ya uaminifu wenye ukarimu na usioharibika wa Mungu kwa Agano lake, inayoweza kuchochea mioyo yao kujitolea na kujisadaka kimatendo hata zaidi. Na kwa kweli wapo watu wa ndoa ambao wanadumisha uaminifu wao pale ambapo mwenzi ameumbuka kimwili, au asipoweza kuridhisha mahitaji yao, hata ikiwa mara nyingi mazingira yanawaalika kukosa uaminifu au kumtelekeza mwenzi. Mwanamke aweza kumwuguza mume wake aliye mgonjwa, na huko, karibu na Msalaba, anarudia ile "ndiyo" ya upendo wake hadi kufa. Katika upendo wa jinsi hii inadhihirishwa kwa namna angavu hadhi ya mwenye kupenda, hadhi iliyo kama kioo cha mapendo, kwa sababu ni sifa ya mapendo kupenda kuliko kupendwa.[172] Twaweza pia kushuhudia katika familia nyingi uwezo wa kujitoa kuwatumikia kwa upendo mwanana wana ambao ni wagumu au hata wanaokosa shukrani. Kuishi hivi kunawafanya wazazi kuwa ishara ya upendo wa Yesu ulio wa hiari na usiotafuta shukrani. Hayo yote yanakuwa mwaliko kwa waseja ili waishi juhudi zao kwa ajili ya Ufalme kwa utayari na ukarimu zaidi. Leo mfumo wa kutukuza malimwengu umeutilia giza muungano wenye kudumu kwa maisha yote, na umepunguza utajiri wa juhudi katika ndoa, na kwa sababu hiyo "inapasa kuyahimiza yale mambo mazuri ya upendo kati ya wanandoa".[173]

Mabadiliko ya upendo

163. Maisha yarefuka, na hivyo inatokea kisichokuwa kawaida zamani: uhusiano wa ndani na hali ya kuwa kila mmoja mali ya mwenzie hupaswa kudumishwa kwa miongo minne, mitano au sita, nalo ladai kurudia kuchaguana tena na tena. Labda mtu wa ndoa havutwi tena na ashiki kali inayomleta karibu na mwenzie, lakini husikia faraja ya kuwa mali yake na kwamba mwenzie ni mali yake, ya kujua kwamba yeye siye peke yake, kwamba anaye "mwananjama" anayejua yote ya maisha yake na ya historia yake, na ambaye anashiriki kila kitu naye. Ni yule mwenzi katika mwendo wa maisha ambaye pamoja naye huwezekana kukabili mambo magumu na kufurahia yaliyo mazuri. Pia hayo yanazalisha ridhaa inayoendana na hamu iliyo pekee ya upendo kati ya wanandoa. Hatuwezi kudai kuwa na hisia zilezile kwa maisha yetu yote. Lakini bila shaka twaweza kuwa na mpango wa pamoja ulio thabiti, kujitahidi kupendana na kuishi pamoja hadi hapo kifo kitakapotutenganisha, na kuishi sikuzote kwa upendo mpevu wa ukaribu sana. Upendo tunaoahidiana unashinda kila mhemuko, hisia au hali ya moyo, hata kama huweza kuvihusisha. Ni kupenda upeo, kwa uamuzi wa moyo unaoathiri kila siku ya maisha. Na hivyo, katika mgogoro usiotulizwa, na ingawa hisia nyingi zinachangamana moyoni bila utaratibu, linadumu hai kila siku azimio la kupenda, la kuwa kila mmoja mali ya mwenzie, la kushiriki maisha yote na kuendelea kupendana na kusameheana. Kila mmoja katika jozi anatimiza mwendo wa ukuzi na ubadiliko wa nafsi yake. Katika mkondo wa mwendo huo, upendo unaadhimisha kila hatua na kila mede mpya.

164. Katika historia ya kila ndoa, sura ya kimwili hubadilika, lakini hilo si sababu ya mvuto wa kimapenzi kupotea. Mtu anamchumbia mtu mzima mwenye tabia na maumbile yake pekee, si tu mwili, ingawa mwili huo, licha ya uchakavu unaosababishwa na wakati, haumalizi kamwe kuonyesha kwa namna fulani ile tabia ya pekee iliyologa moyo wake. Wengine watakaposhindwa kutambua tena uzuri wa tabia ile, mwenzie apendanaye anaendelea kuweza kuuona kwa hisi ya upendo, na mahaba hayatoweki. Anasisitiza tena azimio lake la kuwa mali ya mwenzie, anamchagua tena na kuonyesha uamuzi wake kwa kuwa karibu naye kwa uaminifu na kwa upendo uliojaa tulizo. Ubora wa uamuzi wake kwa ajili ya mwenzie, kwa vile ulivyo na nguvu na wa kina, unaamsha namna mpya ya mhemuko katika kutimiza utume wa mwanandoa. Kwani "mhemuko uliosababishwa na binadamu mwingine kama nafsi [...] hauelekezi moja kwa moja kwenye tendo la ndoa".[174] Unajipatia namna nyingine za kujionyesha kwa sababu upendo “ni uhalisia mmoja, ingawa una hali mbalimbali; kila mara, hali moja au nyingine inajitokeza zaidi”.[175] Kifungo kinapata namna nyingi mpya na kinadai ufanyike uamuzi wa kuanza tena na tena kukiweka. Lakini si tu ili kukihifadhi, bali ili kikuzwe. Ni mwendo wa kujengana siku kwa siku. Lakini hakuna lolote la haya ambalo linawezekana bila kumwomba Roho Mtakatifu, na bila kulia kila siku na kuomba atujalie neema yake, bila kutafuta nguvu zake za kimbingu, na bila kumsihi kwa nguvu ili amimine moto wake juu ya upendo wetu ili kuutilia nguvu, kuuelekeza na kuufanya upya katika kila hali mpya inayojitokeza.

SURA YA TANO

UPENDO UZAAO MATUNDA

165. Upendo huleta uhai daima. Kwa hiyo, upendo wa kindoa “hauishii ndani ya jozi […]. Wanandoa wanapojizatiti hujitoa kila mmoja kwa mwenzie, hutoa - zaidi ya wao wenyewe - hata uwepo wa mtoto wao, ambaye ni kielelezo halisi cha upendo kati yao, ishara ya kudumu ya umoja wao kindoa na ni muhtasari halisi usiogawanyika ya kuwa wao baba na mama”.[176]

Kuukaribisha uhai mpya

166. Familia si tu mahali ambapo uhai mpya unazaliwa, bali pia ni pale ambapo uhai mpya unapokelewa kama zawadi ya Mungu Kila uhai mpya “unatuwezesha kukitambua kipimo cha upendo kisicho na gharama, ambacho hakiishi kutustaajabisha. Huo ni uzuri wa kupendwa kabla: watoto hupendwa kabla ya kuzaliwa kwao”.[177] Hiyo inaonyesha upendo wa awali wa Mungu ambaye daima ndiye mwanzilishi, kwa maana watoto “hupendwa kabla ya kutenda tendo lolote la kuwafanya wastahili”.[178] Hata hivyo, “watoto wengi tangu awali huwa wanakataliwa, wanatelekezwa, wananyang’anywa haki yao ya utoto na ile ya maisha yao ya baadaye. Kuna watu wanaothubutu kusema, labda wakijaribu kujihesabia haki, kuwa watoto hao walikuja duniani kwa bahati mbaya. Aibu iliyoje! […] Je, tunawajibika vipi na haki za binadamu au haki za watoto, ilhali baadaye tunawaadhibu watoto kwa ajili ya makosa ya watu wazima?[179] Kama mtoto anazaliwa katika mazingira yasiyofaa, wazazi wake au wanafamilia wengine yawapasa wampokee kwa hali na mali, kama zawadi ya Mungu, na wakubali kuwajibika kumkaribisha kwa utayari na upendo Kwa maana, “inapowahusu watoto waliozaliwa duniani, hakuna majitoleo ya wazazi yatakayozidi kipimo, ili kuepuka mtoto afikirie kuwa amekuja duniani kimakosa, hana thamani yoyote na amebwagwa katika mahangaiko ya maisha kutokana na kiburi cha binadamu”.[180] Zawadi ya mtoto mpya ambaye Bwana anawatunukia baba na mama, inaanza na mapokezi, kisha inaendelea na malezi katika maisha ya hapa duniani, na mwisho inalenga ile furaha ya uzima wa milele. Mtazamo mtulivu juu ya hatima ya binadamu utawafanya wazazi waitambue vema zawadi madhubuti waliyotunukiwa na Mungu. Kwa hakika, Mungu amewapa wazazi ridhaa ya kumpa kila mtoto wao jina wanalotaka ambalo Mungu pia atalitumia milele yote.[181]

167. Familia zenye watoto wengi ni furaha kwa Kanisa. Katika familia hizo upendo huonyesha uzaaji wake wenye heri. Hilo halimaanishi kupuuzia ilani ya mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa akieleza kuwa uzazi wa busara si ule wa “kuzaa watoto lukuki bila mpango ama kutozingatia matunzo yao, isipokuwa ni utashi wa wanandoa kuzingatia kwa busara na uwajibikaji uhuru wao usionyakulika, kwa kujali hali halisi ya kijamii na ya takwimu za idadi ya watu, pamoja na maisha na mapendekezo halali yao wenyewe.[182]

Upendo wakati wa kusubiri ujauzito

168. Ujauzito ni kipindi kigumu, lakini pia ni wakati mwafaka ajabu. Mama anamsaidia Mungu ili ufanyike mwujiza wa uhai mpya. Hali ya uzazi inatokana na “uwezo asilia wa mwili wa mwanamke, ambao kutokana na sifa yake ya kipekee ya kutoa kiumbe kipya unawezesha utungaji wa mimba na hatimaye kuzaliwa kwa binadamu”.[183] Kila mwanamke hushiriki “katika fumbo la uumbaji, ambalo linajirudia katika kuzaliwa kwa binadamu”.[184] Ni kama isemavyo zaburi: “Ulinitunga tumboni mwa mama yangu” (139:13). Kila mtoto anayetungwa ndani ya mamaye ni mpango wa milele wa Mungu Baba na wa upendo wake wa milele. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa” (Yer 1:5). Kila mtoto yupo katika moyo wa Mungu tangu sikuzote, na wakati anapotungwa mimba inatimilika ndoto ya milele ya Muumbaji. Na sasa tufikiri, je, huyu kiumbe anayetungwa mimba ana thamani gani! Yatupasa tumtazame kwa macho hayohayo yenye upendo ya Mungu Baba, yaonayo mbali zaidi ya mwonekano wa nje.

169. Mwanamke mjamzito anaweza kushiriki katika mpango huo wa Mungu huku akiota juu ya mtoto wake: "Kila mama na kila baba amekuwa akiota juu ya mwanawe kwa kipindi chote cha miezi tisa. […] Haiwezekani iwepo familia isiyo na ndoto. Uwezo wa kuota ndoto unapotoweka katika familia, watoto hawakui tena, upendo pia hauongezeki, maisha yananyongea na kutoweka”.[185] Katika ndoto hiyo, kwa jozi la wanandoa wa kikristo, Ubatizo ndipo unapochukua nafasi. Wazazi wanauandaa kwa njia ya sala, wakimkabidhi mtoto wao kwa Yesu kabla hata ya kuzaliwa kwake.

170. Kutokana na maendeleo ya kiteknolojia leo hii inawezekana kujua hata rangi ya nywele za mtoto ama ugonjwa atakaougua hapo baadaye, kabla hata hajazaliwa, kwa sababu sifa zote za mwili wa mtu yule zinakuwa zimeshaandikwa kwenye mfumo wa kijenetiki wa kiumbe hicho kikiwa bado tumboni. Lakini ni Baba tu aliyemwumba ambaye anamfahamu kwa undani. Ni yeye tu anayejua thamani na umuhimu, maana ndiye pekee anayemjua huyu mtoto, na maumbile yake kiundani. Mama ambaye anambeba huyu mtoto tumboni mwake anahitaji kuomba aangaziwe na Mungu ili aweze kumjua kiundani mtoto wake na kumsubiri jinsi alivyo. Baadhi ya wazazi hujisikia kwamba mtoto wao hafiki muda unaofaa. Wanahitaji kumwomba Mungu ili awaponye na awape nguvu ili waweze kumpokea kikamilifu huyu mtoto, ili waweze kumsubiri kwa moyo. Ni muhimu huyu mtoto ajisikie kwamba anasubiriwa. Mtoto haji kutatua mahitaji binafsi, wala yeye siyo ziada. Mtoto ni binadamu, mwenye thamani kubwa sana na hawezi kutumiwa kwa faida binafsi. Kwa hiyo suala hapa si kwamba huyu mtoto ana maana kwako au la, kama ana sifa zinazokupendeza au la, kama atatimiza mipango na ndoto zako au la. Kwa sababu “watoto ni zawadi. Kila mtoto ni pekee na hajirudii […]. Mtoto anapendwa kwa sababu ni mwana, si kwa sababu ni mzuri au yupo hivi au vile; hapana, kwa sababu ni mwana wangu! Si kwa sababu anafikiri kama mimi, au matakwa yangu nayaona kwake. Mwana ni mwana”.[186] Upendo wa wazazi ni chombo cha upendo wa Mungu Baba ambaye anasubiri kwa mapendo kuzaliwa kwa kila mtoto, anampokea bila masharti na kumkaribisha kwa shukrani.

171. Napenda kumwomba kwa upendo kila mwanamke mjamzito: ilinde furaha yako, na yeyote asikunyang’anye furaha ya ndani ya umama. Huyu mtoto anastahili furaha yako. Usiruhusu hofu, wasiwasi, maneno mabaya wanayosema watu au matatizo yoyote yale yaizime furaha ya kuwa chombo cha Mungu cha kuleta uhai mpya duniani. Jibidiishe na yale ambayo unapaswa kuyafanya au kuandaa, lakini bila kutingwa kwa wasiwasi na hilo tu, na umtukuze Mungu kama Maria: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu, kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake” (Lk 1:46-48). Hata katika usumbufu, uishi huu utulivu wa ndani, ukimwomba Bwana ailinde furaha yako ili uweze kumrithisha mtoto wako.

Upendo wa mama na wa baba

172. “Mara baada ya kuzaliwa, pamoja na kula chakula na kutunzwa, watoto huanza kupokea thibitisho la vipaji vya kiroho vya upendo. Matendo ya upendo hupokelewa kupitia zawadi ya jina binafsi, lugha inayowaunganisha, madhumuni ya mitazamo, minururisho ya tabasamu. Kujifunza kwamba uzuri wa muunganiko kati ya binadamu unaelekezwa kwenye roho yetu, hutafuta uhuru wetu, hupokea utofauti wa mwingine, unamtambua na kumheshimu kama mshiriki katika mazungumzo. […] Na huo ndio upendo ambao huleta cheche ya upendo wa Mungu!”.[187] Kila mtoto ana haki ya kupokea upendo wa mama na baba, wote wawili wakiwa muhimu kwa ajili ya ukomavu mtulivu kiujumla wa mtoto. Kama walivyosema maaskofu wa Australia, wote wawili “wanachangia, kila mmoja kwa namna yake, katika ukuaji wa mtoto. Kuuheshimu utu wa mtoto kuna maana ya kusisitiza mahitaji yake na haki ya asili ya kuwa na baba na mama”.[188] Hatuongelei kuhusu upendo wa baba na wa mama tu kila mmoja binafsi, ila pia upendo kati yao, ambao unatambuliwa kuwa ni chemchemi ya uhai wake mtoto, kama kioto kipokeacho na kama msingi wa familia. Bila hilo mtoto anaweza kudhilika kuwa kitu kinachochezewa. Wote wawili, mume na mke, baba na mama, ni “washiriki wa upendo wa Mungu Muumba na kwa namna fulani ni wahariri wake”.[189] Wanathibitisha kwa watoto wao sura ya upendo wa kimama na wa kibaba wa Bwana Mungu. Pamoja na hayo, wote kwa pamoja wanawafundisha tunu ya kushirikishana, kukutana kwa walio tofauti, ambako kila mmoja huchangia kulingana na nafsi yake na anajua pia kupokea kutoka kwa mwingine. Endapo, kwa sababu isiyozuilika, angekosekana mmojawapo wa wazazi, ni muhimu kutafuta kama kuna namna inayoweza kuziba pengo, ili kumwezesha mtoto akue kwa hekima na busara za kibinadamu.

173. Kujisikia kama yatima ambayo ni hisia wanayong’amua watoto na vijana wengi leo hii, ni kitu kinachowaathiri kwa undani zaidi kuliko tufikirivyo. Leo hii tunatambua kuwa ni haki halali kabisa, pamoja na kuwa matamanio pia, kwamba wanawake watake kusoma, kufanya kazi, kuendeleza vipaji vyao na kuwa na malengo yao. Wakati huohuo hatuwezi kukana mahitaji waliyo nayo watoto ya uwepo wa mama, hasa kwa miezi ya mwanzoni ya maisha yao. Ukweli ni kwamba “mwanamke yupo mbele ya mwanamume kama mama, chombo kinacholeta uhai mpya wa kibinadamu ambao umetungwa mimba na unakua ndani yake, na kutokana naye unazaliwa ulimwenguni”.[190] Udhaifu wa uwepo wa mama pamoja na mawaidha na vipaji vyake vya kike ni hatari kubwa kwa hii dunia yetu. Nathamini harakati ya kutetea haki ya wanawake iwapo haidai kusawazisha jinsia wala kukana hali ya uzazi. Kwani ukuu wa mwanamke unajumuisha haki zote zinazotokana na hadhi yake ya kibinadamu isiyonyang’anyika, lakini pia na vipaji vyake vya kike, ambavyo ni vya lazima kwa jamii. Upekee wao kama wanawake – hasa hali yao ya umama – huwapa pia majukumu maalumu. Kwa sababu akina mama wana majukumu hapa duniani ambayo yanawakabili wao tu, ambayo jamii inapasika kuyalinda na kuyaendeleza kwa manufaa ya wote.[191]

174. Kusema kweli, “akina mama ni dawa inayofaa zaidi dhidi ya kusambaa kwa ubinafsi usiojali. […] Ni wao ambao wanahakikisha uzuri wa maisha”.[192] Bila shaka, “jamii bila akina mama ingekuwa ni jamii mfu, isio na ubinadamu, kwa sababu akina mama daima, hata katika wakati mgumu, hujua kushuhudia wema, majitoleo na hamasa ijengayo. Akina mama mara nyingi hurithisha pia maana ya ndani ya uchaji wa Mungu: katika sala za kwanza, na katika ishara za kwanza za ibada ambazo mtoto hujifunza toka kwao […]. Bila akina mama, siyo tu kungekosekana waamini wapya, lakini pia imani yenyewe ingepoteza sehemu yake kubwa ya ari nyofu na ya ndani. […] Wapendwa akina mama: Asanteni! Asanteni, kwa jinsi mlivyo katika familia na kwa yote myatoayo kwa Kanisa na kwa ulimwengu”.[193]

175. Mama ambaye humtunza mwanae kwa ukarimu na huruma humsaidia mtoto kukua katika imani, na kutambua kwamba ulimwengu ni mahali pema ambapo anapokelewa vizuri. Hilo linamsaidia mtoto kukua katika hali ya kujienzi, na kama matokeo linaendeleza uwezo wa kupenda na kushirikiana na wengine. Na baba, katika nafasi yake, humsaidia mtoto kuyatambua mapungufu katika maisha, na msaada wake hulenga hasa kumpa mtoto mwelekeo, uhodari wa kutoka na kupambana na ulimwengu na changamoto zake, himizo la kufanya kazi kwa bidii na kuwa na ujasiri mkuu. Baba mwenye kuionyesha furaha na amani ya kuwa mwanaume, na ambaye anaidhihirisha pamoja na kuonyesha mapenzi kwa mke wake katika kumhudumia na kumjali, ni muhimu sawasawa na matunzo ya mama. Hapo huweza kuweko matazamo tofauti katika wajibu na majukumu mbalimbali, yaendanayo na hali na uwezo wa kila familia. Lakini uwepo wa ngao zote mbili katika familia, ya kike na kiume, ni wa muhimu sana katika kujenga mazingira bora yenye kuwezesha ukuaji bora wa watoto.

176. Husemekana mara kwa mara kuwa jamii yetu ni “jamii bila akina baba”. Katika utamaduni wa watu wa Magharibi, ishara ya akina baba inakosekana, imepotea, imedhoofika. Hata uume wenyewe leo upo katika mahojiano. Kimatokeo hayo yalileta fujo inayoeleweka, kwani “hapo awali, jambo hili lilionekana kuwa ni uhuru: uhuru kutoka kwa baba kama mwenye mamlaka, baba kama mwakilishi wa sheria inayotubana kutoka kwa nje, baba kama mwamuzi wa furaha ya watoto na kikwazo kwa maendeleo na kujitegemea kwa vijana. Zamani, katika baadhi ya nyumba ilitawala hali ya mabavu, na wakati mwingine hata ya ukandamizaji”.[194] Lakini, “kama inavyotokea mara nyingi, matokeo ni kufikia hali iliyo kinyume kabisa. Shida ya siku hizi zetu siyo tena ni uwepo wa kimabavu wa akina baba, bali zaidi kutokuwepo kwao, kuwa mbali na familia. Akina baba hujikita zaidi katika kujitunza wenyewe au katika shughuli zao na wakati mwingine katika miradi yao binafsi, kiasi cha kuwasahau hata familia zao. Nao huwaacha peke yao watoto wadogo na vijana”.[195] Uwepo wa baba, na pia mamlaka yake, unadhoofishwa pia na muda mwingi zaidi unaotumiwa kwa vyombo vya mawasiliano na kwa teknolojia ya maburudisho. Zaidi ya hayo, siku hizi mamlaka inaonekana kutiliwa mashaka, na wazee hujadiliwa vikali. Hao wenyewe wanakosa uhakika na hivyo hushindwa kutoa kwa watoto wao maongozi thabiti na yenye misingi bora. Haifai kuchanganya majukumu ya wazazi na ya watoto: hilo linaharibu mchakato mwafaka wa ukuaji ambao watoto wenyewe wanahitaji kuutimiza, na linawanyima upendo uwezao kuwapa dira na kuwasaidia katika kukomaa kwao.[196]

177. Mungu anamweka baba katika familia ili, kwa tunu zake za kiume, “aweze kuwa karibu na mke wake na kushirikishana kila kitu, furaha na huzuni, matumaini na magumu ya maisha. Na kuwa karibu na watoto katika kukua kwao, katika michezo yao na katika juhudi zao, katika wakati wa furaha, wasiwasi na mashaka, wakati wazungumzapo na wakati wa unyamavu, wanapojaribu na wanapokuwa na woga wa kujaribu, wanapoteleza na wanapoona tena njia iliyo sahihi. Kuwa baba ambaye yupo, daima. Kusema yupo si kusema kuwepo kama mnyapara. Kwa sababu akina baba ambao wanafuatilia yote kama wanyapara, huwa kizuizi na kivuli katika ukuaji wa watoto, na watoto huwa hawaendelei mbele”.[197] Baadhi ya akina baba hujisikia si wa muhimu na kwamba hawahitajiki, lakini ukweli ni kwamba “watoto warudipo nyumbani na matatizo yao wanahitaji kumkuta baba akiwasubiri”. Wanaweza kujitahidi kutoonyesha au hata kutokubali, lakini kiukweli ni kwamba wanahitaji”.[198] Sio jambo jema kwa watoto kuwakosa baba zao na kukuzwa kabla ya wakati wao.

Kupanuka kwa uzaaji

178. Wanandoa wengine hawana uwezo wa kupata watoto. Tunafahamu kuwa hili laweza kuwa sababu kubwa ya huzuni. Wakati huohuo tunafahamu kuwa “maisha ya ndoa hayakuanzishwa kwa jukumu wa kuzaa watoto tu […]. Hasa katika hali zile ambazo wanandoa wanapenda kuwapata watoto, na watoto hawapo, ndoa inabaki kuwa imara na yenye lengo la umoja na ushirika wa maisha yote na inalinda thamani yake na hadhi yake ya muungano usiovunjika".[199] Aidha “umama hauji tu kwa kuzaa watoto, kuna njia nyingine pia za kuwa mama”.[200]

179. Kuasili mtoto (adoption) ni njia mojawapo ya kutimiza umama na ubaba kwa namna iliyo na ukarimu mkuu. Nami ninapenda kuwatia moyo wale wasiokuwa na uwezekano kwa kuwazaa watoto wao wenyewe, wapanue na kufungua wazi upendo wao wa kindoa ili kuwapokea watoto ambao wanakosa hali za kifamilia zifaazo. Hawatajilaumu kamwe kwa kuwa wakarimu. Kumwasili mtoto ni tendo la upendo la kumzawadia familia yule asiyekuwa nayo. Ni muhimu kusisitiza kuwa vyombo vya sheria vihusikavyo viweze kurahisisha taratibu za kuasili watoto, hasa katika hali za watoto wasiotakikana, ili kuzuia utoaji mimba au kutelekezwa kwa watoto wachanga. Wale wote wanaoikabili changamoto ya kumwasili mtoto na wanampokea mtu bila masharti bali kwa ukarimu, hawa ni njia pekee ya upendo wa Mungu. Maana anasema “ Hata kaka mama yako atakusahau, lakini mimi sitakusahau kamwe” (taz. Isa 49:15).

180. “Uamuzi wa kumwasili mtoto au wa kumpokea kama walezi kwa muda maalumu ni udhihirisho wa uzaaji mahsusi wa maisha ya kindoa, hata pale ambapo hayaathiriwi na huzuni wa utasa. […] Mbele ya hali zile ambazo kwa udi na uvumba mtoto anatakikana kama haki ya kujitimiliza na wanandoa, kuasili mtoto au kumpokea kama walezi ni hali ambayo, ikieleweka katika udhati wake, inadhihirisha maana muhimu ya kuwa wazazi na kuwa watoto, kwa vile inavyosaidia kutambua kwamba watoto, wa kuzaa wenyewe au wa kuasiliwa, ni watu wengine muhimu mbali na mimi, na wanahitaji kupokelewa, kupendwa, kuhudumiwa, na siyo tu kuletwa duniani. Haki za watoto lazima zilindwe na zipewe kipaumbele daima pale inapofanyika uamuzi kuhusu kuasili mtoto au kumpokea kama walezi”.[201] Kwa upande mwingine “utekwaji na uuzaji wa watoto katika nchi na mabara mbalimbali unahitaji kuzuiliwa kwa njia ya sheria zinazofaa na kwa usimamizi makini ya Serikali.[202]

181. Tunawakumbusha tena kuwa kuzaa na kuasili mtoto si njia pekee za kuishi uwezo wa kuzaa wa upendo. Hata familia kubwa lazima idhihirishe uwepo wake katika jamii inamoishi, ili kuendeleza aina nyinginezo za uzaaji ambazo ni kama mwendelezo wa pendo unaozitegemeza. Familia za kikristo zisisahau kuwa “imani haitutoi ulimwenguni, bali inatuingiza hata zaidi katika ulimwengu. […] Maana, kila mmoja wetu ana jukumu lake maalumu katika kuuandaa ujio wa Ufalme wa Mungu”.[203] Familia isijione kama wigo wa kujikinga dhidi ya jamii. Badala yake, inasonga mbele na kutoka nyumbani, inakwenda katika roho ya mshikamano na wengine. Kwa njia hii inakuwa mahali pa kuwatangamanisha watu na jamii, na chombo cha kuunganisha maisha ya binafsi na yale ya jumuiya Wanandoa lazima wawe na ufahamu wazi na wa hakika juu ya majukumu yao ya kijamii. Hilo likitokea, mapenzi yao yanayowaunganisha hayapungui bali yanastawishwa katika mwanga mpya, kama ushairi huu unavyoelezea:

“Mikono yako ni kumbatio langu
tuni tamu zineemeshazo siku zangu
ninakupenda kwa sababu mikono yako
inajibidisha kwa ajili ya haki.

Kama nakupenda, ni kwa sababu ya wewe kuwa
mpenzi wangu, mwenzi wangu, yote niliyo nayo
na mitaani, bega kwa bega
tu zaidi sana ya wawili”.[204]

182. Hakuna familia inayoweza kuzaa matunda mema ikiwa inajiona tofauti mno na wengine au “kujitenga”. Ili kuzuia hatari hizi, lazima tuikumbuke familia yake Yesu. Imejaa neema na hekima, haikuonekana kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida, kama nyumba ya kigeni na mbali na watu wengine. Ndiyo sababu watu waliona vigumu kuitambua hekima ya Yesu na kusema: “Huyu ameyapata wapi haya? […] Huyu si yule seremala, mwana wa Maria?” (Mk 6:2-3). “Huyu si mwana wa seremala?” (Mt 13:55). Maswali haya yanaonyesha kuwa familia ya Yesu ilikuwa ni familia ya kawaida, yenye ujirani mwema na mshikamano na familia nyingine, familia ambayo ni sehemu ya jumuiya yake. Yesu hakukua na kulelewa katika mahusiano finyu ya Yosefu na Maria, bali alishirikiana na kujihusisha kwa furaha na ujamaa mpana wa ndugu, jamaa na marafiki. Hilo linaeleza kwa nini, katika kurudi kwao toka Yerusalemu, Maria na Yosefu walifikiria kuwa mtoto wao wa miaka kumi na miwili alikuwa ndani ya msafara kwa siku nzima, akisikiliza hadithi na kushirikishana mahangaiko ya wote: “Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa” (Lk 2:44). Badala yake, mara nyingine inatokea kwamba baadhi ya familia za kikristo, kwa sababu ya lugha waitumiayo, na jinsi watamkavyo mambo, au kwa watendavyo, kwa jinsi wanavyorudia mara nyingi mambo yaleyale, wanatazamwa kama za mbali, kama zimejitenga na jamii, na hata ndugu zao wenyewe wanajisikia kufedheheshwa au kuhukumiwa nao.

183. Wanandoa wanaoonja nguvu ya upendo wanafahamu kuwa upendo huo unaitwa kuponya majeraha ya waliotelekezwa, na kukuza utamaduni wa kukutana kati ya watu, na kuipigania haki. Mungu ameipatia familia jukumu la kuufanya ulimwengu kuwa nyumba ya wote,[205] ili wote wafikie hatua ya kuwaona binadamu wote kama ndugu: “Mtazamo wa makini katika maisha ya kila siku ya wanaume na wanawake wa leo unaonyesha mara moja hitaji lililopo popote la kupatiwa sindano maridhawa ya roho ya kifamilia. […] Sio tu mipangilio ya maisha ya pamoja inazidi kukwama katika urasimu ulio geni kabisa kwa vifungu vya misingi vya kibinadamu, lakini hata desturi na mwenendo wa kijamii na kisiasa unaonyesha mara nyingi dalili za kumomonyoka”.[206] Kwa upendo wake, familia zilizo wazi na zinazoshikamana na wengine ili kuwapa nafasi maskini, zinaweza kujenga urafiki na wale wenye hali mbaya kuliko ya kwao. Ikiwa wanaheshimu kwelikweli Injili, hawawezi kusahau aliyosema Yesu: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25:40). Kwa ujumla, wanaishi kile ambacho, kwa wazi kabisa, tunaagizwa kufanya na maneno haya: “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali, wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri” (Lk 14:12-14). Utakuwa heri! Hapa ndipo ilipo siri ya familia yenye furaha.

184. Kwa ushuhuda wao na kwa maneno yao familia zinatangaza kwa familia nyingine habari za Yesu, wanapitisha imani yao, wanaamsha hamu ya Mungu, na kuonyesha uzuri wa Injili na wa jinsi ya kuiishi. Kwa namna hiyo wanandoa wakristo wanaihamasisha jamii iliyokaa kivulini na kuipaka rangi za undugu, za kujali mshikamano wa kijamii, za kutetea haki na kujali mahitaji ya wale wenye hali duni, za imani inayoangaza, ya matumaini hai na tendaji. Uwezo wao wa kuzaa hukua na kupanuka katika namna nyingi zisizohesabika za kudhihirisha uwepo wa upendo wa Mungu katika jamii.

Kuutambua mwili

185. Katika mstari huo wa fikra ni muhimu kuitilia mkazo sehemu ile ya Biblia ambayo kwa kawaida inafasiriwa mbali na muktadha wake, au hata kwa juujuu sana, hali ambayo inasababisha kupoteza maana yake halisi na kamili zaidi, ambayo ni ya kijamii hasa. Ninaongelea juu ya 1Kor 11:17-34, ambako mtakatifu Paulo anapambana na hali ya aibu ya jumuiya. Matajiri wa jumuiya wanawakandamiza na kuwatenga maskini, na utengano huu unapelekwa hata katika karamu ya kijumuiya ambayo yaliambatana na adhimisho la Ekaristi Wakati matajiri wanaifurahia vyakula vyao bora, maskini wanaachwa wabaki na njaa. “Hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je, hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau Kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu?” (a. 21-22).

186. Ekaristi inatudai tuwe tunatangamana katika mwili mmoja wa Kanisa Mwenye kuijongea meza ya Bwana ili kupokea Mwili na Damu ya Kristo hawezi wakati huohuo kuujeruhi Mwili huo kwa kusababisha matengano ya aibu na ubaguzi katika viungo vyake. Hii ndiyo maana ya “kupambanua” Mwili wa Bwana: kuutambua kwa imani na mapendo katika ishara ya sakramenti na vilevile katika jumuiya, na yule asiyetimiza hilo, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake (taz. a. 29). Maneno hayo ya Biblia ni tahadhari nzito kwa familia ambazo zinajifunga ndani ya starehe yao binafsi na wanajitenga, lakini hasa kwa familia zisizojali mateso ya familia zilizo maskini na wahitaji. Maadhimisho ya Ekaristi yanakuwa hivi wakati mwafaka kwa kila mmoja “kujihoji mwenyewe” (a. 28), ili kufungua milango ya familia kwa ushirika mpana zaidi na wale waliotupwa na jamii na hivyo kuipokea kwelikweli Sakramenti ya upendo wa kiekaristi inayotufanya sote tuwe mwili mmoja. Tunapaswa tusisahau kwamba “fumbo la Sakramenti hii lina kipengele kinachohusu tabia ya kijamii”.[207] Wakati wale wanaokomunika wanageuka vipofu kwa maskini na wenye shida, au kutenda vitendo mbalimbali viigawanyavyo jamii, vya dharau na visivyo haki, Ekaristi walioipokea hupokelewa isivyostahili. Kwa upande mwingine, familia zinazojilisha Ekaristi baada ya kujiweka tayari, hawa wanaimarisha hamu yao ya kuishi kindugu, utayari wa kuwajibika kijamii na majitoleo yao ya kuwasaidia wenye shida.

Maisha katika familia pana

187. Familia ndogo inapaswa kuchangamana na familia pana, ambapo wapo wazazi, akina mashangazi na wajomba, binamu wote na hata majirani. Katika familia hii pana inawezekana wawepo wengine ambao wanahitaji msaada au walau ujirani na upendo, au yaweza kuwepo mateso makali yanayohitaji kufarijiwa.[208] Ubinafsi unaoshamiri leo unasababisha mara nyingine familia zijifungie katika viota vya ulinzi, na kuwasikia wengine kama hatari yenye kuzibughudhi. Lakini, kujitenga huko, kweli hakuwezi kumpatia yeyote amani kubwa au furaha, bali inapunguza moyo wa familia na kuyadogoza maisha ya familia.

Kuwa wana

188. Kwanza, tuseme neno juu ya wazazi. Yesu aliwaambia Mafarisayo kuwa kumtelekeza mzazi ni kinyume cha sheria ya Mungu (taz. Mk 7:8-13). Haimfai yeyote kujisahau kuwa mwana. Ndani ya kila mtu, “hata kama mmoja anaufikia utu uzima, au ni mzee, hata kama mtu anafikia hali ya kuwa mzazi, hata ukishika nafasi yenye wadhifa wowote ule, chini ya hayo yote inabaki hali ya kuwa mwana. Sisi sote tu wana. Hili kila wakati huturudisha nyuma ili kukumbuka kuwa hatukujipatia uhai, bali tuliupokea Zawadi kubwa ya uhai ni zawadi ya kwanza tuliyopokea”.[209]

189. Ndiyo sababu “amri ya nne inatutaka watoto […] tuwaheshimu baba na mama (taz. Kut 20:12). Amri hii inakuja mara baada ya zile zimhusuzo Mungu mwenyewe. Kwa kweli, hii inahisisha kitu kitakatifu, kitu cha kimungu, kitu ambacho ni shina la mambo yote yahusuyo heshima kati ya wanadamu. Na katika utungo wa kibiblia wa amri ya nne ya Mungu inaendelea kusema: “siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako”. Kifungu cha kifadhila kati ya vizazi ni uhakika wa kuwa na mustakabali, nacho ni dhamana ya historia iliyo ya kiutu kwelikweli. Jamii yenye watoto wasiowaheshimu wazazi ni jamii bila heshima […]. Ni jamii iliyoachwa mikononi mwa vijana wakali na wenye uroho”.[210]

190. Lakini kuna upande wa pili wa sarafu: “Mwanamume atamwacha baba yake na mama yake” (Mwa 2:24), linatuambia Neno la Mungu. Hili halitokei kila wakati, na ndoa haipokelewi katika thamani yake yote kwa sababu mtu hajatimiliza tendo hili la kuacha na kujitoa. Wazazi hawapaswi kuachwa na kutelekezwa, hata hivyo, ili kufunga ndoa inabidi kuwaacha, ili familia mpya iweze kuwa makazi, mahali pa usalama, jukwaa na mpango, na iwe inawezekana kuwa kweli "mwili mmoja” (ibid.) Katika baadhi ya ndoa, mwanandoa huwa msiri kwa mwenzie, na kuwa wazi zaidi kwa wazazi kuliko kwa mwenzi. Na matokeo yake mawazo ya wazazi huwa ya thamani zaidi kuliko hisia na rai ya mwenzi. Hali hii huwa haiendi mbali na hata kama ikienda, wanandoa wanapaswa kufanya jitihada ili kukuza uaminifu na mawasiliano kati yao. Ndoa hutoa changamoto kwa mke na mume kutafuta namna mpya ya kuwa wana.

Wazee

191. “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache" (Zab 71:9). Hili ni dua la mzee ambaye anaogopa kusahauliwa na kudharauliwa. Kama vile Mungu anavyotuomba kuwa wajumbe wake wenye kusikia kilio cha maskini, vivyo hivyo anatutaka sisi pia tusikilize mlio wa wazee.[211] Hilo ni changamoto kwa familia na jumuiya, kwa sababu “Kanisa haliwezi na halitaki kujikita katika fikra ya kukosa uvumilivu, wala ya kutojali au kudharau, mbele ya hali ya uzeeni. Lazima kufufua hali ya pamoja ya shukrani, ya kuenzi, ya ukarimu, ambayo itamfanya mzee ajisikie kuwa ni sehemu hai ya jumuiya yake. Wazee ni wanaume na wanawake, akina mama na akina baba, ambao walitembea kabla yetu katika njia yetu hiihii, waliishi kabla yetu katika nyumba yetu, katika mapambano kama yetu ya kila siku ili kuishi maisha yaliyo bora”.[212] Kwa hivyo, “ningetamani namna gani Kanisa ambalo linapambana na utamaduni wa kutupatupa kwa njia ya furaha ifurikayo katika kukutana na kukumbatiana upya vijana na wazee!”[213]

192. Mtakatifu Yohane Paulo II alitualika kuwa makini katika kutambua majukumu ya wazee katika familia zetu, kwa sababu kuna tamaduni nyingine ambazo “kwa sababu ya maendeleo ya viwanda na ya miji yasiyo na utaratibu, katika kipindi cha zamani na cha sasa wamewasahau na kuwaweka kando wazee kwa namna zisizokubalika”.[214] Wazee wanatusaidia kuyathamini “mwendo wa kizazi kimoja hadi kingine”, kwa “karama yao ya kuunganisha tena yaliyoraruka”.[215] Mara nyingi ni akina babu na bibi ambao huhakiki kuwa tunu kuu za mila na desturi zimepishwa kwa wajukuu na vitukuu, na “wengi wetu twaweza kuthibitisha kuwa imani tuliyo nayo tumerithishwa kweli toka kwa babu au bibi”.[216] Maneno yao, makumbatio yao au hata uwepo wao tu, unawasaidia watoto kutambua kuwa historia haikuanza na wao. Na kwamba wao ni warithi wa mwendo mrefu wa watu na kwamba wanapaswa kuheshimu yote yaliyotokea kabla yao. Wale watakaovunja vifungo na historia ya zamani watapata shida kujenga mahusiano imara na watashindwa kutambua kuwa uhalisia ni mkubwa zaidi kuliko wao nao hawautawali. Kwa hiyo, “kuwaheshimu wazee ndiko kunakofanya jamii na utamaduni wake kuwa bora. Jamii huonyesha kuwajali wazee? Kuna nafasi kwa wazee? Jamii hii itaendelea kama itajua kuheshimu hekima na busara ya wazee”[217]

193. Ukosefu wa kumbukumbu ya kihistoria ni pungufu kubwa katika jamii zetu. Ni fikra isiyopevuka ya "yaliyopita ni ya kale, na ya sasa ni ya sasa”. Kuyajua matukio ya zamani na kuweza kuyapambanua ni njia pekee ya kujenga mustakabali wenye maana. Haiwezekani kulea bila kukumbuka: “Zikumbukeni siku za kwanza” (Ebr 10:32). Kusikiliza wazee wasimuliapo historia zao kunawafaa sana watoto na vijana, kwani inawafanya wajisikie wameunganishwa na historia hai ya familia yao, pia ya majirani zao na nchi yao. Familia ambayo inashindwa kuheshimu na kuwaenzi babu na bibi zao, ambao ni historia hai yao, hiyo familia tayari imevunjika. Lakini familia yenye kukumbuka, hiyo ina uhakika ya uendelevu wa maisha. Kwa hiyo, “jamii ambayo haiwapi nafasi wazee au imewatupa kwa sababu huleta matatizo, jamii hiyo tayari ina ndani yake virusi viletavyo kifo”,[218] kwa vile “inajikata na mizizi yake yenyewe”.[219] Mang’amuzi yetu ya kujisikia yatima, kwa sababu ya kukosa mwendelezo wa mila na tamaduni kati ya vizazi, ya kung’olewa mbali na mazingira ya asili na ya kupotelea mbali kwa uhakika unaofanya maisha yaumbike, yanatupatia changamoto ya kuzifanya familia zetu ziwe mahali ambapo watoto waweze kutia mizizi katika rotuba ya historia iliyo ya kijumuiya.

Kuwa ndugu

194. Uhusiano kati ya ndugu unaendelea kukua katika mwendo wa muda, na “muungano wa ujamaa ambao huundwa katika familia kati ya watoto, kama ikiimarishwa katika hali ya kimalezi iliyo wazi kuwaheshimu wengine, ni shule kuu ya uhuru na amani. Katika familia, kaka na dada wajifunza maana ya kuishi pamoja wanadamu […]. Labda si wakati wote tunagundua hilo, lakini ndiyo familia inayoingiza udugu duniani! Kutoka mwanzo huu wa mang’amuzi ya udugu, unaoimarishwa na upendo na malezi ya nyumbani, mtindo wa udugu huangaza kama ahadi juu ya jamii nzima”.[220]

195. Kukua pamoja na kaka na dada kunaleta mang’amuzi mazuri sana ya kujaliana, ya kusaidia na kusaidiwa. Kwa hiyo, “udugu katika familia inapendeza kwa njia ya pekee tunapoona roho wa kujaliana, uvumilivu, upendo ambao unadhihirishwa kwa kaka mdogo na dada mdogo ambaye ni dhaifu zaidi, au mgonjwa, au ana ulemavu fulani”.[221] Tunapaswa kutambua kwamba “kuwa na kaka au dada anayekupenda ni zawadi ya pekee, isiyoweza kulipwa na isiyo na kifani”.[222] Lakini watoto wanapaswa kufundishwa kwa uvumilivu thamani ya kujaliana kama kaka na dada. Mafunzo haya, ambayo mara nyingine yaweza kuwa magumu, ni shule halisi ya majumuisho. Katika nchi fulani, ambako imekuwa ni hali ya kawaida kuwa na mtoto mmoja tu, mang’amuzi ya kuwa na kaka au dada siyo tena ya kawaida. Ikiwa imetokea kwamba haikuwezekana kuwa na watoto zaidi ya mmoja, lazima zitafutwe mbinu ili kuhakikisha kuwa huyu mtoto halelewi au kukua peke yake au katika mazingira ya upweke.

Moyo mkuu

196. Zaidi ya duru ndogo ya wanandoa na watoto wao, kuna familia pana ambayo haiwezi kusahauliwa. Maana, “upendo kati ya mume na mke katika ndoa na, kutokana na huo na kwa upana zaidi, upendo kati ya wanafamilia wote – kati ya wazazi na watoto, kati ya akina kaka na akina dada, kati ya ndugu na jamaa - unapewa uhai na unahimizwa kwa njia ya mkikimkiki usiokoma, wenye kuiongoza familia kwenye ushirika wa ndani na wa kina zaidi na zaidi, ulio msingi na roho ya jumuiya ya kindoa na ya kifamilia”.[223] Marafiki na familia nyingine ni sehemu ya hii familia kubwa, hali kadhalika jumuiya za familia wanaoungana mkono katika shida, na katika majukumu yao ya kijamii na katika maisha ya imani.

197. Familia hii pana inatamaniwa ipokee kwa upendo mkuu kina mama vijana, na watoto wasio na wazazi, akina mama wasio na waume, ambao wameachiwa jukumu la kulea watoto peke yao, watu wenye ulemavu, ambao wanahitaji mapendo ya hali ya pekee na ukaribu, vijana wanaopambana na hali tegemezi ya kulevya, watu wasioolewa au kuoa, waliotengana au kutalakiana, wajane wanaohangaika katika upweke, wazee na wagonjwa wasio na huduma toka kwa watoto. Hadi kuchukua majukumu ya kuwapokea ndani yake “hata wale waliopotoka zaidi katika mienendo ya maisha yao”.[224] Hii familia pana yaweza kujihusisha katika kusaidia, eti, hata udhaifu wa wazazi, au kufichua na kushtaki mapema hali ya ukatili, ikiwa pamoja na unyanyasaji wa watoto, na kuwapatia upendo safi na tegemeo ya kifamilia pale ambapo wazazi wao wanashindwa kuyatimiza haya.

198. Hatimaye, hatuwezi kusahau kuwa familia pana hii inajumuisha pia akina baba wakwe, mama wakwe na ndugu wote wa mwenzi wa ndoa. Sifa ya upendo mwanana ni kujifunza kutowatazama hawa ndugu kama washindani, watu wa hatari au wavamizi. Muungano wa wanandoa unadai mila na desturi za ndugu hao ziheshimiwe, zifanyike juhudi katika kuelewa misamiati yao, kupunguza mateto, kuwajali na kuwapa nafasi moyoni, hata pale ambapo ingekuwa lazima kulinda uhuru halali ya jozi na hali ya undani wao. Kuwa tayari kufanya hivyo ni pia njia bora ya kuonyesha unyofu na ukarimu wa upendo kwa mwenzi wa ndoa.

SURA YA SITA

BAADHI YA MITIZAMO YA KICHUNGAJI

199. Majadiliano wakati wa Sinodi yaliibua uhitaji wa kubuni mbinu mpya za kichungaji. Nitajaribu kuorodhesha baadhi yao kwa jumla. Jumuiya tofauti ziandae mikakati ya utendaji na ya kufaa, ambayo iendane na mafundisho ya Kanisa na mahitaji na changamoto za eneo mahalia. Pamoja na kwamba sina nia ya kuelezea humu mpango wa uchungaji wa familia, ningependa kutafakari juu ya baadhi ya changamoto za kichungaji zilizo muhimu zaidi.

Kuitangaza Injili ya familia leo

200. Mababa wa Sinodi walisisitiza kwamba familia za kikristo, kwa msaada wa neema ya sakramenti ya ndoa, ni wahusika wa kwanza katika uchungaji wa familia, hasa kwa njia “ya ushuhuda wa furaha ya wanandoa na familia, zilizo makanisa ya nyumbani”.[225] Kwa sababu hiyo, walisisitiza kwamba “ni muhimu watu waguswe na Injili ya familia kama furaha ambayo ‘huijaza mioyo na maisha yote’, kwa sababu katika Kristo ‘tumekombolewa kutoka dhambi, huzuni, utupu wa mioyo na upweke’ (Furaha ya Injili, 1). Katika mwanga wa mfano wa mpanzi (taz. Mt 13:3-9), wajibu wetu ni kushirikiana katika kupanda: mengine yote ni kazi ya Mungu. Wala tusisahau kwamba Kanisa, ambalo linahubiri juu ya familia, ni ishara ya ukinzani”.[226]Waliofunga ndoa wanashukuru kuwa wachungaji wao wanawahamasisha ili waelekeze kwa ushujaa maisha yao kwenye upendo imara, wenye nguvu, wenye kudumu na wenye uwezo wa kuhimili katika mikikimikiki ya kila aina. Kanisa linatamani kwa unyenyekevu na mguso wa pekee, kuzifikia familia na “kusindikiza kila familia kugundua njia nzuri zaidi ya kupambana na vikwazo inavyokumbana navyo.”[227]Haitoshi kuonyesha mguso wa jumlajumla kwa familia katika mipango mikuu ya kichungaji. Kuziwezesha familia kuchukua wajibu wao kama watu hai wa uchungaji wa familia kunadai “juhudi za uinjilishaji na katekesi kwa ajili ya familia”,[228]inayoielekeza katika njia hiyo.

201. “Juhudi hii inalidai Kanisa zima kuongoka kimisionari: ni lazima kutosimama katika kutangaza habari iliyo ya kinadharia tu, iliyotenganika na matatizo halisi ya watu.”[229]Uchungaji wa familia “ unapaswa kuwezesha kung’amua kwamba Injili ya familia inasaidia kujibu matarajio ya ndani kabisa ya mwanadamu: ni jibu kwa utu wa kila mmoja na kwa utimilifu wake katika kusaidiana na kukamilishana, katika ushirika na katika kuzaa matunda. Si suala tu la kutungwa kwa mlolongo wa taratibu, bali ni kuonyesha tunu, ili kuitika hitaji la hizo linaloonekana leo, hata katika nchi zinazofuata zaidi msimamo wa kidunia (most secularized).”[230]Sambamba, “imesisitizwa kwamba unahitajika uinjilishaji unaoweza kukemea wazi athari za kitamaduni, kijamii, kisiasa na kiuchumi, kama kwa mfano mitazamo ya kimasoko iliyotiliwa mkazo mkubwa, ambayo imekuwa kikwazo kwa maisha ya familia na imesababisha ubaguzi, umaskini, unyanyapaa na ujeuri.” Wakati huohuo, mazungumzano na ushirikiano na mifumo ya kijamii vinapaswa kukuzwa; na pia inatakiwa kuwahamasisha na kuwategemeza waamini walei wanaojihusisha kama Wakristo katika nyanja za kitamaduni na za kijamii-kisiasa.”[231]

202. “Mchango mkubwa kwa uchungaji wa familia unatolewa na parokia, ambayo ni familia ya familia nyingi, ambapo jumuiya ndogondogo, vyama vya kitume na taasisi mbalimbali za kikanisa zinaunganishwa pamoja.”[232]Pamoja na mpango wa kichungaji unaoelekezwa mahsusi kwa familia, tunadhihirishiwa uhitaji wa “malezi madhubuti kwa mapadre, mashemasi, watawa wa kike na wa kiume, makatekista na wadau wengine wa mambo ya kichungaji”.[233]Katika michango kutoka kona mbalimbali ulimwenguni, inaonyeshwa wazi kuwa wahudumu wenye daraja takatifu hawana mafunzo ya kutosha ili kukabiliana na changamoto nzito zinazozikabili familia leo hii. Kuhusu shida hiyo, na desturi ya mapadre wenye ndoa inayopatikana katika hazina kubwa ya mapokeo ya Makanisa ya mashariki, inafaa itazamwe.

203. Ingefaa waseminari wapate mafunzo yenye kuunganisha fani mbalimbali kuhusu mambo ya uchumba na ndoa, yasihusu tu mafundisho ya Kanisa. Aidha, mafunzo yao hayatoshelezi daima kuwasaidia wafunue mtima wao wa kisaikolojia na wa mahabahisia (affective). Wengine wanatoka katika familia zenye matatizo, bila wazazi na zisizo na uthabiti wa mihemuko. Kuna haja ya kuhakikisha kuwa mpango wa malezi unawawezesha kufikia ukomavu wa kiutu, ili wapate utulivu mzuri ule wa kisaikolojia unaodaiwa na majukumu yao ya usoni. Mafungamano ya kifamilia ni muhimu sana kwa ajili ya kukuza uwezo mzuri wa waseminari wa kutambua hadhi yao. Ni muhimu kwa familia ziwe karibu nao katika mchakato mzima wa malezi ya seminari na maisha ya kipadre, kwani zinachangia kuwatia nguvu kwa namna halisi. Inasaidia sana kwa waseminari kuishi muda mwingine seminarini na muda mwingine maparokiani. Hapo parokiani wanapata kukutana na mazingira halisi ya kifamilia; na ni kweli kwamba katika maisha yake yote ya kichungaji, padre hujihusisha hasa na familia. “Uwepo wa walei, familia na hasa uwepo wa wanawake katika malezi ya kipadre, unakuza kutambua uzuri wa tofauti na mkamilishano wa miito mbalimbali ndani ya Kanisa.”[234]

204. Majibu yaliyotolewa kwa mashauriano ya kabla ya Sinodi pia yamehimiza juu ya uhitaji wa mafunzo kwa walei wanaotenda kazi katika uwanja wa uchungaji wa familia, kwa msaada wa walezi wataalamu wa saikolojia, madaktari wa familia na madaktari wa jumuiya, maofisa wa ustawi wa jamii, mawakili wa watoto na familia; pamoja na utayari wa kujifunza kutokana na michango ya saikolojia, sosholojia, elimujinsia, na ushauri nasaha pia. Wataalamu, hasa wale wenye uzoefu wa kusindikiza, wanasaidia kuweka mikakati ya kichungaji inayojikita katika hali halisi na mahangaiko ya kweli ya familia. “Kozi na mipango mbalimbali zilizo maalumu kwa wadau wa mambo ya kichungaji zaweza kuwa na msaada ili wamudu kujumuisha mpango wa maandalizi kabla ya ndoa ndani ya mpango mkubwa endelevu wa maisha katika Kanisa.”[235]Mafunzo bora ya kichungaji ni muhimu, “hasa kwa sababu ya hali maalumu zilizotokana na ukatili wa nyumbani na udhalilishaji wa kijinsia”.[236]Mambo haya yote hayafifishi bali yanakamilisha thamani kubwa ya maongozi ya kiroho, ya hazina kubwa za kiroho za Kanisa na ya sakramenti ya Upatanisho.

Kuwaandaa wachumba kwa ajili ya ndoa

205. Mababa wa Sinodi wamesema kwa namna mbalimbali kwamba tunapaswa kuwasaidia vijana kutambua hadhi na uzuri wa ndoa.[237]Wanapaswa kusaidiwa kutambua mvuto wa muungano kamili ambao hukuza na kutimiliza tabia ya kijamii ya maisha, huipa ujinsia maana bora zaidi, na huwanufaisha watoto kwa kuwapatia mazingira bora ya makuzi na malezi.

206. “Mambo mengi ya jamii ya leo na changamoto zinazozikabili familia zinahitaji juhudi kubwa kwa jumuiya nzima ya kikristo katika kuwaandaa kwa ajili ya ndoa wale wanaokaribia kuoana. Umuhimu wa fadhila ni vema uonyeshwe. Kati ya hizo, usafi wa moyo hudhihirisha thamani ya pekee katika kukua kwa upendo wa kweli baina ya watu. Katika mtazamo huu, Mababa wa Sinodi wamekubali juu ya uhitaji wa kuihusisha jumuiya nzima kikamilifu zaidi kwa kutoa nafasi ya pekee kwa ushuhuda wa familia zenyewe, na kujikita kwa maandalizi ya ndoa ndani ya mchakato wa kuingizwa katika Ukristo, kwa kuonyesha uhusiano baina ya ndoa na ubatizo na sakramenti nyingine. Mababa wamezungumzia pia juu ya uhitaji wa mipango mahsusi kwa ajili ya maandalizi ya ndoa inayowapatia wachumba ushiriki mzuri katika maisha ya kikanisa, na kuangalia kwa undani mambo mbalimbali ya maisha ya kifamilia.”[238]

207. Nazitia moyo jumuiya za Kikristo kutambua faida kubwa zinazopatikana kwao zenyewe kwa kuwasaidia wachumba katika kukua katika upendo. Kama ambavyo imeshabainishwa na Maaskofu wa Italia, kwa ajili ya jumuiya ya kikristo wanandoa ni “tunu ya thamani, jinsi wanavyosaidiana kukua katika upendo na kujitolea kama zawadi kila mmoja kwa ajili ya mwingine, wanachangia kuleta mwamko mpya katika Kanisa zima. Urafiki wao wa pekee waweza “kuwaambukiza” wengine, na kukuza urafiki na udugu katika jumuiya yao ya Kikristo”.[239]Kuna namna nyingi za halali za kupanga maandalizi ya ndoa, na kila Kanisa mahalia litaamua namna ipi ni bora zaidi, kwa kutoa malezi yanayofaa bila kuwaweka vijana mbali na sakramenti. Hawahitaji kufundishwa Katekisimu yote, wala kupewa mafundisho mengi sana. Hata kuhusu hayo, ni kweli kwamba “sio elimu kubwa inayojaza na kuridhisha roho, bali ni kuguswa na kufurahia mambo toka moyoni”.[240]Ubora ni muhimu zaidi kuliko uwingi, na kipaumbele kiwekwe - pamoja na kuhubiri tena mafundisho ya msingi ya Injili (kerigma) - katika kutoa mafundisho yenye mvuto na mguso wa kuwasaidia wachumba kujiandaa kuishi pamoja daima “kwa moyo thabiti na ukarimu”.[241]Maandalizi ya ndoa yanapaswa kuwa ni “mafunzo ya awali” kuelekea sakramenti ya ndoa, yakiwasaidia wachumba kupokea sakramenti kwa nia nzuri na kufanya mwanzo imara wa maisha ya kifamilia.

208. Kwa msaada wa familia za kimisionari, familia za wachumba wenyewe na mambo mbalimbali ya kichungaji, njia mbalimbali zipangwe za kutoa maandalizi ya mapema, ili kwa kuwasindikiza kwa mifano na ushauri mzuri, yawasaidie kukua katika kupendana. Majadiliano katika makundi ya wachumba na mazungumzo juu ya mada mbalimbali zinazopendwa kweli na vijana mara nyingi yanasaidia sana. Pia mikutano ya mmoja mmoja ni mizuri, kwani lengo la msingi ni kumsaidia kila mmoja kujifunza kumpenda mtu ambaye ana mpango wa kuishi naye kwa maisha yote. Kujifunza kumpenda mtu hakuji ghafla, wala hakufundishwi katika semina fupi kabla ya adhimisho la ndoa. Kwa kweli, kwa kila mtu, maandalizi ya ndoa yanaanza baada ya kuzaliwa. Alichopokea katika familia zake kingeweza kumsaidia ajifunze kutokana na maisha yake, na kumwezesha kufanya uamuzi mkamilifu na wa daima. Walioandaliwa vizuri kwa ajili ya ndoa, pengine ni wale waliofundishwa maana ya ndoa ya kikristo toka kwa wazazi wao, waliochaguana bila masharti na kuzidi kuthibitisha uamuzi ule. Katika mtazamo huu, vipaumbele vya kichungaji vinavyoelekezwa katika kuwasaidia wanandoa kukua katika upendo na kuishi Injili katika familia, ni msaada usiopimika kwa watoto, ili wajiandae kwa maisha ya baadaye ya ndoa. Pia tusipuuze michango mizuri inayotolewa na uchungaji wa kitamaduni. Nawaza kwa mfano juu ya siku ya Mtakatifu Valentino; kwa baadhi ya nchi, malengo ya kibiashara yanatawala zaidi katika kujua umuhimu wa siku hii kuliko malengo ya Kanisa.

209. Maandalizi ya wale walioweka hadharani uchumba wao, pale ambapo jumuiya ya parokiani inafaulu kuwasaidia tangu awali, yaweza kuwapa pia nafasi ya kuona changamoto na hatari za usoni. Kwa namna hii, wataweza kufikia hatua ya kutambua kwamba ni busara kuvunja uhusiano ule, ili kuepukana na hatari ya kushindwa ambako kungeleta huzuni nyingi. Kwa sababu ya nguvu ya upendo wa mwanzoni mwa mahusiano yao, wachumba wanaweza kuficha au kupunguza uzito wa mambo mbalimbali na kuepusha migogoro baina yao; na kusukuma mbele tu matatizo, ambayo baadaye huibuka. Kwa sababu hiyo, wahimizwe sana kujadiliana juu ya matarajio yao ya baadaye katika ndoa, wanachojua juu ya upendo na kujitoa, nini kila mtu anataka toka kwa mwenzie na aina gani ya maisha wanataka kujenga pamoja. Majadiliano hayo yatawasaidia kutambua kama maafikiano si mengi, na kutambua kuwa mvuto wa nje hautoshelezi kuwaweka pamoja. Hakuna chenye kudai, kisicho cha uthabiti na kisichoweza kutabiriwa kuliko shauku. Uamuzi wa kuoa usikaziwe sana iwapo hakuna sababu na mazingira mazuri ya kuhakikisha uhalisia na uthabiti kwa mpango ule wa kufanya agano la kudumu.

210. Katika tukio lolote, ikiwa mwenza mmoja ametambua udhaifu wa mwenzake, basi anapaswa kuwa na imani isiyo bandia juu ya uwezekano wa kumsaidia kusitawisha mema aliyo nayo ili kuwiana na uzito wa udhaifu wake, akiwa na nia thabiti ya kuhamasisha maendeleo ya kiutu. Hali hii inadai kukubali kwa utashi thabiti uwezekano wa kukabiliana na majikatalio na matatizo na migogoro; inadai pia maamuzi mazito ya kuwa tayari kufanya hivyo. Wachumba wanapaswa kuwa na uwezo wa kutambua ishara za hatari katika mahusiano yao, na kabla ya ndoa watafute njia sahihi za kukabiliana nazo na kuzishinda. Kwa bahati mbaya, wachumba wengi hufunga ndoa pasipo kujuana vema. Wamefurahia kuwa pamoja na kufanya mengi pamoja, lakini hawakukabiliana na changamoto wa kujifunua walivyo na kujuana vizuri kwa undani.

211. Maandalizi yote ya ndoa, yawe ya muda mfupi au mrefu, yahakikishe kuwa wachumba hawachukulii kuwa sherehe ya harusi ndio mwisho wa nia yao, bali kuichukulia ndoa kama wito wa muda mrefu unaowataka wawe na maamuzi imara na halisi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali na magumu kwa pamoja. Msaada wa kichungaji kwa wachumba na wanandoa lazima ujikite katika uchungaji juu ya kifungo cha ndoa, utakaowasaidia sio tu kukuza upendo baina yao bali kukabiliana na matatizo na magumu mbalimbali. Msaada huo sio tu kuyapokea mafundisho ya Kanisa, wala kuzitumia tunu za thamani za kiroho ambazo daima Kanisa linaweza kutoa, bali lazima uwe kuwasaidia kwa vitendo, ushauri wenye nguvu, mikakati halisi inayotokana na uzoefu wa maisha, na maelekezo ya kisaikolojia. Haya yote yanaunda malezi ya upendo, yanayojikita katika hisia na mazingira ya vijana na uwezo wa kuwasaidia kukua kiundani. Maandalizi ya ndoa yawapatie wachumba pia majina ya mahali na watu, pia taasisi au familia zinazoweza kuwapa ushauri, ambapo wataweza kuzifikia ili kupata msaada mara wapatapo shida fulani. Pia ni muhimu kuwakumbusha juu ya uwepo wa sakramenti ya upatanisho, ambayo itawasaidia kuungama dhambi zao na makosa ya maisha yao, na hata ya mahusiano yao yenyewe, mbele ya Mungu, na kupokea msamaha wa huruma yake na ya nguvu yake ya kuponya.

Maandalizi ya adhimisho

212. Maandalizi ya muda mfupi ya ndoa yanajikita katika mialiko, mavazi, sherehe na vitu vingi ambavyo sio tu hugharimu pesa nyingi bali pia nguvu na hata furaha. Wachumba wanakuja kwenye siku ya harusi wakiwa wachovu sana na wanaharakishwa, badala ya kuweka nguvu zao zote katika kujiandaa kama jozi kwa hatua kubwa watakayopiga kwa pamoja. Mawazo kama hayo pia huwaathiri wale wanaoishi pamoja, bila kufikia kamwe katika hatua ya kufunga ndoa, kwa sababu ya kufikiria sherehe zenye gharama kubwa mno, badala ya kuiwekea kipaumbele hali yao ya kupendana na kuidhihirisha rasmi mbele ya watu. Wachumba wapendwa, muwe na ujasiri wa kuwa tofauti. Msitekwe na mambo ya jamii ya ulaji na muonekano. Kilicho muhimu ni upendo unaowaunganisha, wenye kuimarishwa na kutakatifuzwa na neema. Mnaweza kuchagua sherehe kuwa ya kawaida tu, ambapo upendo unatawala juu ya kila kitu. Wadau wa mambo ya kichungaji na jumuiya kwa ujumla wanaweza kusaidia ili kipaumbele hiki kiwe jambo la kawaida wala si la kipekee.

213. Katika maandalizi yao ya siku ya ndoa, ni muhimu wachumba wasaidiwe kujiandaa ili adhimisho la kiliturujia liwaguse ipasavyo, ili kila mmoja aone maana na thamani ya kila ishara. Kwa wale ambao wote ni wabatizwa, nia inayoonyeshwa na mabadilishano ya ukubali wa ndoa, na muungano wa miili ambao huifanya ndoa ikamilike, huweza kufasiriwa tu kama ishara ya upendo wa Mwana wa Mungu aliyetwaa mwili na kuunganika na Kanisa lake katika agano la upendo. Kwa wabatizwa, maneno na vitendo huwa lugha mwanana inayodhihirisha imani. Mwili, pamoja na maana ambayo Mungu alipouumba akaiweka ndani yake, “huwa lugha ya wahudumu wa sakramenti ya ndoa, wanaotambua kwamba katika makubaliano ya ndoa fumbo huonyeshwa na kudhihirishwa ambalo hutoka kwa Mungu mwenyewe”.[242]

214. Wakati mwingine, wachumba hawapati maana nzuri ya kiteolojia na kiroho ya maneno ya ukubaliano, ambayo huangaza maana ya vitendo vyote vinavyofuata. Ihimizwe kwamba maneno yale hayahusu wakati wa sasa tu; bali ni kwa nyakati zote pamoja na wakati ujao: “mpaka kifo kiwatenganishe”. Maneno ya ukubaliano yanaonyesha maana hii, kwamba “uhuru na uaminifu hayakinzani, ila yanabebana, katika mahusiano ya mtu na mtu na mahusiano ya kijamii. Halafu, tufikirie madhara yaliyosababishwa katika utamaduni wetu wa mawasiliano ya kiutandawazi, kwa ongezeko kubwa la kutotimiza ahadi […]. Mtu kuheshimu maneno aliyotoa, na kuwa mwaminifu kwa kile alichoahidi: haya ni mambo yasiyonunuliwa wala kuuzwa. Hayawezi kudaiwa kwa nguvu, wala kuyatunza bila kujitoa sadaka.[243]

215. Maaskofu wa Kenya wamegundua kuwa “wanaotarajia kufunga ndoa, wakiwa wanaitazama zaidi siku ya harusi, wanasahau kwamba wanajiandaa kwa jukumu ambalo watakuwa nalo kwa maisha yote”.[244]Wanapaswa wasaidiwe kuona kuwa sakramenti si kitu cha mara moja tu na kisha kusahaulika, bali inatia nguvu kwa maisha yote ya ndoa, kwa namna ya kudumu.[245]Maana ya uumbaji shirikishi katika masuala ya kujamiiana, lugha ya mwili na alama za upendo zinazojionyesha wakati wote wa maisha ya ndoa, zote zinakuwa “mwendelezo usio na mwisho wa lugha ya kiliturujia” na “maisha ya ndoa yanakuwa, na namna fulani, liturujia”.[246]

216. Wachumba wanaweza pia kutafakari juu ya masomo ya Biblia, na maana ya pete watakazobadilishana na ishara mbalimbali zinazopatikana katika madhehebu ya ndoa. Wala haitakuwa vizuri kwao kuifikia siku ya kufunga ndoa huku hawakuwahi kusali pamoja, kuombeana, kuomba msaada wa Mungu ili kuwa waaminifu na wakarimu, kumwuliza Bwana nini anataka kutoka kwao, na kuweka wakfu pendo lao mbele ya taswira ya Bikira Maria. Wale wanaowasindikiza katika maandalizi ya ndoa ingefaa wawaelekeze ili wapate uzoefu wa kusali ambao utaweza kuwafaa sana. “Liturujia ya ndoa ni tukio la pekee, ambalo linaadhimishwa kwa furaha katika mazingira ya kifamilia na kijamii. Ishara ya kwanza ya Yesu ilifanyika katika karamu ya harusi ya Kana. Divai njema, iliyotokana na muujiza wa Bwana na kuleta furaha mwanzoni mwa familia mpya, ni divai mpya ya agano la Kristo na waume kwa wake wa vizazi vyote. [...] Mara nyingi, kiongozi wa ibada anapata fursa ya kuongea na kusanyiko la watu ambao si washiriki wa mara kwa mara wa maisha ya kikanisa, au ni Wakristo wa madhehebu mengine au dini tofauti. Kumbe ni nafasi nzuri ya kutangaza Injili ya Kristo”.[247]

Kusindikiza mwanzoni mwa maisha ya ndoa

217. Ni muhimu ndoa ionekane kuwa ni suala la upendo, na kwamba wale tu ambao wamechaguana kwa uhuru na wanapendana ndio wafunge ndoa. Lakini ikiwa upendo ni mvuto wa kimwili au mahusiano ya juujuu tu, wanandoa wataingia katika hatari pale ambapo ukaribu au mvuto wa sura utapungua. Kutokana na hali hii kutokea mara kwa mara, ni muhimu sana wanandoa wasindikizwe katika miaka ya mwanzo ya maisha yao ya pamoja ili wazidi kusitawisha na kuimarisha uamuzi wao wa dhati na huru wa kuwa kila mmoja wa mwenzake na wa kupendana mpaka mwisho wa maisha. Mara nyingi kipindi cha uchumba hakitoshi, uamuzi wa kufunga ndoa unaharakishwa kwa sababu mbalimbali, na mbaya zaidi vijana wanachelewa kukomaa. Basi, matokeo yake wanandoa wapya wanalazimika kuendelea kumalizia ile safari ambayo ingetakiwa kutimilika katika kipindi cha uchumba.

218. Kwa upande mwingine, napenda kusisitiza kwamba katika uchungaji wa familia changamoto mojawapo ni kusaidia kutambua kwamba ndoa si jambo la siku moja tu basi. Muungano wa wanandoa ni halisi na usioweza kuvunjika kamwe, umethibitishwa na kutakaswa na sakramenti ya ndoa. Lakini katika kuungana kwao, wanandoa wanajikita katika wajibu wa kuendesha maisha yao na katika kubuni mpango wa maisha wa kutimiliza kwa pamoja. Mtazamo wao unaelekezwa kwenye mambo ya mbele yapasayo kujengwa siku kwa siku kwa msaada wa neema ya Mungu. Kwa sababu hiyo, kila mmoja asitegemee mwenzie kuwa mkamilifu. Kila mmoja anapaswa kuweka kando mawazo yasiyo halisi na kumkubali mwenzake kama alivyo: kuwa ni mtu anayeendelea kutimilika na kukua. Ukosoaji mkali wa mara kwa mara kwa mwenzi wa ndoa ni ishara ya kuwa ndoa imefungwa kwa kukosa wazo la kwamba yenyewe ni mpango wa kujenga pamoja maisha, kwa uvumilivu, kuelewana, msamaha na ukarimu. Taratibu upendo utafifia kiasi cha kuanza kukosoana vikali, kuishi kwa kupimana madai na haki, kukaripiana, kushindana na kujitetea. Kisha wanandoa wanajiona kushindwa kusaidiana katika kukomaa kwao na katika kukuza muungano wao. Hali hii inapaswa kudhihirishwa wazi mapema kwa wanandoa wapya, ili watambue kuwa harusi ni “mwanzo tu” wa maisha yao ya pamoja. Kwa kuambiana “ndiyo” wakati wa ibada wameanza safari inayowataka kukabiliana na kushinda magumu na vikwazo vyote vitakavyokuwepo mbele yao. Baraka ya ndoa wanayoipokea ni neema na kichocheo kwa safari hii iliyo mbele yao. Mara nyingi kuketi na kujadili kuhusu mpango wa maisha, kupanga malengo, njia na hatua mbalimbali kunasaidia.

219. Nakumbuka msemo wa zamani: maji yanayotuama yanakuwa mgando na kuharibika. Ni kile kinachotokea endapo katika miaka ya mwanzo ya maisha ya ndoa pendo litapoa, litakosa kuwa kichocheo bora cha kuyakuza na kuyasukuma mbele. Ngoma ya kusonga mbele inayochezwa na upendo mchanga, ngoma ya mshangao uliojaa tumaini isikome kamwe. Wakati wa uchumba na katika miaka ya mwanzo ya maisha ya ndoa matumaini ndiyo kama kichocheo kinachosukuma kutazama mbali zaidi kwa kushinda migogoro, magomvi, mazingira magumu, na kinachowezesha kuona daima mbele. Matumaini ndiyo yanayochochea kila matarajio yetu ili kuendelea katika kukua. Matumaini yenyewe yanatutaka tuishi kikamilifu muda wa sasa, kwa kujitoa kikamilifu kwa maisha ya familia, kwa sababu njia bora ya kuandaa maisha bora ya baadaye ni kuishi vizuri sasa.

220. Safari hii ina hatua mbalimbali ambazo zinatudai kujitoa kwa ukarimu: Hisia za nguvu za kwanza za mvuto zinafungua njia ya kudhihirisha kuwa sasa mwenzangu ni sehemu ya maisha yangu. Kutoka hapa tunaingia katika hatua ya utamu wa kuwa kila mmoja mali ya mwenzie, na baadaye kuyaelewa maisha yote kama mpango wa wote wawili, na uwezo wa kuhakikisha kwanza furaha ya mwenzio, na furaha ya kuona kwamba ndoa hii inaifaidisha jamii. Pendo litakua ikiwa wahusika watajifunza pia “namna ya kufikia mwafaka”. Majadiliano hayo yasipohusishwa na ubinafsi au mchezo wa nipe nikupe, ni njia nzuri ya kuonyeshana upendo, kwa sababu ni mfumo wa kupeana na kujinyima, kwa manufaa ya familia. Katika kila hatua mpya ya maisha ya ndoa, kuna kila haja ya kuketi chini na kurudia makubaliano, ili asiwepo anayeshinda na anayeshindwa, bali wote wawili wawe washindi. Nyumbani, maamuzi yasifanywe na upande mmoja tu, kwani wanandoa wote wawili wana wajibu kwa familia; hata hivyo kila familia ni ya pekee na kila ndoa itatafuta namna bora zaidi itakayowafaa.

221. Miongoni mwa sababu za kuvunjika ndoa ni matarajio makubwa mno juu ya maisha ya ndoa. Pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo na kuleta changamoto kinyume na mtu alivyotegemea, suluhisho si kufikiria haraka na bila busara kufikiria bora kutengana, bali ni kutambua kuwa maisha ya ndoa ni safari ya ukomavu, ambapo kila mmoja ni njia ya Mungu ya kumsaidia mwingine kukua. Mabadiliko, maendeleo, kushamiri kwa mambo mazuri yaliyoko kwa kila mmoja - haya yote yanawezekana. Kila ndoa ni aina ya “historia ya wokovu”, nayo ina maana kwamba inakubalika ianzie katika udhaifu fulani, na ambayo kutokana na zawadi ya Mungu na itikio la wanandoa lenye ubunifu na ukarimu, polepole inageuka kuwa zaidi na zaidi kitu cha thamani na cha kudumu. Tuseme kwa hakika kuwa mkakati mkubwa kati ya watu wawili katika upendo ni kusaidiana na kuwa mwanaume hasa au mwanamke hasa. Kuchochea kukua maana yake ni kumsaidia mtu kujitengeneza kadiri ya utambulisho wake mwenyewe. Kwa sababu hiyo upendo ni jambo la kiufundi. Tunaposoma katika Biblia juu ya kuumbwa kwa mtu, tunamwona Mungu akimwumba kwanza Adamu (Taz. Mwa 2:7); Halafu anatambua kuna kitu muhimu kimepungua, na hivyo anamwumba Eva, na kisha anamsikia mwanaume akisema kwa hisia ya mshangao, “Naam, huyu ndiye anayenifaa!”. Na baadaye ni kama twaweza kusikia yale mazungumzo mazuri sana mwanaume na mwanamke wanapoanza kutambuana. Katika maisha ya wanandoa, hata katika kipindi kigumu, mmoja aweza kumshangaza mwingine, na milango mipya kufunguliwa ili kukutana tena; utadhani ndiyo wanakutana kwa mara ya kwanza. Katika kila hatua mpya, wanarudia “kuundana” wao kwa wao. Upendo hufanya wavumiliane kwa subira kama ile ya fundi, waliyoirithi kwa Mungu mwenyewe.

222. Kuwasindikiza kiuchungaji wanandoa wapya ni pamoja na kuwahimiza kuwa wakarimu katika kurithisha uhai duniani. “Kadiri ya tabia ya ujumla na binafsi ya binadamu juu ya upendo wa kindoa, uzazi wa mpango hufaa kama ni maafikiano ya mazungumzano ya wanandoa, ukizingatiwa muda na hadhi ya kila mmoja. Kwa maana hii, mafundisho ya Ensiklika Humanae Vitae (taz. 10-14) na Wosia wa kitume Familiaris consortio (taz. 14; 28-35) lazima yaangaliwe upya kwa lengo la kuamsha utayari wa kuzaa na kupambana na dhana mbaya dhidi ya uhai […]. Maamuzi yahusuyo uzazi wenye uwajibikaji yanategemea malezi ya dhamiri, ambayo “ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu, na hekalu lake. Humo yeye yumo peke yake pamoja na Mungu, ambaye sauti yake ndimo inamosikika” (Gaudium et spes, 16). Kadiri wanandoa wanavyojitahidi kuisikiliza sauti ya Mungu katika dhamiri na sheria zake (taz. Rum 2:15), na kusindikizwa kiroho, ndivyo maamuzi yao yatakuwa siyo ya kukurupuka na ya kufuata mkondo tu”.[248] Mafundisho yaliyo wazi ya Mtaguso wa pili wa Vatikano bado yana uzito: “Wenzi wa ndoa [...] watajitengenezea fikra zilizo nyofu kwa njia ya kutafakari na juhudi za pamoja, wakiyazingatia manufaa yao wenyewe na ya watoto wao, wale waliokwisha zaliwa kama vile wanaotarajiwa kuzaliwa. Wataipima hali ya maisha ya nyakati zao na ya wao wenyewe kwa upande wa kimwili na wa kiroho. Na hatimaye watautunza utaratibu ulio bora wa manufaa ya familia, ya jamii, na ya Kanisa. Wanandoa wenyewe tu wafanye maamuzi haya mbele ya Mungu.”[249] Kwa upande mwingine, “matumizi ya njia zinazojikita katika ‘mfumo wa asili wa uzazi’ (Humanae Vitae, 11) yakuzwe. Iwekwe wazi kwamba ‘njia hizi zinaheshimu miili ya wenzi, zinachochea kujaliana na kukuza maadili ya uhuru wa kweli’ (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2370)., Daima mkazo uwekwe katika hoja kuwa watoto ni zawadi ya ajabu kutoka kwa Mungu, na furaha ya wazazi na ya Kanisa. Kwa njia yao, Bwana huupyaisha ulimwengu.”[250]

Baadhi ya mbinu za kufanya

223. Mababa wa Sinodi walionelea kuwa “miaka ya mwanzo ya ndoa inahusu kipindi muhimu na makini ambacho wanandoa hutambua changamoto na maana ya maisha ya ndoa. Kwa hiyo msaada (usindikizaji) wa kichungaji unapaswa uendelee kutolewa hata baada ya adhimisho lenyewe la sakramenti (Familiaris Consortio, Sehemu ya III). Katika hili, wanandoa wenye uzoefu wana nafasi nzuri ya kusaidia. Parokia ni mahali ambapo wanandoa hao wenye uzoefu wanaweza kuwasaidia wanandoa vijana, kwa kushirikiana na taasisi, vyama vya kitume na jumuiya mpya. Wanandoa vijana wanahitaji kutiwa moyo kupokea zawadi kubwa ya watoto. Mkazo pia utolewe juu ya umuhimu wa maisha ya kiroho ya familia, sala na ushiriki wa Ekaristi siku za Dominika; wanandoa watiwe moyo kukutana mara kwa mara ili kusaidia maendeleo ya maisha ya kiroho na mshikamano katika mahitaji halisi ya maisha. Liturujia, namna mbalimbali za kusali na adhimisho la Ekaristi kwa ajili ya familia, hasa katika kumbukumbu ya siku ya kufunga ndoa, zimetajwa kama nafasi muhimu sana katika kufanikisha uinjilishaji kupitia familia.”[251]

224. Safari hii huchukua muda. Upendo unahitaji muda ulio wazi na usio na madai; vingine vyote hufuata baadaye. Unahitajika muda kwa kuzungumza, kwa kukumbatiana bila haraka, kwa kushirikishana mipango, kwa kusikilizana, kwa kuangaliana usoni, kwa kutambua thamani ya kila mmoja na kuimarisha uhusiano. Mara nyingine, mambo ya haraka haraka ndani ya jamii na shinikizo la majukumu ya kazi vinaibua matatizo. Nyakati nyingine, tatizo ni kwamba watu hawaishi vizuri muda wanapokaa pamoja. Watu wanaweza kukaa mahali pamoja, lakini bila kujaliana. Wahudumu wa mambo ya kichungaji na makundi ya watu wa ndoa ingetakiwa wasaidie wanandoa wachanga au wanandoa walio hatarini kujifunza kukutana katika nafasi hizo, kutulia mmoja mbele ya mwingine, na pia kushiriki katika nafasi za ukimya zinazomlazimisha kila mmoja aelewe uwepo wa mwenzake.

225. Wanandoa waliojifunza kufanya hili vizuri wanaweza kupendekeza njia na mbinu halisi walizoziona kuwa zinafaa: kupanga muda wa kuwa pamoja bila madai, nyakati za burudani na watoto, namna mbalimbali za kusherehekea matukio muhimu, kushirikishana nafasi mbalimbali za makuzi ya kiroho. Lakini wanaweza pia kufundisha mbinu zitakazosaidia nafasi hizo ziwe na uzito na ziwe za maana zaidi, na hivyo kukuza mahusiano yao. Hii ni hatua muhimu sana wakati upya wa uchumba unapopoa Ikifikia mmoja haoni thamani ya kuwa na muda na mwenzie, basi mmoja au wote watatafuta njia mbadala, atakimbilia kwenye teknolojia, atabuni majukumu mengine, atatafuta ukaribu na mwingine au kutafuta njia nyingine za kuwa mbali na yule ambaye ukaribu wake umemchosha.

226. Wanandoa vijana watiwe moyo kuanzisha mazoea yao, ambayo yatawafanya wajisikie katika hali ya uimara na salama, mazoea yanayojengwa kwa njia ya taratibu za kila siku zinazokubaliwa nao. Ni jambo jema la kila wakati busu la asubuhi, baraka ya jioni, kusubiriana mlangoni na kupokeana, matembezi ya pamoja na kufanya pamoja kazi za nyumbani. Lakini wakati huohuo ni vizuri kusitisha mazoea kwa kufanya sherehe, bila kushindwa kusherehekea nyumbani, kufurahia na kuadhimisha matukio mazuri. Wanahitaji nyakati hizi za kufurahia zawadi za Mungu, na kuongeza kwa pamoja utamu na uchangamfu wa maisha. Tukijua kuadhimisha, uwezo huo unafanya upya nguvu ya upendo, nao hautawaliwi tena na hali ya uchokevu wa kurudiarudia tu bali utajaza mazoea ya kila siku kwa uchangamfu na tumaini.

227. Sisi wachungaji tunapaswa kuzitia moyo familia kukua katika imani. Hii ikihusisha kuwashawishi kufanya mara kwa mara kitubio, kupata maongozi ya kiroho na kufanya mafungo. Pia kushawishi kufanya sala za pamoja za wiki, kwani “familia inayosali pamoja hukaa pamoja”. Tunapowatembelea watu makwao, tusali pamoja wanafamilia kwa ufupi na kuwaalika kuombeana kila mmoja kwa wengine na kuikabidhi familia katika mikono ya Bwana. Wakati huohuo, inafaa kuwatia moyo wanandoa, ili kila mmoja wao ajitafutie nafasi zake za sala peke yake mbele ya Mungu, kwa sababu kila mmoja ana misalaba yake ya siri ya kuibeba. Kwa nini tusimwambie Mungu shida zetu zinazotuhangaisha moyoni, na kumwomba atujalie nguvu za kuponya majeraha yetu, na mwanga tunaohitaji ili kuyakabili majukumu yetu ? Mababa wa Sinodi wamesisitiza kuwa “Neno la Mungu ni chemchemi ya uhai na ya mambo ya kiroho ya familia. Kazi zote za kichungaji kwa ajili ya familia lazima ziruhusu kuundwa kiundani na kuwajenga wanafamilia kama washiriki wa Kanisa la nyumbani kwa kupitia masomo ya tafakari na sala ya Maandiko Matakatifu kwa mtazamo wa Kanisa. Neno la Mungu sio tu ni Habari Njema kwa maisha ya binafsi ya watu lakini pia ni kigezo cha hukumu na mwanga unaopambanua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanandoa na familia.”[252]

228. Katika baadhi ya mazingira, mmoja wa wanandoa hajabatizwa au hataki kuishi imani. Katika hali hiyo, hamu ya mmojawapo kuishi na kukua kama mkristo inasababisha kwamba hali ya kutojali ya mwenzake iwe sababu ya huzuni. Hata hivyo inawezekana kuwa na tunu za kushirikishana pamoja na kuzikuza kwa dhati. Kwa vyovyote, kuonyesha upendo kwa mwenzi asiye mwamini, kumfurahisha, kumfariji katika mateso yake, na kushirikishana maisha pamoja, kunaashiria njia ya kweli ya utakatifu. Upendo, daima ni zawadi ya Mungu, na pale unapoenea hudhihirisha nguvu yake ya kuleta mabadiliko, mara nyingine kwa namna ya kifumbo, hata “mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe” (1Kor 7:14).

229. Maparokia, vyama, shule mbalimbali na taasisi nyingine za Kanisa zaweza kusaidia familia kwa njia mbalimbali ili kuzitunza na kuzistawisha familia. Hii ni pamoja na: mikutano ya wanandoa majirani au marafiki, mafungo ya muda mfupi kwa wanandoa; mafunzo ya wataalamu juu ya mambo halisi yahusuyo maisha ya familia, vituo vya ushauri nasaha wa ndoa, wamisionari walioandaliwa kuwasaidia wanandoa kujadili matatizo yao na shauku zao, huduma za kijamii zinazohusu matatizo ya familia (kama ulevi wa kupindukia, kukosa uaminifu katika ndoa na ukatili wa kinyumbani), nafasi za makuzi ya kiroho, semina kwa wazazi wenye watoto wenye matatizo, na mikutano ya familia. Ofisi ya parokia inapaswa kujiandaa kusaidia na kuwa macho juu ya mahitaji ya familia na kuwa tayari kuelekeza kwa urahisi penye mahali ambapo misaada inapatikana. Pia kuna mchango wa kichungaji unaotolewa katika makundi ya wanandoa, kama huduma na utume, sala, malezi na kusaidiana. Makundi hayo yanawawezesha wanandoa kuwa wakarimu, kusaidia familia nyingine na kushirikishana imani; lakini wakati huohuo wanaziimarisha ndoa na kuzisaidia kukua.

230. Ni kweli kwamba wanandoa wengi, mara baada ya ndoa, wanajitoa katika jumuiya ya Kikristo. Lakini mara nyingi hatutumii fursa ya matukio ambapo hawa wanarudi tena, hapo tungeweza kuwakumbusha juu ya mambo mazuri ya ndoa ya kikristo na kuwavuta katika nafasi ambapo msaada wa usindikizaji huweza kupatikana: naongea, kwa mfano, juu ya Ubatizo na Komunyo ya kwanza ya watoto wao, au mazishi au arusi za ndugu au marafiki. Karibu wanandoa wote wanakuwepo katika matukio haya, na tungeweza kutumia vizuri zaidi fursa hizo. Njia nyingine ya kuwa karibu ni zoezi la kubariki nyumba, au kutembeza manyumbani sanamu ya Bikira Maria; nafasi hizi zinatoa fursa ya kuendeleza mazungumzo ya kichungaji kuhusu hali ya kifamilia. Pia linaweza kuwa jambo linalofaa kuwakabidhi walio katika ndoa kwa muda mrefu jukumu la kuwasaidia wanandoa wapya waishio maeneo ya jirani, kwa kuwatembelea na kuwapa mwongozo wa ukuzi katika miaka yao ya awali ya ndoa. Kutokana na mwendo wa haraka wa maisha ya kisasa, wanandoa walio wengi hawatakuwa tayari kushiriki mikutano ya mara kwa mara; hata hivyo hatuwezi kukubali kuwa na huduma ya kichungaji kwa makundi ya watu wa pekee wachache tu. Siku hizi, uchungaji wa familia unapaswa kuwa wa kimisionari, kuwafuata walengwa mahali walipo. Hatuwezi kuendelea kuwa kama kiwanda cha kuandaa kozi ambazo mahudhurio yake ni hafifu.

Kutia mwanga kwenye migogoro, fadhaa na magumu

231. Neno moja lisemwe kwa wale ambao upendo wao, kama divai njema, baada ya uchumba umefika mahali pake. Kama divai inavyoanza “kuwa nzuri” kadiri muda unavyoenda, pia uzoefu wa kila siku wa uaminifu huyapatia maisha ya ndoa utajiri na utimilifu. Ni uaminifu wa subira na uvumilivu Uaminifu huo uliojaa furaha na sadaka huzaa tunda kadiri miaka inavyoenda na yote “yakomaa” nayo macho yao yanang’aa katika kuwatazama kwa furaha watoto wa watoto wao. Uliokuwako tangu mwanzo, unazidi kudhihirika, kutulia na kukomaa, katika ushangao wa kuugundua siku hadi siku zaidi, mwaka hadi mwaka. Kama alivyofundisha mtakatifu Yohane wa Msalaba, kwamba “wapenzi wa muda mrefu wamejaribika na kuthibitika”. Wao hawatawaliwi tena na “hisia zenye nguvu, na mihemko na moto wa vionjo vya nje, ila kwa sasa wanaonja utamu wa divai ya upendo halisi, iliyochemka tayari na kutulia sasa mioyoni mwao.”[253] Hali hiyo imepatikana kwa sababu wanandoa wamefanikiwa kukabiliana kwa pamoja na migogoro na magumu, bila kuzikimbia changamoto au kuficha matatizo.

Changamoto ya migogoro

232. Maisha ya kila familia hupitia katika migogoro ya kila namna, nayo ni pia sehemu ya uzuri wake. Wanandoa wasaidiwe kutambua kuwa kuushinda mgogoro sio sababu ya kudhoofisha uhusiano wao; isipokuwa kunauboresha na kunautuliza, na kunaifanya divai ya umoja wao kuwa mzuri zaidi. Maisha ya pamoja yasififishe furaha, bali yafundisha kufurahi kwa namna mpya; kila hatua mpya yaweza kuwasaidia wanandoa kupata nafasi mpya ya kufurahi. Kila mgogoro unakuwa ni njia ya kukua pamoja kwa karibu, au walau kuona maana mpya ya maisha ya ndoa. Kamwe wasivumilie kukubali upendo wao upoe, maisha yao yaishie katika hali ya vuguvugu ya kuvumiliana tu. Kinyume chake, pale ndoa inapoeleweka kama jukumu linalohusisha pia kuvishinda vikwazo, kila mgogoro unakabiliwa kama fursa ya kufikia hatua ya kunywa pamoja divai iliyo bora. Ni jambo jema kuwasindikiza wanandoa ili waweze kuikabili migogoro itakayokuja, kupokea changamoto hizo na kutambua nafasi zao katika maisha ya familia. Wanandoa wazoefu na waliokomaa wawe tayari kuwapa wengine msaada wa mwongozo, ili wanandoa wachanga wasitishiwe na migogoro wala wasishawishike kufanya maamuzi ya kukurupuka. Kila mgogoro unaficha habari njema inayopaswa kusikilizwa kwa kuboresha usikivu wa moyo.

233. Tunapokumbana na mgogoro, huwa tunajihami sana haraka, kwa kuwa tunadhani tutapoteza mwelekeo, au tunadhani tuna matatizo katika namna yetu ya kuishi, na hii inatufanya tujisikie vibaya. Tunawahi kulikimbia tatizo, kulificha au kulifanya lionekane dogo tukitumaini litayeyuka kwa kuvuta muda. Lakini hii haisaidii; itafanya hali kuwa mbaya zaidi, kupoteza nguvu na kuchelewesha suluhisho. Vifungo vinalegea na wanandoa wanajiimarisha katika upweke unaoharibu mawasiliano yao ya ndani. Tunapokataa kulikabili tatizo, kinachoharibika zaidi ni mawasiliano. Katika hali hiyo, polepole, upendo na ukaribu wa wanandoa hupungua: yule aliyekuwa "mpenzi wangu” anakuwa "anayenisindikiza katika maisha yangu”, halafu si zaidi ya "baba au mama wa watoto wangu”, na hatimaye ni mgeni tu.

234. Migogoro ikabiliwe kwa pamoja. Hii ni muhimu kwa sababu wakati mwingine watu wanajitenga ili kukwepa kueleza wanavyojisikia; wanakaa kimya tu, lakini ukimya huu si mzuri na unajaa udanganyifu. Katika mazingira ya namna hii ni muhimu sana kutengeneza nafasi ya mazungumzo ya wazi na ya ndani kati ya wote wawili. Tatizo ni kwamba kama wanandoa hawajajifunza mfumo huo mapema, kuja kujifunza wakati migogoro imeshaanza ni vigumu sana. Mtu hujifunza ufundi huo wa kweli wakati wa utulivu, ili usaidie katika kipindi kigumu. Lazima kuwasaidia wanandoa wazitambue sababu zilizofichwa zaidi mioyoni mwao, na kuzikabili kama kuzaa mtoto, hii ni hatua chungu inayoleta hazina mpya. Majibu yaliyotolewa kwenye maandalizi ya sinodi yanaonyesha kuwa wengi wanapopata matatizo au changamoto huwa hawatafuti msaada wa kichungaji kwa kuwa hawaoni kama ni wa msaada, wenye uhalisia, au hawaoni ukaribu wa ndani wa wachungaji. Kwa sababu hiyo, sasa tutajitahidi kuyakabili migogoro ya ndoa kwa umakini mkubwa unaojali uzito wa mateso na fadhaa.

235. Baadhi ya migogoro ni ya kawaida katika kila ndoa, kama kwa mfano migogoro ya mwanzoni, ambapo wanandoa wapya wanapaswa kujifunza jinsi ya kupokea tofauti zao na kuachana na wazazi. Au kama migogoro inayozuka wakati wa kupata mtoto, jambo liletalo changamoto za hisia mpya. Kulea mtoto kunasababisha mabadiliko katika maisha ya wazazi, na kipindi mtoto anapobalehe, kipindi kinachodai nguvu nyingi zitumike, huweza kuwasababishia wazazi shida mbalimbali na hata mvutano kati yao. Mgogoro wa "kiota kitupu”, ambapo wazazi wanalazimishwa kutafakari upya mahusiano yao; mgogoro wa kuwatunza wazazi wa wanandoa katika uzee wao, matunzo hayo yanadai kuwa karibu nao zaidi, umakini zaidi na maamuzi magumu. Hali hizi zote ngumu zaweza kumtisha mtu na kumsababisha kujisikia ana hatia fulani, kuwa na msongo wa mawazo na uchovu wa akili, na hatimaye kusababisha matatizo makubwa kwenye ndoa.

236. Pia kuna migogoro binafsi ambayo huwaathiri wanandoa wote, na hasa inayohusu shida za uchumi, matatizo ya kazini, ya kihisia, ya kijamii na ya kiroho. Mambo yasiyotegemewa yaweza kuibuka na kuathiri maisha ya familia na yanahitaji kusameheana na kupatana. Katika kuwekana sawa kwa njia ya kusameheana, kila mmoja ajiulize kwa unyenyekevu kama mwenyewe hakuchangia kuandaa mazingira yaliyomsukuma mwingine atende makosa. Baadhi ya familia zinaparaganyika kwa sababu ya kurushiana tuhuma, lakini “uzoefu unaonyesha palipo na msaada wa kufaa na upatanisho utokanao na nguvu ya neema, ndoa nyingi zenye matatizo hupata suluhisho muafaka. Kujua namna ya kusamehe na kujisikia umesamehewa ni mazoea msingi katika maisha ya familia.”[254] “Ufundi mgumu wa upatanisho, ambao huhitaji msaada wa neema, unahitaji ushirikiano mzuri wa ndugu na marafiki na hata msaada wa nje na msaada wa wataalamu.”[255]

237. Imekuwa ni jambo la kawaida kufikiri kwamba, ikiwa mmoja hajaridhishwa, au matarajio yake yameyeyuka, basi hii ni sababu tosha kwa kukomesha ndoa. Kama hali ndiyo hii, hakuna ndoa itakayodumu. Wakati mwingine, kwa kuamua kwamba kila kitu kimekwisha inatosha siku moja kutoridhishwa, au kutokuwepo kwa mwenzi wakati anapohitajika sana, au jeraha litokanalo na majivuno (kuaibishwa), au hofu isiyoeleweka. Kuna hali zisizoepukika, zitokanazo na udhaifu wa kibinadamu, lakini zinachukuliwa kihisia kwa uzito mno. Kwa mfano, mmoja wa wanandoa anaweza kujiona kama hachukuliwi kwa uzito kama anavyostahili, wivu na mivutano vinavyoweza kuibuka kati yao, kuvutiwa na wengine, au vivutio vipya vinavyoelekea kuuteka moyo, mabadiliko ya kimwili ya mwenzi. Mambo haya na mengine mengi, kuliko kuwa tishio kwa upendo, ni fursa zinazoelekeza kuufanya upya tena.

238. Katika mazingira hayo, wengine wana ukomavu ule unaohitajika ili kumchagua tena mwingine kama mwenzi katika safari ya maisha, licha ya madhaifu ya uhusiano kati yao, na wanapokea kwa kukubali hali halisi ya kuwa mwenzi hataweza kutekeleza ndoto zote. Watu wa namna hii hukwepa kujiona kama wahenga pekee; huwathamini uwezo wanaopewa na maisha katika familia ingawa mdogo na wenye mipaka, na hufanya kila liwezekanalo kwa kuimarisha kifungo kati yao, kazi ambayo itachukua muda na nguvu. Wanakiri kuwa kila mgogoro unakuwa kama “ndiyo” mpya, inayouwezesha upendo kupyaishwa, kuimarishwa, kukomaa, kupata sura mpya na kung’arishwa. Kutokana na mgogoro inawezekana kupata ujasiri wa kuchimbachimba ili kupata mizizi ya yale yanayotokea, kujadili na kuelewana tena kuhusu makubaliano ya msingi, kufikia muafaka mpya na kusonga mbele pamoja kuelekea hatua nyingine. Kwa msimamo huo wa uwazi, wanaweza kukabiliana na mazingira magumu mengi. Kwa vyovyote, tukitambua kwamba upatanisho unawezekana, tunagundua kwamba “kinachohitajika haraka leo hii ni huduma yenye kuwashughulikia wale ambao uhusiano wao wa ndoa umevunjika.”[256]

Vidonda vya zamani

239. Inaeleweka kwamba familia hukumbana na matatizo mengi pale ambapo mmoja wa wanafamilia hajakomaa katika namna yake ya kuhusiana na wengine, kutokana na majeraha aliyoyapata maishani mwake kuchelewa kuponywa. Kukosa furaha utotoni au wakati wa kubalehe huweza kusababisha matatizo binafsi yanayoathiri ndoa ya mtu. Ikiwa wote wangekuwa watu waliokomaa kawaida, migogoro isingetokea mara kwa mara au isingeumiza sana. Lakini ukweli ni kwamba mara nyingine ni katika miaka ya arobaini hivi, ambapo watu wanafikia kwa kuchelewa ukomavu ambao wangeufikia kipindi cha kubalehe. Mara nyingine watu wanapenda na upendo ule ulio wa mtoto ambao ni wa kibinafsi, umeganda katika hatua ambapo hushindwa kuelewa hali halisi na hudai kwamba wote wamwangalie yeye na kila kitu ni chake. Ni upendo usioridhika ambao huwa na kelele na majonzi pale usipotimiziwa matakwa yake. Mara nyingine upendo umeganda katika kipindi cha kubalehe, ni wenye malumbano, wenye ukosoaji mkali na mazoea ya lawama kwa wengine; unaoongozwa na hisia na ndoto, ambapo watu wa namna hii wanataka wenzao kuwaridhisha kwa kila hitaji wanalotaka.

240. Watu wengi wanatoka utotoni bila kuonja upendo wa dhati. Hali hii inaathiri uwezo wao wa kuwaamini na kujiaminisha kwa wengine, na kujitoa kwao. Mahusiano mabovu na wazazi na ndugu, kama hayajarudi katika hali nzuri, madhara yake yatajitokeza na kuharibu maisha ya ndoa. Basi, lazima kuwa na safari ya ukombozi ambayo haijawahi kufanyika. Kama kati ya wanandoa uhusiano unaanza kuwa magumu, kabla ya maamuzi mazito kuchukuliwa, ni muhimu kuhakikisha kuwa kila mwanandoa ametimiza safari yake ya kuiponya historia yake. Safari hii inadai kutambua uhitaji wa kuponywa, kuomba kwa mkazo kwa ajili ya neema ya kusamehe na kujisamehe, ukubali wa kupokea msaada, na uamuzi wa kutokata tamaa bali kuendelea kujaribu. Kila mmoja lazima awe mkweli kabisa kwa nafsi yake ili aweze kutambua kwamba namna yake ya kupenda ina upungufu. Hata kama ni jambo lililo wazi kuwa mwenye kosa ni mwingine, mgogoro hauwezi kutatuliwa kirahisi kwa kutegemea abadilike yeye mwenyewe tu. Tunapaswa kujiuliza katika maisha yetu ni kipi kinahitaji kukua au kuponywa ili kurahisisha kushinda migogoro.

Kusindikiza baada ya kuvunjika uhusiano wa ndoa na baada ya talaka

241. Katika nafasi nyingine, kwa kuzingatia heshima ya mwenyewe na manufaa ya watoto lazima kuyawekea mipaka thabiti madai ya ajabu ya mwingine, kuzuia ukiukwaji mkubwa wa haki, ukatili au ukosefu wa heshima uliokuwa sugu. Lazima tukiri kwamba “zipo nafasi ambapo kutengana hakuepukiki. Wakati mwingine, kimaadili hatua hii inalazimika, hasa pale inapolazimu kumwepusha mwenzi mwenye hatari zaidi ya kuumia au watoto wadogo wasiumizwe vibaya kwa sababu ya ubabe, ukatili, udhalilishaji na ukandamizaji, utelekezaji na kutokujali.”[257] Hata hivyo, “kutengana kuchukuliwe kuwa ni hatua ya mwisho, baada ya jitihada zingine zote kushindikana.”[258]

242. Mababa wa Sinodi wamegundua kuwa “upambanuzi maalumu ni muhimu sana kwa ajili ya kuwasindikiza kichungaji wale waliotengana, waliopeana talaka na waliotelekezwa. Yapokelewe na kuthaminiwa hasa maumivu ya wale ambao pasipo haki walitengwa, walipewa talaka au kutelekezwa au ya wale ambao wameshinikizwa kuvunja maisha ya pamoja kutokana na minyanyaso waliofanyiwa na mume au mke wao. Kusamehe ukatili huu sio kitu rahisi, ila ni safari inayowezeshwa na neema. Kutokana na hilo kuna haja ya kuwa na huduma ya kichungaji inayolenga upatanisho na mazungumzo kupitia vituo maalumu vya ushauri nasaha majimboni.”[259] Wakati huohuo, “waliopewa talaka na hawajafunga ndoa nyingine, na ambao mara nyingi ni mashahidi wa uaminifu wa ndoa, watiwe moyo kwa kushibishwa na Ekaristi ili wasaidiwe katika hali waliyo nayo. Jumuiya mahalia na Wachungaji wawe karibu na kuwasindikiza watu hawa, na hasa kukiwa na watoto au wanapobanwa sana na umaskini.”[260] Kuvunjika kwa familia kunakuwa mbaya zaidi na kunaleta maumivu zaidi katika hali ya umaskini, kwani wana vitu vichache vya kuweza kuanza maisha mapya. Mtu maskini, akiondolewa katika mazingira salama ya familia, hali yake huwa mbaya mara mbili zaidi kutokana na upweke na hatari ya kila aina kwa usalama wake.

243. Ni muhimu kwamba waliotalikiana na kuwa na mwenzi mpya waendelee kujiona ni sehemu ya Kanisa. Kwamba “hawajatengwa na Kanisa” na wasifanywe kana kwamba wametengwa, kwani wanaendelea kuwa sehemu ya ushirika wa Kanisa.[261] Hali hizi “zinahitaji upambanuzi makini na ukaribu wenye heshima kubwa. Lugha au tabia yoyote itakayoashiria kuwadharau iepukwe, na watiwe moyo kushiriki katika maisha ya jumuiya. Matunzo yanayotolewa na jumuiya ya Kikristo kwa watu wa namna hiyo yasichukuliwe kuwa ni kudhoofisha imani na ushuhuda juu ya kutovunjika kwa ndoa; bali kwa njia ya matunzo hayo inadhihirisha mapendo yake.”[262]

244. Tena, idadi kubwa ya Mababa wa Sinodi “wamesisitiza ulazima wa kufanya taratibu za kesi za kutangaza ubatili wa ndoa kuwa nyepesi zaidi na ikiwezekana ziendeshwe bila kudai malipo.”[263] Mwendo wa polepole wa hukumu hizo unachosha na kuweka watu katika hali mbaya. Nyaraka zangu mbili za hivi karibuni zinazojikita katika mambo haya[264] zimerahisisha hatua za kutangaza ndoa batili. Kupitia nyaraka hizo, nilipenda “kuweka wazi kuwa askofu mwenyewe, katika Kanisa analolichunga na kuliongoza, ni hakimu wa waamini waliokabidhiwa kwake.”[265] Hivyo, “utekelezaji wa nyaraka hizi ni wajibu mkubwa wa maaskofu mahalia majimboni, ambao wameitwa ili kutoa wenyewe hukumu katika baadhi ya kesi na kwa vyovyote kuhakikisha waamini wanarahisishwa kupata haki zao. Hii inadai kuwaandaa watenda kazi wa kutosha, waklero na walei, ambao katika utendaji wao wataweka kipaumbele kwa huduma hiyo ya kikanisa. Huduma za taarifa, ushauri na mazungumzano zinazohusiana na uchungaji wa familia zinapaswa ziwafikie wale waliotengana au walio katika mgogoro. Huduma hizi zaweza kuhusisha mapokezi ya watu kwa uchunguzi wa awali wakati wa kuanzisha kesi ya ndoa. (taz. Mitis Iudex, art. 2-3).”[266]

245. Mababa wa Sinodi pia waliangazia “madhara ya kutengana au kutalikiana kwa watoto, ambao kwa vyovyote ni wahanga wasio na hatia”.[267] Pamoja na mambo mengine yote, maendeleo ya watoto yapewe kipaumbele zaidi, na yasifunikwe kamwe na madai au malengo mengine. Natoa ombi hili kwa wazazi waliotengana: “Kamwe, kamwe, kamwe msithubutu kuwafanya watoto wenu mateka! Mlitengana kwa matatizo na sababu nyingi. Maisha yamewapa haya majaribu, lakini watoto wenu wasiwe wahanga wa kutengana kwenu wala wasitumike kama mateka dhidi ya mwenzi wa ndoa. Wakue wakimsikia mama yao akinena mazuri juu ya baba yao, hata kama hawako pamoja, na baba akinena mazuri juu ya mama.”[268] Huwa sio sawa kumdhalilisha mwenzi ili watoto wakupende zaidi wewe, au kumlipizia kisasi au kujifanya mwenye haki. Kwa kufanya hivi, watoto wataumizwa kwa ndani, na vidonda hivi huwa vigumu kupona.

246. Kanisa, ingawa linaelewa mazingira ya migogoro ndani ya ndoa, haliwezi kukoma kuwa sauti ya walio dhaifu zaidi ambao ni watoto wanaoumia, mara nyingi kimyakimya. Leo, “pamoja na utaalamu na maendeleo yote ya kisaikolojia, najiuliza kama hatujapigwa ganzi ili tusijali majeraha ya roho za watoto. […] Tunatambua mzigo mkubwa wa kisaikolojia unaowaangukia watoto katika familia ambapo ndugu wanajeruhiana kiasi cha kuvunja uaminifu wa ndoa?”[269] Mazingira hayo mabaya hayawasaidii watoto kukua vema kuelekea katika majukumu ya kudumu. Kwa sababu hiyo, jumuiya za Kikristo zisiwatelekeze wazazi waliotalikiana na kuungana na mwenzi mpya, bali wawakumbuke na kuwasaidia katika kazi yao ya malezi. Kwa kweli, “tutawezaje kuwatia moyo wazazi hawa waendelee kuwalea watoto kikristo, na kuwaonyesha mfano wa maisha ya imani hai, ikiwa tumewaweka mbali na maisha ya jumuiya kana kwamba wametengwa na Kanisa? Lazima tuangalie namna ya kutozidisha mizigo ambayo tayari watoto, katika mazingira kama haya, wameshaibeba!”[270] Kusaidia kutibu majeraha ya wazazi na kuwapokea kiroho, ni faida kwa watoto pia, ambao wanahitaji kuuona uso wa kifamilia wa Kanisa katika kipindi hiki kigumu kwao. Talaka ni uovu, na ongezeko kubwa la talaka linahangaisha sana. Kumbe wajibu wetu muhimu wa kichungaji juu ya familia ni kuuimarisha upendo, na kusaidia kutibu majeraha; kwa namna hiyo tunaweza kuweka kinga dhidi ya uenezaji wa janga hilo la nyakati zetu

Baadhi ya mazingira magumu

247. “Masuala yahusuyo ndoa ya mseto yanahitaji jicho la pekee. Ndoa baina ya Wakatoliki na wabatizwa wengine “ingawa ni za namna yake ya pekee, zina vitu vingi ambavyo vyaweza kuthaminiwa na kuendelezwa, kutokana na thamani yake yenyewe, na pia kwa mchango ambao zaweza kutoa kwa ajili ya mchakato wa kiekumeni”. Kwa lengo hili, “juhudi zifanywe kuimarisha [...] mahusiano kati ya mhudumu mkatoliki na yule asiye mkatoliki, kuanzia kipindi cha maandalizi ya ndoa mpaka siku ya ndoa yenyewe’ (Familiaris Consortio, 78). Kuhusu kushiriki Ekaristi, “maamuzi ya wasio Wakatoliki katika ndoa kuweza kupokea Ekaristi yafuate taratibu zilizopo za kisheria, kwa Wakristo wa Mashariki na Wakristo wengine, na hasa kwa kuzingatia hali hii ya pekee, yaani kwamba wanapokea sakramenti ya ndoa ya kikristo wawili ambao ni wakristo waliobatizwa. Ingawa wanandoa katika ndoa ya mseto wanashiriki sakramenti ya ubatizo na ya ndoa, ushiriki katika Ekaristi ni jambo la pekee na, kwa vyovyote, taratibu zilizowekwa zifuatwe.” (Baraza la Kipapa la ukuzaji wa Umoja wa Kikristo, Mwongozo wa matumizi ya kanuni na maadili ya ekumeni, 25 Machi 1993, 159-160).”[271]

248. “Ndoa za watu wenye dini tofauti zinatoa fursa mahususi kwa mazungumzano kati ya dini tofauti [...], zinaambatana na shida maalumu zinazohusu utambulisho wa Kikristo wa familia, na malezi ya kidini ya watoto. [...] Idadi ya watu wanaofunga ndoa na watu wa dini nyingine inaongezeka sana hasa katika maeneo ya kimisioni na hata katika nchi zenye utamaduni wa Kikristo kwa muda mrefu. Familia hizo zinahitaji haraka iwezekanavyo, matunzo mbalimbali ya kichungaji kadiri ya mitizamo ya kijamii na kitamaduni ya eneo mahalia. Katika baadhi ya nchi ambazo hazitambui uhuru wa dini, mwenzi mkristo analazimishwa abadili dini ili aweze kufunga ndoa, na hivyo hawezi kuadhimisha ndoa baina ya wenzi wa dini tofauti kadiri ya sheria ya Kanisa na hata kubatiza watoto. Lazima tuhimize tena juu ya umuhimu wa uhuru wa dini kuheshimiwa kwa watu wote.”[272] “Uangalizi maalumu uwekwe kwa wale ambao waingia ndoa za namna hiyo, sio tu katika kipindi kabla ya ndoa. Changamoto za pekee huwakumba wanandoa na familia ambazo mwanandoa mmoja ni mkatoliki na mwingine hana dini. Katika hali hiyo, ushuhuda wa uwezo wa Injili kupenya katika mazingira hayo utawezesha malezi yanayofaa kwa watoto katika imani ya Kikristo.”[273]

249. “Matatizo ya pekee huibuka pale ambapo watu walioko katika ndoa za aina yake wanataka kubatizwa. Tunaongea kuhusu watu ambao wamefunga ndoa wakati walau mmoja kati yao alikuwa hana ufahamu juu ya imani ya Kikristo. Katika hali hizo, Maaskofu wanatakiwa kufanya upambanuzi wa kichungaji ambao yanaendana na manufaa ya roho zao.”[274]

250. Kanisa linaiga kwa dhati kabisa msimamo wa Bwana Yesu, ambaye kwa upendo usio na mipaka amejitoa afe kwa ajili ya kila mtu bila ubaguzi.[275] Pamoja na Mababa wa Sinodi niliangalia hali za familia ambapo ndani yake wapo watu wenye mwelekeo wa ushoga, hali ambayo ni mgumu kwa upande wa wazazi na wa watoto pia. Tungependa kwa mara nyingine tena kusisitiza kuwa, pasipo kujali mwelekeo wake wa kijinsia, kila mtu anastahili kupewa heshima kwa utu wake na anastahili kupokelewa kwa heshima na hivi “kila hali ya ubaguzi usio haki”[276] iepukwe, na hasa kila aina ya mashambulizi na ukatili. Familia za namna hii lazima zipewe kwa heshima huduma za kichungaji, ili wale wenye mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja wapate msaada wanaouhitaji ili katika maisha yao wayatambue na kuyatekeleza kikamilifu mapenzi ya Mungu.[277]

251. Katika kujadili hadhi na utume wa familia, Mababa wa Sinodi waliona kuwa “kuhusu mipango ya kutambua muungano kati ya watu wa jinsia moja kuwa sawa na ndoa, hakuna sababu za msingi za kuweka katika hadhi sawa au ya mfanano baina ya mapenzi ya jinsia moja na ndoa katika mpango wa Mungu juu ya ndoa na familia”. Haikubaliki, “kwa Makanisa mahalia kushinikizwa katika mambo haya, na mashirika ya kimataifa kupanga kutoa misaada kwa masharti kwa nchi maskini ikiwa tu zinaweka sheria za uanzishwaji wa ‘ndoa’ za jinsia moja.”[278]

252. Familia za mzazi mmoja mara nyingi zinatokana na “kutokuwa tayari kwa baba na mama halisi kuwa sehemu ya familia, mazingira ya ukatili ambapo mzazi mmoja analazimika kukimbia na watoto; kifo cha mmoja wa wazazi; kutelekezwa kwa familia na mmoja wa wazazi, na mazingira mengine. Kwa sababu yoyote ile, mzazi mmoja anayekaa na mtoto inabidi atiwe moyo na apate msaada kutoka familia nyingine za jumuiya ya Kikristo, na kutoka taasisi za kichungaji za parokia. Mara nyingi, familia hizi hukutana na magumu, kama matatizo mazito ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, shida katika kutunza watoto, ukosefu wa makazi.”[279]

Maumivu makali ya kifo

253. Wakati mwingine maisha ya familia yanapata changamoto kwa wanafamilia kuondokewa na mpendwa wao. Tusiache kutoa mwanga wa imani kwa kuzisindikiza familia zilizo katika huzuni kwa matukio kama haya.[280] Kuipa kisogo familia yenye majonzi kutokana na msiba ni kutokuonyesha huruma, kukosa nafasi ya kichungaji, na hali hiyo inaweza kufunga milango kwa juhudi za uinjilishaji.

254. Natambua maumivu ya aliyefiwa na mpendwa wake, mwenzi aliyeshiriki naye mengi. Yesu mwenyewe aliguswa sana hadi alilia kwa kifo cha rafiki yake (taz.. Yn 11:33,35). Na tunawezaje kushindwa kuelewa kilio cha wazazi waliopotewa na mtoto wao? Maana, “ni kama siku haziendi kabisa: ni shimo linalomeza ya jana na ya kesho”, [...] na wakati mwingine tunaenda mbali zaidi, hata kumshtaki Mungu. Wapo watu wengi tu - nawaelewa – ambao wana hasira na Mungu.”[281] “Hali ya ujane ni vigumu kuuvumilia. [...] Wengine wana juhudi za kuelekeza nguvu zao zote katika malezi ya watoto na wajukuu; na katika hali hii ya upendo wanakuta namna nyingine ya kuwa walezi. Wale wasio na ndugu wa kukaa nao na kuwasaidia au kupata faraja kutoka ukaribu wao, wasaidiwe na jumuiya ya kikristo kwa jicho la pekee, na hasa wakiwa katika hali ngumu ya umaskini.”[282]

255. Katika hali ya kawaida, msiba huchukua muda na pale mchungaji anapoungana nao wafiwa, anapaswa kuendana na mahitaji ya kila hatua waliyofikia wafiwa. Safari nzima inagubikwa na maswali: juu ya sababu za kuondokewa na mpendwa wao, juu ya yote ambayo yangaliweza kufanyika, juu ya hali aliyo nayo mtu wakati wa kifo... Kwa moyo wa utulivu na uvumilivu kwa njia ya sala kutoka moyoni, amani hupatikana. Kwenye msiba, tunafikia mahali ambapo tunapaswa kuwasaidia wafiwa watambue kuwa, baada ya kumpoteza mpendwa wao, bado wana kazi za kufanya, na haisaidii kurefusha muda wa uchungu, kana kwamba ni tendo la kumheshimu marehemu. Mpendwa wetu marehemu hahitaji sisi tuteseke, wala hafurahi kuona tunaharibu maisha yetu. Wala sio njia nzuri ya kuonyesha upendo kwa marehemu wetu kuendelea kumlilia muda wote na kumtaja kwa jina muda wote, kwa sababu inamaanisha kwamba tumeganda katika yaliyopita, badala ya kuonyesha upendo kwa mtu halisi ambaye tayari anaishi peponi. Hawezi kuendelea kuwa nasi kimwili, lakini, ingawa mauti na kifo kina nguvu, “upendo una nguvu kama mauti” (Wim 8:6). Upendo unatuwezesha kusikia na kuona visivyosikika na kuonekana. Hii haimaanishi kuwaona wapendwa wetu kama walivyokuwa, bali kuwa tayari kupokea mabadiliko yao, na hali kama walivyo sasa. Yesu mfufuka, wakati rafiki yake Maria alipotaka kumkumbatia, alimwambia asimshike (taz. Yn 20:17), ili amwongoze katika namna nyingine ya kukutana naye.

256. Inatufariji kujua kuwa wale waliotangulia hawapotei kabisa, na imani inatuhakikishia kwamba Bwana mfufuka hatatutelekeza kamwe. Kwa hiyo, tunaweza kufanya kifo na msiba usiue maisha yetu, kutufanya tushindwe kuonyesha upendo na kutuzamisha katika giza nene ”.[283] Biblia inatuambia kuwa Mungu alituumba kwa sababu ya upendo na kufanya maisha yetu yasiyeyushwe na kifo (taz. Hek 3:2-3). Mtakatifu Paulo anazungumza nasi juu ya kukutana na Kristo mara baada ya kufa: “Ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo” (Flp 1:23). Pamoja na Kristo, baada ya kifo, tunasubiria “yale Mungu aliyowaandalia wampendao” (taz. 1Kor 2:9). Utangulizi wa Liturujia ya wafu unasema vizuri sana: “Sisi tunaosikitika kwa sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, tufarijiwe kwa ahadi ya uzima wa milele. Maana, uzima wa waamini wako, ee Bwana, hauondolewi, ila unageuzwa tu”. Kimsingi, “wapendwa wetu hawajapotelea mahali pasipo na maana; tumaini linatuhakikishia kuwa wako katika mikono iliyojaa mema na thabiti ya Mungu”.[284]

257. Njia mojawapo ya kuendeleza mahusiano na wapendwa wetu waliofariki ni kuwaombea.[285] Biblia inatuambia kuwa “kuwaombea marehemu” ni “tendo la uchaji na utakatifu” (taz. 2Mak 12:44-45). Sala yetu kwao “ina nguvu siyo tu ya kuwasaidia, lakini pia ya kuwafanya kuwa waombezi wetu wa dhati.”[286] Kitabu cha Ufunuo kinatoa taswira ya mashahidi wakiwaombea wale walionyimwa haki hapa duniani (taz. Ufu 6:9-11), wakishikamana na ulimwengu huu ulio safarini. Baadhi ya watakatifu, kabla ya kufa, waliwafariji wapendwa wao kwa kuwaahidi kwamba watakuwa karibu nao na kuwasaidia. Mtakatifu Teresa wa Lisieux alijisikia kuendelea kuwatendea mema tokea mbinguni wapenzi wake.[287] Mtakatifu Dominiko alisema kwamba “atatusaidia zaidi baada ya kufa, [...] mwenye nguvu zaidi wa kupatia neema”.[288] Ni vifungo vya upendo,[289] kwa sababu “umoja wa wale wanaosafiri duniani na wa ndugu waliolala katika amani ya Kristo haukatiki hata kidogo, kinyume chake, […] huimarishwa kwa kubadilishana mema ya kiroho”.[290]

258. Tukikubali kifo, tunaweza kujiandaa nacho. Njia yenyewe ni kukua katika upendo kwa wale wanaotembea pamoja nasi, mpaka siku ambapo “mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena” (Ufu 21:4). Hivyo tutajiandaa pia kukutana tena na wapendwa wetu waliotutangulia. Kama vile Yesu alivyomrudisha kwa mama yake mtoto wake aliyekuwa amekufa (taz. Lk 7:15), vivyo hivyo atafanya na sisi. Tusipoteze nguvu kwa kuwaza sana yaliyopita. Kadiri tunavyoishi vema katika dunia hii, ndivyo tutakavyofurahia pamoja na wapendwa wetu huko mbinguni. Kadiri tunavyokua vema na kusonga mbele katika dunia hii, ndivyo tutakavyokuwa na vitu vizuri vya kutolea katika karamu ya mbinguni.

SURA YA SABA

KUIMARISHA MALEZI KWA WATOTO

259. Wazazi wana wajibu mkubwa siku zote katika mafundisho ya kimaadili ya watoto, kwa wema na ubaya. Kwa hiyo, kitu cha msingi ni kupokea wajibu huo usiokwepeka na kuutekeleza kwa dhamira, furaha, akili na uzuri. Na kwa sababu jukumu hili la familia la kulea ni la muhimu hivi na linaendelea kuwa na changamoto nyingi, ningependelea nitumie fursa hii ya pekee kulijadili hilo.

Watoto wako wapi?

260. Familia haiwezi kamwe kujinyima kuwa mahali pa msaada, usindikizaji na uongozi, hata kama itapaswa daima kutumia ubunifu ili kutafuta njia mbadala na maarifa mapya. Inahitaji kuandaa mwelekeo mzima wa maisha ya watoto wake. Na kwa malengo hayo haiwezi kukwepa kujiuliza juu ya wale wanaowashughulikia katika michezo na maburudisho, wale wanaoingia katika makazi yao kupitia luninga, wale wanaokabidhiwa majukumu ya kuwaongoza wakati wa mapumziko yao. Ni wakati ule hasa tunaokuwa nao, tukiongea lugha rahisi na yenye mapendo juu ya mambo muhimu, na pia nafasi nzuri tunayojitengea ili wapate kutumia vyema muda wao, ndivyo vitakavyoruhusu kukwepa nafasi zinazowapotosha. Kuna umuhimu sikuzote wa kuwa macho. Kuwaacha hakusaidii hata kidogo. Wazazi wanatakiwa kuelekeza na kuandaa watoto na vijana ili waweze kujua namna ya kukabiliana na mazingira hatarishi, kama vile hatari za kushambuliwa, kudhalilishwa kingono au kupatiwa madawa ya kulevya.

261. Hata hivyo ufuatiliaji uliokithiri si malezi, na haiwezekani kufuatilia na kuhakiki kila mazingira ambayo mtoto anayapitia. Hapa ni msingi kuzingatia kuwa “muda unazidi nafasi”.[291] Hii inamaanisha kuandaa mifumo endelevu ya malezi kuliko kuyadhibiti mazingira. Kama mzazi ni mfuatiliaji aliyekithiri na anataka kujua kila sehemu alipo mtoto wake na anahakiki chochote kile atakachokifanya, atatafuta tu namna ya kudhibiti mahali pake binafsi pa kuishi. Na kwa namna hiyo hatamfundisha, hatamwimarisha, na hatamwandaa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto. Cha msingi ni kuzalisha katika maisha ya mtoto, kwa mapendo makuu, michakato ya kukomaza uhuru wake, ya kumwandaa kijana akue kijumla, na kumjengea mazingira ya uwajibikaji katika kila analolifanya. Kwa namna hiyo tu yule mtoto atajijengea ndani yake ile hali anayoihitaji kwa ajili ya kujilinda na kuamua kwa akili na busara katika mazingira magumu. Kwa hiyo swali la msingi siyo tu mahali alipo mtoto wako, au yuko na nani, ila amefikia wapi katika mpango mzima wa kimaisha, wapi anakoelekeza mawazo yake, malengo yake na matazamio yake katika utaratibu mzima wa maisha yake. Ndiyo sababu maswali ninayowauliza wazazi ni haya: “Tujaribu kujiuliza ‘ni wapi’ watoto wetu wanakoelekea katika safari yao ya maisha? Tunafahamu kweli moyo wao uko wapi? Na zaidi sana: je, tunataka kujua kwelikweli?”[292]

262. Kama kukua ingekuwa tu ni suala la maumbile ambalo lipo tayari kwenye mfumo wa jene, hatungekuwa na cha kufanya. Busara, maamuzi sahihi na dhamira safi havitegemei kuongezeka kwa miaka, bali ni ule mlolongo mzima wa hatua za kujilea zinazokuja kuunda utu wa ndani, na, hasa, kiini cha uhuru wake. Haikwepeki kwamba kila mtoto hutushangaza kwa mipango inayotokana na uhuru huo, kwamba anavunja taratibu zetu, na hilo ni jambo jema litokee. Malezi ni pamoja na juhudi ya kuchochea matumizi ya uhuru kwa kuwajibika, ambao katika njia panda uweze kuongoza kufanya maamuzi kwa busara na akili. Ni kuandaa watu wanaoelewa bila vipingamizi kwamba maisha yao e yale ya jumuiya yao yapo mikononi mwao na kwamba uhuru huo ni zawadi kubwa sana.

Mafundisho ya kimaadili kwa watoto

263. Haka kama wazazi wana uhitaji mkubwa wa shule ili kuhakikisha mafundisho ya msingi kwa watoto wao, hawawezi kamwe kuukabidhi wajibu wa malezi ya kimaadili. Kukua kimapendo na kimaadili kwa mtu kunategemea mang’amuzi haya ya msingi: kuamini kuwa wazazi wako wanaweza kuaminika. Hilo linajumlisha wajibu wa kimalezi: kwa mapendo na mifano imani hujengeka katika watoto, na kuamshwa ndani yao heshima yenye mapendo. Mtoto anapohisi kutopendeka na wazazi wake kwa sababu ya mapungufu yake, au haonji kama wao kiukweli wanahangaika juu yake, jambo hilo litamjengea madonda makubwa ndani yake yanayosababisha magumu mengi katika makuzi yake. Kutokuwepo huko, kutelekezwa kimapendo, kunasababisha machungu ya ndani makali zaidi kuliko karipio linalotolewa mbele ya tendo baya.

264. Wajibu wa wazazi unahusisha kuelimisha moyo, kusitawisha mazoea mazuri na desturi njema ya kupenda kutenda mema. Hii inamaanisha kuonyesha kama za kutamaniwa desturi za kujifunza na mielekeo ya kukomazwa. Lakini hayo daima ni mchakato unaoanza kwenye mapungufu kuelekea kwenye ukamilifu. Hamu ya kulandana na jamii au mazoea ya kujinyima ridhaa ya papo hapo, kwa lengo la kuheshimu taratibu zilizopo na kujihakikishia maisha mema ya pamoja, hii ni dalili tosha kuwa ndani yake kuna thamani kianzio inayoandaa mazingira kwa ajili ya kukua kuelekea tunu kubwa zaidi. Malezi ya kimaadili inabidi siku zote yatimilike na njia hai na majadiliano ya kimalezi yanayohusisha hisia na lugha zilizo maalumu kwa watoto. Zaidi ya hayo, malezi hayo ni lazima yafanyike kwa mtindo wa dhamiri, kiasi cha kumfanya mtoto aweze kufikia kutambua mwenyewe umuhimu wa maisha yanayoongozwa na maadili, kanuni misingi na sheria, badala ya kumlazimisha azishike kama ukweli usiopingika.

265. Ili kutenda vema haitoshi “kuhukumu inavyotakiwa” au kuelewa wazi nini cha kufanya, ingawa hayo ni utangulizi muhimu. Mara nyingi mienendo yetu ya maisha haiendani na mawazo yetu, hata yakiwa thabiti kabisa. Hata kama dhamiri inatuongoza katika kufanya maamuzi ya kimaadili, mara nyingine kinachochukua uzito zaidi ni vitu vingine tu vinavyotuvutia, ikiwa tutakuwa hatujajijenga kuwa wema tuliouelewa kwa akili zetu lazima uote mizizi ndani yetu kama mwelekeo wa hisia zetu, kama uzoefu wa kutamani utamu wa wema kuliko vivutio vingine na unaotufanya tuhisi kwamba yale tuliyoyaona kama wema ni wema hata “kwa ajili yetu” hapahapa na sasa hivi. Malezi mazuri ya kimaadili yanamwonyesha mtu jinsi ilivyo vyema kwake pia kutenda mema. Mara nyingi siku hizi haisaidii kuagiza kitu kinachodai juhudi na sadaka, bila kuonyesha kwa uwazi wema ambao ungeweza kupatikana kwa kutenda vile.

266. Ni muhimu kukomaa katika mazoea mazuri. Hata desturi za kurithi toka utotoni zina malengo mazuri, kwani zinaruhusu maadili mazuri waliyojifunza yatafsiriwe katika matendo ya nje yaliyo sahihi na thabiti. Mmoja anaweza kuwa mchangamfu na mwenye mwelekeo wa urahisi kwa wengine, ila kama kwa muda mrefu hajajizoesha kupitia mafundisho ya wakubwa kusema, “tafadhali”, “samahani”, “asante”, tabia yake njema ya ndani haiwezi kutafsiriwa vyema na kuonekana. Kukomaza maamuzi na kurudia baadhi ya matendo kunatengeneza maisha ya kimaadili, na bila marudio ya dhati, huru na yanayokubalika ya baadhi ya matendo mema haiwezekani kutimiza malezi ya tabia njema kama hiyo. Shauku, au mvuto tunaosikia kwa tunu fulani ya kimaadili, haviwezi kuwa fadhila bila ya kuwepo matendo hayo yanayosukumwa na uthabiti.

267. Uhuru ni kitu cha thamani kubwa sana, ila tunaweza kuupoteza. Malezi ya kimaadili ni kupalilia uhuru kupitia mapendekezo, maelezo, utendaji, vichocheo, zawadi, mifano, ishara, alama, tafakari, maonyo, marudio ya mitindo ya kuishi na majadiliano yanayowasaidia watu kuziendeleza zile kanunimsingi imara za ndani zinazoweza kusukuma ili wema utendeke kwa hiari kabisa. Fadhila ni dhamiri fulani iliyogeuka kuwa sababu ya ndani na thabiti ya kutenda. Kwa hiyo, maisha yenye fadhila yanajenga uhuru, yanauimarisha na kuulea, yakikwepa kumfanya mtu awe mtumwa wa mielekeo iliyolazimishwa mbali na utu wake na yenye kuchukia kuishi kijamii. Kiuhalisia hadhi yenyewe ya binadamu inamtaka kila mtu “atende kadiri ya chaguo lake kwa kujua na kwa uhuru; yaani awe amesukumwa na kuhimizwa kutoka ndani”.[293]

Umuhimu wa adhabu kama kichocheo

268. Vivyo hivyo, ni lazima kuwahimiza watoto na vijana ili watambue kuwa matendo mabaya yana madhara yake. Inafaa kuamsha ile ari ya kujiweka mahali pa mwingine na kujutia kwa ajili ya uchungu tuliomsababishia kwa kumtendea mabaya. Adhabu nyingine - kwa ajili ya matendo ya ukatili dhidi ya jamii - zinaweza kusaidia ili kufikia malengo hayo. Ni muhimu kumwongoza mtoto kwa msimamo ajifunze kuomba msamaha na kulipia fidia ya madhara aliyosababisha kwa wengine. Pale ambapo utaratibu wa malezi unaonyesha matunda hasa katika kukua kwa uhuru binafsi, mtoto mwenyewe ataanza kutambua kwa shukrani kwamba ilikuwa ni vizuri kwake kukua katika familia na kuvumilia magumu aliyolazimishwa kuyatekeleza wakati wa malezi yake.

269. Kuonya ni kichocheo endapo papo hapo tunathamini na kufahamu juhudi za mtoto na endapo yeye anagundua kwamba wazazi wake wanadumu kuwa na tumaini kwake kwa uvumilivu. Mtoto anayeonywa kwa mapendo anajisikia kuthaminiwa, anajitambua kuwa wa maana, anahisi kuwa wazazi wake wanatambua pia vipaji vyake. Hali hii haiwataki wazazi wasiwe na kosa, ila kwamba watambue kwa unyenyekevu mapungufu yao na waonyeshe juhudi zao katika kuwa wazazi wema. Ila ushuhuda ambao watoto wanahitaji kuona kutoka kwa wazazi wao ni kwamba wasiongozwe na hasira. Mtoto anayetenda tendo ovu, anatakiwa kurekebishwa, ila kamwe kama adui au kama mmoja wa kumtupia hasira binafsi. Zaidi ya hayo, mtu mzima anapaswa kutambua kuwa baadhi ya matendo mabaya yanaendana na udhaifu na mapungufu ya umri wa utoto. Kwa sababu hiyo tabia ya kutoa adhabu za mara kwa mara inaharibu, wala haisaidii kuelewa tofauti ya uzito iliyopo katika matendo mbalimbali, nayo inaweza kusababisha kukata tamaa na uchungu: ’’Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu” (Efe 6:4; taz. Kol 3:21).

270. Kitu cha muhimu ni kwamba kanuni za nidhamu zisigeuzwe kukatisha matamanio, ila ziwe kama kichocheo cha kwenda daima mbele zaidi. Ni namna gani tuunganishe kanuni za nidhamu na mhemuko wa ndani? Kwa namna gani kuweza kuifanya sheria iwe ni kizingiti cha kujenga njia ambayo mtoto anatakiwa kupitia na siyo ukuta wa kumpoteza au sehemu ya malezi yanayomdhoofisha? Inafaa kutafuta uwiano kati ya mipaka hiyo miwili inayoharibu: Kwa upande mmoja ni kule kudhani kwamba lazima kumtengenezea kijana ulimwengu unaoendana na matamanio yake, mtoto anayekua akidhani kuwa yeye ndiye mwenye haki tu, wala si wajibu. Au pia kumlea kijana aishi bila kutambua hadhi yake, upekee wake na haki zake, anayeteswa na wajibu na anayetakiwa tu kutimiza matakwa ya wengine.

Kukubali hali halisi kwa uvumilivu

271. Malezi ya kimaadili ni pamoja na kuagiza kwa mtoto au kijana mambo yale tu ambayo kwake siyo sadaka isiyowezekana, na kudai tu kiwango kile cha juhudi kisichomletea chuki au kufanya matendo ya kulazimishwa tu. Njia ya kawaida ni kumshauri hatua ndogondogo ambazo zinaeleweka, zinakubalika na kuthaminika, na zinazomsababishia sadaka inayowezekana. Tofauti na hapo, kutaka zaidi ni kutopata kitu. Huyo mtu pale atakapoweza kujikomboa na mwenye mamlaka, pengine ataacha kutenda vizuri.

272. Malezi ya kimaadili mara nyingine yanasababisha dharau inayotokana na mazoea ya kutelekezwa, kukata tamaa, ufinyu wa upendo, au picha mbaya ya wazazi. Kuelekeza kwenye tunu za kimaadili picha za ovyo za baba na mama, au mapungufu ya wakubwa. Ni kwa sababu hiyo lazima kusaidia vijana wanaokua kuweka kimatendo ulinganifu huu: tunu za kimaadili zinatimilizwa hasa na baadhi ya watu maarufu, lakini pia zaweza kutekelezwa kwa namna zisizo kamili na katika kiwango tofauti. Pia, kwa kuwa upinzani wa vijana unatokana na uzoefu mbaya, inafaa kuwasaidia watembee katika njia ya uponyaji wa huo ulimwengu wa ndani uliojeruhiwa, kusudi waweze kufikia hatua ya kuelewa na kupatana na watu na jamii.

273. Tunapofundisha juu ya maadili, ni vyema kuanza taratibu, na kuendelea kwa namna tofauti kadiri ya umri na uwezo halisi walizo nazo watu, bila kulazimisha kutumia njia ngumu na zisizobadilika. Michango mizuri ya saikolojia na ya sayansi ya ufundishaji inaonyesha kuwa inatakiwa kwenda kwa hatua katika kuyafikia mabadiliko ya kitabia, lakini pia kuwa uhuru unahitaji kuongozwa na kuchochewa, kwa sababu ukiachwa tu hivyo hauwezi kukomaa. Uhuru kamili, halisi una mipaka yake na masharti yake. Uhuru si uwezo tu wa kuchagua lililo jema bila kubughudhiwa. Si rahisi daima kutofautishwa kati ya tendo la “makusudi” na tendo “huru”. Mtu anaweza kutamani kitu kibaya kwa makusudi yake yote, lakini kwa sababu ya tamaa isiyotawalika au malezi mabaya. Katika mazingira hayo, anafanya maamuzi kwa makusudi yake kabisa, kwa sababu hayapingani na mapenzi yake, lakini si huru, kwa sababu kwake inaonekana kuwa ni kama vile haiwezekani kutochagua uovu. Nacho ndicho kinachotokea kwa walevi wa madawa ya kulevya. Anapoitamani anafanya hivyo kwa nguvu zake zote, lakini analazimishwa hivi kwa sababu wakati huo hawezi kuchukua maamuzi mengine. Hivyo maamuzi yake ni ya makusudi, lakini si huru. Haina maana ’kuacha mtu achague kwa uhuru’, kwa sababu kiuhalisia hawezi kuchagua, na kumwacha penye madawa ya kulevya hakufanyi kingine zaidi ya kumwongezea utegemezi. Huyo anahitaji msaada wa wengine na malezi endelevu.

Maisha ya familia kama mazingira ya malezi

274. Familia ni shule ya kwanza ya maadili ya kibinadamu, ndiko huko tunakojifunza matumizi mazuri ya uhuru. Kuna mielekeo iliyokomaa katika utoto ambayo inasharabu maisha ya ndani ya mtu na inabaki kwa maisha yake yote kama mvuto mwema kwa ajili ya tunu fulani, au kama katazo la dhati la vitendo fulani vya kitabia. Watu wengi wanatenda kwa maisha yao yote kwa mtindo fulani kwa sababu wanadhani kuwa ni sahihi kutenda vile kwani ndiyo walivyojifunza tangu utoto wao, kama kwa osmosi: “Mimi nimefundishwa hivi”; “hivi ndivyo nilivyorithi”. Katika mazingira ya familia mtu anaweza kujifunza namna ya kudadisi aina za taarifa za vyombo vya habari. Hata kama, mara nyingi vyombo vya mawasiliano kama televisheni au aina fulani za matangazo yanawaharibu na kupunguza nguvu za tunu za kimaadili zinazopatikana katika familia zenyewe.

275. Katika zama zetu hizi, ambapo tunatawaliwa na mfadhaiko na taharuki ya kiteknologia, wajibu muhimu sana wa familia ni kufundisha umuhimu wa subira. Hii haimaanishi kuwazuia vijana wasicheze na vifaa vya kielektroniki, bali kutafuta namna ya kuwajengea uwezo wa kutofautisha mantiki tofauti na kutotumia huo mwendo kasi wa kidijitali katika kila sehemu za maisha. Kusubiri si kukataza kuwa na tamaa, ila kuahirisha tu utimilizaji wake. Pale ambapo watoto na vijana hawafundishwi kupokea kwamba vitu vingine lazima visubiri kwanza, wanakuwa na kiburi, wakilazimisha kila kitu kiweze kutekeleza matakwa binafsi ya sasa na hivyo wanakua katika upotofu wa “kutaka kila kitu haraka haraka”. Huo ni udanganyifu mkubwa usiosababisha uhuru, bali unautilia uhuru sumu. Isipokuwa, pale unapoelimishwa kuahirisha vitu vingine na kusubiri muda muafaka, unajifunza maana halisi ya kujitawala, kuwa huru katika mihemko yako. Na ndiyo pale ambapo mtoto anang’amua kwamba ana uwezo wa kuwajibika juu yake mwenyewe, anazidi kujithamini. Na wakati huohuo, hii inamfundisha namna ya kuheshimu uhuru wa wengine. Kwa vyovyote vile hii haimaanishi kuwataka watoto watende kama watu wazima, lakini pia haitakiwi kudharau uwezo wao wa kuzidi kukomaza uhuru wenye kuwajibika. Katika familia yenye malezi bora, ukufunzi huo unafanyika kwa kawaida kwa njia ya madai ya maisha ya pamoja.

276. Familia ndiyo mazingira ya msingi ya kuishi kijamii, kwa sababu ndiyo mahali pa kwanza kabisa ambapo mtu anajifunza namna na kukaa na wengine, namna ya kuwasikiliza, kushirikishana, kuvumiliana, kuheshimiana, kusaidiana na kuishi pamoja. Kazi ya malezi ni kufundisha kuhisi ulimwengu na jamii kama “mazingira ya kifamilia”, ni kuelimisha namna ya kujua “kuishi”, nje ya mipaka ya nyumba yako. Katika muktadha wa familia tunafundishwa kutambua tena umuhimu wa ujirani mwema, wa kuhudumiana, na wa kusalimiana. Na ndipo hapo ambapo kwa mara ya kwanza ubinafsi unaoua unapopigwa vita, tupate kutambua kuwa tunaishi na wengine, pamoja nao, hao ambao wanauhitaji usikivu wetu, ukarimu wetu na mapendo yetu. Hakuna mahusiano ya kijamii bila sehemu hii ya maisha ya kila siku, ndogo ya kuonekana isipokuwa kama kwa darubini tu: kukaa pamoja katika ujirani, kukutana katika nafasi mbalimbali za kila siku, kujishughulisha katika yale yanayohusu wote, kusaidiana katika shida ndogondogo za kila siku. Familia lazima ibuni kila siku njia mpya za kuendeleza kutambuana.

277. Katika mazingira na nyumbani mtu anaweza kujipanga na kubadili hata mazoea yake ya ulaji ili kuacha nafasi kwa ajili ya jumuiya: Familia ndiyo mhusika mkuu wa ikolojia sahihi, kwa sababu ndiyo mhusika wa kwanza katika jamii, ambayo ndani yake ina misingi miwili ya ustaarabu wa binadamu duniani: msingi wa muungano na msingi wa uzaaji”.[294] Vivyo hivyo, wakati mgumu wa maisha ya familia unaweza kuwa muda mzuri wa kujifunzia. Hicho ndicho kinachotokea, kwa mfano, pale yanapoingia magonjwa, kwa sababu “mbele ya ugonjwa, hata ndani ya familia ndipo yanapozaliwa matatizo, yanayoendana na udhaifu wa kibinadamu. Lakini, kwa kawaida, wakati wa ugonjwa ndio wakati wa kuimarisha mahusiano ya kifamilia.. [...] Malezi yasiyojali sana mazingira ya ugonjwa, yanaukandamiza moyo. Na yanawafanya vijana wawe kama wenye “ganzi” mbele ya mahangaiko ya wengine, wasioweza kukabiliana na mateso na wasioweza kuishi hali yetu pungufu ya kibinadamu.”[295]

278. Mkutano wa kimalezi kati ya wazazi na watoto wao unaweza kurahisishwa au kuharibiwa na teknologia za mawasiliano na burudisho, ambazo kila siku zinakuwa tata zaidi. Pale ambapo zitatumika vizuri zinaweza kusaidia kuwakutanisha wanafamilia hata kama wapo mbali. Mawasiliano yanaweza kuwa ya mara kwa mara na kusaidia kutatua shida.[296] Lakini, lazima tukubaliane kwamba umuhimu wa mawasiliano ya ana kwa ana na ya kina unabaki kuwa ya msingi, wala hayana mbadala, kwa vile inavyohitajika na hamu ya kuwa karibu, au walau, ya kusikia sauti ya mwingine. Tunafahamu kuwa mara nyingine vyombo hivyo vya mawasiliano vinawatenga badala ya kuwaweka pamoja ndugu, kama wakati wa chakula kila mmoja akijali simu yake, au pale ambapo mmoja wa wanandoa analala akimngojea mwingine, anayeshinda muda mwingi akitumia chombo cha kielektroniki. Katika familia, jambo hilo pia lazima liwe sababu ya mazungumzano na makubaliano, yanayowezesha kuweka kipaumbele katika kukutana kwa wanafamilia, bila kutia vizuizi visivyo na tija. Kwa vyovyote, tunapaswa tusisahau hatari za mitindo mipya ya mawasiliano kwa watoto na vijana, ambao mara nyingine wanakuwa watepetevu, wakijitenga na ulimwengu halisi. Hali hii ya “tawahudi (autism, yaani ugonjwa wa kujitenga) ya kiteknolojia” inawaweka kwenye hatari ya kurubuniwa na wale wanaojaribu kupenya hisia za mioyo yao kwa maslahi ya ubinafsi wao.

279. Wala si vizuri kwamba wazazi wanakuwa kama miungu kwa watoto wao, ambao wangeweza kuwa na imani na wao tu peke yao, kwani kwa kufanya hivyo wangezuia ule mchakato unaofaa wa kuzoea maisha ya kijamii na wa kukomaa katika mapendo. Ili kufanikisha kurefusha matumizi sahihi ya hali ya ubaba na umama kwa ajili ya hali halisi iliyo mpana zaidi, “jumuiya za kikristo zinaitwa kusaidia katika utume wa kimalezi wa familia”[297], hasa kwa kupitia katekesi za kuingizwa [katika Ukristo]. Ili kurahisisha malezi sahihi lazima “kuimarisha mapatano kati ya familia na jumuiya ya kikristo.[298] Sinodi imeweka wazi umuhimu wa shule za kikatoliki, ambazo “zinatekeleza dhima muhimu sana ya kuwasaidia wazazi katika wajibu wao wa kulea watoto. [...] Shule za kikatoliki zinapaswa kutiwa moyo katika utume wao wa kuwasaidia wanafunzi ili wakue kama watu wazima waliokomaa na wanaoweza kuuona ulimwengu kwa mtazamo wa mapendo ya Yesu na kuelewa kuwa maisha ni wito wa kumtumikia Mungu.”[299] Katika maana hiyo, “lazima kusisitiza kwa wazi juu ya uhuru wa Kanisa wa kufundisha imani yake na haki ya ukinzani wa dhamiri kwa upande wa walezi.”[300]

Hitaji la elimu ya jinsia

280. Mtaguso mkuu wa pili wa Vatikano ulidokeza kwamba watoto na vijana, “kadiri wanavyokua, lazima wapewe kwa busara elimu ya jinsia iliyo na tunu nzuri” kwa “kuthaminiwa sawasawa maendeleo katika saikolojia, pedagojia na ufundishaji”.[301] Inabidi tujiulize kama taasisi zetu za malezi zimeshaipokea changamoto hii. Ni vigumu kufikiri juu elimu ya jinsia katika zama ambapo wengi wanapunguza uzito wa suala la ujinsia na kudhoofisha umuhimu wake. Tungeweza kuiweka elimu hii katika mtaala tu wa malezi ya mapendo, ya kujitoa kila mmoja kwa mwenzake. Ni katika hali hiyo kwamba muktadha wa ujinsia hauwezi kuwa na muonekano huu dhaifu, ila muonekano wa mwanga. Ashiki ya kijinsia inaweza kupaliliwa katika utaratibu wa kujitambua na kukua katika kujitawala, na hivyo kusaidia katika kuelekeza kwenye furaha ya kweli na kukutana katika mapendo.

281. Elimu ya jinsia inatoa taarifa, bila kusahau kuwa watoto na vijana hawajafikia ule ukomavu kamili. Taarifa lazima ifike katika wakati muafaka kwa namna inayoendana na hatua yao ya makuzi. Haisaidii kuwamezesha vijana na watoto taarifa hizo bila kuwapa mantiki au udadisi kwa taarifa wanazozipokea, mbele ya picha za ponografia bila udhibiti, na msongamano wa taarifa za vishawishi vinavyohaiharibu ujinsia. Vijana wawezeshwe kutambua kuwa wanarushiwa mno taarifa ambazo haziwalei wala kuwaelekeza kwenye mema yao na ukomavu. Inatakiwa kuwasaidia wajitambue na watafute mafundisho mazuri, na wakati huohuo wachukue hatua stahiki dhidi ya yale yote yanayouharibu uwezo wao wa kupenda. Vilevile, inabidi tukubali kuwa “hitaji la kuwa na lugha mpya na yenye kuwafaa zaidi linajitokeza kwanza wakati wa kuwaingiza watoto na vijana kwenye mada ya ujinsia”.[302]

282. Elimu ya jinsia inayoheshimu soni sahihi ina thamani kubwa sana, hata kama siku hizi wengine wanadhani ni suala la kizamani. Ni ngome ya asili ya mtu inayomlinda katika utu wa ndani na kumwepusha asigeuke kuwa kitu cha kushikwa tu. Bila soni, tungepunguza thamani ya upendo na ujinsia hadi kujifanya kama kupagawa na mapepo yanayotuvamia katika sehemu zetu za siri, na ugonjwa sugu unaouharibu uwezo wetu wa kupenda kweli, na katika aina mbalimbali za ubakaji zinazotupelekea kuwa kama si watu na kuwaumiza wengine.

283. Mara nyingi elimu ya jinsia inaelekezwa tu juu ya namna ya “kujikinga”, kwa kutafuta “ngono salama”. Lugha hizi tata hazifundishi msimamo mwema juu ya lengo la asili la ujinsia, ambalo ni kuzaa, kana kwamba mtoto atakayepatikana anatazamwa kama adui ambaye mtu anatakiwa kujikinga naye. Na hivyo tunaendekeza ukatili wa ubinafsi badala ya ukaribu. Ni kukosa uwajibikaji kila mafundisho yanayowalenga vijana kucheza na miili yao na hisia zao, kana kwamba wangekuwa watu wakomavu, waadilifu, wenye kuweza kushika tayari masharti na malengo halisi ya ndoa. Ndivyo wanavyoshawishiwa kwa furaha kumtumia mtu mwingine kama kitu cha mang’amuzi yao ili kuridhisha upungufu na udhaifu wao. Kinyume chake, ni muhimu sana kuwafundisha njia sahihi kuhusu sura halisi na pana za upendo, namna ya kuhudumiana, kuhurumiana kwa kuheshimiana, na ya kuwasiliana juu ya mambo yenye maana. Kwani, hayo yote yatamwandaa kijana katika kujitoa kikamilifu sadaka kwa upendo utakaojionyesha, baada ya kuweka ahadi hadharani, katika kupeana sadaka ya miili yao. Muungano wa kijinsia katika ndoa utaonekana wazi kuwa alama ya ahadi na wajibu kamili, ambayo imetajirishwa na safari nzima ya mwanzo.

284. Haitakiwi kuwadanganya vijana kwa kuwapelekea kuchanganya hatua: kuvutiwa “kunatengeneza, wakati huo, udanganyifu juu ya muungano, hata hivyo bila mapendo ‘muungano’ huo utawafanya hao wawili wabaki wageni na kuwatenga kama mwanzo.”[303] Lugha ya mwili inahitaji uvumilivu wa msingi utakaoruhusu kutafsiri na kufundisha matamanio ya binafsi kwa ajili ya kujitoa kweli. Unapodhani kujitoa kila kitu kimwili mara moja, ni rahisi kutojitoa hata kidogo kama sadaka. Kitu kimoja ni kutambua udhaifu wa kiumri na mchanganyiko wake, kitu kingine ni kuhimiza vijana waendelee katika kutokomaa kwa namna zao za kupenda. Lakini ni nani anayeyazungumzia hayo leo hii? Ni nani anayewathamini kweli vijana? Ni nani anayewasaidia vijana katika kujiandaa vizuri kupenda kweli na kwa kujisadaka? Inachukuliwa kirahisi mno elimu ya jinsia.

285. Elimu ya jinsia inatakiwa kuhusisha heshima e staha ya utofauti, inayomwonyesha kila mmoja uwezekano wa kujikwamua katika mapungufu yako na kujifungua katika kumpokea mwingine. Zaidi ya magumu yale ambayo kila mmoja anaweza kuyaishi, inatakiwa kusaidia kuutambua mwili wako vile ulivyoumbwa, kwa sababu “mantiki ya kutaka kutawala mwili wako unaweza kugeuka mara nyingine kuwa mantiki ya kutaka kutawala viumbe vyote pia [...]. Pia kuuthamini mwili wako katika hali yake ya kike au kiume ni muhimu ili kuweza kujitambua mwenyewe katika kukutana na mwingine ambaye ni tofauti nawe. Kwa mtindo huo itawezekana kupokea kwa furaha sadaka maalumu ya mwingine, kazi ya Mungu muumbaji, na kujitajirisha kila mmoja kwa mwingine.”[304] Katika kuondokana na hofu ya utofauti tu, ndipo itakapowezekana kujikomboa katika kubaki kwenye umimi na kujipendelea wewe mwenyewe. Elimu ya jinsia lazima isaidie katika kujipokea katika mwili wako, ili mtu asidhani “kufuta utofauti wa kijinsia kwa sababu hawezi kabisa kukabiliana nao.”[305]

286. Na haiwezekani kutotambua kuwa katika kujitengenezea mtindo wako wa maisha, wa kike au wa kiume, haziingii tu sababu za kibayolojia au kijenetiki, bali hata uwingi wa masuala yahusianayo na hulka, historia ya kifamilia, utamaduni, mang’amuzi ya maisha, malezi na elimu, ushawishi wa marafiki, wanafamilia au watu unaowajali, au hata mazingira halisi mengine yanayotaka juhudi fulani ili kupatana nayo. Ni kweli kwamba hatuwezi kugawanya kile kinachomhusu mwanamme na mwanamke na kazi ya Mungu, ambayo ipo kabla ya maamuzi na mang’amuzi yetu na ambamo mna uhalisia wa kibayolojia ambao hatuwezi kuukataa. Hata hivyo ni kweli pia kwamba vilivyo vya mwanamume au vya mwanamke si hali ambayo imeganda. Kwa hiyo inawezekana, kwa mfano, kwamba mtindo wa kuwa mwanamume wa mume mtu unaweza kujitengeneza ili endana na hali za kikazi ya mke wake. Kujishughulisha katika kazi za nyumbani au katika fani fulani za kuwalea watoto hakumfanyi mwanamume kuwa si mwanamume, au kumfanya ajisikie kama ameshindwa, amejidhalilisha au amejiaibisha. Inatakiwa kuwasaidia watoto wawapokee wazazi wao katika mabadilishano haya mema kama jambo la kawaida, na kwamba hayapunguzi heshima ya baba wa familia. Ugumu wa kubadilika unaleta hali unaosisitiza mno hali ya kiume au ya kike, wala haisaidii watoto na vijana kutambua uzuri wa kupokezana katika matendo ya kawaida ya hali halisi ya ndoa. Ugumu huo, kwa upande mwingine, unazuia ukomavu wa vipaji vya kila mmoja, mpaka kumdhania kuwa huyu ni mwanamume nusu yule anayejishughulisha na sanaa au ngoma na kwamba si mwanamke halisi yule anayeshika nafasi za uongozi. Mtazamo huu, tumshukuru Mungu, umebadilika, ila katika baadhi ya mazingira dhana hizi zisizofaa zinaendelea kudumishwa na hivyo kuathiri haki ya uhuru na kufifisha ukomavu wa tabia thabiti ya watoto na wa vipaji vyao.

Kurithisha imani

287. Malezi ya watoto yanapaswa kuwa pamoja na mwendo wa kuirithisha imani, ambao unafanywa kuwa mgumu na changamoto za maisha ya sasa, kama vile ratiba za kazi, mchangamano wa ulimwengu wa leo, ambamo wengi wanajaribu kuishi wakikimbizana.[306] Hata hivyo, familia lazima iendelee kuwa mahali pa kufunzia namna ya kupokea sababu na uzuri wa imani, kusali na kuhudumia jirani. Hilo linaanza kwa Ubatizo, ambamo, kama anavyosema Mtakatifu Agustino, akina mama wanaowachukua watoto wao “wanashiriki katika uzazi mtakatifu.”[307] Hapo ndipo inapoanza safari ya kukua kwa yale maisha mapya. Imani ni kipaji cha Mungu, tunachopewa kwa sakramenti ya Ubatizo, wala si matokeo ya kazi za binadamu, lakini wazazi ni vyombo ambavyo Mungu anavitumia kwa ajili ya kuikomaza na kuisitawisha. Kwa hiyo “ni vizuri sana pale akina mama wanapowafundisha watoto wadogo kumbusu Yesu na Bikira Maria kwa mbali. Ni upendo mkubwa namna gani katika kitendo kama hicho! Wakati huo moyo wa watoto unabadilika na kuwa hazina ya sala.”[308] Kurithisha imani kunawataka wazazi waishi kweli maisha ya kumwamini Mungu, kumtafuta na kumhitaji, kwa sababu kwa mtindo huo ndivyo “kizazi kwa kizazi kitakavyoyasifu matendo yako, kitayatangaza matendo yako makuu” (Zab 145:4), na “baba atakavyowajulisha watoto kweli yako” (Isa 38:19). Hilo linatudai kumwomba Mungu afanye kazi ndani ya mioyo, pale ambapo hatuwezi kwa nguvu zetu. Chembe ya haradali, hata kama ni ndogo hukua na kuwa mmea mkubwa (taz. Mt 13:31-32), na hivi ndivyo tunavyofahamu kutokuwiana kati ya tendo na matokeo yake. Ndiyo maana tunafahamu kuwa sisi siyo wamiliki wa zawadi ya Mungu ila ni mawakili wenye uangalifu. Hata hivyo juhudi zetu za kiuvumbuzi ni sehemu ya mchango wetu unaotuwezesha kushiriki katika kazi ya Mungu. Kwa hiyo, “inabidi kuwathamini wazazi, akina mama kwa akina baba, kama waalimu wa kwanza wa katekesi [...]. Ni msaada mkubwa sana katekesi ya kifamilia, kama njia salama ya kuandaa wazazi vijana na kuwafanya wajitambue juu ya wajibu wao kama wainjilishaji wa familia zao.”[309]

288. Mafundisho ya imani yana tabia ya kuendana na kila mtoto, kwa sababu nyenzo zilizotumika hapo zamani, au miiko, mara nyingine hazifanyi kazi. Watoto wanahitaji alama, ishara na hadithi. Vijana wanaokua ni kawaida kuingia katika msukosuko na watu wenye madaraka na pia sheria, kwa hiyo ina faida zaidi kuchochea mang’amuzi yao wenyewe ya imani na kuwapa ushuhuda unaong’aa utakaopokelewa nao kutokana na uzuri wake wenyewe. Wazazi wanaotaka kuwasindikiza watoto wao katika imani wa makini katika mabadiliko yao, kwa sababu wanafahamu wazi kwamba maisha ya kiroho hayalazimishwi bali yanalelewa kwa uhuru kamili. Ni muhimu sana kwa watoto kuona kwa mifano hai kwamba kwa wazazi wao kusali ni jambo la msingi kabisa. Kwa sababu hiyo, wakati wa sala katika familia na vitendo vya ibada za watu vinaweza kuwa na nguvu zaidi katika uinjilishaji kuliko katekesi zote na semina mbalimbali. Ninapenda kupongeza kwa namna ya pekee akina mama wote wale wanaosali kwa moyo mkuu, kama alivyofanya Mtakatifu Monika, kwa ajili ya watoto wao ambao wamejitenga na Kristo.

289. Kazi ya kurithisha imani kwa watoto, katika maana ya kurahisisha vitendo vyake na makuzi yake, inaifanya familia kuwa mwinjilishaji, na kwamba – bila kujilazimisha – ianze kuitangaza kwa wale wote wanaoikaribia, hata nje ya mazingira ya familia yenyewe. Watoto wanaokua katika familia za kimisionari wanakuja kuwa wamisionari, kama wazazi wakiweza kuishi kazi hiyo kwa namna ambayo hata wengine wanawaona karibu nao na marafiki zao, na hivyo watoto nao wanakua katika msimamo huo wa kimahusiano na ulimwengu, bila kuacha imani yao e mang’amuzi yao. Tukumbuke kuwa Yesu mwenyewe alikula na kunywa pamoja na wenye dhambi (taz. Mk 2:16; Mt 11:19), aliweza kuzungumza na mwanamke msamaria (taz. Yn 4:7-26), na kumpokea Nikodemu usiku (taz. Yn 3:1-21), aliruhusu kupakwa mafuta na mwanamke mzinzi (taz. Lk 7:36-50), na hakukwepa kuwashika wenye ugonjwa (taz. Mk 1:40-45; 7:33). Hivyo ndivyo walivyofanya mitume wake, ambao hawakuwa watu waliowadharau wengine, waliojitenga kama vikundi vya wateule, mbali na maisha ya jamii. Wakati wenye mamlaka walikuwa wakiwatesa, wao walikuwa wakikubalika na watu wote (taz. Mdo 2:47; 4:21.33; 5:13).

290. “Familia inakuwa ni mlengwa mkuu wa kazi ya kichungaji kwa kupitia utangazaji wa Injili na urithi wa aina mbalimbali za ushuhuda: mshikamano na maskini, uwazi katika kupokea watu wa aina mbalimbali, hifadhi ya huluka, mshikamano wa hali na mali na familia nyingine hasa zile zenye matatizo mengi zaidi, juhudi katika kusitawisha manufaa ya wote pia kwa njia ya kurekebisha mifumo ya kijamii isiyo haki, kuanzia katika mazingira familia inamoishi, kwa kutenda matendo ya huruma ya kimwili na ya kiroho”.[310] Hilo linapasika kulichukua katika muktadha wa ile imani yenye thamani zaidi kwa wakristo: yaani upendo wa Mungu Baba unaotutegemeza ka kukomaza, ulioonekana katika sadaka kamili ya Yesu, aliye hai kati yetu, anayetuwezesha kupambana katika umoja na dhoruba zote na hatua zote za maisha. Hata ndani kabisa ya kila familia inabidi usikike mwangwi wa kerigma, katika kila mazingira yanayofaa na yasiyofaa, ipate kutumulikia njia. Wote tungetakiwa tuweze kusema, kutokana na maisha tunayoishi ndani ya familia: “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini” (1Yoh 4:16). Kutokana na mazoea haya tu, uchungaji wa familia utaweza kufanikisha kwamba familia ziwe Kanisa la nyumbani na, wakati huohuo, chachu ya uinjilishaji katika jamii.

SURA YA NANE

KUSINDIKIZA, KUPAMBANUA NA KUTEGEMEZA UDHAIFU

291. Mababa wa Sinodi walisema kwamba, ingawa Kanisa linahesabu kuwa kila tendo la kukivunja kifungo cha ndoa “ni kwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu, linaelewa pia kwamba wanae wengi ni dhaifu”.[311] Likiangazwa na mtazamo wa Kristo, “Kanisa linawaangalia kwa upendo wale wanaoshiriki maisha yake kwa namna isiyotimilika, likitambua kuwa neema ya Mungu hufanya kazi pia katika maisha yao kwa kuwapa moyo wa kutenda mema, wa kutunzana kwa upendo, na kuihudumia jumuiya yenyewe ambamo wanaishi na kufanya kazi”.[312] Kwa upande mwingine, msimamo huo unaimarishwa na mazingira ya mwaka huu wa Jubilei ya huruma. Ijapokuwa Kanisa linawaelekeza sikuzote wote kwenye ukamilifu na kuwaalika wamwitikie Mungu zaidi na zaidi, “linapaswa kuwasindikiza kwa makini na kwa upendo wanae dhaifu zaidi, walioathirika na upendo uliojeruhiwa na kupotewa, kwa kuwatia moyo na tumaini, kama vile mwanga unaomulika juu ya mnara bandarini, au mwenge unaopelekwa kati ya watu ili kuwaangaza waliopotea njia au wanaokumbwa na tufani”.[313] Tusisahau kuwa mara nyingi kazi ya Kanisa inafanana na ile ya hospitali ya dharura.

292. Ndoa ya kikristo, iliyo kioo cha muungano wa Kristo na Kanisa lake, inatimilizwa kikamilifu katika muungano kati ya mwanamume na mwanamke, ambao wanajitoa mmoja kwa mwenzake tu katika upendo maalum na uaminifu huru, na kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzie hadi siku ya kufariki, na wote wawili wapo tayari kuzaa watoto, wakiwa wamewekwa wakfu kwa njia ya sakramenti yenye kuwapa neema ili wawe Kanisa la nyumbani na chachu ya maisha mapya kwa jamii. Mitindo mingine ya muungano inapinga kabisa makusudio haya, lakini mingine tena inayatimiza walau kwa sehemu na kimfanano. Mababa wa Sinodi walisema kwamba Kanisa halina budi kuyathamini mambo yanayoweza kujenga, katika hali ambazo haziwiani bado na mafundisho yake juu ya ndoa au zimeacha kuwiana nayo.[314]

Kazi ya kichungaji hatua kwa hatua

293. Mababa wa Sinodi wameangalia pia hali maalum ya ndoa ya kiserikali tu; na hata ile hali ya kuishi pamoja bila ndoa. Maana, ingawa tofauti zipo kati ya hali hizo, “pale ambapo huo muungano unafikia uthabiti mkubwa wa kutosha kwa njia ya kifungo cha hadharani, ukiwa unaonyesha kuwepo kwa upendo mkuu, uwajibikaji mbele ya watoto, uwezo wa kukabiliana na magumu, huweza kutazamwa kama fursa ya kusindikizwa ili ichanue hadi kufikia hatua ya kuadhimisha sakramenti ya ndoa”.[315] Kwa upande mwingine, inahangaisha kuona kwamba nyakati hizi vijana wengi hawategemei ndoa na wanakaa pamoja wakiahirisha bila kikomo kifungo cha ndoa, na tena kuna wengine ambao wanakatisha kifungo chao na mara wanafunga kingine kipya. Wale “walio sehemu ya Kanisa, wanahitaji uangalizi wa kiuchungaji wenye huruma na wa kutia moyo”.[316] Maana, wajibu wa Wachungaji si tu kuhamasisha ndoa ya kikristo, bali pia “kufanya upambanuzi wa kichungaji juu ya hali za watu wengi ambao hawaishi tena hali hiyo”, ili “kuanzisha mazungumzano ya kichungaji na watu hao kwa lengo la kuangalia mambo yaliyomo kwenye maisha yao yanavyoweza kusaidia kuwaongoza kupokea Injili ya ndoa katika utimilifu wake”.[317] Kwa ajili ya upambanuzi wa kichungaji yafaa “kujitahidi kugundua katika maisha ya watu hao viashiria vya uwezekano wa uinjilishaji na ukuaji wa kibinadamu na kiroho”.[318]

294. “Uamuzi wa kufunga ndoa ya kiserikali au, katika hali nyingine, wa kuishi pamoja bila ndoa, mara nyingi hausababishwi na kukadiria vibaya au kupinga muungano wa kisakramenti, ila na hali za utamaduni au hali nyingine za dharura”.[319] Katika hali hizo zitaweza kuthaminiwa alama zile za upendo ambazo, kwa namna fulani, zinaakisi upendo wa Mungu.[320] Tunajua kwamba "inaendelea kukua idadi ya majozi ambayo baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu, wanaomba kuadhimisha ndoa kanisani. Kuchagua kuishi pamoja bila ndoa mara nyingi hutokana na kasumba ya jumla iliyozoea kupingana na wajibu wowote ulio rasmi na wa kudumu, lakini pia unatokana na kusubiri kuwa na uhakika wa maisha kiuchumi (kazi na mshahara wa kudumu). Mwisho, miungano isiyo rasmi katika baadhi ya nchi ni mingi si tu kutokana na kukataa tunu za familia na ndoa, bali hasa kutokana na ukweli kwamba, kwa wanaoishi katika hali ya chini kijamii, kufunga ndoa kunatazamwa kama starehe ya matajiri, kiasi kwamba umaskini wa mali unawasukuma kuiishi miungano isiyo rasmi”.[321] Lakini, "hali zote hizi zishughulikiwe kwa mtindo wa kujenga, kwa kujaribu kuzigeuza ziwe fursa za makuzi kuelekea utimilifu wa ndoa na wa familia katika mwanga wa Injili. Yaani, inatakiwa kuzipokea hali hizo na kuzisindikiza kwa uvumilivu na umakini”.[322] Ndivyo alivyofanya Yesu na mwanamke Msamaria (taz. Yn 4:1-26): alimwambia neno la kugusa hamu yake ya upendo wa kweli, ili amponye na yote yaliyokuwa yanatia giza maishani mwake, na kumwongoza kwenye furaha kamili ya Injili.

295. Kwa mtazamo kama huo, mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa akishauri kutumia utaratibu ule unaoitwa “sheria ya hatua kwa hatua”, kwa kutambua kwamba binadamu “hufahamu, hupenda na kutimiza wema wa kimaadili kwa kupitia hatua mbalimbali za ukuaji”.[323]. Si kwamba sheria yenyewe ina hatua nyingi ndani yake; bali ni kwamba watu wasio katika hali ya kuelewa, kukubali na kutekeleza kikamilifu madai halisi ya sheria, wafikie hatua kwa hatua kutenda kwa busara matendo huru. Maana, pia sheria ni zawadi ya Mungu yenye kuelekeza njia, zawadi kwa ajili ya wote bila ubaguzi, inayoweza kupokelewa maishani kwa nguvu ya neema, ingawa kila mwanadamu “anaendelea hatua kwa hatua katika mwendo wake kwa kutangamanisha kwa utaratibu vipawa vya Mungu na madai ya upendo wake wa kudumu na usio na mipaka katika maisha mazima ya kibinafsi na ya kijamii ya mtu”.[324]

Upambanuzi wa hali zinazoitwa “zisizo kadiri ya kanuni”[325]

296. Sinodi imezungumza juu ya hali mbalimbali za udhaifu au za kukosa ukamilifu. Kuhusu hilo, napenda hapa kukumbusha kile nilichotaka kubainisha wazi kwa Kanisa lote, tusije tukakosa njia: "Mantiki mbili huelekeza historia nzima ya Kanisa: ile ya kutenga, na ile ya kukaribisha tena [...]. Njia ya Kanisa, kuanzia Mtaguso wa Yerusalemu na kuendelea, ndiyo daima ileile ya Yesu: yaani, ya kuhurumia na kutangamanisha [...]. Njia ya Kanisa siyo ile ya kumhukumu mtu hata milele; bali ni ile ya kuwatolea huruma ya Mungu watu wote wanaoiomba kwa moyo mnyofu [...]. Kwa maana mapendo ya kweli daima hayastahiliwi, hayana sharti yoyote, ni bure!”.[326] Kwa hiyo, “lazima kuachana na hukumu ambazo hazizingatii ugumu wa mazingira mbalimbali, na inabidi kuangalia kwa makini jinsi watu wanavyoishi na kuumia kwa sababu ya hali yao”.[327]

297. Ni suala la kuwatangamanisha wote; ni lazima kumsaidia kila mmoja kupata namna yake wa kushiriki katika jumuiya ya kikanisa, ili ajisikie amejaliwa huruma "isiyostahiliwa, bila masharti, na ya bure". Hakuna mtu anayeweza kuhukumiwa kwa daima, kwa maana hiyo siyo mantiki ya Injili! Siwaongelei tu wenye talaka wanaoishi muungano mpya, bali wote, katika mazingira yoyote wanamoishi. Ni dhahiri kwamba endapo mtu mmoja anaringa kuishi katika dhambi halisi kana kwamba hiyo inayo makusudio ya kikristo, ama hutaka kulazimisha kitu kilicho tofauti na linachofundisha Kanisa, hawezi kudai kufundisha katekesi au kuhubiri, na, kwa maana hiyo, kuna kitu fulani kinachomtenganisha na jumuiya (taz. Mt 18:17). Anahitaji kusikiliza upya ujumbe wa Injili na mwaliko kwa wongofu. Lakini hata kwa mtu huyo inaweza kupatikana njia fulani ya kushiriki maisha ya jumuiya: katika shughuli za kijamii, katika mikutano ya sala, au kadiri anavyomsukumwa na moyo wake, pamoja na upambanuzi wa Mchungaji. Kuhusu namna ya kuyashughulikia hali mbalimbali zilizoitwa “zisizo kadiri ya kanuni”, Mababa wa Sinodi wameyafikilia makubaliano ya kijumla, ambayo nayategemeza: “Kwa lengo la kuwashughulikia kiuchungaji watu waliofunga ndoa kiserikali, au wenye talaka waliofunga ndoa tena, au wale ambao wanaishi tu pamoja, ni juu ya Kanisa kuwafunulia malezi ya kimungu yanayohusu kazi ya neema katika maisha yao, na kuwasaidia kuufikia utimilifu wa mpango wa Mungu ndani yao”,[328] unaowezekana sikuzote kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

298. Wenye talaka ambao wanaishi muungano mpya, kwa mfano, wanaweza kujikuta katika hali ya maisha zinazotofautiana sana kati yao, ambazo si halali ziainishwe au kufungwa katika matamko yaliyo magumu mno bila kuacha nafasi ya upambanuzi wa kufaa wa kadhia moja moja na wa kichungaji. Kitu kimoja ni muungano wa pili ambao umeimarika baada ya muda mrefu wa kuishi pamoja, ulioleta na watoto wapya, ambao una uaminifu uliohakikishwa, majitoleo yenye ukarimu, bidii ya kikristo, utambuzi wa hali yao isiyo kadiri ya kanuni na ugumu mkubwa wa kurudi nyuma bila kuhisi katika dhamiri kwamba huko kungesababisha kuingia katika makosa mengine. Kanisa linatambua hali zile ambazo “mwanamume na mwanamke, kwa sababu nzito – kama, kwa mfano, malezi ya watoto wao – hawawezi kutekeleza sharti la mafarakano”.[329] Wapo pia wale ambao walifanya juhudi kubwa kusudi waokoe ndoa ya kwanza, nao wametelekezwa bila haki, au wengine “ambao walifunga muungano wa pili, kwa ajili ya malezi ya watoto, na pengine wanayo hakika katika dhamiri yao ya kwamba ndoa ya kwanza, iliyovunjika moja kwa moja, ilikuwa si halali tangu mwanzo”.[330] Lakini ni kitu kingine muungano mpya unaotokana na talaka ya karibuni, pamoja na yatokanayo yote ya mateso na mahangaiko yawapatayo watoto na familia zote husika, ama hali ya mtu ambaye, mara kwa mara, amekosa kuyashika majukumu yake ya kifamilia. Lazima iwe dhahiri kwamba hayo siyo makusudio ambayo Injili inashauri kwa ndoa na familia. Mababa wa Sinodi walisema pia kwamba upambanuzi wa Wachungaji inabidi ufanyike daima “kwa kuzibainisha inavyotakiwa hali mbalimbali za watu”,[331] kwa mtazamo wenye “kuelewa vizuri utofauti wa hali mbalimbali”.[332] Tunajua kuwa hazipo “mbinu rahisi”.[333]

299. Nipokee maoni ya Mababa wengi wa Sinodi, ambao wamekubaliana kutamka kwamba “wabatizwa wenye talaka ambao wamefunga ndoa tena kiserikali lazima washirikishwe zaidi katika jumuiya za kikristo kwa mbinu zote zinazowezekana, kwa kukwepa kila nafasi ya kusababisha kikwazo. Mantiki ya tangamano ndiyo ufunguo wa juhudi ya kuwasindikiza kiuchungaji, kusudi wajue kuwa ni viungo vya Mwili wa Kristo ulio Kanisa, ila si hilo tu, bali pia kwamba waweze kung’amua kwa furaha ukweli huo na kutoa matunda mema. Hao ndio wabatizwa, ndio kaka na dada zetu, naye Roho Mtakatifu anawamiminia mapaji na karama kwa manufaa ya wote. Kushiriki kwao kunaweza kuchukua sura za huduma mbalimbali za kikanisa: kwa hiyo inabidi kupambanua, kati ya aina mbalimbali za kutenga watu zinazotumiwa mpaka wakati huu katika liturujia, uchungaji, malezi na mambo ya taasisi, ni zipi zile ambazo zinaweza kufutwa. Hao hawatakiwi kujisikia wametengwa na Kanisa, lakini si hilo tu, bali pia waweza kuishi na kukua kama viungo hai vya Kanisa, wakilihisi ni kama Mama mwenye kuwakaribisha daima, kuwatunza kwa upendo na kuwapa moyo katika njia ya maisha na ya Injili. Tangamano hii inahitajika pia ili kuwatunza na kuwalea kikristo watoto wao, wanaopaswa kuhesabiwa wa muhimu kuliko wote”.[334]

300. Kama tukizingatia idadi kubwa sana ya namna tofauti za hali halisi ya watu, kama yale tuliyotaja hapo juu, inaeleweka wazi kwamba isingetarajiwa kupata, kutokana na Sinodi au Wosia huu, sheria mpya za jumla za mtindo wa kikanoni, zenye kufaa kwa hali zote. Inawezekana kutoa tu himizo jipya lenye kutia moyo ili ifanyike upambanuzi wa wahusika na wa kichungaji, ambao utasaidia kuzishughulikia kwa uwajibikaji kila kadhia maalumu; upambanuzi huo ungetakiwa kutambua kwamba, kwa vile “kiwango cha wajibu si sawasawa kwa kadhia zote”,[335] yatokanayo au matokeo ya kanuni fulani haibidi yawe daima yaleyale.[336] Mapadre kazi yao ni “kuwasindikiza wahusika katika njia ya upambanuzi kadiri ya mafundisho ya Kanisa na maelekezo ya Askofu. Katika mchakato huu itafaa kufanya uchunguzi wa dhamiri, kwa njia ya vipindi vya matafakari na vya toba. Wenye talaka waliofunga ndoa tena wangepaswa kujiuliza jinsi walivyowatendea watoto wao wakati muungano wa ndoa ulipoingia kwenye mgogoro; ikiwa walitafuta njia ya kupatana tena; ikoje hali ya mwenzi aliyeachwa; uhusiano mpya una athari gani kwa ajili ya ndugu wengine wa familia na ya jumuiya ya waamini; nao unatoa mfano gani kwa vijana wanaotakiwa kujiandaa kwa ndoa. Tafakuri ya dhati inaweza kuiimarisha imani juu ya huruma ya Mungu ambayo hapana mtu anayenyimwa”.[337] Ndio utaratibu wa usindikizaji na upambanuzi ambao “unawaelekeza waamini hawa wafahamu ukweli wa hali yao mbele ya Mungu. Mazungumzo na padre, faraghani, yanachangia katika kupata utambuzi sahihi juu ya kinachozuia uwezekano wa kushiriki kikamilifu zaidi maisha ya Kanisa, na juu ya hatua zinazoweza kuusaidia na kuuendeleza ushiriki huo. Kwa vile katika sheria yenyewe hamna utaratibu wa kwenda hatua kwa hatua (gradualness, taz. Familiaris consortio, 34), upambanuzi huo hautaweza kamwe kusahau masharti ya ukweli na ya upendo ya Injili yanayopendekezwa na Kanisa. Kusudi hilo litokee, inabidi yahakikishwe masharti ya lazima ya unyenyekevu, usiri, upendo kwa Kanisa na kwa mafundisho yake, katika kuyatafuta kiadilifu matakwa ya Mungu, na katika matamanio ya kufikia kuyaitikia kwa ukamilifu zaidi”.[338] Msimamo wa namna hii ni ya msingi ili kuepukana na hatari nzito ya kueneza taarifa zisizo sahihi, kama vile wazo la kwamba mapadre wengine waweze kutoa haraka “ruhusa zisizo kawaida”, au la kwamba wawepo watu wanaostahili kupata mapendeleo kuhusu sakramenti baada ya kutoa ufadhili. Mtu mtaratibu na wa busara, asiyedai kuweka tamaa zake juu ya manufaa ya wote katika Kanisa, anapokutana na Mchungaji ambaye anajua kutambua uzito wa suala analopambana nalo, inakwepwa hatari ya kwamba aina fulani ya upambanuzi isababishe wazo la kwamba Kanisa linashika maadili mawili.

Mambo tetezi katika upambanuzi wa kichungaji

301. Kusudi tuelewe jinsi ipasavyo kwa nini upambanuzi maalum unawezekana na kuhitajika katika kuzishughulikia hali zile “zisizo kadiri ya kanuni”, kama zinavyoitwa, pana suala ambalo inabidi daima kulitilia maanani, ili mtu asifikiri kamwe kuwepo lengo la kupunguza masharti ya Injili. Kanisa limetafakari kwa kina kuhusu athari zinazosababisha matendo na juu ya mambo tetezi. Ndiyo maana haiwezekani tena kusema kwamba wale wote wanaojikuta katika hali fulani inayosemwa “isiyo kadiri ya kanuni” wanaishi katika hali ya dhambi ya mauti, na wamenyimwa neema ya utakaso. Mapungufu hayatokani tu na kutokujua sheria. Mtu, hata akijua vizuri sheria, anaweza kuona ugumu mkubwa katika kuelewa “tunu zilizomo ndani ya kanuni ya kimaadili”[339] au anaweza kujikuta katika hali halisi ambazo hazimruhusu kutenda kwa mtindo tofauti na kufanya maamuzi mengine bila kukosa tena. Kadiri walivyojieleza vema Mababa wa Sinodi “inawezekana ziwepo sababu zinazopunguza uwezo wa kuamua”.[340] Mtakatifu Tomaso wa Aquino tayari alikiri kwamba wengine wanaweza kuwa na neema na upendo, ila hawawezi kutekeleza vizuri mojawapo ya fadhila,[341] kwa namna ya kwamba, hata ingawa wanazo moyoni fadhila zote za kimaadili, hawaonyeshi kidhahiri uwepo wa mojawapo, kwa sababu matendo ya nje ya fadhila hiyo yanapatwa na magumu: “Husemwa kuwa watakatifu wengine hawana fadhila fulani, kwa sababu ya magumu wang'amuayo katika kuzitenda, [...] ijapokuwa hao wanayo tabia ya fadhila zote”.[342]

302. Kuhusu athari hizo Katekisimu ya Kanisa Katoliki inajieleza kwa jinsi isiyoweza kupingwa: “Shutuma na uwajibikaji juu ya tendo fulani huweza kupunguzwa au kuondolewa kwa sababu ya ujinga, kupitiwa, kutendwa ukatili, hofu, mazoea, mapenzi yasiyo na taratibu na vitu vingine vya kisaikolojia na kijamii”.[343] Katika kipengele chake kingine inazidokeza tena hali zinazopunguza uwajibikaji wa kimaadili na inataja, kwa upana sana, “kutokomaa kihisia, nguvu ya mazoea yaliyojijenga, hali za fadhaa na mambo mengine ya kisaikolojia au kijamii.[344] Kwa sababu hiyo, kuihukumu hali fulani halisi kuwa ni kosa hakusababishi hukumu juu ya kushutumiwa na uhalifu wake mtu anayehusika.[345] Katika muktadha wa mambo hayo, naona kwamba yana maana sana waliyotaka kusema Mababa wengi wa Sinodi: “Katika hali fulani, watu wanakutana na magumu makubwa katika kuamua kutenda vinginevyo. [...] Upambanuzi wa kichungaji, ijapokuwa unaitia maanani dhamiri ya watu iliyolelewa kiadilifu, lazima ujitwike hali hizo. Pia matokeo ya matendo yalilofanyika, siyo yaleyale bila shaka katika kila hali”.[346]

303. Tunapokumbuka athari ya hali halisi ya mambo kama haya, tunaweza kuongeza kusema kuwa dhamiri ya mtu binafsi yatakiwa ishikamanishwe vizuri zaidi ndani ya desturi ya utendaji wa Kanisa katika mazingira fulani yale yasiyojumuisha uelewa wetu wa ndoa. Ama hakika, nguvu zote zitumike kuongeza makuzi ya dhamiri yenye uelewa sahihi, iliyoundwa na kusindikizwa na upambanuzi makini na unaowajibika wa Mchungaji, na kuhimiza ili kuiaminia zaidi na zaidi neema ya Mungu. Hata hivyo, dhamiri inaweza kutenda zaidi ya kule kutambua kwamba mazingira fulani maalum hayapatani kiukweli na madai ya jumla ya Injili. Inaweza pia kutambua kwa unyofu na moyo safi kuwa ni mwitiko upi kwa sasa unaonyesha moyo wa ukarimu unaoweza kuelekezwa kwa Mungu, na kuweza kutambua kwa uhakika wa kiwango fulani cha uadilifu kwamba hili ndilo analolitaka Mungu katikati ya mwingiliano huu wa mapungufu ya mtu binafsi, ijapo siyo bado hali ile timilifu inayotazamiwa. Kwa vyovyote, tukumbuke kuwa upambanuzi unaendelea kufanyika, na ni lazima uwe tayari kuingia hatua nyingine ya makuzi na kuwa tayari kufanya maamuzi mapya yanayowezesha litekelezwe vizuri zaidi lengo timilifu.

Kanuni na upambanuzi

304. Ni kidogo mno kufikiria tu ikiwa matendo ya mtu mmoja yanapatana na sheria ama kanuni ya jumla au la, kwa sababu hilo halitoshi kwa ajili ya kupambanua na kuthibitisha uaminifu kamili kwa Mungu katika maisha halisi ya mwanadamu. Naomba kwa moyo kabisa tulikumbuke fundisho la mtakatifu Tomaso wa Akwino na tujifunze ili tuliunganishe na upambanuzi wetu wa kichungaji: “Hata kama kuna ulazima katika kanuni za jumla, tunavyozidi kutelemka na kusogelea vipengee vya kinaganaga, ndivyo mara nyingi zaidi tunakutana na mapungufu. [...] Kuhusu hali za tendo, ukweli au kanuni ya utendaji siyo sawa kwa wote unapoangalia kwa kinaganaga, ila tu inapohusu kanuni za jumla; na hata palipo na makubaliano kuhusu kanuni ya utendaji unapoangalia kwa kinaganaga, hiyo kanuni haijulikani kwa namna ileile na wote. [...] Kanuni itaonekana kuzidi kutoeleweka kadiri tunavyoelekea katika hali ya kinaganaga zaidi”.[347] Ni kweli kwamba kanuni za jumla zinaonyesha jambo jema ambalo haliwezi kupuuzwa ama kudharauliwa, lakini katika kutamkwa kwake haiwezekani kuonyesha vipengele vya mazingira yote. Na wakati huohuo, inabidi kusema kwamba, hasa kwa sababu hiyohiyo, jambo linalohusu upambanuzi wa kiutendaji katika hali ya mazingira maalumu haliwezi kuwekwa katika kiwango cha kuwa kanuni ya jumla. Kufanya hivyo kungaliishia siyo tu katika mkanganyiko usiovumilika wa hoja za kutetea mambo yasiyo ya kweli, bali pia kungalihatarisha tunu na thamani zinazopaswa kutunzwa kwa uangalifu wa pekee.[348]

305. Kwa sababu hiyo, Mchungaji hawezi kuchukulia kuwa inatosha kutumia tu kanuni za maadili juu ya wale wanaoishi katika hali “isiyo kadiri ya kanuni”, kana kwamba zingalikuwa ni mawe ya kuwatupia watu. Hii ingedhihirisha moyo uliojifungia wa mtu aliyefichama nyuma ya mafundisho ya Kanisa, “akikalia kiti cha Musa akitoa hukumu, mara nyingine kwa kujiaminia ukuu na kwa kurashia tu, juu ya matatizo mazito ya familia zilizojeruhiwa”.[349] Kwa mtiririko huohuo, Tume ya Kimataifa ya Teolojia imetamka hivi: “Sheria asilia haingeelezwa kuwa tayari ni orodha ya kanuni zinazolazimika kuwapo na kutumia awali ya yote (a priori) wakati wa kuhukumu mambo ya maadili; bali ni chemchemi ya mshituo halisi kwa mchakato wa hiyo hukumu, ambao hasa ni wa binafsi, ya kufikia uamuzi”.[350] Kutokana na mambo yanayomweka mtu katika hali ya maelekeo ya kufanya jambo, na mambo yanayopunguza makali ya lawama, inawezekana kwamba mtu akiwa katika hali ambayo kwa yenyewe ni hali ya dhambi – lakini yeye asiwe na lawama, ama asiweze kulaumiwa kikamilifu – aweze kuishi katika hali ya neema ya Mungu, akawa na upendo na pia akaongezeke katika maisha ya neema na upendo, huku akipokea msaada wa Kanisa kwa nia hiyo.[351] Upambanuzi lazima usaidie kupata njia zinazowezekana za kumwitikia Mungu na kukua katikati ya mapungufu. Kwa kuamini kuwa kila kitu kinakuwa ama cheupe ama cheusi, nyakati nyingine tunafungia mbali njia za neema na makuzi, na hivyo kuziponda moyo safari za utakaso zinazomtukuza Mungu. Ebu tukumbuke kuwa “hatua moja katikati ya mapungufu makubwa ya kibinadamu, inaweza ikampendeza zaidi Mungu kuliko maisha yanayoonekana kwa nje kuwa ni mazuri, lakini yanatiririka kwa siku nzima bila kuyashinda magumu yoyote mazito”.[352] Utekelezaji wa kazi ya uchungaji wa wahudumu na jumuiya za kikristo lazima uzingatie ukweli wa hali hii.

306. Katika kila hali, mbele ya wale wenye shida ya kushika kikamilifu sheria ya Mungu, mwaliko wa kufanya bidii ya kufuata njia ya upendo (via caritatis) usikike wazi kabisa. Upendo wa kindugu ndiyo sheria ya kwanza ya Wakristo (Yn 15:12; Gal 5:14). Na tusisahau maneno ya kitulizo yaliyoahidi Maandiko Matakatifu: “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana, kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi” (1Pet 4:8); “ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha” (Dan 4:27); “Maji huuzimisha moto uwakao, na sadaka huwa upatanisho wa dhambi” (YbS 3:29). Hivi ndivyo pia alivyofundisha mtakatifu Agustino akiandika: “Kama vile tungalikuwa katika hatari kwa sababu ya moto, tungekimbia mara moja kwenda kuchota maji ili tuuzimishe, [...] ndivyo pia, iwapo miali ya dhambi inalipuka katika manyasi ya tamaa zetu na tunatikiswa, kama tunapata fursa ya kufanya tendo la huruma, ebu tulifurahie kana kwamba ingalikuwa chemchemi ya maji tuliyopewa ili kuuzimisha moto huo mkali”.[353]

Mantiki ya huruma ya kichungaji.

307. Ili kuepusha uelewa mbaya, ninasisitiza kwamba kwa namna yoyote ile Kanisa lisisitize kufundisha hali ya ndoa timilifu inayotamaniwa, ambayo ndiyo mpango wa Mungu katika utakatifu wake: “Vijana waliobatizwa wahimizwe kuelewa kwamba sakramenti ya ndoa ina uwezo wa kutimiliza matumaini yao ya kufanikiwa katika upendo wao na kwamba wanaweza kupata nguvu kwa neema ya Kristo katika sakramenti na kwa uwezekano wa kutumia fursa nyingi za kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kanisa”.[354] Msimamo usio na mwelekeo, ama aina yoyote ya kuamini kuwa ukweli na uadilifu unategemea mazingira, ama kuona aibu wakati wa kuitangaza, ingekuwa ni kukosa uaminifu kwa Injili na kwa upande wa Kanisa ni kukosa pia upendo kwa vijana wenyewe. Kuonyesha uelewa kwa mazingira ya pekee hakumaanishi hata kidogo kuficha nuru ya kusudio timilifu, ama kupunguza yale ambayo Yesu anataka kuwajalia binadamu. Leo, kazi muhimu zaidi kuliko kuchunga ndoa zilizoshindwa, ni kufanya juhudi za kiuchungaji ili kuimarisha ndoa na hivyo kuzuia zisivunjike.

308. Lakini, kutokana na kutambua uzito wa vitendo na hali zinazopunguza uzito wa kulaumiwa - yaani hali ya kisaikolojia, kihistoria na hata kimaumbile – inafuata kwamba “bila kupunguza lengo timilifu la kiinjili, kuna haja ya kuzisindikiza kwa huruma na uvumilivu hatua za kukua binafsi kuelekea lengo hilo zinavyojitokeza moja baada ya nyingine”, tukiachia nafasi kwa ajili ya “huruma ya Mungu, inayotuhimiza tutende mema yanayowezekana”.[355] Ninawaelewa wale wanaopendelea kuchukua hatua kali zaidi za kichungaji ambazo haziruhusu mwanya wa kutoeleweka vizuri. Lakini ninaamini kwa unyofu wote kwamba Yesu analitaka Kanisa linalotambua uzuri anaoupanda Roho Mtakatifu katikati ya udhaifu wa kibinadamu: Kanisa ambalo ni Mama ambaye kwa upande mmoja anaonyesha mafundisho yake jinsi yalivyo, na upande mwingine “linafanya kila jema linalowezekana, hata kama katika utendaji huo lina hatari ya kuchafuka kwa matope ya njiani”.[356] Wachungaji wa Kanisa, wanapowafundisha waamini ukweli kamili wa Injili na mafundisho ya Kanisa, yawapasa pia kuwaelekeza jinsi ya kuwasaidia wadhaifu kwa huruma, wakiepuka kuongeza maumivu ama kutoa hukumu kali ama za haraka haraka. Injili yenyewe inatufundisha tusihukumu wala kulaumu (Mt 7:1; Lk 6:37). Yesu “anatutazamia kuwa tuache kutafuta vijishimo vya kufichama binafsi ama kama jumuiya, vinavyotukinga na mafuriko ya majanga ya kidinadamu, na badala yake tuingie katika ukweli wa mambo ya maisha ya watu na kutambua nguvu ya upendo upole. Kila tunapofanya hivyo, maisha yetu yanakuwa yana mchangamano mzuri wa kustaajabisha”.[357]

309. Ni maongozi ya Mungu kwamba tafakari hii inafanyika katika Mwaka Mtakatifu unaosherehekea Huruma ya Mungu, kwa sababu hata mbele ya hali mbalimbali zinazohusu familia, “Kanisa limeagizwa kazi ya kuitangaza huruma ya Mungu, iliyo moyo hai wa Injili, ambayo kwa njia ya Kanisa lazima ipenye akili na moyo wa kila mtu. Kanisa, lililo Bibi Harusi wa Kristo, linapanga mwenendo wake kumwiga Mwana wa Mungu anayemwendea kila mmoja bila kubagua”.[358] Kanisa linajua kuwa Yesu mwenyewe ni Mchungaji wa kondoo wote mia moja, na siyo wa tisini na tisa tu. Anawapenda wote. Kwa msingi wa kutambua hilo, sasa itawezekana “marhamu ya huruma ya Mungu kumfikia kila mmoja, mwamini na yule aliye mbali kabisa, iwe ni ishara kwamba ufalme wa Mungu tayari u katikati yetu”.[359]

310. Hatuwezi kusahau kuwa “huruma si utendaji wa Baba tu; inakuwa ni kipimo cha kutambua ni akina nani ambao ni wanae wa kweli. Kifupi, tunaitwa tuishi kwa huruma, kwa sababu sisi tulipewa huruma kwanza”.[360] Hili si swala la hisia tupu ama mwitiko vuguvugu kwa upendo wa Mungu, ambao daima unatafuta kilicho bora kabisa kwa ajili yetu, kwa sababu “huruma ndiyo msingi wenyewe wa maisha ya Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinatakiwa ziunganishwe mara na upendo mpole ambao Kanisa linawaonyesha waamini; huruma isikosekane popote katika mahubiri yake na ushuhuda wake kwa ulimwengu”.[361] Ni kweli kwamba wakati mwingine “tunatenda kama wadhibiti wa neema kuliko kuwa wawezeshaji. Lakini Kanisa siyo nyumba ya ushuru; ni nyumba ya Baba, ambamo kuna nafasi kwa kila mmoja, licha ya kuwa na matatizo yake”.[362]

311. Ufundishaji wa somo la teolojia ya maadili usiache kujumuisha vipengele hivi, kwa sababu ingawa ni kweli kabisa kuwa yapasa kuwajibika ili kufundisha kikamilifu maadili ya Kanisa, uangalifu wa pekee uonyeshwe ili kusisitiza na kutengeneza mazingira ya usitawi wa mafundisho makuu na ya kina juu ya tunu za Injili,[363] hasa kuhusu nafasi ya kwanza ya upendo kama mwitiko kwa zawadi tusiyostahili ya upendo wa Mungu. Wakati mwingine, katika kazi zetu za kichungaji, tunaona vigumu kutoa nafasi kwa upendo wa Mungu usio na masharti.[364] Tunaweka masharti mengi sana ya kupata huruma na msamaha, kiasi kwamba tunafuja maana yake inayolingana na ukweli wa mambo na makusudio yake halisi. Hii ndiyo njia mbaya kabisa ya kuichujua Injili. Ni kweli, kwa mfano, kwamba huruma haijitengi na haki pamoja na ukweli, lakini kwanza juu ya yote lazima tuseme kwamba huruma ni utimilifu wa haki na ndiyo ushahidi unaong’ara kabisa wa ukweli wa Mungu. Kwa sababu hii, tunapaswa kutambua kuwa “ni uelewa usiotosha wa kiteolojia ule ambao mwishoni unatilia mashaka kuhusu uwezo mkuu wa Mungu, na hasa kuhusu huruma yake”.[365]

312. Hii inatupatia kipimo na mpangilio ambavyo hutusaidia kuepuka ubaridi na urasimu wa kimaadili tunaposhughulikia maswala nyeti. Badala yake, yanatuweka katika mazingira ya upambanuzi wa kichungaji, uliojaa upendo wenye huruma, ambao upo tayari daima kuelewa mambo, kusamehe, kusindikiza, kutumainia, na zaidi ya yote kuwakaribisha na kutangamanisha wote. Hii ndiyo namna ya mtazamo wa mambo ambao yapasa utawale katika Kanisa na kutufanya “tufungue mioyo yetu na kuwaelekea wale wanaoishi pembezoni kabisa mwa jamii”.[366] Nawahimiza waamini wanaojikuta katika hali ya mkanganyiko wazungumze na wachungaji wao kwa matumaini ama na walei wengine wenye maisha yaliyoshikamana na Bwana. Yawezekana wasikute daima ndani yao uthibitisho wa mawazo na hamu zao, lakini kwa hakika watapata nuru fulani itakayowasaidia kuielewa vizuri zaidi hali yao na kugundua njia ya kukomaa binafsi. Pia nawahimiza wachungaji wa Kanisa kuwasikiliza kwa moyo wa uelewa na utulivu, kwa nia nyofu ya kuielewa hali yao ngumu na mtazamo wao, ili kuwasaidia waishi maisha mema zaidi na watambue nafasi yao husika katika Kanisa.

SURA YA TISA

TASAUFI (MAISHA YA KIROHO) KATIKA NDOA NA FAMILIA

313. Mapendo yana namna mbalimbali ya kujidhihirisha, kwa kadiri ya hali tofauti ya maisha ambayo kila mtu ameitwa kuishika. Hata miongo kadhaa iliyopita, Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, katika Dikrii juu ya utume wa walei, ulisisitiza tasaufi itokayo katika maisha ya kifamilia. Mtaguso Mkuu ulisema kwamba tasaufi ya walei “inatakiwa kuwa na sura ya pekee kutokana na hali ya ndoa na ya familia”[367], na kwamba “mahangaiko kwa ajili ya familia ... hayatakiwi kuwa mbali na mwelekeo wa kiroho wa maisha”.[368] Kwa hiyo inafaa tueleze kwa kifupi sifa chache za msingi za tasaufi hii ya pekee inayositawi kwenye mahusiano hai yaliyomo katika maisha ya familia.

Tasaufi ya ushirika wenye kupita maumbile

314. Tumesema daima juu ya Mungu kukaa moyoni mwa mtu anayeishi katika neema yake. Leo tunaweza kuongeza kusema kwamba Utatu Mtakatifu umo katika hekalu la ushirika wa kindoa. Kama Utatu Mtakatifu unavyokaa juu ya sifa za watu wake (taz. Zab 22:4), ndivyo unavyoishi kwa undani katika mapendo ya wanandoa yanayoutukuza.

315. Uwepo wa Bwana hukaa katika familia halisi, na kama ilivyo katika hali yake, pamoja na taabu zake, mapambano yake, furaha zake na azma zake za kila siku. Tunapoishi katika familia, ni vigumu kwetu kujisingizia au kusema uongo; hatuwezi kujificha nyuma ya kinyago. Iwapo upendo ni moyo wa juhudi hiyo ya kutenda kiukweli, ndipo Bwana anapotamalaki huko kwa furaha yake na amani yake. Tasaufi ya upendo wa kifamilia inajumuisha maelfu ya vitendo halisi na vya kweli. Mungu ana makao yake katika wingi huu wa vipawa na mahusiano mbalimbali vinavyokuza ushirika. “Upendo wa namna hii unaunganisha pamoja tunu za kibinadamu na za kimungu”,[369] kwa sababu umejaa upendo wa Mungu. Kwa jumla, tasaufi ya ndoa ni tasaufi ya kifungo (cha kindoa) ambacho katika hicho upendo wa Mungu hukaa.

316. Ushirika wa kifamilia, mtu anapouishi vizuri, ni mwendo halisi wa kutakatifuzwa katika maisha ya kawaida, na wa kukua katika maisha ya kifumbo; tena ni namna ya kuunganishwa kwa ndani na Mungu. Maana, haja zinazoibuka katika maisha ya familia, ziwe za kindugu au za kijumuiya, zinakuwa ni nafasi ya kufungua moyo zaidi na zaidi; na hilo linawezesha uhusiano na Bwana unaotimilika zaidi na zaidi. Neno la Mungu linasema kwamba, “Yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza; ... akaa katika mauti; ... hakumjua Mungu” (taz. 1Yoh 2:11, 3:14, 4:8). Mtangulizi wangu Benedikto XVI alisema kwamba “kufumba macho mbele ya jirani, kunafanya mtu awe kipofu hata mbele ya Mungu”,[370] na kwamba, kwa msingi, upendo ni nuru pekee “inayoangaza upya sikuzote ulimwengu uliomo gizani”.[371] Kama tu “tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu” (1Yoh 4:12). “Kwa asili na maumbile yake, binadamu ana tabia ya kijamii”,[372] na “dhihirisho la kwanza na la asili la tabia ya kijamii ya mtu ni jozi la mume na mke na familia”.[373] Kwa hiyo, tasaufi inapata umbo katika ushirika wa kifamilia. Kwa hiyo, watu wenye hamu za kiroho za undani wasifikiri kuwa familia inawazuia wasikue kiroho; kinyume chake, familia ni njia anayotumia Bwana ili awaongoze kwenye kilele che muungano wa kifumbo naye.

Kuungana katika sala kwa mwanga wa Pasaka

317. Endapo familia ina kiini chake katika Kristo, Yeye anaunganisha na kuangaza maisha yote ya kifamilia. Mateso na matata yanavumiliwa kwa kushiriki Msalaba wa Bwana; na kukumbatiana naye kunawezesha kustahimili magumu yanapoibuka nyakati fulani. Katika siku za uchungu za familia, pana muungano na Yesu ulio na nguvu ya kuzuia familia isivunjike. Familia zinafikia kwa utaratibu, na “kwa neema ya Roho Mtakatifu, utakatifu wao kwa njia ya maisha ya ndoa, kwa kushiriki pia fumbo la msalaba wa Kristo, linalogeuza shida na mateso viwe sadaka ya upendo.”[374] Na, kwa upande mwingine, siku za furaha, pumziko, sherehe, na ujinsia pia, vinakuwa namna ya kushiriki uhai kamili wa Ufufuko wake. Wenzi wa ndoa wanajenga kwa vitendo vyao mbalimbali vya kila siku “nafasi hii ya kuangazwa na Mungu (spazio teologale) ambapo uwepo wa kifumbo wa Bwana mfufuka unahisika.[375]

318. Kusali katika familia ni njia ya pekee ya kuonyesha na kuimarisha imani hii ya kipasaka.[376] Dakika chache kila siku zipatikane ili wanafamilia wakae kwa pamoja mbele ya Bwana aliye hai, na kumwambia mahangaiko yao, kumwomba kwa mahitaji ya familia, kumwomba kwa ajili ya mwanafamilia aliye katika hali ngumu, kumwomba awasaidie kupendana, kumshukuru kwa maisha waliyojaliwa na kwa mambo mema yote, kumwomba Bikira awalinde kwa ulinzi wake wa mama. Kwa kutumia maneno machache, kipindi hiki cha sala kinaweza kuleta mema mengi sana kwa familia. Aina mbalimbali za ibada za watu ni hazina ya kiroho kwa familia nyingi. Mwendo wa pamoja wa sala una kilele chake katika kushiriki kwa pamoja Ekaristi Takatifu, hasa siku za Dominika, iliyo siku ya mapumziko . Yesu anabisha hodi mlangoni kwa familia ili kushirikishana nayo karamu ya Ekaristi (taz. Ufu 3:20). Hapo, wanandoa wanaweza daima kuthibitisha agano la kipasaka lililowaunganisha, linaloakisi kama kioo Agano alilofunga Mungu na wanadamu msalabani.[377] Ekaristi ni sakramenti ya Agano Jipya ambapo tendo la ukombozi la Kristo linafanya kazi hadi sasa (taz. Lk 22:20). Hivyo, vifungo vya undani kati ya maisha ya ndoa na Ekaristi vinaonekana wazi.[378] Chakula cha Ekaristi ni nguvu na kichocheo ili kuishi kila siku agano la ndoa kama “Kanisa la nyumbani”.[379]

Tasaufi ya upendo unaojitoa kwa mwenzake tu kwa uhuru

319. Katika ndoa mtu anaishi ukweli wa kuwa kabisa wa mwingine mmoja tu. Wanandoa wanakubali changamoto na tarajio la kuzeeka na kujisadaka kwa pamoja; na hivyo wanakuwa ni mfano wa uaminifu wa Mungu. Uamuzi thabiti huu, unaoathiri mtindo wa kuishi, ni “haja ya ndani ya agano la upendo kati ya wanandoa”,[380] kwa sababu “mtu asiyeamua kwamba atapenda kwa daima, ni vigumu aweze kupenda kwa dhati hata siku moja tu”.[381] Lakini uaminifu huu usingekuwa na maana kiroho kama ungekuwa tu sheria iliyoshikwa kama jambo lililopaswa kuvumiliwa tu. Kinyume chake, hali ya kuwa wa mtu mwingine inapaswa kukaa moyoni, ambamo Mungu tu anaweza kuona (taz. Mt 5:28). Kila asubuhi, tunapoamka, tunachukua tena mbele ya Mungu uamuzi huu wa kuwa waaminifu, licha ya mambo yoyote yatakayotokea baadaye. Na kila mtu, anapokwenda kulala, anatarajia aamke tena ili kuendelea katika safari hiyo, kwa kutegemea msaada wa Bwana. Hivyo, kila mwenzi wa ndoa ni kwa mwingine ishara ya Bwana aliye karibu naye, ambaye hatuachi peke yetu: “Mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Mt 28:20).

320. Pana wakati maalumu ambapo upendo wa jozi unapata kuwa huru kwa namna kuu, na unakuwa nafasi ya uhuru safi: ni hapo kila mwanandoa anapogundua kwamba mwenzie si mali yake, bali ni wa mwingine aliye muhimu kabisa kuliko yeye: Bwana wake pekee. Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa anamiliki undani wa nafsi ya mpenzi wake, ule wa siri zaidi. Bwana tu anaweza kukaa katika kiini cha maisha yake. Wakati huohuo, kanuni ya uhalisia wa kiroho inafanya mwenzi wa ndoa asiweze kudai mwenzie aridhishe kikamilifu haja zake. Kama alivyoeleza vizuri Dietrich Bonhoeffer, mwendo wa kiroho wa kila mtu unatakiwa kumsaidia kutambua kuwa mwingine si kama ambavyo angalimtaka yeye,[382] na kumsaidia kuacha kutarajia kutoka kwake mambo yaliyo ya pekee ya upendo wa Mungu tu. Hayo yanadai mtu ajinyenyekeze kwa ndani. Nafasi ya pekee ambayo kila mwenzi wa ndoa huitenga kwa ajili ya uhusiano wake wa binafsi na Mungu, haisaidii tu majeraha ya maisha ya pamoja yaponywe, bali pia inawawezesha wenzi wa ndoa kuona maana ya maisha yao katika upendo wa Mungu. Tunahitaji kuomba kila siku Roho Mtakatifu atende kazi ili tupate kuwa na uhuru huu wa ndani.

Tasaufi ya kujali, kufariji na kuhamasisha

321. “Wanandoa wakristo ni washiriki wa neema na mashahidi wa imani, mwenzi mmoja kwa mwenzie, kwa watoto wao na kwa jamaa zao wengine wote”.[383] Mungu anawaita kuzaa na kutunza. Ndiyo sababu familia “imekuwa ni daima ’hospitali’ iliyo jirani zaidi”.[384] Tutunzane, tutegemezane, tuhamasishane, na tufikirie hayo yote kama sehemu ya maisha yetu ya kiroho katika familia. Maisha ya pamoja ya jozi ni kushiriki tendo lenye kuzaa la Mungu; na kila mwenzi ni kwa mwenzie kichocheo cha kudumu cha Roho. Upendo wa Mungu unadhihirika “kupitia maneno hai na halisi ambayo kwayo mume na mke wanaambiana upendo wao wa kindoa”.[385] Hivyo, hao wawili, kila mmoja kwa mwenzie, ni kama kioo cha upendo wa kimungu unaofariji kwa neno, kwa mtazamo au mguso wa mapendo, kwa kusaidia na kwa kukumbatia. Kwa hiyo, “kutaka kuunda familia ni kuwa na ushujaa wa kushiriki ndoto ya Mungu, ushujaa ya kuota ndoto pamoja naye, ushujaa wa kujenga pamoja naye, ushujaa wa kujishughulisha pamoja naye katika maisha haya, wa kujenga ulimwengu ambapo hakuna mtu anayejisikia peke yake”.[386]

322. Maisha yote ya familia ni kama “malisho” ya huruma. Kila mwenzi “anachora” na “anaandika” kwa mapendo katika maisha ya mwenzie. “Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu [...] si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai” (taz. 2Kor 3:2.3). Kila mtu ni “mvuvi wa watu” (taz. Mt 4:19) ambaye “anawashushia wengine nyavu” (taz. Lk 5:5) kwa jina la Yesu, au mkulima anayelima ardhi yenye rutuba, yaani wapendwa wake, kwa kustawisha mambo bora waliyo nayo. Ndoa kuzaa matunda ni jambo linalotegemea kazi ya kustawisha, kwa sababu “kumpenda mtu ni kutarajia toka kwake mambo yasiyotabirika wala kupangika, na wakati huohuo ni kwa namna fulani kumwezesha atimize matarajio hayo”.[387] Nayo ni ibada kwa Mungu, kwa sababu yeye ndiye aliyepanda mambo mema mengi ndani ya wengine; naye anatumaini kwamba sisi tutayakuza.

323. Kumtazama mtu mpendwa kwa macho ya Mungu, na kumtambua Kristo katika yeye, ni mang’amuzi ya kiroho ya kina. Hayo yanadai kuwa tayari kujitolea kwa hiari, na hivyo kuthamini hadhi yake. Unaweza kuwa na mahusiano makamilifu na mwenzio endapo tu unajitolea bila kutafuta sababu, na kusahau mambo mengine yote yanayokuzunguka. Mpenzi wako anastahili wewe umjali kwa nafsi yako yote. Yesu ni mfano, kwa sababu, mtu alipomkaribia aongee naye, yeye alikuwa anamkazia macho na kumwangalia kwa upendo (taz. Mk 10:21). Mbele ya Yesu, hapakuwa na mtu aliyejisikia amesahauliwa, kwa sababu maneno yake na vitendo vyake vilikuwa vikidokeza swali hili, “Wataka nikufanyie nini?” (Mk 10:51). Nalo ndilo tunaloonja katika maisha ya kila siku ya familia. Katika familia twakumbuka kwamba mtu anayeishi pamoja nasi anastahili yote, kwa sababu hadhi yake haina mipaka, kwa kuwa Mungu anampenda kwa upendo usiopimika. Hivyo, upendo mwororo unastawi, ulio na nguvu ya “kuamsha moyoni mwa mwenzi furaha ya kujisikia mtu mwenye kupendwa. Upendo mwororo hudhihirika kwa namna ya pekee mmoja anapogeuka kuangalia kwa hisani mapungufu ya mwingine, hasa yanapoibuka wazi”.[388]

324. Kwa msukumo wa Roho, familia haiwapokei tu watoto ndani yake kwa kuwazaa, bali pia inafungua milango yake, inatoka nje ya mazingira yake ili kuwagawia wengine wema wake, kuwajali na kuwasaidia wawe na furaha. Huko kufungua milango yake kunaonyeshwa hasa kwa kukaribisha,[389] kama linavyohamasisha Neno la Mungu kwa namna nzuri, “Msisahau kuwafadhili wageni; kwa maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika bila kujua” (Ebr 13:2). Familia inapowakaribisha na iko tayari kuwasaidia wengine, hasa watu maskini na waliotelekezwa, inakuwa ni “ishara na ushuhuda wa umama wa Kanisa, na inaushiriki nalo.”[390] Upendo wa kijamii, ulio kioo cha Utatu Mtakatifu, ndio unaounganisha maana ya kiroho ya familia na utume ambao familia hutoa nje yake, kwa sababu upendo huo hutimiza “kerigma” na sharti zake za kijumuiya. Familia huishi tasaufi yake maalumu huku ikiwa, wakati huohuo, Kanisa la nyumbani na chembe hai ya kugeuza ulimwengu.[391]

****

325. Maneno ya Yesu, Mwalimu wetu (taz. Mt 22:30), na yale ya mtakatifu Paulo kuhusu ndoa (taz. 1Kor 7:29-31), – kwa kusudi maalumu – yanahusianishwa na kweli ya mwisho na ya kudumu ya kuishi kwetu, ambayo tunahitaji kurudi kuizingatia. Hivyo, wanandoa wataweza kuitambua maana ya kweli ya mwendo wao. Kwani, kama tulivyokumbuka mara nyingi katika Wosia huu, hakuna familia iliyo timilifu na kuwekwa tayari kabisa, bali kila familia inahitaji kukuza kwa utaratibu uwezo wake wa kupenda. Pana wito endelevu unaotokana na ushirika kamili wa Utatu Mtakatifu, na umoja wa ajabu wa Kristo na Kanisa lake, na jumuiya nzuri sana ile iliyo familia ya Nazareti, na undugu usio na doa wa watakatifu wa mbinguni. Kutazama ukamilifu ambao hatujaupata bado, kunatufanya tuangalie mwendo wetu wa kifamilia katika maisha haya kwa mtazamo wenye uwiano, ili tuache kudai kwamba katika mahusiano kati ya watu pawepo utimilifu, usafi wa nia na msimamo thabiti vitakavyopatikana tu katika Ufalme wa milele. Tena, kunatuzuia tusihukumu kwa ukali watu wale wanaoishi katika hali ya udhaifu mkubwa wa kiroho. Tunaitwa sote kuendelea kuelekeza mioyo yetu kwenye mambo yanayopita nafsi zetu wenyewe na mapungufu yetu; na kila familia inapaswa kuishi kulingana na msukumo endelevu huu. Enyi familia, tusonge mbele, naam, tuzidi kusonga mbele! Mambo tuliyoahidiwa yapita daima fikra zetu. Tusikate tamaa kwa sababu ya mapungufu yetu; lakini pia tusiache kutafuta utimilifu wa upendo na wa ushirika tulioahidiwa.

Sala kwa Familia Takatifu

Yesu, Maria na Yosefu,
katika ninyi tunatazama
mwangaza wa upendo wa kweli;
tunajikabidhi kwenu tukiwategemea.

Familia Takatifu ya Nazareti,
zifanye familia zetu pia ziwe
mahali pa kushirikiana, na nyumba za sala,
shule halisi za Injili
na Makanisa madogo ya nyumbani.

Familia Takatifu ya Nazareti,
katika familia visiwepo tena
visa vya ukatili, unyanyapaa, matengano;
mtu yeyote aliyejeruhiwa rohoni au kukashifiwa
afarijiwe na kuponywa mara.

Familia Takatifu ya Nazareti,
utujalie tutambue sote
tabia ya wakfu na isiyodhurika ya familia,
na uzuri wake katika mpango wa Mungu.

Yesu, Maria na Yosefu,          
mtusikie na kupokea dua yetu.

Amina.

Imetolewa Roma, penye kanisa la Mtakatifu Petro, katika Jubilei isiyo ya kawaida ya Huruma, tarehe 19 ya mwezi wa Machi, sherehe ya Mtakatifu Yosefu, ya mwaka 2016, wa nne wa Upapa wangu.

Fransisko

 

 


[1] Mkutano wa Dharura wa Tatu wa Sinodi ya Maaskofu, Relatio Synodi, 18 Oktoba 2014, 2.

[2] Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Nne wa Sinodi ya Maaskofu, Relatio finalis, 24 Oktoba 2015, 3.

[3] Hotuba ya kuuhitimisha Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Nne wa Sinodi ya Maaskofu (24 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 26-27 Oktoba 2015, uk. 13; taz. Tume ya Kipapa ya Biblia, Imani na utamaduni katika mwanga wa Biblia. Hati za Kikao cha jumla cha mwaka 1979 cha Tume ya Kipapa ya Biblia, Turin, 1981; Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 44; Yohane Paulo II, Waraka Ensiklika Redemptoris Missio (7 Desemba 1990), 52; AAS 83 (1991), 300; Wosia wa Kitume Evangelii gaudium (24 Novemba 2013), 69, 117: AAS 105 (2013), 1049, 1068-1069.

[4] Hotuba katika mkutano wa familia uliofanyika huko Santiago wa Cuba (22 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 24 Septemba 2015, uk. 7.

[5] Jorge Luis Borges, “Calle desconocida”, katika Fervor de Buenos Aires, Buenos Aires 2011, 23.

[6] Homilia katika Misa huko Puebla de los Ángeles (28 Januari 1979), 2: AAS 71 (1979), 184.

[7] Taz. ilivyotangulia.

[8] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 4: AAS 74 (1982), 84.

[9] Relatio Synodi 2014, 5.

[10] Baraza la Maaskofu la Uhispania, Matrimonio y familia (6 Julai 1979), 3, 16, 23.

[11] Relatio finalis 2015, 5.

[12] Relatio Synodi 2014, 5.

[13] Relatio finalis 2015, 8.

[14] Hotuba kwenye Bunge la Marekani (24 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 26 Septemba 2015, uk. 7.

[15] Relatio finalis 2015, 29.

[16] Relatio Synodi 2014, 10.

[17] Mkutano wa Dharura wa Tatu wa Sinodi ya Maaskofu, Ujumbe, 18 Oktoba 2014.

[18] Relatio Synodi 2014, 10.

[19] Relatio finalis 2015, 7.

[20] Taz. ilivyotangulia, 63.

[21] Baraza la Maaskofu la Korea, Towards a culture of life! – Kuelekea utamaduni wa uhai! (15 Machi 2007).

[22] Relatio Synodi 2014, 6.

[23] Baraza la Kipapa la Familia, Hati ya haki za familia (22 Oktoba 1983), 11.

[24] Taz. Relatio finalis 2015, 11-12.

[25] Baraza la Kipapa la Familia, Hati ya haki za familia (22 Oktoba 1983), Utangulizi.

[26] Taz. ilivyotangulia, 9.

[27] Relatio finalis 2015, 14.

[28] Relatio Synodi 2014, 8.

[29] Taz. Relatio finalis 2015, 78.

[30] Relatio Synodi 2014, 8.

[31] Relatio finalis 2015, 23; taz. Ujumbe kwa Siku ya Dunia kwa ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi 2016 (12 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 2 Septemba 2015, uk. 8.

[32] Relatio finalis 2015, 24;

[33] Taz. ilivyotangulia, 21.

[34] Taz. ilivyotangulia, 17.

[35] Taz. ilivyotangulia, 20.

[36] Taz. kama ilivyotangulia, 15.

[37] Hotuba ya kuuhitimisha Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Nne wa Sinodi ya Maaskofu (24 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 26-27 Septemba 2015, uk. 13.

[38] Baraza la Maaskofu la Argentina, Navega mar adentro (31 Mei 2003), 42.

[39] Baraza la Maaskofu la Meksiko, Que en Cristo Nuestra Paz México tenga vida digna (15 Februari 2009), 67.

[40] Relatio finalis 2015, 25.

[41] Taz. ilivyotangulia, 10.

[42] Katekesi (22 Aprili 2015): L’Osservatore Romano, 23 Aprili 2015, uk. 7.

[43] Katekesi (29 Aprili 2015): L’Osservatore Romano, 30 Aprili 2015, uk. 8.

[44] Relatio finalis 2015, 28.

[45] Taz. ilivyotangulia, 8.

[46] Taz. ilivyotangulia, 58.

[47] Taz. ilivyotangulia, 33.

[48] Relatio Synodi 2014, 11.

[49] Baraza la Maaskofu la Kolumbia, A tiempos difíciles, colombianos nuevos (13 Februari 2003), 3.

[50] Wosia wa Kitume Evangelii gaudium (24 Novemba 2013), 69, 117: AAS 105 (2013), 1049, 1068-1069.

[51] Taz. ilivyotangulia, 164: AAS 105 (2013), 1088.

[52] Taz. ilivyotangulia.

[53] Taz. ilivyotangulia, 165: AAS 105 (2013), 1089.

[54] Relatio Synodi 2014, 12.

[55] Taz. ilivyotangulia, 14.

[56] Taz. ilivyotangulia, 16.

[57] Relatio finalis 2015, 41.

[58] Taz. ilivyotangulia, 38.

[59] Relatio Synodi 2014, 17.

[60] Relatio finalis 2015, 43.

[61] Relatio Synodi 2014, 18.

[62] Taz. ilivyotangulia, 19.

[63] Relatio finalis 2015, 38.

[64] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 13: AAS 74 (1982), 94.

[65] Relatio Synodi 2014, 21.

[66] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1642.

[67] Taz. ilivyotangulia.

[68] Katekesi (6 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 7 Mei 2015, uk. 8.

[69] Leo Mkuu, Epistola Rustico narbonensi episcopo, inquis. IV: PL 54, 1205A; taz. Inkmaro wa Reims, Waraka 22: PL 126, 142.

[70] Taz. Pius XII, Waraka Ensiklika Mystici Corporis Christi (29 Juni 1943): AAS 35 (1943), 202: “Kwenye [sakramenti ya] Ndoa kila mmoja wa wana harusi ni mhudumu wa neema kwa ajili ya mwenzie”.

[71] Taz. Mkusanyo wa Sheria Kanoni, kann. 1116; 1161-1165; Mkusanyo wa Kanoni za Makanisa ya Mashariki, 832; 848-852.

[72] Mkusanyo wa Sheria Kanoni, kan. 1055 § 2.

[73] Relatio Synodi 2014, 23.

[74] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 9: AAS 74 (1982), 90.

[75] Relatio finalis 2015, 47.

[76] Taz. ilivyotangulia.

[77] Homilia katika Misa ya kuhitimisha Mkutano wa Nane wa Dunia wa familia, Philadelphia (27 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 28-29 Septemba 2015, uk. 7.

[78] Relatio finalis 2015, 53-54.

[79] Taz. ilivyotangulia, 51.

[80] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 48.

[81] Mkusanyo wa Sheria Kanoni, kan. 1055 § 1: “imewekwa kwa ajili ya mema ya wanandoa na ya uzazi na malezi ya watoto”.

[82] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2360.

[83] Taz. ilivyotangulia, 1654.

[84] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 48.

[85] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2366.

[86] Taz. Paulo VI, Waraka Ensiklika Humanae vitae (25 Julai 1968), 11-12: AAS 60 (1968), 488-489.

[87] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2378.

[88] Idara Takatifu ya Mafundisho ya Imani, Maelek. Donum vitae (22 Februari 1987), II, 8: AAS 80 (1988), 97.

[89] Relatio finalis 2015, 63.

[90] Relatio Synodi 2014, 57.

[91] Taz. ilivyotangulia, 58.

[92] Taz. ilivyotangulia, 57.

[93] Relatio finalis 2015, 64.

[94] Relatio Synodi 2014, 60.

[95] Taz. ilivyotangulia, 61.

[96] Mkusanyo wa Sheria Kanoni, kan. 1136; taz. Mkusanyo wa Kanoni za Makanisa ya Mashariki, 627.

[97] Baraza la Kipapa la Familia, Ujinsia wa binadamu: ukweli na maana yake (8 Desemba 1995), 23.

[98] Katekesi (20 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 21 Mei 2015, uk. 8.

[99] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 38: AAS 74 (1982), 129.

[100] Taz. Hotuba kwenye Mkutano wa kijimbo huko Roma (14 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 15-16 Juni 2015, uk. 8.

[101] Relatio Synodi 2014, 23.

[102] Relatio finalis 2015, 52.

[103] Taz. ilivyotangulia, 49-50.

[104] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1641.

[105] Taz. Benedikto XVI, Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 2: AAS 98 (2006), 218.

[106] Mazoezi ya kiroho, Taamuli kwa ajili ya kupata upendo, 230.

[107] Octavio Paz, La llama doble, Barcelona 1993, 35.

[108] Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae II-II, q. 114, a. 2, ad 1.

[109] Katekesi (13 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 14 Mei 2015, uk. 8.

[110] Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae II-II, q. 27, a. 1, ad 2.

[111] Taz. ilivyotangulia, a. 1.

[112] Katekesi (13 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 14 Mei 2015, uk. 8.

[113] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 21: AAS 74 (1982), 106.

[114] Hotuba iliyotolewa kwenye Kanisa la Kibaptisti la Dexter Avenue, Montgomery, Alabama, 17 Novemba 1957.

[115] Mt. Tomaso wa Akwino anatambua upendo kama “nguvu inayounganisha” (Summa Theologiae I, q. 20, a. 1, ad 3), akinukulu usemi liotumia kwanza Dionigi Ps.-Areopagita (De divinis nominibus, IV, 12: PG 3, 709).

[116] Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae II-II, q. 27, a. 2.

[117] Waraka Ensiklika Casti connubii (31 Desemba 1930): AAS 22 (1930), 547-548.

[118] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 13: AAS 74 (1982), 94.

[119] Katekesi (2 Aprili 2014): L’Osservatore Romano, 3 Aprili 2014, uk. 8.

[120] Taz. ilivyotangulia.

[121] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 9: AAS 74 (1982), 90.

[122] Tomaso wa Akwino, Summa contra Gentiles, III, 123; taz. Aristotele, Etica Nic., 8, 12 (ed. Bywater, Oxford 1984, 174).

[123] Waraka Ensiklika Lumen Fidei (29 Juni 2013), 52: AAS 105 (2013), 590.

[124] De sacramento matrimonii, I, 2: in Id. Disputationes, III, 5, 3 (ed. Giuliano, Napoli 1858, 778).

[125] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 50.

[126] Taz. ilivyotangulia, 49.

[127] Taz. Summa Theologiae I-II, q. 31, a. 3, ad 3.

[128] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 48.

[129] Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae I-II, q. 26, a. 3.

[130] Taz. ilivyotangulia, q. 10, a. 1.

[131] Maungamo, VIII, 3, 7: PL 32, 752.

[132] Hotuba kwa familia za dunia nzima kwenye hija yao huko Roma katika Mwaka wa Imani (26 Oktoba 2013): AAS 105 (2013), 980.

[133] Malaika wa Bwana (29 Desemba 2013): L’Osservatore Romano, 30-31 Desemba 2013, uk. 7.

[134] Hotuba kwa familia za dunia nzima kwenye hija yao huko Roma katika Mwaka wa Imani (26 Oktoba 2013): AAS 105 (2013), 978.

[135] Summa Theologiae II-II, q. 24, a. 7.

[136] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 48.

[137] Baraza la Maaskofu la Chile, La vida y la familia: regalos de Dios para cada uno de nosotros (21 Julai 2014).

[138] Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 49.

[139] A. Sertillanges, L’amour chrétien, Paris 1920, 174.

[140] Taz. Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae I-II, q. 24, a. 1.

[141] Taz. ilivyotangulia, q. 59, a. 5.

[142] Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 3: AAS 98 (2006), 219-220.

[143] Taz. ilivyotangulia, 4 : AAS 98 (2006), 220.

[144] Taz. Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae I-II, q. 32, a. 7.

[145] Taz. ilivyotangulia, II-II, q. 153, a. 2, ad 2: “Utele wa furaha uliopo katika tendo la kujamiiana linalofanyika kadiri ya akili, haukinzani na utaratibu wa kiasi wa fadhila”.

[146] Yohane Paulo II, Katekesi (22 Oktoba 1980), 5: Mafundisho III, 2 (1980), 951.

[147] Taz. ilivyotangulia, 3.

[148] Yohane Paulo II, Katekesi (24 Septemba 1980), 4: Mafundisho III, 2 (1980), 719.

[149] Katekesi (12 Novemba 1980), 2: Mafundisho III, 2 (1980), 1133.

[150] Taz. ilivyotangulia, 4.

[151] Taz. ilivyotangulia, 5.

[152] Taz. ilivyotangulia, 1: 1132.

[153] Katekesi (16 Januari 1980), 1: Mafundisho III, 1 (1980), 151.

[154] Josef Pieper, Über die Liebe, München 2014, 174.

[155] Yohane Paulo II, Waraka Insiklika Evangelium vitae (25 Machi 1995), 23: AAS 87 (1995), 427.

[156] Taz. Paulo VI, Waraka Insiklika Humanae vitae (25 Julai 1968), 13: AAS 60 (1968), 489.

[157] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 49.

[158] Katekesi (18 Juni 1980), 5: Mafundisho III, 1 (1980), 1778.

[159] Taz. ilivyotangulia, 6.

[160] Taz. Katekesi (30 Julai 1980), 1: Mafundisho III, 2 (1980), 311.

[161] Katekesi (8 Aprili 1981), 3: Mafundisho IV, 1 (1981), 904.

[162] Katekesi (11 Agosti 1982), 4: Mafundisho V, 3 (1982), 205-206.

[163] Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 5: AAS 98 (2006), 221.

[164] Taz. ilivyotangulia, 7.

[165] Relatio finalis 2015, 22.

[166] Katekesi (14 Aprili 1982), 1: Mafundisho V, 1 (1982), 1176.

[167] Glossa in quatuor libros sententiarum Petri Lombardi, IV, XXVI, 2 (Quaracchi 1957, 446).

[168] Yohane Paulo II, Katekesi (7 Aprili 1982), 2: Mafundisho V, 1 (1982), 1127.

[169] Kama ilivyotangulia, Katekesi (14 Aprili 1982), 3: Mafundisho V, 1 (1982), 1177.

[170] Taz. ilivyotangulia.

[171] Yohane Paulo II, Waraka Ensiklika Redemptor hominis (4 Machi 1979), 10: AAS 71 (1979), 274.

[172] Taz. Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae II-II, q. 27, a. 1.

[173] Baraza la Kipapa la Familia, Familia, ndoa na “miungano isiyo rasmi” (26 Julai 2000), 40.

[174] Yohane Paulo II, Katekesi (31 Oktoba 1984), 6: Mafundisho VII, 2 (1984), 1072.

[175] Benedikto XVI, Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 8: AAS 98 (2006), 224.

[176] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 14: AAS 74 (1982), 96.

[177] Katekesi (11 Februari 2015): L’Osservatore Romano, 12 Februari 2015, uk. 8.

[178] Taz. ilivyotangulia.

[179] Katekesi (8 Aprili 2015): L’Osservatore Romano, 9 Aprili 2015, uk. 8.

[180] Taz. ilivyotangulia.

[181] Taz. Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 51: Ni “wazi kwa wote kwamba uhai wa binadamu na jukumu la kuuendeleza uhai huo havifungwi katika mipaka ya maisha ya hapa duniani, wala haviwezi kupimwa na kueleweka katika ulimwengu huu tu, bali vinahusu daima kikomo cha milele cha wanadamu.”

[182] Waraka kwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya watu na Maendeleo (18 Machi 1994): Mafundisho XVII, 1 (1994), 750-751.

[183] Yohane Paulo II, Katekesi (12 Machi 1980), 3: Mafundisho III, 1 (1980), 543.

[184] Taz. ilivyotangulia.

[185] Hotuba katika mkutano wa familia uliofanyika huko Manila (16 Januari 2015): AAS 107 (2015), 176.

[186] Katekesi (11 Februari 2015): L’Osservatore Romano, 12 Februari 2015, uk. 8.

[187] Katekesi (14 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 15 Oktoba 2015, uk. 8.

[188] Baraza la Maaskofu Katoliki la Australia, Waraka wa kichungaji Don’t Mess with Marriage (24 Novemba 2015), 11.

[189] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 50.

[190] Yohane Paulo II, Katekesi (12 Machi 1980), 2: Mafundisho III, 1 (1980), 542.

[191] Taz. Yohane Paulo II, Waraka wa kitume Mulieris dignitatem (15 Agosti 1988), 30-31: AAS 80 (1988), 1727-1729.

[192] Katekesi (7 Januari 2015):L’Osservatore Romano, 7-8 Januari 2015, uk. 8.

[193] Taz. ilivyotangulia.

[194] Katekesi (28 Januari 2015): L’Osservatore Romano, 29 Januari 2015, uk. 8.

[195] Taz. ilivyotangulia.

[196] Taz. Relatio finalis 2015, 28.

[197] Katekesi (4 Februari 2015): L’Osservatore Romano, 5 Februari 2015, uk. 8.

[198] Taz. ilivyotangulia.

[199] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 50.

[200] Kongamano la Tano la Maaskofu wa Marekani ya Kusini na Kati na Karaibi, Hati ya Aparecida (29 Juni 2007), 457.

[201] Relatio finalis 2015, 65.

[202] Taz. ilivyotangulia.

[203] Hotuba katika mkutano wa familia uliofanyika huko Manila (16 Januari 2015):AAS 107 (2015), 178.

[204] Mario Benedetti, “Te quiero”, in Poemas de otros, Buenos Aires 1993, 316: “Tus manos son mi caricia / mis acordes cotidianos / te quiero porque tus manos / trabajan por la justicia. / Si te quiero es porque sos / mi amor mi cómplice y todo / y en la calle codo a codo / somos mucho más que dos”.

[205] Taz. Katekesi (16 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 17 Septemba 2015, uk. 8.

[206] Katekesi (7 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 8 Oktoba 2015, uk. 8.

[207] Benedikto XVI, Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 14: AAS 98 (2006), 228.

[208] Taz. Relatio finalis 2015, 11.

[209] Katekesi (18 Machi 2015): L’Osservatore Romano, 19 Machi 2015, uk. 8.

[210] Katekesi (11 Februari 2015): L’Osservatore Romano, 12 Februari 2015, uk. 8.

[211] Taz. Relatio finalis 2015, 17-18.

[212] Katekesi (4 Machi 2015): L’Osservatore Romano, 5 Machi 2015, uk. 8.

[213] Katekesi (11 Machi 2015): L’Osservatore Romano, 12 Machi 2015, uk. 8.

[214] Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 27: AAS 74 (1982), 113.

[215] Yohane Paulo II, Hotuba kwa walioshiriki kwenye Jukwaa la kimataifa kuhusu kuzeeka hai (5 Septemba 1980), 5: Mafundisho III, 2 (1980), 539.

[216] Relatio finalis 2015, 18.

[217] Katekesi (4 Machi 2015): L’Osservatore Romano, 5 Machi 2015, uk. 8.

[218] Taz. ilivyotangulia.

[219] Hotuba katika mkutano pamoja na wazee (28 Septemba 2014): L’Osservatore Romano, 29-30 Septemba 2014, uk. 7.

[220] Katekesi (18 Februari 2015): L’Osservatore Romano, 19 Februari 2015, uk. 8.

[221] Taz. ilivyotangulia.

[222] Taz. ilivyotangulia.

[223] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 18: AAS 74 (1982), 101.

[224] Katekesi (7 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 8 Oktoba 2015, uk. 8.

[225] Relatio Synodi 2014, 30.

[226] Taz. ilivyotangulia, 31.

[227] Relatio finalis 2015, 56.

[228] Taz. ilivyotangulia, 89.

[229] Relatio Synodi 2014, 32.

[230] Taz. ilivyotangulia, 33.

[231] Taz. ilivyotangulia, 38.

[232] Relatio finalis 2015, 77.

[233] Taz. ilivyotangulia, 61.

[234] Taz. ilivyotangulia.

[235] Taz. ilivyotangulia.

[236] Taz. ilivyotangulia.

[237] Taz. Relatio Synodi 2014, 26.

[238] Taz. ilivyotangulia, 39.

[239] Baraza la Maaskofu la Italia. Tume ya Kiaskofu kwa ajili ya familia na uhai, Maelekezo ya kichungaji kuhusu maandalizi kabla ya ndoa na kuunda familia (22 Oktoba 2012), 1.

[240] Ignasi wa Loyola, Mazoezi wa kiroho, maelezo na. 2.

[241] Taz. ilivyotangulia, na. 5.

[242] Yohane Paulo II, Katekesi (27 Juni 1984), 4: Mafundisho VII, 1 (1984), 1941.

[243] Katekesi (21 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 22 Oktoba 2015, uk. 12.

[244] Baraza la Maaskofu la Kenya, Ujumbe wa Kwaresima (18 Februari 2015).

[245] Taz. Pius XI, Waraka Ensiklika Casti connubii (31 Desemba 1930): AAS 22 (1930), 583.

[246] Yohane Paulo II, Katekesi (4 Julai 1984), 3.6: Mafundisho VII, 2 (1984), 9.10.

[247] Relatio finalis 2015, 59.

[248] Taz. ilivyotangulia, 63.

[249] Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 50.

[250] Relatio finalis 2015, 63.

[251] Relatio Synodi 2014, 40.

[252] Taz. ilivyotangulia, 34.

[253] Cántico Espiritual, B, XXV, 11.

[254] Relatio Synodi 2014, 44.

[255] Relatio finalis 2015, 81.

[256] Taz. ilivyotangulia, 78.

[257] Katekesi (24 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 25 Juni 2015, uk. 8.

[258] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 83: AAS 74 (1982), 184.

[259] Relatio Synodi 2014, 47.

[260] Taz. ilivyotangulia, 50.

[261] Taz. Katekesi (5 Agosti 2015): L’Osservatore Romano, 6 Agosti 2015, uk. 7.

[262] Relatio Synodi 2014, 51; taz. Relatio finalis 2015, 84.

[263] Relatio Synodi 2014, 48.

[264] Taz. Motu proprio Mitis Iudex Dominus Iesus (15 Agosti 2015): L’Osservatore Romano, 9 Septemba 2015, uk. 3-4; Motu proprio Mitis et Misericors Iesus (15 Agosti 2015): L’Osservatore Romano, 9 Septemba 2015, uk. 5-6.

[265] Motu proprio Mitis Iudex Dominus Iesus (15 Agosti 2015), Dibaji, III:  L’Osservatore Romano, 9 Septemba 2015, uk. 3.

[266] Relatio finalis 2015, 82.

[267] Relatio Synodi 2014, 47.

[268] Katekesi (20 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 21 Mei 2015, uk. 8.

[269] Katekesi (24 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 25 Juni 2015, uk. 8.

[270] Taz. Katekesi (5 Agosti 2015): L’Osservatore Romano, 6 Agosti 2015, uk. 7.

[271] Relatio finalis 2015, 72.

[272] Taz. ilivyotangulia, 73.

[273] Taz. ilivyotangulia, 74.

[274] Taz. ilivyotangulia, 75.

[275] Taz. Bula Uso wa Huruma (Misericordiae Vultus), 12: AAS 107 (2015), 409.

[276] Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2358; taz. Relatio finalis 2015, 76.

[277] Taz. kama iliyotangulia.

[278] Relatio finalis 2015, 76; taz. Idara Takatifu ya Mafundisho ya Imani, Tafakari kuhusu mipango ya kutambua kisheria muungano wa watu wa jinsia moja (3 Juni 2003), 4.

[279] Relatio finalis 2015, 80.

[280] Taz. kama ilivyotangulia, 20.

[281] Katekesi (17 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 18 Juni 2015, uk. 8.

[282] Relatio finalis 2015, 19.

[283] Katekesi (17 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 18 Juni 2015, uk. 8.

[284] Taz. ilivyotangulia.

[285] Taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 958.

[286] Taz. ilivyotangulia.

[287] Taz. Maneno ya mwisho, “Daftari ya njano” ya Mama Mkuu Agnesi, 17 Julai 1897: Opere complete, Città del Vaticano - Roma 1997, 1028. Kuhusu hilo, ni muhimu ushuhuda waliotoa masista wenzake kuhusu ahadi ya mtakatifu Teresa kwamba kufariki kwake dunia hii kutakuwa kama “mvua ya waridi” (taz. ilivyotangulia, 9 Juni, 991).

[288] Yordani wa Saksonia, Libellus de principiis Ordinis prædicatorum, 93: Monumenta Historica Sancti Patris Nostri Dominici, XVI, Roma 1935, 69.

[289] Taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 957.

[290] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kidogma Lumen Gentium, 49.

[291] Wosia wa Kitume Evangelii gaudium (24 Novemba 2013), 222: AAS 105 (2013), 1111.

[292] Katekesi (20 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 21 Mei 2015, uk. 8.

[293] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 17.

[294] Katekesi (30 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 1 Oktoba 2015, uk. 8.

[295] Katekesi (10 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 11 Juni 2015, uk. 8.

[296] Taz. Relatio finalis 2015, 67.

[297] Katekesi (20 Mei 2015): L’Osservatore Romano, 21 Mei 2015, uk. 8.

[298] Katekesi (9 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 10 Septemba 2015, uk. 8.

[299] Relatio finalis 2015, 68.

[300] Taz. ilivyotangulia, 58.

[301] Tamko Gravissimum educationis, 1.

[302] Relatio finalis 2015, 56.

[303] Erich Fromm, The Art of Loving, New York 1956, uk. 54.

[304] Waraka Ensiklika Laudato si’ (24 Mei 2015), 155.

[305] Katekesi (15 Aprili 2015): L’Osservatore Romano, 16 Aprili 2015, uk. 8.

[306] Taz. Relatio finalis 2015, 13-14.

[307] De sancta virginitate, 7, 7: PL 40, 400.

[308] Taz. Katekesi (26 Agosti 2015): L’Osservatore Romano, 27 Agosti 2015, uk. 8.

[309] Relatio finalis 2015, 89.

[310] Taz. ilivyotangulia, 93.

[311] Relatio Synodi 2014, 24.

[312] Taz. ilivyotangulia, 25.

[313] Taz. ilivyotangulia, 28.

[314] Taz. ilivyotangulia, 41.43; Relatio finalis 2015, 70.

[315] Relatio Synodi 2014, 27.

[316] Taz. ilivyotangulia, 26.

[317] Taz. ilivyotangulia, 41.

[318] Taz. ilivyotangulia.

[319] Relatio finalis 2015, 71.

[320] Taz. kama iliyotangulia.

[321] Relatio Synodi 2014, 42.

[322] Taz. ilivyotangulia, 43.

[323] Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 34: AAS 74 (1982), 123.

[324] Taz. ilivyotangulia, 9: 90.

[325] Katekesi (24 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 25 Juni 2015, uk. 8.

[326] Homilia katika Misa iliyoadhimishwa pamoja na Makardinali wapya (15 Februari 2015): AAS 107 (2015), 257.

[327] Relatio finalis 2015, 51.

[328] Relatio Synodi 2014, 25.

[329] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 84: AAS 74 (1982), 186. Katika hali kama hizi, wengi, wakijua na kuukubali uwezekano wa kuishi pamoja kama “kaka na dada”, ambao Kanisa linaruhusu, wanagundua kwamba, ikiwa vitendo fulani vya upendo wa ndani vinakosekana, “mara nyingi uaminifu huhatarishwa, na manufaa ya watoto huathirika” (Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 51).

[330] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 84: AAS 74 (1982), 186.

[331] Relatio Synodi 2014, 26.

[332] Taz. ilivyotangulia, 45.

[333] Benedikto XVI, Hotuba kwenye Mkutano wa Saba wa Dunia wa familia, Milan (2 Juni 2012), jibu na. 5: Mafundisho VIII, 1 (2012), 691.

[334] Relatio finalis 2015, 84.

[335] Taz. ilivyotangulia, 51.

[336] Wala kwa yale yanayohusu nidhamu ya kisakramenti, kwa vile upambanuzi unavyoweza kugundua kwamba katika kadhia mahususi hakuna hatia nzito. Hapa lifuatwe nililotamka katika hati nyingine: taz. Wosia wa Kitume Evangelii gaudium (24 Novemba 2013), 44, 47: AAS 105 (2013), 1038, 1040.

[337] Relatio finalis 2015, 85.

[338] Taz. ilivyotangulia, 86.

[339] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 33: AAS 74 (1982), 121.

[340] Relatio finalis 2015, 51.

[341] Taz. Summa Theologiae II-II, q. 65, a. 3, ad 2; De malo, q. 2, a. 2.

[342] Taz. ilivyotangulia, ad 3.

[343] Na. 1735.

[344] Taz. ilivyotangulia, 2352; Idara Takatifu ya Mafundisho ya Imani, Tamko Iura et bona kuhusu kifo laini (5 Mei 1980), II: AAS 72 (1980), 546. Yohane Paulo II, kwa kukosoa dhana ya “chaguo la kimsingi”, alikubali kwamba “bila shaka inawezekana kuwepo hali changamani na za kigiza kwa upande wa saikolojia, ambazo zinaathiri uwezo wa kumshutumu binafsi mtu aliyetenda dhambi” (Wosia wa Kitume Reconciliatio et paenitentia (2 Desemba 1984), 17: AAS 77 (1985), 223.

[345] Taz. Baraza la Kipapa kwa ajili ya hati za Kisheria, Tamko kuhusu uwezekano wa kuruhusu kupokea Ekaristi wenye talaka waliofunga ndoa nyingine (24 Juni 2000), 2.

[346] Relatio finalis 2015, 85.

[347] Summa Theologiae I-II, q. 94, a. 4.

[348] Akifafanua kuhusu ufahamu wa jumla wa sheria na ufahamu binafsi wa upambanuzi wa kiutendaji, mtakatifu Tomaso anafikia kusema kwamba “ikiwa upo ufahamu wa aina moja tu kati ya hizo, bora uwe ule ufahamu binafsi wa uhalisia, ambao unakaribia zaidi utendaji” (Sententia libri Ethicorum, VI, 6 [ed. Leonina, t. XLVII, 354]).

[349] Hotuba ya kuuhitimisha Mkutano wa Kawaida wa Kumi na Nne wa Sinodi ya Maaskofu (24 Oktoba 2015): L’Osservatore Romano, 26-27 Oktoba 2015, uk. 13.

[350] Tume ya Kimataifa ya Teolojia, Kutafuta kanuni za maadili kwa wote: mtazamo mpya kuhusu sheria asilia (2009), 59.

[351] Katika kadhia fulani, ingeweza kuwa pia msaada wa Sakramenti. Kwa hiyo, “ninawakumbusha mapadre kwamba sanduku la kitubio halipaswi kuwa chumba cha mateso, bali mahali pa kuona huruma ya Bwana” (Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium (24 Novemba 2013), 44: AAS 105 [2013], 1038). Vilevile, ninasisitiza kuwa Ekaristi “si tuzo kwa walio wakamilifu, bali ni dawa na chakula kilichotolewa kwa ukarimu kwa wale walio dhaifu” (kama ilivyotangulia, 47: 1039).

[352] Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium (24 Novemba 2013), 44: AAS 105 (2013), 1038-1039.

[353] De catechizandis rudibus, I, 14, 22: PL 40, 327; taz. Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium (24 Novemba 2013), 193: AAS 105 (2013), 1101.

[354] Relatio Synodi 2014, 26.

[355] Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium (24 Novemba 2013), 44: AAS 105 (2013), 1038.

[356] Taz. ilivyotangulia, 45: AAS 105 (2013), 1039.

[357] Taz. ilivyotangulia, 270: AAS 105 (2013), 1128.

[358] Taz. Bula Uso wa Huruma (Misericordiae Vultus, 11 Aprili 2015), 12: AAS 107 (2015), 407.

[359] Taz. ilivyotangulia, 5: 402.

[360] Taz. ilivyotangulia, 9: 405.

[361] Taz. ilivyotangulia, 10: 406.

[362] Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium (24 Novemba 2013), 47: AAS 105 (2013), 1040.

[363] Taz. ilivyotangulia, 36-37: AAS 105 (2013), 1035.

[364] Huenda kwa hofu ya kukosea, iliyofichwa nyuma ya hamu kubwa ya kuwa waaminifu katika kushika ukweli, mapadre wengine wanadai kwamba wanaofanya kitubio waweke nia ya kutubu pasipo mashaka yoyote, kiasi kwamba – kwa kudai hivyo – huruma hufifia chini ya utafutaji wa haki kamili ambayo ni ya ndoto tu. Kwa hiyo, ni muhimu kukumbuka mafundisho ya mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye alitamka kuwa ukitazamiwa kuwa mtu ataanguka tena “hii si sababu ya kukataa ukweli wa nia iliyowekwa” (Waraka kwa Kard. William W. Baum kwenye nafasi ya semina kuhusu medani ya ndani iliyoandaliwa na Penitensiari ya Kitume [22 Machi 1996], 5: Mafundisho XIX, 1 [1996], 589).

[365] Tume ya Kimataifa ya Teolojia, Tumaini la wokovu kwa watoto waliokufa bila kubatizwa (19 Aprili 2007), 2.

[366] Bula Uso wa Huruma (Misericordiae Vultus, 11 Aprili 2015), 15: AAS 107 (2015), 409.

[367] Tamko Apostolicam actuositatem, 4.

[368] Taz. kama iliyotangulia.

[369] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kichungaji Gaudium et Spes, 49.

[370] Waraka Ensiklika Deus caritas est (25 Desemba 2005), 16: AAS 98 (2006), 230.

[371] Taz. ilivyotangulia, 39: AAS 98 (2006), 250.

[372] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume wa baada ya Sinodi Christifideles laici (30 Novemba 1988), 40: AAS 81 (1989), 468.

[373] Taz. ilivyotangulia.

[374] Relatio finalis 2015, 87.

[375] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume wa baada ya Sinodi Vita consecrata (25 Machi 1996), 42: AAS 88 (1996), 416.

[376] Taz. Relatio finalis 2015, 87.

[377] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 57: AAS 74 (1982), 150.

[378] Tusisahau kwamba Agano la Mungu na watu wake linaonyeshwa kuwa kama uchumba (taz. Eze 16:8.60; Isa 62:5; Hos 2:21-22), na Agano Jipya linachukua pia sura ya ndoa (taz. Ufu 19:7; 21:2; Efe 5:25).

[379] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konstitusyo ya kidogma Lumen gentium, 11.

[380] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 11: AAS 74 (1982), 93.

[381] Yohane Paulo II, Homilia katika Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwa ajili ya familia za Córdoba – Argentina (8 Aprili 1987), 4: Mafundisho X, 1 (1987), 1161-1162.

[382] Taz. Gemeinsames Leben, München 1973, 18 (tafsiri ya Kiing.: Life Together, New York, 1954, uk. 27)

[383] Mtaguso Mkuu Vatikano II, Tamko Apostolicam actuositatem, 11.

[384] Katekesi (10 Juni 2015): L’Osservatore Romano, 11 Juni 2015, uk. 8.

[385] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 12: AAS 74 (1982), 93.

[386] Hotuba kwenye Sherehe ya Familia na kesha la sala, Filadelfia (26 Septemba 2015): L’Osservatore Romano, 28-29 Septemba 2015, uk. 6.

[387] Gabriel Marcel, Homo viator. Prolégomènes à une métaphysique de l´espérance, Paris 1944, 63.

[388] Relatio finalis 2015, 88.

[389] Yohane Paulo II, Wosia wa Kitume Familiaris consortio (22 Novemba 1981), 44: AAS 74 (1982), 136.

[390] Taz. ilivyotangulia, 49: AAS 74 (1982), 141.

[391] Kuhusu masuala ya kijamii ya familia, taz. Baraza la Kipapa linaloshughulikia masuala ya Haki na Amani, Mkusanyiko wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii, 248-254.

 



Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana